Karamagi ashtuka kujiuzulu kwa Dk. Rashid

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,794
287,947
Waungwana huyu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kajiuzulu au la!? Maana bado kuna utata kuhusiana na habari hii. Ama kweli siri kali!

Karamagi ashtuka kujiuzulu kwa Dk. Rashid

na Prisca Nsemwa
Tanzania Daima

WAZIRI wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, ameeleza kushitushwa kwake na taarifa za kujiuzulu kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dk. Idris Rashid.
Amesema uamuzi wa Dk. Rashid umeishutua serikali na atakutana naye kujua kama ameufikia baada ya kupata shinikizo kutoka kwa mtu au kikundi cha watu au ni uamuzi wake mwenyewe.

Karamagi aliyasema hayo jana baada ya kufungua warsha ya wadau wa mafuta nchini iliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo la Mafuta ya Petroli (TPDC), ili kupata maoni kuhusu mkakati wa TPDC wa kuanza kuchimba mafuta ya petrol nchini kwa kufanya utafiti katika mikoa matatu.

"Uamuzi wa Dk. Rashid umenishtua, ninapanga kumuita nizungumze naye, ili nijue kama kujiuzulu kwake kumetokana na uamuzi wake binafsi au amepata shinikizo kutoka sehemu nyingine yoyote," alisisitiza Karamagi.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Dk. Rashid alitangaza kujiuzulu kutokana na kukabiliwa na upinzani mkali kwenye mkakati wa Tanesco wa kupandisha gharama za uunganishaji umeme na uniti majumbani na viwandani.

Hatua ya mwisho iliyomfanya ajiuzulu, imeelezwa kuwa ni baada ya kugongana na Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Balozi Fulgence Kazaura kuhusu uamuzi huo, ambako balozi huyo baada ya mvutano alikaririwa akimweleza Dk. Rashid kama hawezi kubadili msimamo ajiuzulu nafasi hiyo.

Hata hivyo, Tanzania Daima ilipotaka kufahamu sababu za Dk. Rashid kwa kumpigia simu, alijibu kwa ufupi; 'No Comments'. Aidha, alikanusha sababu za kujiuzulu kwake zilizoandikwa kwenye vyombo vya habari jana.

Waziri Karamagi akizungumzia suala la upandaji wa mafuta ya petroli nchini, alisema TPDC itekeleze mapendekezo ambayo Ewura iliyatoa ya kuwataka wafanyabiashara wa mafuta kuagiza kwa wingi, ili kuweza kupunguza bei.

"Wakiagiza mafuta mengi lazima bei itapungua, kwahiyo tutaweza kuyatunza na bei itakuwa ni nafuu, lakini kutokana na wafanyabiashara kuagiza mafuta kidogo, inachangia kupanda kwa bei ya petroli," alisema Karamagi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Yana Kilagane, alisema mkakati wao ukiwezeshwa ili shirika hilo liweze kutafuta mafuta kwa wingi nchini, itasaidia kupungua kwa bei ya mafuta ya petroli.

Alisema mkakati huo utakwenda sambamba na kufanya utafiti katika maeneo ambayo wanatarajia kuchimba mafuta kuwa ni sehemu za pwani, eneo lenye kina kirefu na bonde la ufa.

"Mkakati huu ukiwezeshwa bei ya mafuta inaweza kupungua kutokana na kuwepo kwa mafuta mengi, mafuta yakiwa mengi bei itapungua na uchumi utakua na nchi itaokoa fedha nyingi," alisema Kilagane.

Pia alisema mkakati huo unahitaj kuwezeshwa kwa kiasi kikubwa, na itakuwa ni vigumu kueleza ni kiasi gani ambacho kinatakiwa, hadi serikali ifikie uamuzi wa kukubali ombi hilo la kuwawezesha kutafuta mafuta.

Kilagane alisema TPDC inaiomba serikali sehemu ya pato la gesi iweze kuiachia ili itumike kuendesha shirika na kuwekeza kwenye miradi ya gesi iliyopo kwa kuwa pato lote lililokuwa likipatikana lilikuwa linakwenda serikalini.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Masoko wa TPDC, Dismas Fuko alieleza kuwa mpango wa kutumia nishati ya gesi utawawezesha Watanzania kuokoa kiasi kikubwa cha fedha wanachokitumia kununua mkaa.

"Kama gesi nayo ikipatikana kwa wingi, nchi itaokoa kiasi kikubwa kwa kuwa kila Mtanzania anatakiwa atumie nishati hii ambayo ni rahisi na inaweza kusambazwa kote nchini," alieleza Fuko.

Wadau hao kutoka mashirika na wizara mbalimbali, walitoa maoni mbalimbali ili kuuwezesha mkakati huo ambao utasaidia kupungua kwa bei ya mafuta nchini ambapo utawasilishwa katika Baraza la Mawaziri.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom