Katka uundaji wa serikali yafuatayo yazingatiwe

Kilbark

JF-Expert Member
Feb 25, 2008
569
250
UCHAGUZI mkuu umekwisha huku hadhi ya chama kikongwe cha siasa nchini, CCM ikionekana kuporomoka kiasi cha kutisha, sababu kubwa ikielezwa kuwa ni kushindwa kutekeleza nyingi ya ahadi ilizotoa katika uchaguzi wa mwaka 2005.

Mojawapo ya ahadi hizo, ni kuboresha maisha kwa wananchi, mgombea wake Jakaya Kikwete, alijinadi akisema ‘maisha bora kwa kila Mtanzania’ ahadi ambayo katika kampeni ya mwaka huu, hakuizungumzia sana na wala haikuwa kwenye mabango yake ya kuomba kuchaguliwa.

Maisha ya Watanzania wengi ni magumu, idadi ya watu wanaolala nje pia katika miji mbalimbali ikiongezeka kwa kutokuwa na fedha za kupanga vyumba, kwani sasa chumba chenye umeme si chini ya Sh30,000 kwa mwezi, wakati mishahara mingi ni kidogo, na makato ya kodi kwa mshahara nayo imekuwa kubwa.

Mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali nchini ni wa juu, kwa mfano wakati serikali ya awamu ya nne inaingia madarakani, bei ya gunia la mkaa lilikuwa Sh8000, sasa ni zaidi ya Sh30,000, sababu kubwa ikielezwa ni kitendo chake cha wakati fulani kuzuia biashara hiyo, hali iliyosababisha bei kupanda na hata ilipolegeza masharti, bei haikuweza kupunguzwa.

Ninachotaka kusema katika makala haya ni kwamba wakati umefika kwa chama tawala kubadilika.Si kweli kwamba KANU iliwahi kuwaza kwamba siku moja kitakuwa vile, wala hakuna mwanachama aliyependa kuona KANU, kinakuwa dhaifu kama kilivyo sasa, bali ni kwa sababu ya maamuzi ya viongozi.

Kwa mpinzani kupata asilimia 26 ni jambo la kushtua, lakini la kushtua zaidi ni kwanini Kikwete ambaye katika uchaguzi wa awali alipata asilimia 80 ya kura, leo anaambulia asilimia 61.

Ni jambo la msingi sasa kwa CCM kuanza kuonyesha mabadiliko kwanza katika kumchagua waziri mkuu, ambaye kweli kazi zake zinaweza kuonekana kwa jamii.

Tunaambiwa Edward Lowassa alikuwa ana kasoro zake zilizosababisha alazimike ajiuzuru, vema, lakini ni katika utawala wake shule za kata zilijengwa.

Naamini kwa kila Mtanzania mwenye macho anaweza kukubaliana na mimi, licha ya ukweli mwingine kuwa alihusishwa na kashfa ya ufisadi katika mradi wa umeme wa dhararu wa Richmond.

Hadi sasa hajapandishwa mahakamani kama ni kweli aliiba fedha kwenye kashfa hiyo au la, kwa maana hiyo inatuwia vigumu kwa Watanzania kuamini kama ni kweli alihusika au ni visa vya kisiasa…kama alihusika nini kinaendelea?
Ninachotaka kusema hapa ni kwamba matendo ndiyo yanayoweza kuharibu au kujenga chama cha siasa. Ahadi zisizo na utekelezaji ni sumu kubwa inayoonekana kupoteza umaarufu wa chama.

Inakera zaidi pale hata ahadi ndogo nazo zinaposhindwa kutekelezwa, kwa mfano katika hotuba ya kwanza kabisa bungeni baada ya kuwa rais, Kikwete alisema angezungumza na wenye benki ili kupunguza riba za mikopo.

Miaka mitano imepita hakuna kilichofanyika, riba za mikopo zinaumiza watu, kwani baadhi ya benki riba ni hadi asilimia 25. Kuna ugumu gani wa kuzungumza na wenye benki ili ipungue kama njia ya kuwawezesha watu wengi kupata mitaji.

