JK: Madai ya walimu hayalipiki | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

JK: Madai ya walimu hayalipiki

Discussion in 'Jukwaa la Sheria (The Law Forum)' started by MziziMkavu, Aug 3, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Aug 3, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,613
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  Rais Jakaya Kikwete akizungumza na wahiriri na waandishi wa vyombo vya habari nchini Ikulu jijini Dar es Salaam jana.


  Wakati mgomo wa walimu ukiendelea, Rais Jakaya Kikwete, amesema kuwa madai yao wanayoidai Serikali hayalipiki.

  Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari Ikulu, Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema kuwa madai hayo kwa sasa hayatekelezeki na kuwaomba walimu kukaa katika mazungumzo na serikali ili kufikia mwafaka.

  Alisema kuwa madai ya nyongeza ya mshahara kwa asilimia 100, posho ya kufundisha kwa walimu wa sayansi ya asilimia 55, asilimia 50 walimu wa sanaa na posho ya mazingira magumu ya asilimia 30 ya mshahara itafikisha fungu la mshahara kwa watumishi wa umma kuwa Sh. trilioni 6.874 kati ya mapato yote ya ndani ya serikali ya Sh trilioni 8.

  "Si haki kulipa watumishi wa umma 500,000 kulipwa fedha hizo zote na kubakia na trlioni mbili tu. Hii inaweza kuleta mgogoro wa wananchi. Kuna watu milioni 43, nao watahoji," alisema Rais Kikwete.

  Alisema hata kama wakilipwa mishahara hiyo hawatakuwa na kazi ya kufanya kwa sababu hakutakuwa na fedha za kugharimia mambo mengine.

  “Madai haya ni magumu kuyatekeleza... sioni uwezekano huo,” alisisitiza Rais Kikwete.
  Hata hivyo, alisema serikali inatambua mchango wa walimu pamoja na mawazo yao katika kuwalea na kuwafundisha watoto, hivyo aliwaomba wakae katika mazungumzo na serikali kutatua mgogoro huo.

  CWT YAJA JUU

  Wakati Rais Kikwete akitoa msimamo huo, Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kimelaani kitendo cha kukamatwa kwa baadhi ya walimu na viongozi wa chama hicho na serikali kuingilia uhuru wa Mahakama kwa kudai kuwa mgomo wao unaoendelea kote nchini ni batili.

  Akizungumza na Waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Rais wa CWT, Gratian Mukoba, alisema chama hicho kimepokea kwa masikitiko kukamatwa kwa baadhi ya walimu na viongozi wake katika wilaya za Tarime, Rungwe, Kyela, Babati na mikoa ya Pwani, Morogoro na Ruvuma.

  Alisema katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa, Mecki Sadiki amewatishia wanachama na viongozi wao kwa kuamuru wakamatwe na kuidanganya jumuiya ya Watanzania kwa kuwaambia kuwa kiongozi wa CWT amewatangazia walimu wagome wakati yeye alikwenda kusaini kazini kwake na kuondoka.
  Alisema kitendo alichokifanya mkuu huyo wa mkoa ni kitu cha uzushi.

  Aidha, Mkoba alisema mgomo wa walimu ni halali tofauti na serikali ilivyodai kupitia Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, aliyedai kuwa ni batili na kuitaka serikali kuacha kuingilia uhuru wa Mahakama.

  Ametoa wito kwa walimu waendelea kubakia majumbani badala ya kwenda shuleni kwa kuwa wanasingiziwa kuwa wanawashinikiza wanafunzi kuandamana na kuitaka serikali kuwaachia huru walimu na viongozi wao waliokamatwa na kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya kuacha kutumia madaraka yao kuwatisha.

  Alisema serikali ikiwa sikivu chama hicho kiko tayari kukaa nayo meza moja ikiwa itakuwa na mapendekezo yenye tija badala ya kutoa vitisho kwa kutumia vyombo vya dola.

  MGOMO WAZIDI KUSHIKA KASI

  Mgomo wa walimu umeendelea kushika kasi kufuatia mahudhurio ya walimu kupungua.

