CCM YA MWALIMU NYERERE HAIWEZI KUTOKEA
TENA TUSIJIDANGANYE
Nashuhudia nia za urais ndani ya chama cha
mapinduzi zikitangazwa kwa mbwembwe za aina
yake.Lowassa, Wasira, Mwigulu n.k na wengine wengi
ambao bado wanatarajia kutangaza nia. Naziita
mbwembwe kwa sababu kuu moja, nia hizi hazina
uhalisia. Sio nabii, na pia kuliona na kufahamu hili
haliitaji unabii historia inajieleza. Mwaka 2005
tuliwashudia watu kama Prof. Mwandosya, Salim
ahmed Salim, J.Kikwete n.k wakichuana ndani ya
CCM, ili kupata nafasi ya kuwania urais. Mbio za
watu hawa mwaka 2005, zilionesha sura ya uhalisia
wa jambo piganiwa, ingawaje matokeo yaliigeuza
sura ile. Lakini leo miaka kumi baadaye (2015),
watanzania tunaaminishwa tena kuwa urais ni lele
mama. Yamesemwa mengi, na watangaza nia, kila
mmoja akija na kauli yake lakini je, dhamira ya
kweli ipo? Kwa ufupi niseme tu kuwa, inawezekana
kuwa na watangaza nia wengi sana ndani ya ccm huu
mwaka lakini swali ni je wametoka wapi?kwa nini
wamejitokeza sasa?miaka ya nyuma hawakuwepo?
Je yale makundi ndani ya ccm yamepotea? Wakwapi
Tanzania kwanza? Vikwapi vile vyama vya misimu?
Wakwapi wale wapinga ufisadi?
Si jambo dogo hata kidogo, na tusipokuwa makini
Tanzania itayeyuka mithili ya theluji. Kwa ufupi
naona makundi mawili ndani ya ccm, na makundi
hayo yametoa watu wawili ambao watashindana
ndani ya ccm katika nani awanie urais. Wengi
wametangaza nia kama kivuli cha ushawishi kwa
wananchi, ila nyuma ya pazia ukweli ni kuwa wote
wapo nyuma ya watu hao wawili, ambao ni zao la
makundi mawili yaliyojengeka ndani ya ccm,
makundi yaliyoanza kujengeka mara tu baada ya
uchaguzi mkuu 2005, makundi ambayo yameifikisha
Tanzania na watanzania hapa walipo sasa. Makundi
yenye nguvu ndani ya ccm, na makundi ambayo
yapo tayari kufanya lolote kuhakikisha yanaendelea
kujilinda ndani ya ccm na nje ya ccm. Pengine
yalikuwepo awali lakini sasa ndio yanaonyesha
makucha yake hadharani. Zao la ufisadi, chuki,
umasikini, na unganganizi wa madaraka.
Vyote ni zao la utengano ndani ya ccm. Kwa
mwanachama anayetafuta kula, HILI
HALITAMWINGIA AKILINI. Halikadhalika kwa
mwanasiasa anayetafuta na kushikilia madaraka
kwa ajili ya kula, hili halitamwingia akilini. Lakini
kwa raia ambaye alishaenda zahanati ya kata
kupatiwa matibabu huku ikiwa ndio tegemeo lake la
mwisho, kwa mtumiaji wa daladala dar es salaam,
kwa mwanafunzi aliyeko chuoni, pengine kakosa
mkopo kabisa ama pengine kapata lakini amekaa
miezi mitatu hajapatiwa fedha ya kujikimu, na kwa
mwalimu aliyepangia kule kijijini, hana pa kushukia,
mshahara mdogo, hali ngumu, na watanzania
wengine wengii, waliovaa sura zinazofanana na hizi
HILI LITAWAAINGIA AKILINI.
CCM iliyokuwa chini ya waziri mkuu, hayati Edward
Moringe Sokoine, na CCM iliyokuwa chini ya rais
hayati mwalimu J.K.Nyerere, sio CCM tuliyonayo
sasa, na siyo CCM itakayokumbukwa Tanzania.Nilise
ma 2012 KIFO CHA CCM KIMETIMIA, nikiwa nalenga
mwaka 2015. Lakini yote yatatokana na uamuzi wa
wananchi juu ya hili. Kwanza ndani ya ccm je ni
Lowassa? Au ni Membe? Nani awanie urais kwa
chama hicho? Wanaccm wakijitambua, watautambua
uamuzi wa kufanya. Na je, ni TLP,UDP,CHADEMA
,CUF,NCCR,ACT au ni UKAWA? Wale wapinzani
wakijitambua watapata pia uamuzi wa kufanya lakini
yote wananchi ndio wenye maamuzi ya mwisho.
Tusijidanganye ccm ya mwalimu itarudi tena,
tutizame watu kwa jicho la tatu, tuwakatae
mapema na kuwapinga kama mwalimu alivyofanya,
ama tukae kimya tuwaache waendelee kututafuna
na kubaki masikini. Nimalize kwa kusema urais si
lele mama, narudia urais si lele mama, nenda
kajiandikishe kwa gharama yeyote ile.
Mungu ibariki Tanzania Mungu ibariki Afrika.