Kesi ya Uchochezi ya Zitto Kabwe: Shahidi akiri kumuona Zitto jasiri. Asema analichukia Jeshi la Polisi

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,808
11,973
Kesi ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe inayohusu mashtaka matatu ya uchochezi katika kesi ya jinai namba 327/2018 imeendelea leo Mei 16, 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

Katika kesi ya msingi, Zitto anadaiwa kutenda makosa hayo, Oktoba 28, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za Makao Makuu ya chama cha ACT Wazalendo.

IMG_20190516_122011_2.jpg


Upande wa Jamhuri umewakilishwa na Wakili Tumaini Kweka akishirikiana na Wakili Nassoro Katuga, Upande wa Utetezi umewakilishwa na Wakili Peter Kibatala, Wakili Jebra Kambole, Wakili Jeremiah Mtobesya

Wakili Kweka anasema shauri limekuja kwa ajili ya kusikilizwa na wamejiandaa kwani wamekuja na Mahahidi.

Shahidi wa kwanza anaitwa mbele ya Makama kujieleza.

Karani wa Mahakama: Shahidi unaitwa nani? Una miaka mingapi na ni muumini wa dini gani?

Shahidi: Naitwa Mashaka Juma, nina miaka 29 na ni Muislamu.

Wakili wa Jamhuri, Tumaini Kweka anaanza kumuongoza shahidi huyo

Wakili Kweka: Unaishi wapi?

Shahidi: Kimara Korogwe

Wakili Kweka: Shughuli zako ni nini?

Shahidi: Msanii wa filamu na tamthilia

Wakili Kweka: Unaposema Msanii, una maana gani?

Shahidi: Ni muigizaji kwa hiyo naishi kwa kufanya Sanaa ya maigizo. Nimeigiza katika tamthilia na ‘Utata ya chaneli 5, filamu ya ‘Wazee wa Pamba’ na filamu ya ‘Yakiose’

Wakili Kweka: Umeanza lini usanii?

Shahidi: Nina kama miaka 10 kwa sasa

Wakili Kweka: Umesema unaishi Kimara Korogwe, upo tangu lini?

Shahidi: Sina muda mrefu, ni kama miaka miwili tu

Wakili Kweka: Mnamo tarehe 29/10/2018 unakumbuka ulikuwa wapi?

Shahidi: Nilikuwa Dar es Salaam siku hiyo

Wakili Kweka: Katika siku hiyo unakumbuka nini?

Shahidi:
Nilikuwa Kimara Korogwe na nilikuwa na wenzangu wengi tukicheza draft. Alikuja mchezaji mwingine tunayecheza naye kila siku anaitwa Frank Zongo, alipofika akatuuliza "Mna habari yoyote?" Tukamjibu “Hatuna habari”.

Akauliza “Habari ya hivi leo hamuijui?” Tukajibu, “Hapana labda jamaa hapa kanifunga mbili na mimi nimemfunga 3”. Akasema Mheshimiwa Zitto ndio habari ya Jiji

Wakili Kweka: Habari ya Jiji kwa maana gani?

Shahidi: Alituambia Subirini. Kisha akatoa simu yake ya ‘Smartphone’ na kufungua YouTube na kutuonesha habari ya Mhe. Zitto Kabwe. Tukamuona Mheshimiwa Zitto Kabwe akilialumu Jeshi la Polisi kwa mambo kadha wa kadha. Kuwa Jeshi la Polisi limekuwa likinyanyasa Wananchi, kuteka Watu akiwemo Mheshimiwa Mo. Kuwa Polisi imekuwa ikienda hospitalini kuchukua watu na kwenda kuwaua. Kwa kweli baada ya hapo nilijiuliza mambo mengi sana!

Wakili Kweka: Alikuwa anasema wanachukuliwa hospitalini katika mazingira gani?

Shahidi: Ya kutekwa

Wakili Kweka: Matukio hayo yanatokea wapi alisema?

Shahidi: Kigoma, Uvinza

Wakili Kweka: Chochote kingine?

Shahidi: Alisema Mkuu wa Polisi, Simon Sirro kashindwa kudhibiti Askari wake

Wakili Kweka: Zitto Kabwe ni nani hasa?

Shahidi: Kiongozi wa chama cha siasa, ACT Wazalendo

Wakili Kweka: Wewe binafsi unamfahamu?

Shahidi: Ndio

Wakili Kweka: Kwa vipi na tangu lini?