  MANISPAA YA ILALA

  Walimu katika Manispaa ya Ilala, mkoani Dar es Salaam jana walikutwa katika vikundi wakiwa wamepumzika na wengine kutokuwepo kabisa katika sehemu zao za kazi.

  Katika Shule ya Msingi Ilala, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Esther Kyomo na wakaguzi wa elimu waliofika shuleni hapo kwa ajili ya kutathmini hali ya mgomo huo, Fredrick Mtaita, Odeta Sezary, Elizabeth Malembeki, walisema walimu walikuwepo na wanaendelea kufundisha.

  Katika Shule ya Msingi Hekima, iliyopo Buguruni, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Adelphina Matia, alisema baadhi ya walimu walifika shuleni hapo mapema asubuhi na kuondoka baada ya kusaini na kwamba kati ya walimu 70, walimu 34 ndiyo waliosaini.

  Aliongeza kuwa kutokuwepo kwa walimu shuleni hapo kumeathiri ufundishaji na kwamba wanapata shida kwani wanafunzi wamekuwa wakizagaa hovyo.

  Godrick Ruta, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mtakuja iliyopo Vingunguti, alisema hali shuleni hapo ni ya mkanganyiko kwani kuna walimu ambao wanafundisha na wengine wamekuwa wakifika shuleni na kusaini,bila ya kuingia darasani.

  Alisema mahudhurio ya walimu, yalipungua jana kutoka walimu 53 na kufikia 36, baada ya viongozi CWT kufika shuleni juzi na kuwashawishi walimu kurudi nyumbani.

  Kwa upande wa Shule ya Msingi Kombo, Mwalimu Mkuu Msaidizi, Joel Barua, alisema walimu shuleni hapo wanafika, lakini hawaingii madarasani.

  MANISPAA YA TEMEKE

  Katika Manispaa ya Temeke, NIPAHE lilishuhudia baadhi ya shule za msingi na sekondari walimu wake wakiendelea na mgomo.

  Shule ya Msingi Yombo Vituka, walimu waliendelea na mgomo ambapo baadhi yao walifika katika sehemu zao za kazi wakasaini kisha kuondoka na wengine kutokufika kabisa.

  Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Otmari Ngakwira, alisema mgomo unaendelea, lakini walimu wa darasa la kwanza, pili na saba wanaendelea kufundisha.

  Alisema, shule hiyo ina walimu 67, lakini waliofika shuleni hapo kwa siku ya jana ni 45 tu.
  Aidha NIPASHE lilishuhudia ofisi ya walimu shuleni hapo ikiwa wazi pasipo kuwepo na mwalimu yoyote, tofauti na kabla ya mgomo.

  Shule ya Msingi Ukombozi, Mwakilishi wa CWT ambaye pia ni Mwalimu wa Shule hiyo, Fatuma Kabika, alithibitisha kuwepo kwa mgomo huo.

  Katika Shule ya Sekondari Barabara ya Mwinyi, NIPASHE lilishuhudia walimu wakiwa wamekaa ofisini pasipo kufanya kazi yoyote.

  KINONDONI WANAFUNZI WAANDAMANA

  Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mchangani katika Manispaa ya Kinondoni, wliandamana hadi kwa ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni wakilalamikia kitendo cha walimu wao kutoingia madarasani kuwafundisha kwa siku tatu mfululizo.

  Wakizungumza na NIPASHE nje ya ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo, walisema walimu wao wamekuwa wakifika shuleni hapo na baada ya kusaini kwenye daftari la mahudhurio huondoka huku wakiwaagiza wafundishane wao kwa wao kwani wao hawawezi kufundisha kwa vile mgomo huo ni wa nchi nzima.

  Akizungumza na NIPASHE, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, alisema wanafunzi kulalamikia elimu ni haki yao ambapo aliwatahadharisha walimu wanaowachochea wanafunzi kutoandamana akisema wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria.

