......Nina hakika mwaka 2015 ndani ya vyama vya upinzani hakutakuwa na uteuzi kama tulivyozoea huko nyuma bali kutakuwa na uchaguzi. Utakuwa uchaguzi wenye ushindani mkali sana katika baadhi ya majimbo. Hata baadhi ya walio wabunge wa upinzania kwa sasa, 2015 watapingwa ndani ya vyama vyao.
Nimekutana na watu mbalimbali katika nyakati na mazungumzo tofauti tofauti wakiwa tayari wanajitambulisha kama Wabunge wa Majimbo husika kwa kipindi kijacho 2015-2020! Na mara nyingi kama si mara zote hawa "wabunge" wanajinasibu kuupata Ubunge kupitia chama kile kile. Hata wakati mwingine nakutana na watu zaidi ya watatu kwa nyakati tofauti na wote wanajitambulisha ni Wabunge watarajiwa wa eneo lieliele kupitia chama kile kile kwa kipindi kilekile 2015-2020! Unaweza kubashiri toka leo hicho chama kitakuwa na hali ngumu kiasi gani muda ukifika wa kuwapata wagombea.
Rai yangu kwa wabunge watarajiwa wanaotangaza nia kuanzia sasa wafikirie upya juu njia sahihi ya kujitambulisha. Wasijiwekee akiba ya msongo pale watakapojikuta safari yao haikuvuka hata mzingiti wa mlango! Nadhani wengi hawako sahihi pale wanapojitangaza kama vile tayari wana tiketi za kuwakilisha vyama vyao. Badala ya kusema Nitagombea Ubunge XXX 2015 kwa tiketi ya YYY Labda watakuwa sahihi zaidi wakisema Nitaomba ridhaa ya chama YYY kugombe Ubunge wa Jimbo XXX mwaka 2015. Ukilijua hili na kuliweka akilini, itakusaidia pia kujua kwamba vita yako haianzii hatua ya pili bali hatua ya kwanza. Itakupa fursa ya kujijenga mapema na kuweka mkakati wa kushinda kwanza hatua ya awali.
Vinginevyo nawatakia maandalizi mema.