Karume Usiwe Mnafiki: CUF

Junius

JF-Expert Member
Mar 11, 2009
3,181
139
Taarifa kwa Vyombo vya Habari 15 Julai, 2009
Sisi Chama cha Wananchi (CUF) tumepokea kwa tafakari kubwa kauli ya Mhe. Amani Karume ya kumtaka kila Mzanzibari mwenye sifa na haki ya kupatiwa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi (ZAN ID) kwenda katika Ofisi za Idara ya Vitambulisho kupatiwa kitambulisho hicho. Kauli hiyo aliitoa juzi alipokuwa kwenye Bustani ya Victoria alipokuwa akizungumza na wahitimu wa Chuo cha Utalii, Zanzibar, na kunukuliwa katika gazeti la Zanzibar Leo la leo.
Kwa upande mmoja tunataka tuamini kwamba Mhe. Karume alimaanisha hasa alichokuwa anakisema na kwamba ni haja yake kuona kwamba kila Mzanzibari mwenye haki na sifa anapata kitambulisho hicho. Kwa upande mwengine tunataka tuamini kwamba, anatoa kauli hiyo kufurahisha wahisani tu, ambao wameshajulishwa kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupitia mtandao wake usio mtakatifu (unity of the demons) unaowajumuisha masheha, Tume ya Uchaguzi (ZEC) na Idara yenyewe ya Vitambulisho, inafanya kila lililo kwenye uwezo wake kuhakikisha kuwa Wazanzibari wengi ambao inaamini kwamba hawaiungi mkono serikali na chama chake tawala hawapatiwi vitambulisho hivyo na hatimaye wanaenguliwa katika zoezi la uandikishaji kwa ajili ya kushiriki kwenye chaguzi.
Hoja ya Mhe. Karume kwamba SMZ imeamua kuvitumia vitambulisho hivyo kwenye uchaguzi ili kuzuia uwezekano wa watu wasiokuwa na haki kupiga kura na pia kuondosha malalamiko yanayojitokeza mara kwa mara, haina mashiko hata kidogo. Ukweli ni kuwa utumiaji wa vitambulisho hivi kwa ajili ya uchaguzi ndio hasa unaochochea uchaguzi usio huru na wa haki, kwani tayari uzoefu wa uandikishaji katika Wilaya ya Micheweni Pemba unaonesha kwamba mtandao huo usio mtakatifu umeanza kutumia suala la vitambulisho hivyo kama kikwazo dhidi ya Wazanzibari kushiriki kwenye chaguzi.
Kwa mantiki hii, tunamtaka Mhe. Karume aongeze maana katika kauli yake, sio tu kwa kuwataka Wazanzibari wakachukuwe ZAN ID, bali pia – na zaidi – kuitaka Idara ya Vitambulisho na mtandao mzima tulioutaja utoe vitambulisho hivyo kwa Wazanzibari, maana watu hawataweza kwenda kuchukua kile kisichotolewa. Na ukweli ni kuwa mtandao huo unawazuia Wazanzibari kupata ZAN ID. Tunasema haya tukiwa na ushahidi wa zaidi ya wananchi 100 wa wilaya ya Micheweni ambao ingawa walipatiwa risiti za ZAN ID tangu mwaka 2006, hadi sasa hawajapewa vitambulisho vyao kwa kisingizio kwamba vitambulisho hivyo havijaletwa kutoka Ofisi Kuu Unguja. Vile vile tuna ushahidi wa maelfu ya wengine ambao wamenyimwa kabisa fursa ya kuandikishwa kuwa Wazanzibari licha ya kwamba wamefikia umri kwa sababu tu masheha wamekataa kuwapa barua za kuwathibitisha.
Kama kweli Mhe. Karume anamaanisha kauli yake hii, basi achukuwe hatua za makusudi kuisimamia na kuona kwamba inatekelezwa. Vile vile kwa watendaji walio chini yake, kama kweli wanaamini kuwa kauli ya bosi wao ni agizo kwao, basi waifuatilie na kuifanyia kazi. Vyenginevyo, hatuna sababu ya kutokuendelea kuwa na shaka kwamba SMZ na mtandao wake usio mtakatifu ina dhamira ya kuuchafua uchaguzi ujao wa Zanzibar kwa kutumia suala la vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.

Pamoja na salamu za Chama.

