Je Mnafahamu ya Kwamba John Mashaka anasukumwa na Mafisadi?? Hbari ndo hiyo......
Soma Hotuba yake
HOTUBA YA JOHN MASHAKA KATIKA
VIWANJA VYA BIAFRA, KINONDONI
Mheshimiwa Profesa David Mwakyusa, Waziri wa Afya na ustawi wa Jamii, wadhamini wetu kampuni ya zain, clouds FM na Business Times, wageni waalikwa na watanzania wenzangu.
shukrani za dhati kwa kuukubali huu mwaliko, na kujumika nasi wa siku ya leo kujikumbushia maswala muhimu kuhusu taifa letu hasa maswaa ya haki na usawa. Huu ni uzalendo wa aina yake, ni uzalendo unaotukumbushia uhuru wetu wa mwaka 1961, nchi hii iliposaini hati ya makabidhiano ya uhuru,
Hati ya mwaka 61 iliikabidhi nchi yetu haki yake ya msingi, haki ya maamuzi yaliyo mhakikishia kila raia maisha bora, na usawa. Hati hiyo ya mwaka 1961, ilitoa matumaini kwa kila mmoja. Raia wa Tanzania, walihaidiwa maendeleo makubwa.Watanzana hawakuahidiwa haya yanayojitokeza kwa sasa ; hawakuhaidiwa ahadi zisizotekelezeka, Walipewa ahadi za dhati za kukabiliana na maradhi, ahadi za kuondokana na umasikini na ujinga. Watanzania walipewa ahadi za haki, bila kujali matabaka, walihaidiwa usalama kwa raia wote.
Ahadi za mwaka 1961 hazikuwa za kuleta ufisadi kama huu tunao ushuhudia sasa. Hati ya Uhuru ilikuwa ni ya manufaa kwa raia wote. Kwa hakika katika miaka 48 ya uhuru wetu, yapo mambo kadhaa ya kujivunia.
Kuna mabadiliko makubwa hasa katika jiji la Dar es Salaam na hata kwingineko Ambako Kuna majengo marefu, mazuri ya kisasa, yanayoelekea mawinguni. Miaka 48 imeleta mabadiliko ya kijamii, kuna matabaka ya wasomi wenye maisha ya juu. Kuna makundi ya watawala na wenye mamlaka; Kuna kundi la matajiri wanaoshi katika sayari tofauti na watanzania walio wengi.
Watanzania wenzangu, wakati wapo wenye maisha mazuri, wanaoishi katika raha na utukufu, wapo pia wengi ambao wana maisha ya dhiki, wapo mamillioni wanaoshi katika ukiwa. Wapo wengi wanaoishi kwa kubahatisha na kwa kukata tamaa; wale ambao hawaoni faida waliyoitegemea kutokana na kupatikana kwa uhuru wao. Wapo maalbino wanaoishi kwa ukiwa na wasiwasi mkubwa.
Umbali mfupi tu kutoka hapa tulipo wapo wenzetu ambao wanaishi kwa hofu; wanaume kwa wanawake walio na wasiwasi, siyo tu juu ya maisha yao wenyewe, bali maisha ya umbele ya kiafya, na kielimu kwa watoto wao.Hawa ni raia wenye hofu kuhusu usalama wao. Ni raia wenye hofu jinsi watakavyowalisha watoto wao.Ni raia wenye wasiwasi ni jinsi gani watawasomesha watoto wao, siyo katika shule za ng'ambo bali katika shule za humu nchini. Hawa ni raia wenye hofu ya kupata hata mmlo mmoja kwa familia zao nahuu ndio ukweli wa mambo; Ni ukweli unaouma.
Ukweli wa mambo wenye machungu,haupo mbali nasi, ukweli huu upo manzese, upo kigogo na kule Temeke. Hali mbaya zaidi ya ukweli huu upo pale msimbazi center ambapo vitoto vichanga vya miezi mitatu vinaishi kwa uwezo wa mwenyezi Mungu ili hali nchi yao inayo uwezo wa kuwapa maisha yenye uhakika. Ukweli unaosononesha tunao hapa kati yetu, ambapo maelfu ya vijana hawana ajira, ni wachovu katika lindi la ufukara. Ukweli huu unaoumiza tunauona kwa vijana wetu ambao, licha ya kuwa wamesoma vya kutosha, wanabakia wakichuuza maji ya kunywa ili kujikidhi kimaisha.
Wengine wanaamua kuchukua silaha na kufikia hatua ya kuyachukua maisha ya wengine ili kujipatia riziki. Huu dio ukweli wa mambo; ni ukweli unaouma.