Zimetolewa fedha maarufu kama mabilioni ya JK, inasitikisha hata hazijulikani namna zilizovyogawiwa, kiasi kwamba hadi JK mwenyewe amekuwa akilalamikia wale waliopewa kazi ya kuyagawa hayo mabilioni yake.

Ndio nasema ni lazima kufanya mabadiliko makubwa kwenye baraza la mawaziri kwani lile lililopita kwani kuna baadhi yao walikuwa na kashfa za hapa na pale na baadhi yao walipoteza mwelekeo, kiasi cha jamii kuwachukia.

Pia ni lazima kuwe na umakini katika kumpata spika, ni lazima apatikane mtu ambaye atawaweka wabunge kuwa huru kuzungumza, pia ni lazima spika awe ni mwenye sifa nzuri katika jamii.

Kwa upande wa waziri mkuu, iko haja ya kupatikana kwa waziri mkuu mwanamke, kitu ambacho kinaweza kuongeza heshima ya Tanzania kwa nchi za nje na pia angalau kuimarisha usawa katika utawala. Tumekuwa tukipigia debe sana usawa, lakini katika safu za uongozi wa juu wanawake ni kama wanaonekana hawafai.

Mbaya zaidi tunawaona wanawake hawawezi, hawafai na kuwapa nafasi chache za uwaziri wa kawaida tu, ni hao hao wanateuliwa na Umoja wa Mataifa kushika nyadhifa kubwa zikiwemo naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa..

Hili pia linaweza kuharibu au kukijenga CCM katika uchaguzi ujao…kidumu chama cha mapinduzi…kidumu chama tawala, makofi tafadhari!!! Muungwana ni vitendo…tusichague baraza la mawaziri kwa mazoea, kesho tutasutwa, heshima yetu itapotea.

Ni lazima tuchague mawaziri na manaibu ambao kweli wanaweza kusimamia vizuri maendeleo, kwa mfano kama kweli tunataka maendeleo, ni lazima sera za madini vifumuliwe na kuwa na nzuri zaidi, ambazo zitamsaidia Mtanzania kuondokana na umaskini.

Wawekezaji katika sekta ya madini, wanapaswa kuingia ubia na serikali kwa asilimia 50 kwa 50, sio kwa serikali kuwaacha wanachimba wanavyotaka na yenyewe kusubiri kodi tu kama inavyofanya sasa.

Anayekataa hili tunapaswa kumshangaa, kwani ndilo lililosababisha Bostwana leo watoto wanasoma bure kuanzia chekechea hadi sekondari, huduma za maji, afya ni bora na uchumi wake unapaa kila kukicha.

Huwezi kutegemea kodi tu na ukatarajia mkuze uchumi haraka hasa katika nchi inayolalamikiwa kwa ufisadi na rushwa… mfanyabiashara gani anapenda kulipa kodi sahihi? Kama kweli tunataka uchumi ukue, tunapaswa kubadilisha sera ya madini haraka iwezekanavyo, ya sasa haiwezi kutusaidia.


Kazi kubwa inayomkabili Rais Jakaya Kikwete baada ya siku chache zilizopita kuapishwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kipindi cha pili cha miaka mitano, ni kuunda serikali yenye kukidhi viwango, mategemeo na matazamio ya wananchi. Rais anakabiliwa na kazi ngumu sana, kwani siyo siri kwamba wananchi walio wengi kwa kiasi kikubwa hawakuridhishwa na kiwango cha utendajikazi wa mawaziri wengi katika baraza lake la mawaziri katika miaka yake mitano aliyokuwa Ikulu.