Shahidi: Namfahamu tangu akiwa CHADEMA na mimi ni mfuasi wake tangu muda huo hadi sasa

Wakili Kweka: Tupo wengi Mahakamani, huyo Zitto Kabwe yupo?

Shahidi: Ndio. Yule pale (akimyooshea kidole)

Wakili Kweka: Ulipoona hiyo habari ambayo mliambiwa ni ya Jiji, uliichukuliaje?

Shahidi: Nilichukulia kwa namna tofauti, niliona Jeshi la Polisi halina thamani tena, kama limeshindwa kulinda raia na mali zake hakuna haja ya Jeshi la Polisi kuwepo

Wakili Kweka: Umesema mlikuwa wengi mkicheza draft, sasa wewe na wenzako kwa ujumla wenu mlifikiriaje?

Shahidi: Asilimia kubwa ya waliokuwepo walilichukia Jeshi la Polisi

Wakili Kweka: Kwanini wasema hilo?

Shahidi: Sasa kama wameua Kigoma, wataacha kuua Dar!?

Wakili Kweka: Sasa nini ulikuwa muitikio wenu?

Shahidi: Wengi tulimpongeza Zitto kwa ujasiri na ukakamavu wake na ndio iliyopelekea sisi kulichukia Jeshi la Polisi

****
Hakimu Huruma Shaidi: Yaani mpaka hapo ulipo unalichukia?

Shahidi: Bado siliamini mpaka Zitto aje aniambie limekaa vizuri
****

Wakili Kweka: Hali ilikuwaje?

Shahidi: Tulipaniki sana! Lakini huwa kuna jamaa anakuja pale tunacheza naye draft na hatujui anakaa wapi. Sasa alinivuta pembeni akaniuliza “Kwanini unapaniki?” Nikajibu kama Sirro kashindwa kuzuia mauaji unadhani mimi nitakuwa salama? ......Basi, aliongea mengi pale na akaniomba namba zangu za simu

Wakili Kweka: Baada ya kumpa namba za simu ilikuwaje?

Shahidi: Nakumbuka ilikuwa tarehe 30/10/2018 nilipigiwa simu na yule bwana aliyechukua namba ya simu na kunitaka nifike Oysterbay (Polisi)

Wakili Kweka: Baada ya kukuambia hivyo?

Shahidi: Nilitii wito huo na tarehe 31 nilifika Oysterbay Polisi na kufanya mahojiano. Niliongea kile nilichoongea na kulilaumu sana Jeshi la Polisi kwa walichokifanya.... mauaji, utekaji wa Watu na kushindwa kusimamia haki za raia na mali zao

Wakili Kweka: Ulieleza kuwa uliona kwenye simu, labda nini kilikufanya useme huyu ni Zitto Kabwe?

Shahidi: Kwasababu namfahamu na nilipomuona nilijua huyu ni Zitto Kabwe. Siku ile alikuwa anaongea na Waandishi wa Habari maana mbele yake kulikuwa na vipaza sauti vingi. Alitania watu kidogo na kufunguka alichofunguka

Wakili Kweka: Hiyo video ukiiona utaitambua?

Shahidi: Ndio

Wakili Kweka: Nini kitakufanya uitambue?

Shahidi: Alichosema kitabaki kile kile tu. Na alikuwa amevaa kaunda suti

****
Wakili Kweka anasema mbele ya Mahakama kuwa amemaliza kumuongoza shahidi wake. Hakimu Huruma Shaidi sasa anauambia upande wa Utetezi uanze kumuuliza maswali Shahidi huyo
****

Wakili Kibatala: Umesema wewe ni msanii, msingi wa kipato chako ni kuigiza?

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Nitakuwa sahihi nikisema kwamba kuna muda katika uigizaji wako unatakiwa uigize kuwa umefiwa na unalia kabisa kabisa?

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Na kuna saa unaweza kuigiza una hasira kabisa kabisa?

Shahidi: Wakati wa kazi?

Wakili Kibatala: Ndio

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Nikisema wewe ni mzoefu wa maigizo ya sanaa maana umefanya kwa kiama 10 ni sahihi?

Shahidi: Ndio, hujakosea

Wakili Kibatala: Umesema wewe ni mkazi wa Kimara Korogwe, unakumbuka kuongozwa kusema hii sehemu ipo wapi?

Shahidi: Korogwe

Wakili Kibatala: Okay

Shahidi: Korogwe, Dar

Wakili Kibatala: Ukimuacha Frank Zongo, hao wengine unakumbuka kuwataja majina?

