Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewaambia wapinzani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuwa inaweza kuwachukua muda mrefu mno kupata nafasi ya kuunda Serikali, ama pengine wasiipate kabisa, na hivyo ni muhimu kwao kushirikiana na Serikali ya CCM katika kuwaletea wananchi wa Tanzania Visiwani maendeleo.
Rais pia amesema kuwa ni fitina za kisiasa kwa wapinzani wa Serikali ya SMZ kuibeza na kuikejeli Serikali hiyo kwa madai kuwa haijaleta maendeleo yoyote Tanzania Visiwani.
Aidha Rais amewaambia wananchi wa Pemba kuwa wanayo haki ya kuendelea kumchagua yoyote wanayemtaka ili awe mbunge ama mwakilishi, ili mradi tu waendelee kukabidhi dhamana ya kuendesha Serikali kwa Chama cha Mapinduzi.
Amesisitiza kuwa Serikali ya SMZ na ile ya Muungano zitaendelea kuwaletea maendeleo wananchi wa Visiwani bila upendeleo wala kubagua yoyote kwa sababu huo ndiyo mkataba kati ya Serikali na wananchi, na kwa sababu kuleta maendeleo ni dhamana ya Serikali iliyoko madarakani, na wala siyo wapinzani.
Madai kuwa Serikali haijafanya lolote wala chcochote ni fitina tu za kisiasa. Unajua midomo kazi yao ni kusema. Unaweza kusema lolote hasa inapokuwa usemaji wenyewe ni wa kufitini, yaani kudanganya watu, ili wakuchague. Mafanikio yamepatikana mengi ndugu wananchi katika elimu, katika barabara. Na hizi barabara tutazijenga pote, hata pale Mtambwe, alisema na kuongeza:
Tutamwendeleza kila mtu kwa sababu dhamana ya maendeleo ni yetu katika Serikali. Hawa wengine hawana Serikali. Kazi yao, na wabunge wao, na wawakilishi wao, ni kufoka tu. Sisi ndio wenye dhamani ya Serikali na wala hatubagui.
Rais aliyasema hayo wakati aliposalimiana na wananchi katika nyakati na matukio tofauti jana, Jumatano, Januari 21, 2009 kwenye siku yake ya pili na ya mwisho ya ziara yake katika Kisiwa cha Pemba ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku sita Tanzania Visiwani. Rais ameanza ziara ya siku nne katika Kisiwa cha Unguja leo, Alhamisi, Januari 22, 2009 baada ya kuwa amekamilisha ziara yenye mafanikio katika Pemba.
Akizungumza na wananchi baada ya kuwa amefungua mradi wa maji wa Kengeja, Mkoa wa Kusini Pemba, Rais alisema kuwa ni muhimu kwa wananchi wote, bila kujali itikadi zao za kisiasa, kushirikiana na Serikali iliyoko madarakani katika kusaka maendeleo.
Alisema kuwa ni kinyume cha taratibu za ushindani wa kidemokrasia kwa chama kimoja kusema kuwa hakiwezi kushirikiana na Serikali iliyoko madarakani kikidai kuwa kinasubiri mpaka kitakapoweza kuunda Serikali.
Ni muhimu kwa watu kukubali kuwa ipo Serikali iliyoko madarakani hata kama wanakataa jinsi ilivyoingia madarakani. Ukweli ni kwamba ipo na ni muhimu kwa watu wote kushirikiana nayo katika kuleta maendeleo. Maana ukisubiri hiyo Serikali yako inaweza ikachelewa sana ama pengine isije kabisa katika uhai wako, alisema na kuongeza:
Akizungumzia mabezo na kejeli za wapinzani wa CCM kuwa Serikali ya SMZ haijaleta maendeleo yoyote kwa wananchi, Rais Kikwete aliwaambia wananchi hao wa Kengeja: Wananchi, hizi ni fitina tu. Unajua midomo kazi yake ni kusema. Unaweza kusema lolote hasa inapokuwa kwenye kufitini, kudanganya watu ili wakuchague.
Aliongeza Rais Kikwete: Ukweli ni kwamba mafanikio yamepatikana mengi
iwe kwenye elimu ama barabara. Nimesema kuwa tutatoa huduma za kijamii kwa wananch wote bila kubagua kati ya wale waliotupigia kuara ama wale waliokipigia kile chama kingine. Hata ile barabara ya Mtambwe tutaijenga tu.
Rais Kikwete alisema kuwa ni muhimu kwa Serikali kuendelea kutoa huduma kwa wananchi bila kubagua kwa sababu Serikali ndiyo yenye dhamana ya kuleta maendeleo, akisisitiza: Maana wao hawana Serikali, kazi yao na wabunge wao na wawakilishi wao ni kufoka tu. Sisi ndio wenye dhamana ya Serikali. Ujumbe wetu kwa wapinzani wetu ni rahisi kabisa kuwa nyie endeleeni kuwachagua mnaowataka, lakini sisi endeleeni kutukabidhi Serikali na dhamana ya kuleta maendeleo.
