Hivi hamuoni kwamba suala zima la kuzungumzia MAFISADI na UFISADI limewekwa ili kupotosha maana nzima ya dhana hii? Tutakaa kuzungumza ufisadi na mafisadi huku wenyewe wanajichukulia kana kwamba ni nyumbani kwao.
Walipoanza kuchota - TENA ZAMANI, enzi zile za mashirika ya umma (SU) - mbona hatukusema? Kwani ule ulikuwa ni nini? Watu walichota mpaka mashirika yakafilisika na kufa kabisa. Sisi KIMYA!
Leo hii ndio TUNAAMKA, kana kwamba tumezinduliwa usingizini? Wa kulaumiwa ni SISI WENYEWE! Tuliwapa ruksa ya kuchota, kwa kusingizia kwamba hao ni WAKUBWA, wako juu ya Sheria? Hivi kweli sisi tuna akili nzuri? NANI yuko juu ya Sheria, kama sisi wenyewe hatujawaruhusu?
Nawapeni mfano. Basi linatembea mwendo wa kasi kupitiliza. Lina abiria 65! Hakuna abiria hata mmoja anayediriki kusema lolote. Anatokea kijana, jasiri - MIMI - na kwenda mbele kwa dereva, kumwambia aendeshe kwa mwendo unaoruhusiwa, kwani tunataka kufika sio kuishia MORTUARY!
Unajua kinachotokea? Naanza kupigiwa kelele, tena kwa matusi ya nguoni - siwezi kuyataja hapa - na watu wazima wenye akili zao. Wanadai wana haraka. Haraka ya kufika au kufa?
Bahati nzuri tunafika, ninaomba dua kumshukuru Mola.
MARA NGAPI tumeona abiria wanaonusurika kufa kwenye ajali lukuki wakisema "Dereva alikuwa akiendesha kwa mwendo mkali kweli!" Enhe? Na ninyi mlifanya nini?
Unapokataa kumwajibisha mtu anayefanya makosa - kuendesha mwendo wa kasi kupitiliza ni KOSA, kwani anahatarisha usalama wako na wa wenzako - nawe pia unakuwa unashiriki katika kosa. Ni sawa na kumwona mwizi akivunja nyumba ya jirani yako, ukamwona na hukumzuia, kwa kusema "Si kazi yangu!" Kama kuna ambaye alikuona ukishuhudia, unaweza kuhusishwa kwenye uhalifu huo, kwani, kutokuzuia kosa kufanyika ni kushiriki kwenye kosa... accessory to the crime!
Sasa, kama sisi tunaendelea - tena wengine kuwahimiza madereva kwenda mwendokasi kupitiliza - kufanya hayo, huu nao si ufisadi?
Kabla hujamtoa mwenzako boriti jichoni mwake, angalia la kwako!
Tusilalamike UFISADI na MAFISADI wakati sisi tunashiriki katika yote hayo. Huko BOT na Hazina, Grey Mgonja hakupitisha hizo barua za kuitetea Alex Stewarts Assayers PEKE YAKE! Kulikuwa na makarani, wahasibu, wakurugenzi, makamishna! Walikuwa wapi wasiseme wakiona MKUU WAO WA KAZI akiharibu? NAO WALISHIRIKI! Wasisimame mbele ya Pilato na kusema "Nilimwona fulani akifanya hivi, na hivi, na hivi!" Wewe ULIKUWA WAPI?
Mnawalenga wenzenu kidole kimoja, viwili vinawalenga ninyi wenyewe!
Atakayekerwa na maoni haya, basi yeye ndiye FISADI NAMBARI WANI!
./Mwana wa Haki
P.S. TUACHE UNAFIKI!