Siku za karibuni baada ya Bunge kuteua wenyeviti na wajumbe mbambali wa kamati za kudumu za Bunge kusimamia sekta tofauti, imekuwa mwiba kwa baadhi ya mawaziri na watendaji husika katika sekta zao. Mojawapo ya sekta inayooneka kuwekwa katika tishio ni sekta ya madini na nishati. Mojawapo ya mambo anayozungumzia ni pamoja na haya;
January Makamba anadai siasa ndiyo imepeleka nchi gizani. Anamsuta Waziri wa Nishati na Madini kuwa aache kuorodhesha miradi ya uzalishaji umeme kwa sababu kinachohitajika ni umeme si orodha ya miradi. Tumewahi kusikia kauli kama hizi siku za nyuma pale kundi fulani la wanasiasa walipokuwa wanashinikiza taifa lifunike kombe ili mwana haramu aweze kupita.
Kadhalika aliahidi kuishinikiza serikali kutafuta suluhisho la mgao wa umeme nchini.
January Makamba anaweka hoja mezani kuwa mitambo ya Dowans iwashwe kwa mkataba wa muda wakati kesi yake inaendelea mahakamani. Ikibidi fedha zinazopatikana ziwekwe katika mfuko maalumu kusubiri kesi iliyo mahakamani. Rais Kikwete amekuwa akisema wazi kuwa hapendi serikali yake kuingilia uhuru wa Mahakama
Tumeshuhudia kuja kwa anayedaiwa kuwa ni mmiliki wa DOWANS nchini ili kufanya mazungumzo na serikali ili kuona uwezekano wa mitambo hiyo kuwashwa. Haya yote yanamweka Ngeleja katika kona mbaya kwa mtazamo wangu. Hata ikatokea kukawa na mabadiliko katika baraza la mawaziri, basiNgeleja anaweza kuwa kakalia kuti kavu na nafasi yake kuchukuliwa na Makamba.
Katikati ya harakati hizi, yapo madai kuwa January Makamba anakuja na pendekezo alilopewa na mafisadi kuwa, Dowans wapunguze au kusamehe deni wanaloidai TANESCO lakini nao wapate mkataba wa kuzalisha umeme kwa muda usio na ukomo.
Nimesema kuwa hayo ni madai, lakini kama itabainika kuwa kweli, basi, lugha yake ya kizalendo itageuka kuwa ya kidalali na isiyo ya kizalendo. Wakati hakuna bei itoshayo kununua uzalendo, lakini tuna hakika kuna bei ya udalali, na ni wenyewe Dowans wanaojua wametenga kiasi gani cha fedha kunadi mitambo yao ndani ya Bunge na Serikali.