Imetolewa na:
Salim Bimani
Mkurugenzi wa Uenezi na Mahusiano na Umma
The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi)
Simu: +255 777 414 112
E-mail: cufhabari@yahoo.co.uk
Weblog: Haki Sawa kwa Wote
 
Mjumbe hauwawi.
Hivi CUF mnataka nini. Si ndio nyinyi mliolalamika kuwa watu wa bara wanapigishwa kura katika uchaguzi wa Zanzibar,. Si ndio nyinyi mliokubali(kwa kweli mlioshindikiza) tuwe na identification maalum ambayo itawazuwia (mamluki) kutoka bara kupiga kura katika uchaguzi wa Zanzibar. Nakushangaeeni kukana kitambulisho cha Mzanzibari hivi sasa. Chambilecho CUF.
 
Hivi CUF mnataka nini. Si ndio nyinyi mliolalamika kuwa watu wa bara wanapigishwa kura katika uchaguzi wa Zanzibar,. Si ndio nyinyi mliokubali(kwa kweli mlioshindikiza) tuwe na identification maalum ambayo itawazuwia (mamluki) kutoka bara kupiga kura katika uchaguzi wa Zanzibar. Nakushangaeeni kukana kitambulisho cha Mzanzibari hivi sasa. Chambilecho CUF.
Pakacha, sasa hii itakuwa ile hadithi ya fundi mshona nguo, unamwambia akushonee kanzu anakwambia na kaptula pia atakushonea.
Sasa kama CUF wameshinikiza wasiandikishwe mamluki hii haina maana kua wanaostahiki wanyimwe ati! na hizo ZAN ID wanaostahiki si wapewe wajiandikishe kama utaratibu unavyotaka! CUF hawajakana kitambulisho cha Mzanzibar wanacho kataa ni namna matumizi ya kitambululisho hicho yanavyokiuka makusudio yake. Sasa badala ya kutumika kwa makusidio ya kuwapatia haki wahusika kimekuwa kama kitambulisho cha kuwakosesha haki zao za msingi.
 
Junius,
Mkuu hapa nashindwa hata kuwaelewa CUF wanachojaribu kusema..
Nachoelewa mimi hivi ni vitambulisho vya makaazi (Residential) kwa Wazanzibar na sio vitambulisdho vya Uraia (Citizenship) kwa wazanzibar wote.. na kama nimeelewa, sababu kubwa ni kuuwezesha uchaguzi uwe wa haki kuwawezesha wakaazi tu ndio wapige kura..
sasa napoona kingozi wa CUF anapinga muundo huu kwa madai kwamba kila Mzazibar apewe kitambulisho hiki ina maana kwamba hata wale waishio bara watarudi visiwani kupiga kura au watapiga kura wakiwa bara sehemu wanayoishi..
na tuseme serikali ifanye kama wanavyotaka wao hao wa Bara wataonyesha vitambulisho vyao wapi maanake huko bara Wabara hawana vitambulisho vya makaazi (residential) hivyo ni utaratibu gani utatumika kwa pande zote mbili kuwezesha uandikishaji au uppigaji kura maanake waliolalamika kuhusiana na upigaji kura ni wao wakisema CCM huleta watu kutoka bara..Sasa unapompa kila Mzanzibar hata mkaazi wa nje kitambulisho hiki sii utawawezesha hata Wazanzibar wa Bara kupiga kura kote bara na visiwani!..
Tatizo kubwa naloweza kusema mimi ni huu mpangoi wa kuwa na serikali mbili (Marais wawili) wakati tunataka kuendesha mambo kama nchi yenye serikali Tatu au Moja, hatuwezi kuwa katikati wala kupanda mbegu za tungule tukitegemea tuvuna chungwa..
 
