Kifo cha Usama Bin Laden, karata ya Marekani (uchambuzi wa kisiasa)

mdau wetu

JF-Expert Member
Apr 20, 2011
548
58
Baada ya kupita miezi 116 tangu kujiri tukio la Septemba 11, hatimaye Wamarekani wametangaza kumuua Usama Bin Laden kiongozi wa mtandao wa al Qaeda.

Akitangaza habari hiyo huko White House, Rais Barack Obama sambamba na kuashiria tukio la Septemba 11 mwaka 2001, amesema kuwa uadilifu umetendeka.

Kisa cha kudhihiri na kuporomoka Usama Bin Laden kinachukuliwa kubeba mafunzo mengi ya kuzingatiwa kihistoria.

Tajiri huyo mwenye asili ya Saudi Arabia alielekea nchini Pakistan katika mlongo wa 1980 ili kuwasaidia mujahidina wa Kiafghani katika vita na Jeshi Jekundu la Shirikisho la Umoja wa Sovieti.

Bin Laden kwa haraka alianza kushirikiana na Shirika la Kijasusi la Marekani, CIA na kwa msaada wa shirika hilo alianzisha kambi za mafunzo kwa ajili ya mujahidina wa Kiafghani.

Hadi mwishoni mwa mungo wa 1980 kulikuwa na mfungamano mkubwa kati ya pande hizo mbili, lakini kufuatia vita vya Iraq na Kuwait mwaka 1990 na kupelekwa askari wa Marekani katika ardhi ya Saudi Arabia, kidhahiri Bin Laden aligeuka kuwa adui wa Wamarekani na Wasaudia.

Katika muongo wa 1990, serikali ya Marekani ilitangaza kuwa makundi yaliyo chini ya Bin Laden yalitekeleza matukio kadhaa ya kigaidi ikiwemo milipuko iliyotokea katika balozi za nchi hiyo nchini Kenya na Tanzania.

Vilevile ilisema kwamba, meli ya Marekani ililipuliwa na kundi hilo katika Ghuba ya Aden mwaka 2000.

Lakini si lolote kati ya matukio hayo lililotumiwa na Marekani kama kisingizio cha kukabiliana moja kwa moja na kundi la al Qaida, kama lilivyokuwa tukio la kushambuliwa kwa ndege majengo mawili pacha ya kibiashara mjini New York na Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) huko Washington tarehe 11 Septemba mwaka 2001.

Hivi sasa karibu muongo mmoja umepita, lakini bado kuna maswali mengi ambayo bado hayajapatiwa majibu kuhusu jinsi tukio hilo lilivyopangwa na kutekelezwa, na uwezekano wa kushiriki duru za ndani za utawala wa Marekani katika tukio hilo.

Hata hivyo, hakuna shaka kuwa, milipuko ya Septemba 11 na kukiri Bin Laden kuwa alishiriki katika mashambulizi hayo, kuliipa Marekani kisingizio tosha cha kuishambulia Afghanistan na kuikalia kwa mabavu, na kisha kuanzisha vita nchini Iraq.

Kama Bin Laden analaumiwa kwa kusababisha vifo vya karibu watu elfu 3 katika tukio la Septemba 11, Wamarekani katika kulipiza kisasi cha tukio hilo, wamewaua moja kwa moja au katika matukio yasiyo ya moja kwa moja zaidi ya watu milioni 1 nchini Afghanistan, Iraq na hivi karibuni nchini Pakistan.

Nchini Pakistan pekee, kwa kila muhanga mmoja wa tukio la Septemba 11, Wapakistan 17 wameuawa katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Marekani dhidi ya nchi hiyo.

Kwa vyovyote vile, kuchelewa kuuawa Usama bin Laden ni jambo jingine lenye utata kuhusiana na kadhia hiyo.

Licha ya Wamarekani kudai kuwa wana zana za kisasa kabisa za ujasusi na upelelezi, lakini imewachukua karibu miaka 10 kuweza kumuua mtu ambaye kama anavyoitwa ni 'adui hatari zaidi wa Marekani'.

Ushahidi wa kuaminika unaonyesha kwamba, katika muda wote huo, makomandoo wa Marekani mara kadhaa walikaribia kumtia mbaroni kiongozi huyo wa mtandao wa al Qaida, ama katika dakika za mwisho White House na Pentagon zilitoa amri ya kusimamishwa operesheni hizo.

Ni wazi kuwa Usama Bin Laden aliingia katika uwanja wa kisiasa kwa maslahi ya Marekani na hata katika kukabiliana kwake na Wamarekani mwishowe alipelekea kudhaminiwa maslahi haramu ya nchi hiyo duniani.

Hivi sasa pia inaonekana kuwa hata habari za kuuawa kiongozi huyo wa al Qaida ni kwa faida ya Marekani au kwa uchache zitamsaidia Obama katika kampeni zake za uchaguzi ujao nchini humo.


Kwa hisani ya Redio Tehran, Iran
 
Back
Top Bottom