Shahidi: Hapana, sijawataja

Wakili Kibatala: Unakumbuka umesema mlikuwa mnacheza draft eneo gani? Kwamba bar au kijiweni au wapi?

Shahidi: Sijasema

Wakili Kibatala: Ni sahihi kuwa ulipokuwa unaangalia simu, anayeweza kuisemea hiyo simu na umiliki wake ni Frank Zongo?

Shahidi: Ndio

Wakili Kibtala: Unamiliki simu ya aina gani?

Shahidi: Smartphone

Wakili Kibatala: Una YouTube kwenye simu yako?

Shahidi: Sina YouTube kwenye simu na sina uzoefu sana maana hata vitu vingine huwa watu ndio wana-download kwa niaba yangu

Wakili Kibatala: Kwa hiyo Frank Zongo ndiye aliyeingia kwenye simu yake na kuwaonesha video?

Shahidi: Ndio, yeye alifanya yote na kutuonesha video

Wakili Kibatala: Ni sahihi kwamba kwenye YouTube nyingine hukuingia kuangalia kilichooneshwa na Frank Zongo kwenye simu yake kama vinalingana?

Shahidi: Ndio, sikulinganisha kwa kuangalia kwingine

Wakili Kibatala: Unakumbuka kuongozwa kusema chochote kuwa huyo aliyechukua namba ya siku aliangalia video iliyooneshwa na Frank Zongo?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Ulisema chochote kuhusu mtu huyo kuchukua simu ya Frank Zongo na kwenda nayo Oysterbay?

Shahidi: Hapana, hilo sijui

Wakili Kibatala: Ulisema chochote kuhusu mtu huyo kuchukua namba ya Frank Zongo?

Shahidi: Hapana, hakuchukua namba za Frank Zongo

Wakili Kibatala: Ulisema chochote kuhusu mtu huyo kuongea na wale watu wengine kwenye kundi?

Shahidi: Hapana, mimi nimeongelea mimi sijasemea mtu

Wakili Kibatala: Unakumbuka kusema chochote kuwa unaishi mtaa gani huko Kimara Korogwe? Ili tujue usije kuwa umeletwa?

Shahidi: Kilungure

Wakili Kibatala: Aaanhaah! Uliongozwa kusema hivyo au la?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Je, uliongozwa kusema chochote kuhusu, mwenye nyumba yako labda au Mwenyekiti wa Mtaa labda?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Ulitoa kitambulisho chochote kile ili tukuamini kuwa wewe ni Mashaka Juma, yaani kitambulisho chochote kile?

Shahidi: Kitambulisho nilichokuwa nacho ni cha mpiga kura na pale Polisi waliniomba na nikasema kimepotea

Wakili Kibatala: Okay, hivyo uliongozwa kutoa kitambulisho?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Na hayo unayosema kuhusu kitambulisho kupotea uliongozwa kuyasema hapa?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Hicho kitambulisho unakumbuka ulikipata lini? Taja japo Mwaka tu!

Shahidi: Hapana, sikumbuki

Wakili Kibatala: Unajua kuhusu ‘Police Loss report’?

Shahidi: Kiswahili chake?

Wakili Kibatala: Taarifa unayoenda kutoa Polisi baada ya kupotelewa na kitambulisho cha ili hata kikitumiwa vibaya na watu ijulikane si wewe, na wao wana kupa nyaraka kuonesha umeenda kueleza hayo

Shahidi: Ndio ninayo ila sikumbuki nilipata lini

Kibatala: Umeitoa hapa Mahakamani hiyo ‘Loss Report’?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Uliipata hiyo ‘loss report’ kabla au baada ya tukio la Zitto?

Shahidi: Zamani sana, sikumbuki

Wakili Kibatala: Wakati unakuja hapa ulikutana na Polisi waliovaa sare na kukusindikiza kuja hapa?

Shahidi: Tulifika na kupokelewa kutaelekezwa kesi ilipo huku juu, tukaja

Wakili Kibatala: Swali langu - Ulipofika, Polisi wenye sare uliwaona au la?

Shahidi: Sikuwaona

Wakili Kibatala: Wasio na sare?

Shahidi: Siwajui hao

Wakili Kibatala: Ni sahihi kuwa ulienda kutoa ushahidi baada ya kuona video huko Oysterbay Polisi?

Shahidi: Ndio sahihi kabisa, maana huwezi kutoa ushahidi bila kuona kitu. Unaona, ndio unatoa ushahidi. Umenielewa?