  Kuhusu taarifa za walimu kusaini kwenye daftari la mahudhurio na kuondoka, Rugimbana alisema kuwa hiyo haijalishi bali kitakachoangaliwa ni jinsi gani walimu hao waliweza kutekeleza majukumu waliyokuwa wanapewa na wakuu wao wa shule na majina yaliyoingizwa kwenye fomu ambazo zimesambazwa kwa kila shule kabla ya mgomo kuanza kubaini idadi ya walimu waliogoma na ambao hawakuhusika na mgomo huo.

  Rugimbana, alisema shule zilizoshiriki mgomo zimepungua kutoka 65 hadi kufikia kati ya 50 na 55 kati ya 138 ambayo ni idadi kamili ya shule za msingi wilayani humo ambapo kwa upande wa shule za sekondari zimepungua kutoka 11 hadi tano kati ya 46.

  Katika baadhi ya shule za msingi na sekondari katika Manispaa ya Kinondoni bado hali ni tete.
  NIPASHE ilitembelea shule ya sekondari Kambangwa na kukuta wanafunzi wakicheza wakidai walimu hawajaingia madarasani tangu asubuhi.

  Mohamed Mohamed, mwanafunzi wa shule hiyo alisema anaiomba serikali iwalipe walimu madai yao kwa kuwa wanakosa haki ya msingi ya kufundishwa.

  Naye Kisa Daniel wa Shule ya Msingi Msisiri, alisema wanaumia kuona walimu wao hawaingii madarasani wanachukua jukumu la kucheza nje.

  Nao wanafunzi wa shule ya Msingi Kinondoni darasa la saba walionekana wakiwa wanafundishana darasani huku wakidai baadhi ya walimu walifika asubuhi na kuondoka.

  MKURUGENZI TEMEKE AZUNGUMZA

  Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Photidas Kagimbo, alisema kuwa mgomo katika manispaa hiyo umepungua.

  Kwa mujibu wa Photidas, kati ya shule za sekondari 40 ambazo zimekumbwa na mgomo ni Shule ya Sekondari ya Mwinyi, Kibugumo, Malela, Mikwambe, Tungi, Wailes na Minazini.

  Aliongeza kuwa, walimu 1, 252 kati ya 3, 763 wa shule za sekondari 181 kati ya 1276 wa shule za msingi katika manispaa hiyo mpaka juzi hawakuonekana maeneo yao ya kazi bila taarifa au sababu maalumu.

  MBEYA WALAANI WALIMU KUKAMATWA

  CWT Mkoa wa Mbeya kimedai kuwa walimu viongozi wake wa wilaya waliokamatwa na kufikishwa mahakamani hawana kosa lolote na kuwa kukamatwa kwao kunatokana na shinikizo kutoka juu Serikalini.

  Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Mbeya, Nelusingwe Kajuni, alisema viongozi waliokamatwa walikuwa hawapiti shuleni kushawishi walimu wagome, isipokuwa walikuwa wakifanya tathmini ya kujua walimu wangapi wameitikia mgomo huo.

  Alisema kuwa baada ya kuona viongozi wake wa wilaya wamekamatwa, CWT imepeleka malalamiko kwa Mkuu wa Mkoa na kumweleza kuwa hatua hiyo inayochukuliwa na Serikali kupitia Jeshi la Polisi haiwezi kuwa suluhisho la kumaliza mgomo wa walimu.

  Alisema kuwa kwa vile viongozi hao walikamatwa wakati wakitekeleza majukumu ya chama, CWT itawawekea mawakili wa kuwatetea mahakamani ili kuhakikisha kuwa wanatendewa haki.

  TANGA WALIMU WATISHWA

  Wakuu wa wilaya za Mkoa wa Tanga pamoja na wakurugenzi wa halmashauri zao wametajwa kuhusika na utoaji wa vitisho kwa walimu huku baadhi wakiwataka kujaza fomu iwapo wataendelea na mgomo ili watetee vibarua vyao au la.

  Hayo yalibainishwa jana na Katibu wa CWT mkoa wa Tanga, Ndelamio Mangesho, alisema viongozi hao wamekuwa wakitoa vitisho hivyo kwa kuwatumia waratibu wa wa elimu na maafisa elimu.

