Monday, 31 January 2011 20:14 (Mwananchi) Boniface Meena na Sadick Mtulya
MBUNGE wa Nzega (CCM), Dk Hamisi Kigwangalla, amewasilisha hoja binafsi kwa katibu wa Bunge, akitaka Bunge lijadili na kuridhia kufungwa kwa mradi wa kuchimba dhahabu wa Golden Pride, ulioko mkoani Tabora.
Katika hoja hiyo, Dk Kigwangalla amesema mgodi huo unapaswa kufungwa mara moja kwa kuwa una madhara mengi, kuliko faida kwa nchi nchi na Jimbo la Nzega.
Dk Kigwangalla pia ameitaka serikali iwalipe fidia wachimbaji wadogo na wenyeji wananchi waliokuwa wakiishi katika maeneo yanayozunguka mgodi huo, ambao alisema wamenyanyasika na kusumbuliwa kwa ushirikiano wa serikali na wamiliki wa mgodi.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, mbunge huyo alisema mradi huo unaharibu mazingira na hasa ya vyanzo vya maji.
Alisema mradi huo pia unatumia maji mengi zaidi kuliko yanayotumiwa na wenyeji wa eneo hilo.
Alisema "wawekezaji wote kwenye migodi nchini, bila kuangalia makubaliano ya huko nyuma, lazima waigawie nchi hisa na haki ya kumiliki migodi hiyo kwa asilimia isiyopungua 20 vinginevyo, wafunge migodi hiyo na waondoke.".
Katika hoja yake hiyo, mbunge huyo pia amewataka wawekezaji wote wapewe muda usiozidi miezi sita, kukamilisha mchakato huo na kuchukua hatua za kutekeleza azimio la hoja yake.
Pia ametaka katika kila mgodi kuwe na utaratibu wa wazi wa kutangaza mapato na matumizi yanayotokana na shughuli za uchimbaji wa madini.
Hali kadhalika, imetaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kutengeneza utaratibu mzuri na wa uhakika wa kujua wawekezaji na mitaji iliyotumika katika kuwekeza na mapato yanayotokana na uchimbaji wa madini katika migodi.
"Kwa pamoja sasa serikali na mgodi watekeleze miradi ya kuendeleza jamii zinazozunguka migodi ili kuwafanya wananchi wauone mgodi iliyoko katika maeneo yao kuwa ni yenye manufaa kwao," alisema Dk Kigwangalla.
Dk Kigwangalla pia ametaka uwekezaji katika sekta ya madini usimame hadi hapo nchi itakapokuwa tayari kuchangia kuwekeza na kumiliki asilimia kubwa ya rasilimali za nchi na kufaidika nazo.
Dk Kigwangalla alisema amefanya utafiti kuhusu hoja hiyo na kwamba ana nyaraka nyingi na uthibitisho juu ya mambo anayotaka yafanyike.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), David Kafulila, jana aliwasilisha rasmi hoja binafsi ya kutaka serikali iwajibike, kwa kukukubali kuilipa mabilioni ya fedha, Kampuni ya Dowans na kuliingiza taifa hasara kupitia sekta ya umeme.

Hatua hiyo inakuja baada ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kushindwa kesi, katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) na kutakiwa kuilipa Dowans Sh 94 bilioni, kwa kosa la kuvunja mkataba.


Katika hoja hiyo, Kafulila anataka serikali , kutoa maelezo ya kina kuhusu sakata hilo , kwa sababu haitakuwa sahihi kulipa mabilioni ya fedha kwa kampuni aliyodai kuwa mmiliki wake hafahamiki. 


Kafulila pia , kulitaka Bunge liazimie kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kwa madai kuwa ameshindwa kusimamia utekelezaji wa Sera ya Nishati na Mpango Kabambe wa Usambazaji wa Umeme nchini.


Mbunge huyo aliwasilisha hoja yake jana katika ofisi ndogo ya Bunge akiwa ameongozana na Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa NCCR Mageuzi, Dk Seng'ondo Mvungi.
Alisema kulingana na jinsi alivyoiandaa, anaamini itafanikiwa na kujadiliwa katika kikao cha Bunge, kitakachofanyika mwezi huu.
Dk Mvungi ambaye ni mwamazuoni aliyebobea katika masuala ya katiba, alisema pamoja na kwamba Dowans imekwisha wasilisha tuzo ya hukumu Mahakama Kuu lakini akasisitiza hakuna kizuizi kwa Bunge kujadili hoja hiyo.
"Kujadili hukumu ya Dowans mahakamani si kigezo na kizuizi cha mhimili wa Bunge kutojadili suala hili.
"Hii ni hukumu na si kesi, kisheria hakuna pingamizi lolote kwa Bunge kushindwa kujadili suala la Dowans,'' alisema Dk Mvungi.
Katika hoja yake hiyo, Kafulila alisema kuwa mgogoro wa nishati ya umeme unaelekea kukomaa na kuwa sehemu ya maisha ya Watanzania.