Wakili Kibatala: Ndio nimekuelewa na nimekuelewa kuwa wewe ni shahidi mzoefu

Wakili Kibatala: Ulipoenda kutoa ushahidi ulienda na nani?

Shahidi: Nilienda mwenyewe

Wakili Kibatala: Hukuenda na mtu labda Mwanasheria?

Shahidi: Kama nilivyosema awali mimi sina Mwanasheria wala hizo taratibu sizijui wala, nilienda mwenyewe

Wakili Kibatala: Okay! Ulikuwa na amani wakati unatoa ushahidi hadi mwisho?

Shahidi: Nimesema nachukia Jeshi la Polisi, nitakuwaje na amani? Sikuwa na amani

Wakili Kibatala: Okay! Baada ya kutoka Polisi au ukiwa hapo kuna yeyote ulimpigia simu kumwambia chochote?

Shahidi: Mimi ni Mwanaume ninayejiamini sana, sikumpigia yeyote yule

Wakili Kibatala: Kwenye hiyo video Zitto alitaja jina lolote la Askari au nini?

Shahidi: Hakutaja jina la Polisi alisema Jeshi la Polisi. Hakusema sijui Afande Chacha, sijui Mwita

Wakili Kibatala: Wakati unaongozwa hapa, Wakili Kweka alikuongoza kusema kuthibitisha hizi taarifa za watu kuuawa?

Shahidi: Hayo yote nilieleza Polisi.........

Wakili Kibatala: Shahidi mambo ya Polisi acha. Hapa Mahamani uliongozwa kusema umethibitisha hizo habari?

Shahidi: Hapana, hapa sikuongozwa

Wakili Kibatala: Ni sahihi kwamba mpaka unakuja hapa Mahakamni hujathibitisha kuwa watu wametekwa au la?

Shahidi: Hili swala la Jeshi la Polisi, mimi siwezi kwenda Uvinza huko kuthibitisha wala

Wakili Kibatala: Wakati unatoa ushahidi umesema kuhusu kunyanyaswa kuhusu mtu anaitwa Mo…..

Shahidi: Sio kunyanyaswa kutekwa! Mo Dewji. Uwe makini wakili

Wakili Kibatala: Sawa nitakuwa makini! Na hukusema Mo Dewji

Shahidi: Nilisema Mheshimiwa Mo, sikusema Mo Dewji ndio. Ila kila mtu anamjua aliyetekwa ni Mo Dewji, Mmiliki wa Simba, hakuna mwingine na kila mtu anamjua hapa

Wakili Kibatala: Ulitaja jina la Mo kwa kirefu?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Unasema ulisikia Zitto anasema Sirro kashindwa kuthibiti Askari wake, ulipata nafasi ya kuongea na IGP?

Shahidi: Hapana, nimpate wapi? Nikimuona ni kwenye TV

Wakili Kibatala: Ulipata nafasi ya kuongea na Waziri wa Mambo ya Ndani au Rais wa nchi?

Shahidi: Sijapata nafasi ya kuongea nao maana niwapate wapi? Labda kama nitapata nafasi hiyo sasa hivi nitakwenda

Wakili Kibatala: Unakumbuka umesema Zitto ni Kiongozi wa ACT Wazalendo...una uhakika?

Shahidi: Mpaka anajitangaza kugombea na chama fulani na kukisajili amepitia kwenye nafasi nyingi kwenye chama

Wakili Kibatala: Kwa msajili wa vyama ulikwenda?

Shahidi: Hapana! Huko kote mimi sijaenda wala sina haja ya kwenda nikafanye nini? Kumshtaki yule(akimaanisha Zitto)

Wakili Kibatala: Ni sahihi kuwa hukuongozwa kusema 'yule pale aliyekaa kizimbani' wakati unamtambulisha Zitto Kabwe? Wala hukuenda kumshika bega kusema 'huyu'

Shahidi: Nilisema yule pale amekaa, sikusema kizimbani, ila nikipata hiyo nafasi sasa hivi naenda tu mara moja. Zitto yule pale kila mtu anamjua

Wakili Kibatala: Ukipatwa na dharura ya Kipolisi utaenda wapi?

Shahidi: Umesema ya Kipolisi, nitaenda Polisi

Wakili Kibatala: (Anasoma maneno ya kwenye hati ya mashtaka ambayo Zitto ndio anashtakiwa nayo) Anamuuliza shahidi, “Unakumbuka kuongozwa kuyasema haya maneno au kuomba kujikumbusha?”

