RAIS Jakaya Kikwete anatarajiwa kutangaza wakuu wa mikoa wapya wakati wowote kuanzia leo, Mwananchi Jumapili limedokezwa. Habari zilizopatikana kutoka serikalini zinaeleza kuwa orodha ya wakuu hao imeshaandaliwa na kwamba idadi ya wakuu wa mikoa wanawake imeongezeka ikilinganisha na ya sasa.
Kuna ma DC (wakuu wa wilaya)vijana ambao wamefanya vizuri katika wilaya zao wamepata promosheni (wamepandishwa) kuwa wakuu wa mikoa. Pia kuna ma RC (wakuu wa mikoa) wamepumzishwa kwa sababu ya umri, kilisema chanzo chetu. Baadhi ya wakuu wa mikoa waliotajwa kurudi ni Kanali mstaafu James Simbakali (Kigoma), Kanali Mstaafu Enos Mfuru(Mara), Kanali mstaafu Anatoly Tarimo(Mtwara) na Said Meki Sadiki (Lindi) ambaye kwa sasa anakaimu nafasi hiyo mkoani Dar es Salaam.
Baadhi ya Ma DC wanaotajwa kupata ukuu wa mkoa ni Chiku Galawa ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam na DC wa Lushoto. Chanzo hicho kimemtaja Hilda Ngowe, Injinia Stella Manyanya, ambaye ni mbunge wa viti maalumu, pamoja na Mary Chatanda ambaye ni mbunge viti maalumu na Katibu wa CCM mkoani Arusha kuwa ni miongoni mwa wakuu wa mikoa wapya.
Wengine ni Mary Mwajelwa, Mwaka Abdulham Ramadhan, Dk Charles Chizeba ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Buchosa mkoani Mwanza na Dk Batilda Buriani ambaye alikuwa Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais(Mazingira) katika baraza la mawaziri lililopita. Akiwa katika kampeni za urais, Rais Kikwete aliahidi kuteua wakuu wa mikoa katika mikoa mipya mapema kabla ya kuanza mwaka mpya.
Novemba 24, mwaka huu Rais Kikwete aliteua baraza lake jipya la mawaziri na kubadilisha muundo wa wizara zake. Tangu Rais Kikwete aingie madarakani mwezi Desemba 2005, inakuwa ni mara yake ya pili kufanya uteuzi wa wakuu hao huku akiwa amewafanyia mabadiliko mara moja tu. Kwa mara ya kwanza, Februari 11, 2006 Rais Kikwete aliwaapisha wakuu 21 wa mikoa, wakiwemo 11 wapya na 10 wa zamani. Tukio hilo lilifanyika katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.
Sherehe ambazo zilihudhuriwa na viongozi wakuu wa kitaifa, akiwemo Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, ambaye wakati huo alikuwa Makamu wa Rais, Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri Mkuu kabla ya kujiuzulu na Waziri wa wa Afrika Mashariki Samuel Sitta wakati huo ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa. wakuu wa mikoa walioapishwa wakati huo ni Yussuf Makamba kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, ambaye kwa sasa ni Katibu mkuu wa CCM, Anatoly Tarimo (Manyara), Ditopile Mzuzuri (Tabora), Daniel Ole Njoolay (Rukwa), Jaka Mwambi (Iringa) na Isidore Shirima(Mara).
Wengine ni William Lukuvi (Dodoma), Enos Mfuru (Kagera), Said Meki Sadiki (Lindi), John Mwakipesile (Mbeya), Henry Shekifu (Mtwara), James Msekela (Mwanza), Christine Ishengoma (Pwani), Johannes Balele (Shinyanga), Monica Mbega (Ruvuma), Parseko Kone (Singida) na Mohammed Abdulaziz (Tanga).
Wengine ni Abbas Kandoro (Arusha), Helima Kasungu (Kigoma), Said Kalembo (Morogoro) na Mohamed Babu (Kilimanjaro).
Hata hivyo, kufuatia kifo cha Ditopile Mzuzuri na kumteua Makamba kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Rais alifanya madadiliko kidogo kwa kumhamisha Kandoro mkoa wa Dar es Salaam kutoka Arusha na kumteua Mwinyi Musa ambaye alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Rungwe kuwa mkoa wa Tabora.
Aprili 15, 2009 aliwabadilisha vituo vya kazi wakuu wa mikoa 11 na kuteua wengine wapya ambapo Lukuvi aliamishiwa Dar es Salaam, Kandoro(Mwanza), Msekela (Dodoma), Mfuru (Mara), Machibya (Morogoro), Kalembo (Tanga), Abdulaziz(Iringa), Amina Mrisho(Pwani) Dk Christine Ishengoma(Ruvuma), Monica Mbega(Kilimanjaro), na Mohammed Babu(Kagera)
CHANZO: Gazeti la Mwananchi