BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,789
- 288,015
Kashfa ya kuhonga wabunge iundiwe tume |
Tuesday, 19 July 2011 20:48 |
Mwananchi TANGU kuibuliwa bungeni mjini Dodoma juzi kwa kashfa inayohusu Wizara ya Nishati na Madini ya kuwahonga wabunge ili wapitishe bajeti ya wizara hiyo, maswali mengi yameulizwa ingawa majibu yake imekuwa vigumu kuyapata. Hali hiyo tete imejitokeza kutokana na madhara yatokanayo na tukio hilo kuwa makubwa zaidi kuliko ilivyodhaniwa hapo awali. Hali hiyo tete inatokana na ukweli kwamba tumefanya makosa kama taifa kuangalia kashfa hiyo kwa kutumia miwani ya mbao, kwa maana ya kutokujua tunaingia katika mtego wa kuficha tatizo hilo kwa kuelekeza lawama na laana zetu kwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Katibu Mkuu wake, David Jairo aliyechangisha mamilioni ya fedha kwa lengo la kutoa rushwa kwa wabunge. Kumbe katika kuwasaka papa na nyangumi wanaohusika na kashfa hiyo na nyingine nyingi za aina hiyo, tulipaswa kutupa nyavu zetu mbali zaidi baharini siyo tu kwa lengo la kuwanasa wahalifu wote bali pia kuongeza wigo wa kubaini ukubwa wa tatizo. Kinachoonekana hapa ni kuwa kashfa hiyo ni kubwa zaidi kuliko inavyoonekana mbele ya wananchi. Haiingii akilini kwamba katibu mkuu wa wizara anaweza kupata ujasiri wa kutoa waraka kwa mashirika yote yaliyo chini ya wizara yake akiyaagiza kuchanga Sh50 milioni kila moja ili kutoa rushwa kwa watu mbalimbali, wakiwamo wabunge kwa lengo la kuwezesha kupitishwa kinamna kwa bajeti ya wizara hiyo bungeni. Ni vigumu pia kufikiria jinsi mtu aliyeteuliwa kusimamia matumizi ya fedha za Serikali katika wizara husika kusaliti dhima aliyopewa kwa kuhamasisha wizi na ukwapuaji wa fedha za walipakodi na kuamuru zipitishwe katika akaunti ya mawakala wa utafiti wa masuala ya uchimbaji madini iliyopo katika Benki ya NMB, Tawi la Dodoma. Je, kuna uhusiano gani kati ya mawakala hao na viongozi wa wizara hiyo ya Nishati na Madini? Waraka uliotumwa kwa mashirika zaidi ya 20 yaliyo chini ya wizara hiyo unawakumbusha wakuu wa mashirika hayo kwamba ni utamaduni wa wizara hiyo kufanya zoezi hilo kila mwaka wakati wa kuwasilisha hotuba ya Bajeti Dodoma. Hiyo inadhihirisha pasipo shaka kwamba ukwapuaji huo wa kutisha wa fedha za wananchi umekuwa ukifanyika kila mwaka. Tuliposema hapo awali kwamba kumbe tatizo ni kubwa zaidi kuliko tulivyofikiria tulikuwa na maana kwamba, ukwapuaji huo haupo katika Wizara ya Nishati na Madini pekee, bali katika wizara zote mara linapokutana Bunge la Bajeti. Kikao cha Bunge cha Bajeti kumbe ni wakati wa mavuno kwa viongozi wa wizara na mashirika yaliyo chini ya wizara hizo. Habari zinasema kila wizara hutenga wastani wa Sh900 milioni kwa lengo la kufanikisha upitishwaji wa bajeti za wizara hizo, hivyo fedha hizo hutumika kuhonga pande zote husika na watumishi wa wizara hizo hutumia fedha inayobaki kujinufaisha. Jambo la kushangaza ni kuwa, inakuwaje fedha zote hizo zinatumika kifisadi kila mwaka wakati hazikutengewa bajeti yoyote? Inakuwaje Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anapokagua hesabu za wizara hizo na kukuta madudu yanayotokana na ukwapuaji huo wa kutisha? Je, inakuwaje kamati za Bunge zinazosimamia hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma hazigundui ufisadi huo zinapopitia ripoti hizo za CAG kila mwaka? Lazima tujiulize pia wapi zilipo bodi za wakurugenzi zinazosimamia mashirika ya umma yaliyo chini ya wizara mbalimbali. Kwa mfano, kwa kuwa mashirika hayo yanawajibika kwa bodi hizo, inakuwaje katibu mkuu wa wizara fulani ayaagize mashirika hayo kuchanga fedha za kufanya kazi chafu ya kutoa rushwa? Ina maana bodi hizo hazihusiki na kupitisha ripoti za wakaguzi wa mahesabu ya mashirika yao? Sisi tunasema kuwa jambo hili lina siri kubwa. Tunataka tume huru iundwe ili itoe jawabu kwa kashfa hii ya aina yake katika nchi yetu. |