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Unakumbuka kuyasema haya maneno kama nilivyoyasoma?

Shahidi: Hapana….Itakuwa ngumu

Hakimu Shaidi: Itakuwaje ngumu?

Shahidi: Kuyakumbuka hayo maneno. Kwanza nina matatizo ya macho (watu walio mahakamani wanacheka)

*********
Hakimu Shaidi: Hajakuambia usome, wala hatakuambia usome (watu walio mahakamani wanacheka tena)
*********

Wakili Kibatala: Ni sahihi kuwa si wewe wala Wakili Kweka aliyeomba kujikumbusha uyasome kwenye hati ya mashtaka?

Shahidi: Ndio

Wakili Kibalata: Nakurudisha nyuma, ulisema mtu aliyechukua namba ya simu alikuwa anacheza draft na nyie mara kwa mara na sio kwamba siku hiyo alishuka tu kwenye gari lake?

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Na ni sahihi hukutaja majina yake?

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Ni sahihi kwamba hata namba zako za simu hapa hukuzitaja?

Shahidi: Nilitaja

Wakili Kibatala: Kwa hiyo tukiondoka hapa ni sahihi kwamba ulimwambia Hakimu namba zako ni 07.....

Shahidi: Hapana! Sijazitaja

Wakili Kibatala: Ni sahihi kuwa ulisema ulimkubali Zitto kwa ujasiri wake?

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Na wewe ni mfuasi wake? Umem-follow Facebook, Instagram?

Shahidi: Usinibane sasa. Acha niseme.....maana unanibana sana! Kuna urafiki wa aina tatu, huo wa kufollow FB na Wapi. Wa kuchati naye….ila mimi Bwana yule ananikosha anapoongea napata raha

Wakili Kibatala: Ni sahihi kuwa hukuongozwa kuoneshwa hiyo video hapa?

Shahidi: Sikuongozwa ila kama ipo nikioneshwa nitaitambua kabisa....maana niliiona sijui kama Mheshimiwa Hakimu ameiona

******
Hakimu Shaidi: Sijaona
******

Wakili Kibatala: Usema (Zitto) alivaa kaunda suti, uliongozwa kusema rangi yake?

Shahidi: Hapana

===================

Wakili Kibatala anamaliza kumuhoji Shahidi na sasa Hakimu amemruhusu wakili wa upande wa Jamhuri kufanya Re-examination

===================

Wakili Kweka: Umeulizwa na Wakili Kibatala kuhusu video uliyoiona. Ieleze Mahakama ni aina gani ya simu na ya nani?

Shahidi: Ilikuwa ya Frank Zongo na ni ‘Smartphone’ ila ukisema ni aina gani gani sijui

Wakili Kweka: Uliulizwa kuhusu vitambulisho vyako na majina yako hapa, unaelezeaje?

Shahidi: Mimi ni Mtanzania, na kuja hapa Mahakamani ni utanzania tayari...naongea kiswahili kizuri kabisa na jina langu Mashaka Juma lipo hosptali ya Kilosa

Wakili Kweka: Wakili Kibatala kuuliza kuhusu kuonesha alipokaa Zitto Kabwe hebu rejea swali hilo

Shahidi: Sasa hivi naongezea kabisa, yule pale aliyekaa kizimbani

===================
Wakili Tumaini Kweka anamuambia Hakimu kuwa amemaliza kufanya Re-examination
===================

Hakimu Shaidi: Shahidi una lingine la kuniambia mimi kama mimi?

Shahidi: Mheshimwa nachukia sana Jeshi la Polisi kwa yaliyotekea ila naamini Mahakama yako itanitoa hofu juu la hilo na kuniweka sawa

Hakimu Shaidi: Sawa, Shahidi

===================

Baada ya kumalizana na shahidi huyu upande wa Jamhuri unaieleza Mahakama kuwa bado una shahidi mmoja mwingine! Hakimu anaruhusu shahidi huyo wa pili aje kizimbani

Karani: Majina yako ni nani? Umri wako na dini yako?

Shahidi: Naitwa Shabani Hamisi. Miaka 40, dini ni Muislamu

Wakili Kweka: Shabani Hamisi unaishi wapi?

Shahidi: Manzese Tip Top

Wakili Kweka: Shughuli zako ni nini?

Shahidi: Nauza mitumba, Manzese Bakhresa

Wakili Kweka: Hapo Manzese Bakhresa upo hapo kwa miaka mingapi?

Shahidi: Kwa miaka miwili

Wakili Kweka: Ukiapishwa hapa Mahakamani kuwa unaitwa Shabani Juma, itakuwa sahihi?

