SIKU chache baada ya Mbunge wa Maswa Magharibi, mkoani Simiyu, Bw. John Shibuda (CHADEMA), kudaiwa kukisaliti chama hicho na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa kurudi katika Bunge Maalumu la Katiba ambalo linaendelea na vikao vyake Mjini Dodoma, mbunge huyo ameibuka na kutangaza rasmi kuachana na chama hicho
Alisema tangu amejiunga na CHADEMA, amekuwa akitukanwa, kuitwa masaliti na kunyimwa ushirikiano kutoka uongozi wa juu katika chama hicho ili kuchochea maendeleo na wananchi wake.
"Mimi si mkokoteni na siwezi nikaota juu ya maamuzi ya UKAWA ambayo wamekuwa wakiyajadili katika vikao vya maridhiano, wajumbe wengine wamekuwa wakipewa taarifa kila siku juu ya kinachoendelea hadi sasa lakini mimi nabaguliwa kwa nini," alihoji Bw. Shibuda.
"Siko tayari kupelekwa na chama chochote cha siasa nchini wala viongozi wake, nitaenda bungeni wiki hii kuendelea na vikao ili niweze kuwatetea wakulima wangu wa pamba na wafugaji ambao ni maskini sana," alisema.
"Viongozi wa CHADEMA ni wababe, hawana hekima wala busara, wanataka kuendesha chama watakavyo kama cha kwao lakini mimi nimekataa, nataka niwaambie kuwa, waliposikia nimetoka CCM, wao ndiyo walinifuata nijiunge na chama chao," alisema.
Bw. Shibuda alidai kukerwa na Mwanasheria wa chama hicho ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Bw. Tundu Lissu, akidai amekuwa akimuandama bila ya sababu na kumtaka aache mara moja.
"Amenituhumu mambo mengi na mimi nimemvumilia vya kutosha na sasa, ndani ya siku chache nikirudi Dar es Salaam tutaonana maana siwezi kutukanwa na mtoto mdogo kama Lissu," alisema.
Source: Gazeti la majira