KATIBU Myeka mstaafu wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Samuel Kasori, ameyakimbia makazi yake yaliyopo mjini Arusha na kwenda kujificha kusikojulikana kwa hofu ya kuuawa na wale anaowaita "magaidi wa kisiasa".
Kasori ndiye aliyekuwa Katibu Myeka wa mwisho wa Nyerere kabla hajafariki dunia Oktoba 14 mwaka 1999, amedai kwamba wanaomtishia maisha wanamwona yeye kama kikwazo kwa kundi katika mbio za kuwania Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Mstaafu huyo tayari ametoa taarifa katika ngazi za juu za nchi na katika vyombo vya dola na Raia Mwema linafahamu kwamba tayari Dola inafanyia kazi taarifa zake hizo.
Katika mojawapo ya ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu ya mkononi (SMS), Kasori aliandika kwa mmoja wa viongozi wa juu wa serikali na vyombo vya dola maneno haya;
"Utakumbuka kwamba tarehe 12 Februari 2015, nilikutaarifu kuwa maisha yangu yanatishiwa na Mheshimiwa [amemtaja jina] kupitia kwa ADC [Aide de Camp – Mlinzi] wake [anamtaja jina] ambaye ni mtumishi wa Serikali [Usalama wa Taifa] niliyekuwa naye kwa hayati Mwalimu J. K. Nyerere…..";na akaendelea kuelezea kwa kina kile anachokiita "hali hatarishi" akisema:
"Tarehe 05/03/2015, siku ya Alhamisi, saa 11.00 jioni, wamekuja nyumbani kwangu, watu wawili wanaume, kijana na mzee wakiwa na usafiri wa Toyota, wakagonga geti langu wakitaka wafunguliwe; wakamuuliza mmoja wa wanafamilia yangu: "Mr. Kasori yupo?"; na kutaka waruhusiwe kuangalia "garden" [bustani] yangu; wakaambiwa nimetoka".
"Wakaulizwa walikotoka wakajibu wametoka Moshi na kwamba jamaa yao mmoja amewapa habari za bustani yangu na wakaendelea kuomba wakaribishwe lakini hawakuruhusiwa na badala yake wakapewa simu niongee nao, kisha wakaombwa waje [wakati] nikiwapo; wakasema tarehe 9/3/2015".
Mzee Kasori aliendelea kueleza; "tarehe 7/3/2015, Jumamosi, walikuja tena watu wawili [wengine] vijana wakiwa na nguo zilizofunika sura zao kutoka utosini hadi miguuni, huku machoni wamevaa miwani ya giza na mikononi wamevaa "gloves" [glavu] nyeusi wakiwa na usafiri wa gari aina ya Toyota yenye namba zisizosomeka vizuri.
"Mtu wa familia yangu alipofungua geti na kuona kuona hali hiyo, aliogopa na kujifunika kanga kichwani; nao wakauliza kutaka kujua alikokuwa [yeye Kasori] na waonyeshwe bustani yake.
"Watu hao walijitambulisha kwamba walitoka Dodoma; wakauliza kama nyumba hiyo ilikuwa na mlinzi; na walipojibiwa kwamba inaye, wakasema watamsubiri [Kasori] hapo hapo langoni.
Katibu Myeka huyo wa Rais wa zamani ameeeleza katika ujumbe wake huo kuwa walipotakiwa wampigie [Kasori] simu, watu hao walikataa katakata, kisha wakampiga picha mwanafamilia huyo pamoja na geti hilo kabla ya kuondoka kwa kasi bila kuaga.
Akifafanua zaidi, Mzee Kasori anawataja, mbali na mlinzi wa kigogo anayemtuhumu kufadhili hujuma hii, watu wengine wawili na namba zao za simu, waliokodiwa kufanikisha mauaji; mmoja akiwa mkazi wa Dar es Salaam na mwingine yuko Arusha; na kumaliza kwa kusema:
"Mheshimiwa Rais, niseme tu kuwa, nitakapouawa mwaka 2015, basi kama ilivyo kwa hayati J. K. Nyerere, msitafute kumbukumbu zetu katika makaburi bali katika mioyo ya tulioboresha maisha yao; buriani Tanzania".
Februari mwaka huu, gazeti hili lilifanya mahojiano na Mzee Kasori juu ya kauli kwamba mmoja wa watu wanaotajwa kutaka kuwania Urais kupitia CCM, Edward Lowassa, aliwahi kupata baraka za Mwalimu Nyerere kuingia kwenye kinyang'anyiro kama hicho mwaka 1995.
Kwenye mahojiano hayo, Kasori alikanusha kwa nguvu zote jambo hilo kuwahi kutokea na kwamba ilikuwa ni kinyume chake; na kwamba Mwalimu alimwita kigogo huyo kuwa mtu "asiye na chembe ya sifa kuweza kugombea nafasi hiyo ya juu nchini".
Kasori alisema alielekezwa na Mwalimu ayafikishe maneno hayo kwa hayati Rashid Kawawa ili naye ayafikishe kwa "kigogo" huyo kwa vile Mwalimu hakuwa na muda wa kupoteza kwa ghilba kama hizo.
Katika kinyang'anyiro hicho cha Urais, Mwalimu alimpigia debe Benjamin Mkapa, akimpachika jina la sifa "Mr. Clean" [Mtu msafi] hadi akaweza kushinda na kupokea kijiti cha uongozi kutoka kwa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.
Tangu kuchapishwa kwa mahojiano hayo na gazeti hili, Mzee Kasori amelalamika kupitia vyombo vya habari kuhusu kuandamwa na watu wasiojulikana kiasi cha kuhofia uhai wake.
Gazeti hili limefanikiwa kuzungumza na Kasori akiwa mafichoni kwa njia ya simu na akionekana kutojiandaa wala kuwa tayari kusema mengi, bali kwa kifupi tu, alisema:
"Kweli itashinda tunavyoishi. Kweli haihofu tisho wala nguvu ya majeshi. La uongo lina mwisho, kweli kitu cha aushi/Kweli itashinda kesho kama leo haitoshi, " alisema akinukuu mojawapo ya mashairi ya mshairi namba moja hapa nchini, hayati Shaaban Robert.
Mmoja wa marafiki wa karibu wa Kasori ambaye alihojiwa na gazeti hili wiki hii kutokana na habari hizi alisema; "Je, ni kweli maelezo aliyotoa kwenye mahojiano na gazeti lenu (Raia Mwema) ni ya kuchukiza na hatarishi kufanya mwanasiasa makini, anayejua ‘malumbano' ya kisiasa, kumfanya aape kutoa uhai wa mtu?
"Je, ni kweli muuaji mzoefu, tena kwa ushirikiano na maofisa wazoefu wa dola inavyodaiwa; anaweza kujibwaga nyumbani kwa mtu kufanya tendo hilo mchana kweupe na mbele ya macho makavu ya umma, kama anavyotaka Mzee Kasori tuamini?" alisema.
Samuel Kasori alikuwa Katibu Myeka wa tatu na wa mwisho wa Rais kwa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere; wa kwanza akiwa ni Mama Joan Wickens, tangu uhuru; akafuatiwa na Joseph Butiku, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere nchini.
Chanzo: Raia Mwema