Shahidi: Hapana

Wakili Kweka: Uthibitisho kuwa wewe ni Shabani Hamisi ni nini?

Shahidi: Nina kitambulisho cha uraia

Wakili Kweka: Kioneshe kwa Mahakama (Shahidi anatoa na kuonesha)

Wakili Kweka: Hebu eleza mnamo 29/10/2018 ulikuwa wapi?

Shahidi: Nilikuwa Manzese maeneo ya nyumbani kwangu

Wakili Kweka: Enhe!

Shahidi: Mida ya saa moja, saa moja na nusu ya asubuhi nilikuwa naelekea kazini kwangu. Nilipofika ofisini nikakuta watu wamekaa vikundi wanaongea na mimi nikasongea kuona nini kinaendelea. Nikakuta watu wanaongelea masuala ya Polisi kuwa wameua watu

Wakili Kweka: Eenhe! Ulivyokuta hivyo...?

Shahidi: Nilimuuliza rafiki yangu anaitwa Abilali, akanambia kuwa Bwana Zitto Kabwe amesema kuwa Polisi Uvinza wanaua watu na mbaya zaidi waliwafuata wengine waliokuwa wamejeruhiwa hospitalini na kuwateka na kuwaua

Wakili Kweka: Ulibahatika kumuuliza Bwana Abilali amepata wapi hizo taarifa?

Shahidi: Alinambia zipo kwenye vyombo ya habari mbalimbali. Nikamuuliza wewe umethibitisha vipi? Akanitolea simu na kuniwekea YouTube na kuiona hiyo taarifa kwenye AyoTV. Kweli nilimuona Mheshimiwa akiwa anaongea kuelezea mambo kadhaa ya kisiasa, uchumi, usalama wa raia na mali zao, habari za Tundu Lissu, korosho na mengineyo

Wakili Kweka: Mengineyo yepi?

Shahidi: Mengi tu

Wakili Kweka: Kile alichokueleza Abilal na ulichokiona kwenye AyoTV unaelezeaje?

Shahidi: Kama nilivyosema niliona mengi ila kilichonishtua ni hilo la kwenda kukamata waliokuwa wakipata tiba hosptalini

Wakili Kweka: Umetaja Abilali, wengine ni akina nani, wawili/watatu?

Shahidi: Alikuwepo Paulo, John, Yusuph na wengine

Wakili Kweka: Wewe Zitto Kabwe unamfahamu?

Shahidi: Namuona tu kwenye Vyombo ya Habari; huwa namuona tu, sijawahi kukutana naye hata nikija hapa Mahakamani namuona tu

Wakili Kweka: Yupo hapa?

Shahidi: Yupo pale kwenye kizimba

Wakili Kweka: Umesema unamuona ukija hapa Mahakamani? Kwa namna gani?

Shahidi: Nimuona hapa siku kesi ilipokuwa inasikilizwa hapa, nilimuona hapo chini(group ya mahakama)

Wakili Kweka: Okay! Hili suala ya Polisi kwa Zitto alilolisema ulilichukuliaje?

Shahidi: Nililichukulia kwa kawaida maana yapo mengi na yanaongelewa sana

Wakili Kweka: Kwani kazi ya Polisi ni nini?

Shahidi: Kulinda raia na mali zao na kutazama usalama wa nchi

Wakili Kweka: Ulilichukuaje hilo suala kuhusu Polisi?

Shahidi: Nilichukulia kuwa sio kitu kizuri kama mtu anatibiwa halafu unamchukua unampiga risasi ni jambo linaloweka uadui

Wakili Kweka: Nini kiliendelea baada ya hapo?

Shahidi: Polisi walikuwa wakipita watu walikuwa wanawazomea kuwa wauaji hao wauaji hao? Ndipo mtu mmoja ambaye hakujitambulisha akaniita na kuniuliza tatizo nini. Nikamueleza nini kimetokea, basi aliniomba namba ya simu na kisha nikampa

Wakili Kweka: Nini kilitokea baada ya hapo?

Shahidi:
Tarehe 30 nilipigiwa simu na mtu aliyejitambuliaha kuwa RCO wa Kinondoni! Kwanza nilishtuka...ila watu walinishauri nenda. Tarehe 31 nilienda na kumkuta yule mzee akaniuliza “nadhani unanikumbuka?” Nikamwambia nakukumbuka....wakaja Polisi wakanihoji kuhusu suala hilo na kuniuliza kama nipo tayari kutoa ushahidi kwa kuwa jambo hilo ni la kitaifa.

