BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,376
- 8,120
Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi kwa kipindi cha Februari 2022 hadi Februari 2023 iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma Ijumaa Februari 3, 2023 ilieleza kuwa vijana 147 kati ya 67,299 waliojiunga JKT kwa mujibu wa sheria walikutwa na maambukizi ya VVU.
Takwimu hizo ni sawa na asilimia 0.22 ya vijana waliomaliza kidato cha sita nchini na ambao waliitwa kujiunga na JKT katika kipindi cha miaka ya 2019, 2020 na 2021.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Februari 6, 2023, mkuu wa tawi la utawala wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema taarifa zilizotolewa na kamati ni sahihi lakini wamesikitishwa kutumika picha ambazo sio za wahusika.
Amesema picha hizo zimeleta taharuki kwa familia za vijana wanaopatiwa mafunzo kwamba wameathirika na maambukizi ya VVU.
“Vijana ambao hukutwa na changamoto ya kiafya hufanya mafunzo yao chini ya uangalizi wa wakufunzi ili kuhakikisha wanamaliza mafunzo yao salama,” amesema.
Amesema JKT inaamini kitendo hicho ni cha udhalilishaji wa utu wa binadamu kwa kutumia picha za vijana wasiohusika.
“Huo ni ukosefu wa maadili ya uandishi wa habari na uhuru wa vyombo haukutumika ipasavyo. JKT inavitaka vyombo vyote vya habari na mitandao ya kijamii kuomba radhi na kuondoa picha hiyo mara moja,” amesema mkuu huyo wa tawi la utawala JKT.
MWANANCHI