CCM ya Kikwete imewafikisha watu waamini kwamba amani na usalama ni kukaa kimya kama kondoo wenye hofu. CCM inatumia hofu hii iliyopandikizwa kuendeleza dhuluma, kukalia haki za watu na kutumia polisi kuaminisha kwamba Tanzania leo kuna magaidi. CCM walianza kupandikiza hofu ya "magaidi' katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga mwaka juzi, wakati aliyekuwa Katibu mkuu wa CCM, Wilson Mukama alipotangaza kapata habari kwamba CHADEMA wameingiza Mungiki wa Kenya. Polisi hawakuwa na habari na hawakumhoji Mukama.
Mwaka jana, Katibu wa Uchumi wa CCM, Mwigulu Nchemba alizunguka nchi nzima akidai ana mkanda unaoonyesha ugaidi wa CHADEMA. Polisi walijiweka kando na madai hayo. Na pale walipoona wimbi la watu kuhama analojia na kuingia digitali (CHADEMA) linazidi kuongezeka ndipo ‘CCM' wakamkamata Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare kwa madai ni gaidi.
Mwaka jana Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alizunguka nchi nzima akitangaza kwamba Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa ana kadi ya CCM.
Siku Juliana Shonza alipotimuliwa uanachama wa CHADEMA, alikusanya waandishi wa habari na kutapika mambo mengi, mojawapo ni kwamba kuna matumizi mabaya ya fedha za chama. Baada ya kusomea propaganda ndani ya CCM na wakahitimu, wiki iliyopita Shonza na Mtela Mwampamba waliibuka na kudai Dk. Slaa ana mpango wa kumuua Naibu wake, Zitto Kabwe. Makada wawili hao wakaeleza hata mpango huo ulivyo.
Pamoja na kwamba tuhuma hizo nzito zinahitaji Jeshi la Polisi kufanyia kazi, Shonza na Mwampamba wameachwa huru hata kukemewa tu. Hapo ndipo ujue Shonza na Mwampamba, kama ilivyokuwa kwa Nape, Mwigulu na Mukama wametumwa na CCM kutia hofu kama rais mwenyewe aliyedai amesomewa itikafu na misikiti mitatu, lakini amekaa kimya. Kweli rais wa nchi anaombewa afe lakini hachukui hatua? Hii ndiyo CCM!
Nini maana yake CCM? Mtambo huu wa analojia CCM unapaswa kuzimwa 2015 ili kupitia digitali wananchi wapate usikivu mzuri wa habari na waone picha nzuri ya uhuru wao, demokrasia, uchumi, elimu, afya, ustawi wa jamii, mazao yao, barabara zao, uhusiano wao, heshima yao, utu wao na viongozi wasioshinda misibani.