Mimi binafsi sijauona utata unaoweza kutafsiriwa kwamba Msemakweli anatumiwa na mtu yeyote yule. Tatizo lililopo hapa ni watu kutaka kile wanachokiamini kiendelee kuwa ndiyo ukweli hata kama kuna upotoshaji katika kile wanachokiamini. Suala lililopo hapa ni kulazimisha kwamba fedha za Kagoda zilitumika katika uchaguzi uliomuweka Kikwete madarakani. Ulazimishaji huu umekatwa mbawa na taarifa za Msemakweli na kwa bahati mbaya, wale wanaoshikilia msimamo huu (pengine kwa kutojua) wanabeba ajenda za mafisadi waliohusika na wizi huo, ambao wamekuwa wakishikilia kwamba fedha hizo zilitumika kwa uchaguzi ili kukwepa mkono wa sheria dhidi yao.
Kile kinachoitwa andishi la Sanze ni maelezo aliyopatiwa Sanze na hao waliokuwa wakipanga wizi huo, lakini si lazima maelezo hayo yawe na usahihi, hasa katika mazingira ambayo sasa kuna ushahidi wa dhahiri kwamba fedha hizo, zilizoibiwa kwa kisingizio cha uchaguzi, zilihamishwa na kutumika visivyo. Kwa hiyo kukaa kimya kwa waliotajwa hakudhoofishi hoja ya Msemakweli kuhusiana na matumizi ya fedha hizo.
Watu wamekuwa kila mara wanajificha kwenye hoja dhaifu ya kutumiwa kama utetezi wa tuhuma zinazowakabili. Lakini mimi sijali mtu kutumiwa kwa kusema kitu chenye ushahidi na kitu hicho kuwa ni chenye hatari kwa maslahi ya nchi au umma. Kama Msemakweli anatumiwa katika hili, basi anatumiwa kwa kitu chenye heri na kwa hiyo wanaomtumia na yeye mwenyewe Msemakweli ni watu wa kupongezwa. Mimi kwa maoni yangu kuna ukweli katika mafichuzi ya Msemakweli na ndiyo maana sasa watu, wakiwemo watuhumiwa, wako bize kumshambulia Msemakweli badala ya kushambulia kile alichokizungumza.
Tuwe waangalifu na hoja zenye nia ya kuchochea malumbano yatakayochelewesha kuchukuliwa kwa hatua za kisheria eti tu kwa sababu hatua hizo zinaelekea kuwa-prove wrong watu wenye hoja binafsi.