Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,380
- 39,333
Na. M. M. Mwanakijiji
(Makala hii imetoka kwenye gazeti la Tanzania Daima leo. Kutokana na matatizo ya kiufundi gazeti hilo halikuwa kwenye mtandao)
Kuna msemo wa Kiswahili kuwa "mtu mzima hatishiwi nyau". Msemo huu unapotumika mara nyingi unataka kutuma ujumbe kwa mtu kuwa mtu mzima hapigwi mikwara ya kitoto. Hata hivyo msemo huu unakosa ukweli mmoja ambao ni dhahiri; paka akibanwa hupigana kama simba. Rafiki yangu mmoja hivi majuzi alijikuta yuko kwenye mapambano na paka wa jirani ambaye aliingia kwenye sebule yake bila kukaribishwa. Kwa vile jamaa yangu hapendi paka basi akaamua "kumtolea uvivu" kwenye eneo la baraza lililozungukwa kwa uzio wa nyavu nyavu za chuma huku mlango wa sebule ukiwa umefungwa na ule wa kutokea nje ukiwa umefungwa pia.
Mwenyewe aliliita hilo ni pambano la "karne". Paka wa watu hakutaka ugomvi na mtu alichotaka yeye ni kuruhusiwa kwenda zake nje. Jamaa akajifanya yeye jasiri akaanza kumtandika paka wa watu mangumi na mateke; paka akalia huku akikimbia kujificha akitafuta mahali pa kutokea. Mwishowe yule paka akaona hana la kufanya isipokuwa kujibu mashambulizi. Nilipopigiwa simu huyo bwana alikuwa amekimbizwa hospitali akiwa anavuja damu baada ya kupata kibano cha "nyau". Alipotoka hospitali na kunisimulia kisa hiki nilishindwa kujizuia kuhuzunika bali nilibakia kucheka hadi masikio yakaniuma.
Nikagundua kuwa hata mtu mzima akitishiwa nyau lazima ashtuke kwa maana akijifanya yeye mjanja anaweza kutoka na mikwaruzo na kutolewa nishai na paka. Hata hivyo ninaamini msemo mzuri ni ule usemao (nimeutunga mwenyewe) Simba wa karatasi haungurumi wala hang'ati. Yawezekana kabisa mtu akamchora simba mkali kabisa akiwa amekenua meno na manyoya yametoka huku macho yake makali yakiangalia kwa hasira lakini akimsimamisha na kumuelekeza hata kwa mtoto mdogo zaidi atakachofanya mtoto huyo ni kuigusa hiyo picha ya "simba mkali". Simba wa picha anaweza kutisha wale ambao hawajui vitu vya kuchora au picha (sidhani kama watu hao wapo). Mtu hata hawa na lengo gani akisimama na simba wake wa kuchora kuwatishia watu kinachofanyika watu watadhania ni msanii wa aina fulani ambaye anajaribu kuburudisha watu kwa vikatuni au vikaragosi. Naogopa kuwa mikwara ya Rais Kikwete imekuwa kama picha ya simba mkali asiyeunguruma wala kung'ata!
Akiwa katika ziara yake inayoendelea Mkoani Pwani, Rais Kikwete alipata nafasi ya kutembelea mradi wa miembe inayozaa kwa muda mfupi ambapo walengwa wakubwa ni watu wenye kipato cha chini. Mojawapo ya malalamiko ambayo yamekuwa yakisikika ni madai kuwa kuna baadhi ya viongozi ambao wanatakiwa kusimamia mradi huo wameanza kujigawia "miembe" na hivyo walengwa wenyewe hawanufaiki. Rais Kikwete aliposikia malalamiko hayo alishikilia picha yake ya kuchora ya simba na kusema kuwa "Naomba tuelewane kabisa Mkigawana miradi ya maendeleo ambayo imelengwa kuinua maisha ya wananchi maskini na kuwapatia kipato, mtakiona cha mtemakuni nitawasema hadharani mbele ya wananchi" Watu wakasimama na kuipigia makofi picha hiyo. Waliowajanja wakajisema moyoni, tumeshayasikia hayo huko nyuma.
Sijui lengo la Rais kuwasema hawa viongozi kwa wananchi lilikuwa ni nini na sielewi kama yeye anamaanisha kweli kuwa kukiona cha mtema kuni ni kuwasema hadharani. Ukweli ni kuwa mtu mzima hatishiwi nyau, na simba wa kuchora hang'ati wala hangurumi. Haya ya kusema hadharani na kuwataja hadharani wahalifu au wasiofuata taratibu siyo mambo mageni katika utawala wa Rais Kikwete. Mikwara hii ya Kikwete tumeanza kuizoea sasa kama vile picha ya kuchora ya simba mwenye masharubu ambaye amepanua mdomo! Tumeshatambua ni picha tu, simba haumi.