Natumia nafasi hii kuwasihi wale wote wanaochota raslimali za inchi hii; Wale wote ambao wanahamisha mamilioni ya pesa za walipa kodi na kuyapeleka katika akaunti nje ya nchi, Nawasihi wale wote wenye roho za kifisadi kufikiria mara mbili juu ya maadili na vitendo vyao.
Nawasihi hawa waliopewa dhamani ya kuilinda hii nchi kuvitembelea vyuo vyetu, na tasisi nyingine za elimu ili kuangalia hali halisi ya mahitaji katika taasisi hizo. Nawasihi viongozi wetu kwenda katika vituo vya mabasi, na masokoni na kuwaona vijana na watoto wadogo waliolemewa na ufukara, wanaolala kwenye mabaraza ya majumba na kwenye magenge kwa sababu hawana makazi. Nawasihi viongozi wetu kutega masikio yao ili kuwasikia, vijana wenye majonzi makubwa , vijana wanozishuhudia ndoto zao za kielimu zikitokomea kutokana na ufukara mkubwa walionao wazazi wao.
Siku ya leo ndugu zangu, tunawaomba viongozi wetu wavisikie sauti za ndugu zetu wanaowindwa kutokana na uumbaji wa Mwenyezi mungu. Tunawaomba wazisikie sauti za ndugu zetu maalbino wanaoishi kwa uwoga na ukiwa . Tunaomba walindwe, na kupewa haki zao za kimsingi, na za Usalama. Hii siyo tu kwao maalbino, bali kwao watanzania wote wanaotikiswa na wimbi la ujambazi. Hii siyo hati nchi yetu ilisaini kwa ajili ya raia wake, Hii ni hundi batili MAFISADI wa kimaadili wanawalazimisha raia wema kuvichukua.
Tunawasihi viongozi wetu waondoke nje ya ofisi zao ili watafute muhafaka kwa kushirikiana na wananchi wengine juu ya ulinzi wa watoto albino wasio na hatia. Ninawasihi, msikie kilio cha yule Albino, binti wa miaka 10 ambaye hawezi kukilalia kitanda kimoja kila siku kwa sababu tu anawindwa na watu wenye tamaa na imani potofu. Huu ndiyo ukweli wa mambo, ukweli wa miaka 48 ya uhuru wetu!
Ni ukweli unaouma !
"Miezi michache iliyopita nilighafirika kwamba kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa Kimarekani niliyeongea naye, aliweza kuikumbuka Tanzania kwa mauaji ya albino badala ya mambo mengine mengi mazuri tu yanayoihusu Tanzania".Jambo hili ni la kifedheha! Huu ni umaskini wa kifikra na UFISADI wa kimaadili ambao umetukumba sisi watanzania. Kumuwinda binadamu kutokana na umbile lake siyo utanzania, huu ni ushetani.
Tusiitegemee serikali kuwa na miujiza ya kusuluhisha kila tatizo letu la kijamii na kiusalama. Tatizo hili lipo mikononi mwetu. Sisi raia ndio wenye nguvu na uwezo wa kutokomeza haya mauaji ya kinyama. ni lazima tushirikiane ili kuzuia jambo hili la kiovu. Watanzania wenzangu, wakati wapo wenzetu wanaume kwa wanawake chini ya bahari, angani na kwingineko wakifanya utafiti na shughuli zenye hatari kubwa kwa manufaa yetu, nchini kwetu, wengine wanatafiti namna ya kuwaua maalbino wasiokuwa na hatia. Tuwalindeni maalbino, tuwasaidieni tunapoweza.
Ndugu zangu, tusipojitizama vizuri, basi tunakokwenda ni giza kubwa na majonzi yasiyokuwa na kipimo kwa sababu binadamu ambaye hawezi kuyathamini maisha hana zaidi ya kuthamini.
Tumeumbwa tulindane, si kuwindana.
Tumeumbwa kuwa watumishi, siyo watumikiwa,
Tumeumbwa kuwatendea haki wanyonge, siyo kuwanyanyasa,
Tumeumbwa kujitolea kwa hali na mali kwa manufaa ya wengine.
Hiyo ndiyo maana halisi ya maadili, Hiyo ndiyo maana ya uongozi!
Mwanafalsafa wa Kimarekani , Edmund Burk, alipata kusema kwamba, " tofauti kubwa kati ya kiongozi wa dhati na yule ajifanyaye kuwa kiongozi ni kwamba; kiongozi wa dhati uangalia mbele, wakati yule bandia uangalia ya leo. Kiongozi bandia anaishi kwa ajili ya leo na anatenda udanganyifu, wakati mwenzake anavumilia machungu ili kuyalinda madili na kutizama maisha ya baadae".
Viongozi wanaoipenda hii nchi, badala ya kutafuta utajiri wa kitambo, tunawaomba muangalie ni wapi tunaelekea. Tunawaomba mtafakari mustakabali wa nchi na maisha ya mbeleni ya vijukuu vyenu ambavyo havitahitaji mabillioni ya fedha ya wizi iliyolimbikizwa nchi za nje. Bali mazingira mazuri ya kuishi yenye amani .