  Mangesho alisema hatua hiyo haina tija kwani viongozi hao walipaswa kuzungumza na chama cha walimu badala ya kutoa vitisho kwa walimu kwani ndicho kilichoitisha mgomo huo.

  WALIMU WATISHIWA KUTOSHIRIKI SENSA

  Katika hatua nyingine, CWT, mkoa wa Kilimanjaro, kimemlalamikia Mkuu wa wilaya ya Hai, Novatus Makunga, kwa kutoa kauli za kuwatisha walimu waliogoma kuwa hawatashiriki zoezi la sensa ya watu na makazi kama walivyokuwa wameomba awali.

  Malalamiko hayo yalitolewa na Katibu wa CWT mkoa wa Kilimanjaro, Nathanael Mwandete, na kusema kitendo cha Makunga kuhusisha sensa na mgomo wa walimu ambao upo kisheria si cha kiungwana.

  Hata hivyo, Makunga alipoulizwa, alisema kauli hizo ni za kizushi na hazina ukweli wowote, kwani hajawahi kukutana na kundi lolote la walimu tangu kuanza kwa mgomo huo.

  ASKOFU ATETEA WALIMU

  Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza Mhashamu Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi, amesema hatua ya serikali kukwepa kushughulikia madai ya walimu ni sawa na kuchochea bomu ambalo likilipuka madhara yake ni makubwa katika siku za usoni.

  Askofu Ruwa'ichi alitoa kauli hiyo Jijini hapa jana baada ya kumaliza ibada ya Misa takatifu ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya shule ya Msingi Nyakahoja inayomilikiwa na Kanisa Katoliki.

  Alisema kwamba serikali haipaswi kufanya ujanja ujanja wa aina yoyote katika kushughulikia mgomo wa walimu unaoendelea kote nchini isipokuwa kwa kutambua kuwa madai ya walimu ni ya msingi.

  Kinyume chake alisema kwamba Tanzania ijiandae kuwa taifa la wajinga ambalo halitathaminika kokote duniani kutokana na kushindwa kutoa kipaumbele katika elimu.

  MWALIMU MKUU MBARONI

  Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mtoro iliyopo Kata ya Turwa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Esther Magesa anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwachochea wanafunzi wake kufanya maandamano baada ya walimu wao kugoma.

  Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele, alisema kuwa mwalimu huyo alitiwa mbaroni juzi kwa kuchochea wanafunzi kufanya maandamano hayo yasiyo halali hadi ofisini kwake kabla ya kuzimwa na polisi na kusababisha uvunjivu wa amani katika mji wa Tarime na vitongoji vyake likiwemo eneo la Bomani lenye Ofisi za Serikali.

  Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya, Justus Kamugisha amethibitisha kukamatwa kwa Mwalimu huyo kwa kuwachochea wanafunzi hao.

  MRATIBU ORES ATAHADHARISHA

  Naye Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la ORES Tanzania, Dk. Herman Mayunga linalojishughulisha na malezi ya watoto yatima na kuwajengea uwezo watoto wanaosoma, ameitahadharisha Serikali kutatua mgogoro baina yake na walimu ili kuepuka kuwa na kizazi cha malalamiko na maandamano wakati wa kudai haki.

  Mayunga, alisema mgogoro huo ukiachwa uendelee, taifa litakuja kuwa na kizazi cha aina hiyo kwa sababu watoto mara zote wanajifunza kutoka kwa wazazi wao, hivyo kitendo wanafunzi kuandamana baada ya walimu wao kugoma kitawajengea imani kuwa ni njia ya sahihi ya kudai haki zao na si vinginevyo.

  Imeandaliwa na Gwamaka Alipipi, Ninaeli Masaki, Enles Mbegalo, Samson Fridolin, Zainabu Ngambila, Jimmy Mfuru, Raphael Kibiriti, Isaya Kisimbilu Dar; Emmanuel Lengwa, Mbeya; Lulu George,Tanga; Salome Kitomari, Moshi; George Ramadha, Mwanza; Samson Chacha, Tarime na Nathan Mtega Songea.


  CHANZO: NIPASHE

   
Loading...