Katika kipindi kilichopita, tuliona baadhi ya mawaziri wakimwangusha Rais Kikwete kwa kukosa uadilifu au kukabiliwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi, hivyo kulazimika kujiuzulu. Katika kipindi hichohicho, tulishuhudia pia baadhi ya mawaziri na watendaji wake wakuu wakijiuzuru kutokana na kuwajibika baada ya kushindwa kudhibiti vitendo viovu vya baadhi ya maafisa wao katika mamlaka walizokuwa wakiziongoza

Lakini pia sote tuliona baadhi ya mawaziri wakikaa katika baraza hilo la mawaziri mithili ya watalii na kazi yao kubwa ikiwa tu ni kukaa maofisini na kufanya safari zisizokuwa na tija. Kwa tafsiri yoyote ile, viwango vya utendaji wa kazi zao vilikuwa chini kiasi cha kutisha na bahati mbaya waliendelea kukalia viti hivyo pasipo kunyooshewa vidole au kuondolewa na mamlaka husika. Kwa kweli, mawaziri hao si tu walizitia aibu mamlaka zilizowateua kushika nafasi hizo bali pia walichangia kwa kiasi fulani kufifisha imani ya wananchi kwa serikali ya Rais Kikwete.

Hata hivyo, tunaposema hivyo hatuna maana kuwa baraza hilo la mawaziri halikuwa na mawaziri wachapakazi au waadilifu. Baraza hilo hakika lilikuwa na baadhi ya mawaziri ambao walikuwa mabingwa wa kuongoza kwa kuonyesha njia, kutafuta suluhisho la matatizo mengi yaliyokuwa yanawakabili wananchi na kusimamia sheria, sera na kanuni zilizowekwa katika uendeshaji wa masuala ya kiserikali.

Tumeainisha yote hayo ili kumsaidia kiongozi wetu, Rais Kikwete, ateue mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya walio makini na bora zaidi katika serikali anayotazamia kuiunda katika wiki mbili hivi zijazo. Tunasema pasipo kupindisha maneno kwamba baadhi ya wateule wake katika kipindi chake cha kwanza katika nafasi tulizozitaja hapo juu na nyingine nyingi, walikuwa mzigo mkubwa kwake usioweza kubebeka. Mbali na kutokuwa waadilifu, baadhi yao walikuwa wazembe wa kutupwa na wengine walikuwa hawana karama ya kuongoza hata kidogo.

Ni kwa sababu hiyo tungependa kushauri kwamba katika ngwe hii ya mwisho, Rais Kikwete awatunuku wananchi baraza dogo la mawaziri na viongozi wengine katika nyadhifa mbalimbali ambao ni wachapakazi na waadilifu.

Kwa kuwa Watanzania ni wamoja na kwa kuwa wanataka wapunguziwe kodi itokanayo na gharama zinazotokana na uendeshaji wa serikali iliyo kubwa na isiyokuwa na tija, Rais Kikwete aunde wizara chache ambazo zina ulazima, pasipo kuumiza kichwa sana katika kuangalia mambo ya uwiano wa kimikoa, nakadhalika. Sote tulikuwa mashuhuda wa jinsi Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alivyoteua watendaji bila kwanza kuangalia kabila, dini au jinsia ya mtu aliyemteua.

Tunachokisisitiza hapa ni umuhimu wa sisi kama Watanzania kurudia matendo na uasilia wetu uliotufanya tuwe wamoja na kuifanya nchi yetu iwe kisiwa cha amani na utulivu. Waasisi wa taifa letu walitanguliza upendo, uadilifu, utendaji haki na kuheshimu sheria na katiba pamoja na mambo mengine ya msingi katika kufanya uteuzi wa viongozi katika ngazi mbalimbali za kitaifa. Sera za udini, ukabila, umajimbo na mambo mengine ya utengano kamwe hayakupewa nafasi.

Sisi tunadhani kwamba Rais Kikwete katika kufanya uteuzi azingatie tu uwezo, uadilifu na unyenyekevu wa kila mtu atakayemteua kuanzia kwa wakuu wa wilaya na mikoa, makatibu wakuu, mawaziri na wengineo. Tunategemea pia kwamba waziri mkuu mpya si tu atakuwa mchapakazi wa mfano bali pia atakuwa mtu wa wote, wakiwamo wabunge wa kambi ya upinzani katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom