JUKATA waweka wazi ushiriki wao kwenye maandamano yaliyoitishwa na Chadema

Nyakijooga

Senior Member
Dec 9, 2018
123
202
Kufuatia maandamano ya amani yaliyoitishwa na Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) yaliyopangwa kufanyika kesho January 24, 2024, Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) wamesema kuwa wanatarajia kuungana na wananchi watakaojitokeza katika maandamano hayo wakidai kuwa wameguswa hoja zilizobainishwa na waratibu.

Akizungumzia suala hilo Mkurugenzi wa JUKATA, Bob Chacha Wangwe amesema kuwa wao kama taasisi huru wana sababu za kushiriki katika maandamano hayo, ambapo amebainisha wazi kuwa hoja zinazotajwa kupelekea maandamano hayo ni kati ya mambo ambayo wamekuwa wakiyapigania.

"Sisi Jukwaa la Katiba Tanzania tukiwa kama taasisi kazi yetu kubwa ni kuhakikisha tunasimamia utekelezaji wa Katiba na maswala ya Utawala Bora, tutashiriki na tutakuwa mstari wa mbele kabisa kwenye maandamano hayo yaliyoitishwa CHADEMA na lengo ni kwamba tumeona hoja za msingi za kuandamana kwa sababu ni hoja ambazo sisi kama taasisi tumekuwa tukizipigania"amesema Bob Wangwe

Akitaja mambo hayo amesema "Kwa mfano suala la kudai Katiba Mpya ni ajenda ya muda mrefu ya JUKATA, Tume huru ya Uchaguzi na hata mimi binafsi nimetumia miaka mingi Mahakamani lakini hawajatekeleza uamuzi wa Mahakama ya Afrika kuhusiana na suala wakurugenzi."

Pia ametaja hoja nyingine ambayo inatajwa na Chadema namna inavyowagusa "Suala la ugumu wa maisha ni muhimu kwahiyo baada ya mashauriano tumekubaliana kwamba tutakuwa mstari wa mbele katika maandamano hayo ili tuweze kushiriki kwa ajili ya kuboresha mazingira yetu katika Nchi yetu"

Ili kushiriki kikamirifu katika maandamano hayo Bob Wangwe amesema kuwa tayari JUKATA imeshaiandikia barua Chadema kuwataarifu kuwa watakuwa sehemu ya maandamano hayo ya amani.

"Lazima tuhakikishe kwamba tunakuwa na sheria, Tume huru za uchaguzi, tunakuwa na Katiba mpya lakini maisha ya wananchi ambayo ni mabovu, ambapo sasa kuna suala la tatizo la umeme na mambo mengine, kwahiyo tumeona ni muhimu tushiriki" amesema Bob Wangwe

Aidha ametoa wito kwa watanzania ambao watakuwa na nafasi siku ya kesho kushiriki maandamano hayo yatakayofanyika Jijini Dar es Salaam, huku akisisitiza kuwa ushiriki wao umetokana na msukumo wa hoja hivyo amedai kuwa hata ingekuwa yameitishwa na chama chochote au taasisi yoyote wangeshiriki.

"Tunashiriki kama taasisi huru ambayo imevutwa na mambo ambayo sisi tumekuwa tukiyapigania wakati wote, hata kama wangeitisha CCM kwenye hoja ambazo tumekuwa tukizipigania tungejitokeza na kuwa msatari wa mbele" amesema Bob Wangwe

Sent from my Infinix X665 using JamiiForums mobile app
 
Bob Chacha Wangwe ni mwanachadema, anatarajia kugombea ubunge kwa tiketi ya chadema Tarime mjini, ndio maana katiba itakuwa ngumu kuipata kwa kuwa hivi vitaasisi vya kijamii havina maslahi ya umma
 
Back
Top Bottom