Huyu simba kama angekuwa anauma angeshauma zamani. Miaka miwili sasa vitisho vya serikali ya Rais Kikwete kwa waalifu vimekuwa ni vya kawaida na hasa kwa wale wahalifu wanaotumia kalamu huku wametinga tai zao nzuri na wakiendesha magari yanayoendeshwa kwa gharama za wananchi.
Nakumbuka vizuri ziara yake ya Musoma ambako alisimama na kushikilia picha hiyo ya simba asiyenguruma na kusema kuwa serikali yake haitavumilia viongozi wezi, wala rushwa na na wabovu katika halmashauri mbalimbali nchini. Tukatarajia kuwa "mshikemshike" kwenye halmashauri uko njiani. Kumbe ilikuwa ni picha tu ya simba anayeonekana kama anaunguruma.
Hiyo haikuwa mwisho, tarehe mbili Oktoba mwaka jana akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari nchini Ikulu jijini Dar-es-Salaam alikiri kupokea waraka wenye kutaja majina ya vigogo wanaojihusisha na madawa ya kulevya. Na hivi karibuni Inspekta Jenerali wa Polisi Bw. Saidi Mwema naye alisema kuwa wanayo majina karibu mia mbili na karibu nusu ya majina hayo ya "vigogo wa madawa" yalipelekwa Ikulu. Sasa msiniulize inakuwaje Polisi Mkuu na nambari uno anashindwa kufuata sheria ya kuwatia pingu wahalifu hawa na anaamua kupeleka majina Ikulu. Kumbe na Mwema naye ameshikilia picha ya simba asiyeng'ata.na kupeleka majina kwa Rais.
Bila ya shaka wengi bado wanakumbuka wakati ule Rais Kikwete akiwa ameshikilia picha yake ya simba asiyeng'ata aliwaambia wananchi kuwa anawajua pia viongozi wala rushwa na amewapa muda "wajirekebishe".
Sasa siyo Kikwete tu ambaye anashikilia picha ya simba aliyechorwa kwani yule kiongozi mahiri, shujaa aliyetamba Bungeni na yeye hivi karibuni alikuja na maneno mengine ambayo natumaini alidhani sikuyatilia maanani. Akiwa Morogoro kwenye kuadhimisha kusimikwa kwa Askofu mpya wa Dayosisi ya Morogoro Waziri Mkuu alisimama na kusema kuwa imetosha wananchi kulalamika kuwa kwenye vita dhidi ya madawa ya kulevya wenye kukamatwa ni watu wadogo wadogo huku vigogo wakiangaliwa tu. Akanukuliwa kusema kuwa "Jamani kwa muda mrefu nimekuwa nasikia wanaokamatwa kwa dawa za kulevya na rushwa eti ni watu wadogo wadogo huku vigogo wakitazamwa, tatizo ni kuwa mnasema tu vigogo, vigogo hamuwataji. Nasema watajeni, na ninaahidi tutawashughulikia bila kujali cheo cha mtu au nafasi aliyonayo katika taifa hili na nje ya taifa"
Sasa sisi wengine tunajiuliza hivi Ikulu hawawasiliani na ofisi ya Waziri Mkuu? Je inawezekana kinachofanyika Ikulu Waziri Mkuu hakijui. Wakati Rais wake amesema ameshayapata majina na IGP kasema majina yamepelekwa Ikulu iweje leo Mhe. Lowassa aseme wananchi hawana ujasiri wa kutaja majina ya vigogo hao? Labda anataka wananchi waitishe mkutano wa waandishi wa habari au wafanye kama wapinzani pale Jangwani na kuanza kuorodhesha vigogo wa madawa ya kulevya au waende polisi na kuwanong'oneza vigogo wao. Hata hivyo hapo kuna tatizo.
Tatizo ni kuwa kuwa wananchi wanapowataja vigogo wa ufisadi (na hapa inajumlisha rushwa, matumizi mabaya ya vyeo, madawa ya kulevya n.k) wanaambiwa "hizo ni tuhuma tu leteni ushahidi". Wakiwataja wale wanaowatambua kuwa ndio vilele vya ufisadi nchini Rais anaficha picha yake ya simba na kusema "msijifanye polisi, wapelelezi na mahakimu". Tatizo ni kuwa majina yakitajwa Chama cha Mapinduzi na wapambe wake watajitokeza na kusema "hizo ni kelele za wapinzani, wapuuzieni". Sasa hapa ndio wananchi wanachanganyikiwa. Wasipotaja wanaambiwa "mbona hamuwataji", wakitaja wanaambiwa "acheni kuwazulia viongozi tuhuma zisizothibitishwa". Sasa hata uamuzi wa kusuka au kunyoa siyo rahisi namna hiyo. Vinginevyo waseme kama watanzania wanaotakiwa kutaja wahalifu ni wana CCM peke yao.