Niliwaeleza kuwa kama mtu anaongea haya basi anavithibisho hawezi kuongea tu hivi

Wakili Kweka: Uliwaeleza hayo? Ilikuwa tarehe 31 mwezi gani?

Shahidi: (Baada ya dakika kama 3 za kuwaza) Ilikuwa mwezi wa 8

===================
Wakili Kweka anamaliza kumuongoza Shahidi wake na sasa Hakimu anaruhusu upande wa utetezi kuendelea na kumuhoji shahidi
===================

Wakili Kibatala: Shahidi tuanze kwa utambulisho wako? Nimeona Wakili Kweka akikupa kitu fulani sijui kitambulisho chako. Umeona Wakili Kweka akisema kiingizwe kwenye ushahidi na Hakimu akione?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Uliongozwa kusema kuhusu Mwenyekiti wa mtaa au nyumba namba yako?

Shahidi: Hapana, angeniuliza ningesema

Wakili Kibatala: Uliongozwa kusema chochote kusema kuhusu jina la duka lako?

Shahidi: Hapana, ningeambiwa nitaje ningesema

Wakili Kibatala: Siku hizi kwa Wafanyabiasha wadogo wadogo wana vitambulisho vyao. Je, umeongozwa kukionesha na kusema chochote?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Umeongeozwa kuonesha malipo yoyote ya kodi unayofanya kwa Halmashauri yako husika au nini?

Shahidi: Hapana, ningeambiwa nije navyo ningekuja navyo!

Wakili Kibatala: Siku watu wanabishana unakumbuka ilikuwa ni lini?

Shahidi: Tarehe 29/10/2018

Wakili Kibatala: Leo ni tarehe ngapi?

Shahidi: Tarehe 16/05/2019

Wakili Kibatala: Huyu Abilali, uliongozwa kusema majina yake mawili?

Shahidi: Anaitwa Abilali Salumu, ila sikuongozwa kusema yote mawili

Wakili Kibatala: Uliongozwa kusema chochote kuhusu huyo uliyesema ni RCO kuchukua simu ya Abilali?

Shshidi: Hakuwahi kuchukua, sikuongozwa

Wakili Kibatala: Kipi sahihi?

Shahidi: Sikuongozwa

Wakili Kibatala: Je, uliulizwa swali lolote na Wakili kuhusiana na ulichokiona kwenye simu ya Abilali, mahala pengine?

Shahidi: Hapana, sina simu

Wakili Kibtala: Na ni sahihi kuwa uliongozwa kusema hujui kutumia simu ya ‘smartphone’ wala huna?

Shahidi: Sikuongozwa

Wakili Kibalata: Hapa Mahakamani, wewe ndio uliona kwenye simu ya Abilali, sasa sema kama uliongozwa kuoneshwa video hiyo hapa na kuitambua

Shahidi: Hapana

Wakili Kibalata: Shahidi, ni sahihi kuwa ulipigiwa simu leo kuja hapa?

Shahidi: Hapana, sijapigiwa simu leo

Wakili Kibatala: Umefikaje leo?

Shahidi: Nilipewa maelekezo na Wakili wa Jamhuri mara ya mwisho kuja hapa kwenye kesi hii. Mwezi uliopita ila sikumbuki tarehe

Wakili Kibatala: Uliongozwa na Wakili kwenda kumshika Zitto kumtambua?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Wakili wa Jamhuri alikuelekeza namna ya kumtambua mtu hapa mahakamani?

Shahidi: Hakunielekeza

Wakili Kibatala: Unasema kuwa hali ilikuwa mbaya hadi magari ya Polisi yalipokuwa yakipita walikuwa wanazomewa. Naomba useme kama uliongozwa kusema kama hawa watu walikamatwa au la?

Shahidi: Hapana, hawajakamatwa. Sikuongozwa

Wakili Kibatala: Naomba useme kama kuzomea Polisi ni kosa la jinai au la?

Shahidi: Sina ufahamu wa sheria

Wakili Kibatala: Eleza kama uliongozwa kuzitaja namba zako za simu?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Unajua namna ya kuthibitisha namba ya simu inatumika na nani ni rahisi sana kwa kuwa watu wanasajili namba zao so mitandao inajua majina yao?

Shahidi: Najua ni rahisi hata ukifanya kama unatuma pesa, unajua

Wakili Kibalata: Eleza kama uliongozwa kusema kuhusu jina la Askari aliyechukua maelezo yako?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Unajua kuwa AyoTV ilikuwa na mgogoro na TCRA?