Mkandara,
Ukisoma vizuri taarifa ya CUF hapo juu wamekuwa wazi kabisa kuwa Karume anasisitiza kuwa kila Mzanzibari mwenye sifa na haki ya kupatiwa kitambulisho (ambacho ni sharti uwe nacho ndo uandikishwe katika DKWK) aende katika Idara ya Vitambulisho akapatiwe. Wanacholalamika CUF ni kuwa tokea mapema kabla ya zoezi la kuandikisha halijaanza waliitaka SMZ ihakikishe kuwa kila anaestahiki kupatiwa kitambulisho hicho apatiwe mapema na kama kuna matatizo yasawazishwe mapema ili zoezi likianza liende vizuri kwa kila mwenye haki kuandikishwa.
Matokeo yake wale wote ambao wametimia umri wa miaka 18 hivi sasa ambao ni wakaazi wa Zanzibar hawapatiwi vitambulisho hivyo kwa sababu za kisiasa. Mashea ambao ni wawakilishi wa serikali katika shehia zao wamekuwa wanawabagua wakaazi wao kwa misingi ya itikadi za kisiasa kwa kushindwa kuwapatia barua za uthibitisho wa ukaazi ili wakapatiwe vitambulisho hivyo. Msingi wa malalamiko ya CUF ni kuwa kila Mzanzibar mwenye sifa na haki ya kupatiwa kitambulisho na apatiwe ili ajiandikishi jambo ambalo SMZ wameliwekea vizingiti viiiingi kwa wapinzani.
Mkandara, binafsi masheha wa Zanzibar nawafahamu vizuri kuwa ni makada wa CCM, kwa hayo wanayofanya sishangai kabisa. Katika chaguzi zote wametumika vizuri na chama tawala kuwazuia watu wenye sura ya upinzani kuandikishwa kwa kisingizio kuwa hawawafahamu na kuruhusu mamluki kutoka bara kuandikishwa.
Leo kuna daftari la kudumu, mtu anakwenda kuandikishwa rekodi zake zipo katika daftari la awali anaambiwa huna kitambulisho na sheha hakutambuwi, akilalamika anaambiwa unataka kufanya fujo anaitiwa maafisa wa usalama, haki ipo wapi.CUF hawapigi kelele tu si mmeyaona kule Biharamulo?
 
Junius,
Mkuu wangu nimeisoma na nimeielewa vizuri isipokuwa kinachotakiwa hapa ni barua ya kuthibitisha ukaazi..Sasa tatizo kubwa ni mfumo mzima wa Utawala Bara na visiwani kwani hata barua ya makaazi hutolewa na katibu kata, serikali ya mitaa ambao mara zote ni viongozi wanachama wa chama tawala CCM. Ukienda Ofisini au majumbani mwao utaikuta bendera ya chama CCM ikipepea badala ya Bendera ya Taifa...Hivyo ubovu wa system nzima umeanzia hapo ktk shina.

Sasa tunategemea kitu gani ikiwa kitambulisho tu cha ukaazi kinatolewa na kiongozi aliyeteuliwa toka chama tawala...Nadhani hata Ujumbe wa nyumba kumi unatakiwa uwe mwana CCM ndio hayo ya Masheha wenu.
Binafsi sioni makosa ktk usemi wa Karume kwani huwezi kutoa kitambulisho kwa mtu ambaye hana barua ya kuthibitisha ukaazi wake. Kama CUF wanayo malalamiko yoyote ni muhimu kufuatilia sehemu ambazo barua hizi zimekuwa hazitoki na wahusika wafikishwe ktk sheria. Wa kuwapigia kelele hapa ni hao Masheha, wafuatwe makwao kwa maandamano na hata ujumbe wa chama CUF wakifuatana na waandishi wa habari..Kumlalamikia Karume kwa kauli yake na kumwita Mnafiki kwa sababu tu unavyotaka wewe ni kukiuka baadhi ya kanuni na utaratibu ni kutomtendea haki Karume..
Hata huku majuu huwezi kupewa Kitambulisho cha serikali ikiwa huna barua ama kitu chochote cha kuonyesha ukaazi wako. Ni hatua ya kwanza muhimu sana ktk kuhakikisha only wanopewa vitambulisho hivyo
 
Mkandara,
Nakubaliana na sehemu kubwa ya maelezo yako. Kiufupi tu ni kuwa mtego walioutega CCM unaanza hapo kwa sheha. Maana yake ni kuwa kama huna barua ya uthibitisho wa ukaazi inayotolewa na sheha, hupati kitambulisho, kwa hiyo huandikishwi katika DKWK. Hata uwende wapi ukalalamike bure tu kwakuwa anachofanya sheha ni kufuata maelekezo ya Watawala na si sheria yoyote. Unafiki wa Karume katika hili ni kuwa anatoa kauli hiyo katiaka jukwaa ambalo si la kisiasa kuwafurahisha mabalozi na wageni waalikwa katika hafla ile, tatizo lilishaelezwa kabla na kama hatu zilitakiwa zichukuliwe mapema. Utashangaa hata Waziri anaehusika Othman Nyanga amenukuliwa akiliambia BLW kuwa mpaka sasa hakuna malalamiko ya alikoseshwa kuandikishwa wala kupata kitambulisho cha ukaazi na kuwa kila mwenye sifa ataandikishwa. Huu kama si uanafiki ni kitu gani? Iwe watu wanalalamika bure bure tu bila ya sababu? Ukweli ni kuwa viongozi wetu hawana dhamira ya kweli ya kutenda haki.
 
Back
Top Bottom