Alisisitiza: Wao wacha waendelee kutia fitina, kubeza maendeleo, lakini maji safi wanaendelea kunywa. Barabara wanaendelea kupita wakipepeza bendera zao kwa sababu zinateleza kama mgongo wa ngisi. Anapata taabu sana kuisifia Serikali ya CCM hadharani, lakini akikaa na mkewe chumbani anasema kuwa hawa CCM kiboko kwa maendeleo. Lakini akitoa hadharani anabeza akisema hawa CCM watu gani? Lakini maji anakunywa.
Akizungumza baada ya kuwa amekagua ujenzi wa barabara ya lami kati ya Mkoani na Makombeni katika mkoa huo huo wa Kusini Pemba, Rais Kikwete aliendeleza somo lake kwa wapinzani akisema:
Ndugu wananchi, msije kudanganywa. Kazi ya maendeleo haiku mikononi mwa mbunge ama mwakilishi. Hii ni kazi na dhamana ya Serikali
zote mbili ya SMZ na Muungano. Mbunge hawezi kujenga barabara ya lami. Sisi ndio wenye dhamani kwa waliotuchagua na hata wale ambao hawakutuchagua
Alisema kuwa lazima Watanzania watofautishe vipindi vya uchaguzi na vipindi vya maendeleo. Tutofautishe kipindi cha uchaguzi na kipindi cha maendeleo. Tutambue kuwa siasa za uchaguzi ni siasa za uchaguzi, baada ya hapo mleta maendeleo ni Serikali. Na hata baadhi ya watu wakinuna wakati tukipita, lakini ukweli ni kwamba Serikali tunayo sisi. Anayewaongopea vinginevyo, mwambie hivyo sivyo.
Wakati ya ushindani ni wakati wa uchaguzi. Yakitangazwa matokeo hata kama hukuridhika nayo ni lazima ukubali kushirikiana na washindi. Sasa utafanyaje hata kama huyo ndiye mwenye dhamani. Lakini huyo ndiye binadamu, akishakuwa ameshiba ugali na ngisi, basi maneno yanakuwa mengi.
Akizungumza baada ya kuwa amefungua soko la Mvumoni na kutoa boti na nyavu za uvuvi kwa vikundi mbali mbali, Rais Kikwete amesema kuwa amefurahi kusikia kuwa vikundi vya kupata boti na nyavu havikuchaguliwa kwa ubaguzi wa vyama ana itikadi.
Nafurahi kusikia kuwa tabia hii haiko kwenye mradi huu. Maana baada ya uchaguzi mtu wa CCM alikuwa akinyimwa huduma dukani ama kukataliwa kubebwa kwenye boti. Sasa sukari ina CCM na CUF? Ama kama kila mwanachama wa chama siasa akianzisha duka lake tutakuwa na maduka mangapi? Aliuliza Rais Kikwete na kusisitiza:
Mwanademokrasia wa kweli, akimaliza uchaguzi hushirikiana na wenzake katika kuleta maendeleo. Hivi kama Serikali ingekuwa na fikra kama yule anayemkataza mwenzake kupanda boti yake kwa sababu ya itikadi, hivi Pemba ingekuwa maji, ama barabara nzuri, ama maji, ama skuli?
Rais Kikwete alisema kuwa ni wajibu wa vyama vya siasa kujua kuwa kina mtu anatawala kwa zamu yake ya kutawala kama anachaguliwa na wananchi lakini muhimu ni kushirikiana. Kila mtu kwa zamu yake. Lakini ushirikiano ni wakati wote. Hivi wewe hutaki kushiriki na Serikali iliyopo ukingojea Serikali yako. Hivi itakuja lini? Na kama haikuja je?
Alisema kuwa mfano nzuri ni wa Marekani. Pale Marekani alikuwa ni Rais Bush wa Chama cha Republican. Watu wamekikataa chama hicho zamu hii. Wamemchagua Barak Hussein Obama, Mswahili, tena baba yake Jaluo. Ameapa jana na vyama vyote viwili sasa vitashirikiana katika kuleta maendeleo. Midahalo yako itabakia Bungeni tu.
Kama nilivyosema kila mahali nilipopita. Tupambane wakati wa uchaguzi, baada ya hapo tujenge nchi yetu kwa pamoja. Hata kama hukuridhika na jinsi mwenzako alivyoshinda, yeye ndiye kashinda,yeye ndiye yuko madarakani. Muhimu kushirikiana naye.