Shahidi: Hapana, sifahamu

Wakili Kibatala: Ulienda Polisi na nani?

Shahidi: Sikwenda na mtu

Wakili Kibatala: Uliongozwa kusema kama ulipokuwa unaenda Polisi ulimwambia yeyote?

Shahidi: Nilimwambia mama yangu mzazi.......

Wakili Kibatala: Aaaanhaaa! Uliongozwa kusema hayo?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Asante! Nimemaliza Mheshimiwa Hakimu

***********

Hakimu Shaidi: Mimi binafsi napenda kujua ulimwambia nini mama yako?

Shahidi: Kuwa nimeitwa Polisi. Oysterbay na sijui nini kitatokea

Hakimu Shaidi (huku akitania): Kwa hiyo wewe kwenye kasheshe unamuita mama? Haya

Shahidi anatabasamu
****

Hakimu anamuuliza Wakili wa Jamhuri kama yupo tayari kwa ajili ya Re-examination

Wakili Kweka: Mheshimiwa naomba hilo swali lako liwe kwenye re-axamination tulitaka na sisi kuweka hilo wazi

Mawakili wa pande zote mbili na Hakimu wanakubaliana kuahirisha kesi hiyo hadi kesho - Mei 17, 2019
 
Aisee huyu Kibatala sio wa mchezomchezo duhh,yaani ukipelekwa km shahidi wa kupikwa lazima ushtukiwe.
 
Shahidi:
Tarehe 30 nilipigiwa simu na mtu
aliyejitambuliaha kuwa RCO wa Kinondoni!
Kwanza nilishtuka...ila watu walinishauri
nenda. Tarehe 31 nilienda na kumkuta yule
mzee akaniuliza “nadhani unanikumbuka?”
Nikamwambia nakukumbuka....wakaja Polisi
wakanihoji kuhusu suala hilo na kuniuliza
kama nipo tayari kutoa ushahidi kwa kuwa
jambo hilo ni la kitaifa.
Niliwaeleza kuwa kama mtu anaongea haya
basi anavithibisho hawezi kuongea tu hivi
Wakili Kweka: Uliwaeleza hayo? Ilikuwa
tarehe 31 mwezi gani?
Shahidi: (Baada ya dakika kama 3 za
kuwaza) Ilikuwa mwezi wa 8
===================
Wakili Kweka anamaliza kumuongoza
Shahidi wake na sasa Hakimu anaruhusu
upande wa utetezi kuendelea na kumuhoji
shahidi
===================
Wakili Kibatala: Shahidi tuanze kwa
utambulisho wako? Nimeona Wakili Kweka
akikupa kitu fulani sijui kitambulisho chako.
Umeona Wakili Kweka akisema kiingizwe
kwenye ushahidi na Hakimu akione?
Shahidi: Hapana
Wakili Kibatala: Uliongozwa kusema kuhusu
Mwenyekiti wa mtaa au nyumba namba
yako?
Shahidi: Hapana, angeniuliza ningesema
Wakili Kibatala: Uliongozwa kusema
chochote kusema kuhusu jina la duka lako?
Shahidi: Hapana, ningeambiwa nitaje
ningesema
Wakili Kibatala: Siku hizi kwa
Wafanyabiasha wadogo wadogo wana
vitambulisho vyao. Je, umeongozwa
kukionesha na kusema chochote?
Shahidi: Hapana
Wakili Kibatala: Umeongeozwa kuonesha
malipo yoyote ya kodi unayofanya kwa
Halmashauri yako husika au nini?
Shahidi: Hapana, ningeambiwa nije navyo
ningekuja navyo!
Wakili Kibatala: Siku watu wanabishana
unakumbuka ilikuwa ni lini?
Shahidi: Tarehe 29/10/2018
Wakili Kibatala: Leo ni tarehe ngapi?
Shahidi: Tarehe 16/05/2019
 
Hao mashahidi ni wazoefu.
Mashahidi wametengenezwa na kufundishwa kwa siku nyingi LAKINI siku ya mtihani wanaambulia zero.

Maelezo yanachukuliwa (mwezi wa 8) kabla ya tukio (mwezi wa 10), ujinga mkubwa!!
 
Tunawalipa hawa waendesha mashtaka mishahara ya bure kabisa, ma shahidi wanaisumbua na kupoteza muda wa mahakama
 
Back
Top Bottom