Karibu Jamiiforums tena — mijadala irudi, hoja zijadiliwe, Taifa lijengwe. 🇹🇿✍🏽

Karibu Jamiiforums tena — mijadala irudi, hoja zijadiliwe, Taifa lijengwe. 🇹🇿✍🏽

Manyanza

JF-Expert Member
Joined
Nov 4, 2010
Posts
19,147
Reaction score
43,076
Hongera Jamiiforums Kurudi Hewani Ushindi wa Uhuru wa Kujieleza 👏👏👏

Nawapongeza kwa dhati uongozi wa Jamiiforums kwa ujasiri, uvumilivu na ukomavu mkubwa mliouonesha katika kipindi chote ambacho mtandao huu pendwa ulifungiwa leseni ya uendeshaji. Pamoja na kupewa nafasi ya kukata rufaa, mlijitoa mhanga, mkaheshimu maamuzi ya mamlaka na mkapokea adhabu kwa ustaarabu — jambo lisilo rahisi, hasa katika tasnia ya habari na mijadala ya umma.

Ni ukweli usiofichika kwamba katika hatua hizo kulikuwepo na ukiukwaji wa baadḥi ya taratibu za usimamizi wa leseni, jambo lililoakisi namna ambavyo uhuru wa kujieleza kwenye taifa huru unaweza kukwazwa bila sababu zenye uzito wa kutosha. Hili linapaswa kuwa somo kwa wote: mawazo hayapaswi kuzimwa bali kusikilizwa, kufafanuliwa na kujadiliwa kwa misingi ya hoja.

Kwa mujibu wa taarifa za Muanzilishi, kaka Maxence Melo , Jamiiforums imeajiri zaidi ya wafanyakazi 30, wanaolipwa kuanzia Tsh milioni 1.5 hadi milioni 2 na zaidi. Hivyo kufungiwa kwa mtandao hakukuathiri tu watumiaji, bali pia maisha ya wafanyakazi, familia zao, na hata mapato ya Serikali kupitia PAYE na kodi nyingine. Huu ni ushahidi wa moja kwa moja kuwa madhara ya kuzima jukwaa moja la mjadala yanaweza kugusa watu wengi zaidi ya inavyoonekana.

Ni muhimu kukumbuka pia kuwa Jamiiforums ina zaidi ya majukwaa 32, lakini adhabu ilipoibuka kutoka kwenye kasoro ya jukwaa moja, athari zake zilamgusa kila mtumiaji na kila eneo la mjadala. Wengi walilazimika kutumia VPN kupata huduma ishara kwamba hamu, haja na umuhimu wa jukwaa hili kwa Watanzania upo juu zaidi ya vikwazo.

Ushauri kwa Mamlaka

Ni busara katika siku za usoni adhabu iwe ya kulenga eneo lenye tatizo bila kuzuia shughuli na majadiliano ya maeneo mengine yasiyo na makosa. Adhabu hurekebisha, lakini haitakiwi kuharibu tasnia nzima ya fikra.

Mwisho, Ushauri kwa Viongozi wa Serikali

Mawaziri, Wabunge, Wakuu wa Mikoa na Wilaya naombeni mjifunge mkanda na mujiunge rasmi Jamiiforums. Wekeni badge za uthibitisho (verified) ili muwasiliane moja kwa moja na wananchi, mpokee mrejesho, mijadala, hoja na changamoto halisi kutoka kwa wananchi wenyewe.

Mitandao ya kigeni haina dhamana kubwa kwetu kama tulivyo sisi wenyewe kwenye ardhi yetu. Jamiiforums ni jukwaa letu, la Watanzania, lenye mchango mkubwa katika ujenzi wa Taifa la hoja si propaganda.
 
Back
Top Bottom