Karibu kwenye njia ya mwendokasi kuelekea utajiri na mafanikio, huku ni spidi kali kama unaogopa basi shika

Apr 19, 2018
83
112
Njia ya mwendokasi ni njia spidi kali, kuingia njia hii lazima kwanza uachane na hofu, ukihofu mara nyingi utakanyaga pedali ya breki bila sababu, na spidi yako itapungua na utapitwa na kuachwa nyuma. Njia hii ina changamoto nyingi, na ndiyo maana watu wengi wanaamua kupita kwenye njia ya mguu au ile nyingine ya foleni. Ukweli ni kwamba wanaogopa “Risk” (za ukweli na nyingine feki walizomezeshwa) zinazoambatana na njia hii.​

AMRI KUU 6 ZA NJIA YA MWENDOKASI KUELEKEA UKWASI

Kila mchezo lazima uwe na hakimu au refa, marefa wa njia ya mwendokasi ni asili(nature), serikali na mfumo wa Fedha (monetary systems). Kila refa ana kanuni na sheria zake, ukizizingatia basi utakwenda umbali mrefu sana kwenye njia hii ya mwendokasi na kuongoza mashindano mara kwa mara.

Watu wanaoshindwa kuzingatia kanuni na taratibu za njia hii na hasa hasa kanuni za refa namba moja(asili a.k.a Nature) ndiyo wale unaowaona, wanaanza kwa kasi halafu baadae tunawapoteza (wanafilisika au kufulia)

Ili tusifike huko, basi ni vema tujifunze kanuni hizi 6 tutakazozitumia, wakati tunakanyaga mafuta na kuzungusha usukani, kwenye njia hii ya spidi.​

Amri #1: Kama unataka mamilioni basi achana na habari zako (umimi) kwanza, gusa maisha ya mamilioni, kisha nao watakugusa.

Kanuni ya utajiri kwenye njia ya mwendokasi ni hii;

Kiasi cha pesa = Ukubwa wa matatizo X idadi ya watu uliowatatulia matatizo hayo

Una njia mbili za kutanua uwezo wako kwenye amri hii, aidha uchague tatizo kubwa unalotaka kulitolea suluhu, kama huwezi basi uongeze idadi ya watu kwenye tatizo hilohilo dogo unalolitatua.

Kwa mfano;

Umeanzisha, duka dogo la kuuza unga wa ngano, na kwa kila kilo unapata faida ya sh. 500 tu!, lakini unatamani sana uingie kwenye njia ya mwendokasi kuulekea utajiri. Basi isiwe taabu, kwa sababu tatizo lako unalolitatua (njaa) lina faida ndogo, kwa nini usitafute njia ya mtandaoni yenye wafuasi mabilioni, ili uuze unga wako huo kwa faida hiyo hiyo ya sh. 500? ukitangaza na kuuza kwa watu milioni 1, tayari watakupatia sh. Milioni 500.

Kanuni hii, inakulazimisha mtu wa mwendokasi kutafuta au kutumia njia mbalimbali unazoweza kuzitumia, ili uguse maisha ya mamilioni ya watu. Na siyo watu wa mtaani kwako tu basi!

Bakhresa anauza unga lakini kwa mamilioni ya watu, na hata leo asubuhi inawezekana umekula mkate au andazi lililotokana na unga wa jamaa. Moh Dewji anauza maji ya kunywa kwa hiyo hiyo jelo, lakini wanakunywa mamilioni, na unajua ni mara nyingi inawezekana umekunywa maji hayo na kujaza mfuko wake.​

Amri #2: Wewe siyo muumba, haujui kila kitu

Moh Dewji hajasoma chemistry lakini anatengeneza vinywaji vinavyohitaji ujuzi wa kikemikali, Bakhresa haendeshi Malori lakini malori yake yanatuletea unga wa Azam karibu mikoa yote, Mengi hakuwa na cheti cha uandishi wa habari lakini ITV inawika mpaka leo.

Nafikiri umeanza kupata picha ya msingi huu wa pili, siyo kwamba kila kitu lazima ujue wewe hapana, kinachohitajika kwenye njia hii ya mwendokasi ni kumfahamu ni nani ana ujuzi kukuzidi katika eneo fulani na anafaa kumtumia kuendesha masuala hayo. Kazi yako ni kupata ujuzi wa awali tu, wa mambo hayo ili usije ukaingizwa king.

Unafikiri Bakhresa angejigawaje kila idara kwenye kampuni yake? Kusaga unga wa ngano yupo, kutengeneza vinywaji yupo, mawasiliano na usafirishaji yupo, kusimamia timu ya soka yupo, mahesabu na uhasibu yupo; hiki kitu kinawezekana kweli?

Lazima kama wewe kweli umedhamiria kujiunga na njia ya mwendokasi, utambue kuwa, kuna watu wengi wamekuzidi ujuzi katika maeneo mengi ya biashara yako, kwa hiyo siyo kila kitu utakifanya wewe ni lazima uwajue watu hao, na ujue jinsi ya kuwatumia kwa akili na kanuni za uongozi ili wakukamilishe.

Njia hii ya mwendokasi kuuelekea ukwasi inakuhitaji uguse maisha ya watu maelfu, mamilioni au mabilioni, bila timu ya watu sahihi kukuzunguka, huwezi kuwafikia watu wote hao kwa wakati.

Zingatia;

Tengeneza timu sahihi, yenye mtazamo sahihi ili upate matokeo sahihi.​
 
Back
Top Bottom