Kiongozi wa Azaki agusa umuhimu wa majadiliano ya kitaifa

Kiongozi wa Azaki agusa umuhimu wa majadiliano ya kitaifa

Parabolic

JF-Expert Member
Joined
Dec 3, 2013
Posts
2,743
Reaction score
2,601
770fe4c7-6139-4204-ac62-054ecf309d88.jpg

Geneva, Uswisi. Kiongozi wa asasi za kiraia nchini Tanzania, Martina Kabisama, ameangazia maendeleo yaliyofikiwa na Tanzania katika kuimarisha haki za binadamu, mshikamano wa kijamii na majadiliano ya kitaifa wakati wa kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachoendelea mjini Geneva, Uswisi.

Kabisama, ambaye ni Mratibu wa Kitaifa wa SAHRiNGON Tanzania Chapter na Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Action for Change, alitoa maelezo hayo alipowasilisha mada katika mjadala uliofanyika ndani ya ukumbi wa Palais des Nations Machi 11, 2026.

Katika wasilisho lake, alieleza umuhimu wa kukuza majadiliano ya kitaifa, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuendeleza heshima kwa haki za binadamu, akibainisha kuwa Tanzania imeendelea kujenga msingi imara wa amani, umoja na ustahimilivu wa kijamii kwa muda mrefu.

Alisema Tanzania imeendelea kuimarisha mazingira ya utawala shirikishi na ushiriki wa wananchi katika maendeleo kupitia dhamana za kikatiba zinazolinda uhuru wa kutoa maoni, kujumuika na kushiriki katika shughuli za kijamii na kitaifa.

Kabisama pia alibainisha kuwa, Tanzania imepiga hatua katika kuimarisha haki za kijamii na kiuchumi kupitia upanuzi wa huduma muhimu za jamii, ikiwemo elimu, afya, maji, makazi na fursa za ajira.

Aidha, alitaja mafanikio katika kuwawezesha wanawake kumiliki ardhi kupitia mifumo ya kisheria kama Sheria ya Ardhi ya Vijiji na Sheria ya Ardhi, hatua ambazo zimechangia kuongeza ushiriki wa wanawake katika shughuli za uzalishaji na kuimarisha ustawi wa kaya.

Akizungumzia nafasi ya vijana katika maendeleo ya taifa, alisema uwekezaji katika elimu, ujuzi, ubunifu na teknolojia ni msingi muhimu wa kujenga taifa lenye maendeleo jumuishi na endelevu.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa bado zipo changamoto zinazohitaji juhudi za pamoja, ikiwemo tofauti za maendeleo kati ya maeneo na upatikanaji usio sawa wa baadhi ya huduma za msingi.

Kwa mujibu wa Kabisama, kukabiliana na changamoto hizo kunahitaji kuendelea kuimarisha taasisi, kujenga ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo, kudumisha dhamira ya kisiasa katika kusukuma mbele ajenda ya haki za binadamu na maendeleo jumuishi.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya asasi za kiraia na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, akieleza kuwa ushirikiano huo ni nyenzo muhimu katika kukuza uwajibikaji, kupanua upatikanaji wa haki na kulinda maslahi ya makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.

Alitaja pia mchango wa asasi za kiraia katika utekelezaji wa programu mbalimbali za elimu ya uraia, utoaji wa msaada wa kisheria na ufuatiliaji wa haki za binadamu kuwa umeendelea kusaidia wananchi kutambua haki zao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na taifa.

Katika muktadha huo, alitaja Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kuwa hatua muhimu katika kupanua wigo wa huduma za haki kwa wanawake, watoto na makundi mengine yenye uhitaji maalum.
Akihitimisha wasilisho lake, Kabisama alisema heshima kwa utu wa binadamu inapaswa kuendelea kuwa msingi wa maendeleo endelevu, amani ya kijamii na mshikamano wa taifa.

Alisisitiza kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kutenganishwa na uwepo wa majadiliano ya wazi, taasisi imara na ushiriki jumuishi wa wananchi.

Aidha, alinukuu mwelekeo wa uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, unaojengwa katika misingi ya 4Rs—Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi Upya—akieleza kuwa mfumo huo unaendelea kutoa nafasi kwa Tanzania kuimarisha utawala bora, kujenga mshikamano wa kitaifa na kuendeleza mageuzi yanayowagusa wananchi kwa upana.

Ushiriki wa Kabisama katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa unaakisi nafasi inayozidi kuimarika ya asasi za kiraia za Tanzania katika majukwaa ya kimataifa, pamoja na dhamira ya nchi kuendelea kukuza haki za binadamu, majadiliano ya kitaifa na maendeleo jumuishi.
 
Back
Top Bottom