Binafsi naamini kabisa kuwa Rais Kikwete na viongozi waliopo madarakani wananguvu zote za kisheria na Kikatiba za kuweza kukomesha ufisadi wa aina nyingi nchini. Hawahitaji nguvu zaidi bali dhamira za wazi za kufanya kile ambacho wamekuwa wakikitishia kwa miaka miwili sasa. Semina Elekezi ya ngurdoto hazikusaidia, hotuba Bungeni hazikusaidia, na sasa mikwara hii ya "hatua kali" haijawafanya wajanja kutetemeka. Imetosha kuwasikiliza, maneno yao yamekuwa matamu mno hadi yanatia kichefuchefu. Waoneshe kuwa wanaweza kutekeleza bila woga, haya, husuda, kisasi, au upendeleo.
Kuendelea kuwatishia wahalifu kwa picha ya simba wa kuchorwa haitoshi. Kama mnaye simba wa kweli kwanini msimuweke hadharani muone watu watakavyotimuana. Hata hivyo ninafahamu tatizo la msingi ambalo siyo tu linampa kusita Rais Kikwete lakini linamgwaisha Lowassa. Ni tatizo ambalo bado hawajaweza kulipatia majibu kwa sababu linahusu kuweka dawa kwenye kidonda kilicho kwenye ngozi zao wenyewe.
Kama wameamua kulindana watuambie tu ili tukubali yaishe. Labda umefika wakati Watanzania tuamue kuwaziria nchi ili watafune, wameze, na kusaza. Haina maana kuendelea kuwalalamikia au kuwaonesha mapungufu; Hakuna maana kuwakosoa maana kwao ni wimbo waliouzoea. Tuwaachie BoT, tuwaachie madini, tuwaachie mikataba ya nishati na kila kitu wanachotaka. Tusiwaulize tena, tuwasusie Tanzania ili watawale wanavyopenda maana hizi kelele zetu zinawakera na wanaona tunawatakia mabaya.
Hata tutakapoamua kuzira hivyo watambue kuwa kuna kizazi cha wananchi ambacho hakitazira kitaendelea kuwakalia kwenye shingo zao kama jinamizi na kuendelea kupiga kelele kama mtu aliyefumania. Kizazi hicho kitakapokuwa kimekata tamaa kweli watawala watakichukia. Leo hii tunasikia madini yanaibwa toka kwenye gari la CCM (msiniulize ilikuwaje); ndani ya wiki moja migodi mitatu inavamiwa na watu kuchukua madini kama utani. Tumeyaona Delta kule Nigeria pale wananchi walipokata tamaa baada ya kuona mali yao ya asili ikichotwa na kujenga nchi za watu wengine. Leo hii wameanzisha vitendo vya kuhujumu sekta ya mafuta kule Delta kwa kushambulia visima na kuteka watendaji wa makampuni ya mafuta.
Natumaini na ninaombea kwenye Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema na Mwenye Huruma kuwa yaliyotokea Mwadui, Bukombe na Mererani wiki iliyopita ni matukio ya uhalifu wa kawaida tu na ya nadra. Kwa sababu kama tunachoshuhudia ni mwanzo wa uhalifu wa kupangwa dhidi ya makampuni ya madini au sekta hiyo basi ndugu zangu huko mbeleni ni machozi na hofu. Naomba nitoe wito kwa heshima kubwa na taadhima; Mhe. Rais na wenzako, hatutaki vitisho tena, hatutaki kushikiwa picha ya simba wa kuchorwa, na kwa hakika tumechoka na kibwagizo cha "tumepewa majina ya wahalifu" . Wananchi wasitoe majina tena ya wahalifu hadi yale yaliyokwishatolewa yafanyiwe kazi. Vinginevyo tutaoneshana haya mazingaombwe hadi tusikie kizunguzungu. Simba ambaye mmemshikilia mbele ya wahalifu imegundulika ni mdoli tu na ni wapicha, haumi kwani meno yake ya plastiki! Mkitaka wahalifu wajue mko makini na mliodhamiria, acheni porojo za kisiasa na fanyeni kweli. Vinginevyo, tutawaziria nchi. Najua hilo liwafurahisha maana hatimaye mtaweka picha ya simba chini ili muendelee na "shughuli" zenu bila kusumbuliwa.
Niandikie: mwanakijiji(at)jamboforums.com