Leo, nimemuona na kumsikia Wakili Msomi mwenzangu Peter Kibatala (kupitia video clip) akizungumzia uhalali wa barua iliyotumika kufungia makanisa yanayoongozwa na Askofu Gwajima.
Kwa mujibu wa Kibatala na muktadha wa mazungumzo yake ndani ya Mahakama Kuu kule Dodoma, Kanisa lililofungiwa lilijaribu kukata rufaa juu ya uamuzi huo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa mujibu wa sheria.
Kibatala akaeleza kuwa Waziri husika ametamka kuwa barua husika, pamoja na mambo mengine, SI HALALI. Waziri amesema kuwa hakuna rufaa ya kuishughulikia kwakuwa barua ni batili na uamuzi uliobebwa humo ni batili.
Barua inayosemwa ni batili/si halali ndiyo iliyotumiwa na mamlaka za kiserikali wakiwemo polisi kutekeleza kinachobebwa na barua hiyo. Makanisa Dar es Salaam na Mbeya (penginepo sifahamu) yamefungwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi.
Tumeona na kusikia kuhusu hili. Sasa, imewezekanaje barua batili/isiyo halali kusababisha kufanyika kwa yote haya? Nani huyu aliyeghushi barua hii na kusababisha yote haya? Amefanya haya kwa faida ya nani?
Kama hivyo ndivyo, tupo kwenye tatizo kubwa. Sana! Serikali itusaidie kubaini jambo hili na kukomesha kujirudia kwa jambo kama hili.