Ndugu zangu, muda hauna uhadilifu wala subira. Muda hauwezi kubadilisha au kutatua matatizo yetu, Muda hauwezi kuponya vindonda vilivyosababishwa na umasikini. Muda hauwezi kuyarudisha maisha yaliyopotezwa kutokana na tamaa na ulafi wetu. Muda haupo upande wetu, wala maneno matupu hayawezi kuponya maumivu.Muda hauwezi kutuondoa katika masumbuko yetu, bali unaweza kutuacha ili tuendelee kuumia.
Wakati umefika tujitoe mhanga ili kuleta mabadiliko na kuondokana na maumivu yanayotukabili. Wapo wengi ambao wamekuwa wakihoji haya ninayoyafanya katika jamii, wengine wamekuwa wakidhania kwamba nina malengo ya kisiasa !
Ninachoweza kusema ni kwamba mtu yeyote mwenye hutu ambaye analiona wingu la umasikini uliotanda katika taifa letu, anayo jukumu la kimaadili kutoa mchango wake ili kuondoa kukata tamaa kunakowakabili mamilioni ya wanachi wetu, dhamira hii ipo juu ya dhamira nyepesi za kisiasa.
Ninalilipa deni langu kwa jamii yangu. Nalipa fadhila kwa mwenyezi Mungu. Haraka iliyopo katika hitaji la kuwasaidia ndugu zetu wenye matatizo, ni ya kasi zaidi kuliko haraka ya kukimbilia madaraka ya kisiasa. Hitaji la kumsaidia mtoto mwenye kulala na njaa ni kubwa kuliko tamaa za madaraka ya kawaida ya kisiasa.
Kimsingi huo ndio mvuto mkubwa ambao umekuwa ukiusumbua nafsi yangu kwa muda mrefu. Ninachokifanya ni sehemu tu ya utashi wa kiroho ambao umenifunulia wajibu wangu, na jukumu langu kama binadamu mwingine anayetambua kati ya wema na uovu. Huu ni utashi ulionipa changamoto ya kujitazama upya katika taswira ya maadili. Ni utashi unaotusihi wote kujitolea mhanga kwa ajili ya amani katika taifa letu.
Kila mmoja ana ndoto ya kuishi maisha yenye furaha. Wote mliopo hapa mmekuja kwa sababu mnaamini kwamba tunalindwa na bendera moja, na kutumikiwa na rais mmoja. Hivyo, nawasihi mrudi majumbani kwenu na ujumbe mmoja kwamba, maisha yenye matumaini ni muhimu kuliko maisha ya kukata tamaa.
Ni lazima wote tufahamu kwamba upendo ni muhimu kuliko chuki. Lazima mtambue kwamba ushirikiano ni muhimu kuliko utengano. Hizi ni tunu ambazo tunatakiwa kuzilinda; Ni lazima tuwe sehemu ya mabadiliko kueleka katika maendeleo chanya.
Kufika kwenu hapa leo imekuwa kama chanzo cha uharakati wa watanzania, uharakati wa kijamii ya kuwalinda wenye ulemeavu, wenye ukoma, na wasioona. Ni uharakati wa kuwavalisha wanaotembea uchi. Ni uharakati wa kuwalisha wanaoshinda njaa. Ni uharakati wa kuwalinda maalbino wanaoishi kwa wasiwasi na ukiwa
Ni uharakati na maendeleo ambayo yamevuka mipaka ya siasa, dini, hata asili za watu. Ni maendelao yaliyovuka ubaguzi wa rangi, matabaka, na hata kasumba. Ni maendeleo yanayowakutanisha Watanzania wote. Huu ni uharakati na mchakato wa masikini na matajiri. Mchakato wa wenye madaraka na wanyonge, Ni mchakato kuhakikisha kwamba MAFISADI na masikini wanapewa haki sawa mbele ya sheria.
Ni mchakato na uharakati wa kuleta upendo kwa kila mwanadamu. Ni mchakatona ambao umedhamiria kurudisha yale matumaini ambayo watu walikuwa nayo mwaka 1961 wakati nchi yetu ilipopata uhuru. Uharakati wa kuondokana na magonjwa, ujinga, na umasikini. Uharakati wa kuhakikisha usalama kwa kila raia. Uharakati wa kukomeza Ufisadi.
Haya ni mapambano ya kuwalinda watu wote bila kuwabagua,
Ni mapambano ya kuwalinda maalbino.
Ni mapambano yaliyaonza mwaka 1961;
Ni mapambano yenye manufaa kwa kila mmoja wetu.
Mungu Ibariki Tanzania