Hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani bungeni katika wizara ya maliasili na utalii

Chademakwanza

JF-Expert Member
Jun 11, 2014
6,346
1,871
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, MHESHIMIWA ESTHER NICHOLAS MATIKO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA BAJETI WA MWAKA 2015/16 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KATIKA WIZARA HIYO KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017

(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya kanuni za Bunge toleo la mwaka 2016)
__________________________
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda kuchukua fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge hili kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2016/17. Aidha, napenda kumshukuru Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (Mb) kwa kuendelea kuniamini na kuniteua kuwa Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Maliasili na Utalii. Napenda kumwahidi yeye binafsi na Kambi nzima ya Upinzani Bungeni kwamba; nitatekeleza majukumu yangu kwa uaminifu, uadilifu na weledi mkubwa ili kuboresha utendaji wa Wizara hii kwa maslahi ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Naibu Waziri Kivuli wa Mali Asili na Utalii Mh.Cecilia Daniel Pareso kwa kufanya kazi bega kwa bega ili kuhakikisha kuwa hotuba hii inafanyika kwa ustadi wa hali ya juu ili kuleta tija katika sekta hii ya Mali Asili na Utalii.
Mheshimiwa Spika, kipekee zaidi napenda kuishukuru sana familia yangu kwa kunitia moyo na kunivumilia wakati wote ninapokuwa mbali nao nikitekeleza majukumu yangu ya kibunge.
Mheshimiwa Spika, aidha nitakuwa mkosefu wa fadhila kama nitaacha kutumia nafasi hii adhimu kuwashukuru wanatarime mjini kwa kuniamini na kunichagua kwa kura nyingi kuwa mbunge wao na kumshinda mgombea wa CCM. Maamuzi hayo si tu kwamba yameifanya dunia kutambua mabadiliko ya kiasili ya kimtazamo na kifikra ya kwamba jamii za watu wa Tarime haziongozwi na mwanamke bali pia yameniwezesha mimi kuandika historia ya kuwa mbunge wa jimbo wa kwanza mwanamke kutoka koo za wakurya, hii ni tunu adhimu ambayo nitailinda na kuiheshimu katika uhai wangu wote kwa kuhakikisha naitumikia vema jamii yangu na nchi yangu kwa upendo wangu wote, ujasiri wangu wote na kwa uzalendo wangu wote. Aidha, niwapongeze pia wabunge wanawake wenzangu wote kutoka vyama vyote tulioshinda majimbo, ni wazi kazi iliyombele yetu pamoja na kulitumikia taifa kupitia bunge hili tukufu pia kudhihirishia uwezo wetu na kuwa chachu kwa wanawake wengine wengi zaidi kusaka fursa za kisiasa.
Mheshimiwa Spika, Ni wazi kwamba wanawake tunaweza ni suala tu la kuonyesha utashi na uwezo wetu kwa jamii, kwani kati ya wagombea tisa wanawake wa chadema katika uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015, sita tumeshinda na leo hii ni wabunge wa majimbo tukijumuika na mwenzetu mmoja kutoka CUF, tunaweza na hata wale wanaobeza uwepo wetu humu ndani ya bunge ikiwemo na wabunge wa viti maalum, hadi kutuita majina ya kudhalilisha na yenye vimelea vya dharau wajue hata wao kiti wanachokikalia humu ndani bungeni kilikuwa kikikaliwa na mwanamke.
Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba sasa niwasilishe maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu bajeti ya Wizara hii; ila kabla sijafanya hivyo; napenda kunukuu maneno ya Abraham Lincolin aliyesema kwamba;“The best way to predict your Future is to create it” - yaani namna bora ya kufikia ndoto ya maisha yako, ni kuanza kuyatengeneza maisha hayo sasa.
Mheshimiwa Spika, nimechagua kuanza na nukuu hiyo kwa sababu Serikali zote za CCM ikiwemo hii ya awamu ya tano; zimekuwa zikijigamba kwamba hakuna sababu ya watanzania kuwa maskini kwa sababu Tanzania ina rasilimali nyingi zikiwemo mali asili za nchi yetu. Lakini cha ajabu ni kwamba umaskini umeendelea kuitafuna Tanzania kwa miaka yote 55 ya uhuru chini ya utawala wa CCM licha ya rasilimali lukuki tulizo barikiwa kama taifa.
Mheshimiwa Spika, bila shaka, Serikali zote za CCM ikiwemo hii ya hapa kazi tu, hazikuwekeza vya kutosha katika maliasili za nchi yetu ili kuweza kuwa na mavuno endelevu ambayo yangesaidia kufikia ndoto za wananchi za kuondokana na umasikini lakini badala yake zikageuka kuwa madalali wa maliasili zetu tena kwa wageni jambo ambalo limeendelea kuchochea kasi ya umasikini nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo wa maneno ya Abraham Lincolin, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuanza kuboresha maisha ya watanzania sasa kwa kuwekeza vya kutosha katika maliasili na utalii wa nchi yetu, ili taifa lifikie ndoto yake ya kuwa na uchumi wa kati na kuondokana na umasikini kama Mpango wa Taifa wa Maendeleo unavyoelekeza.
SEKTA YA UTALII
HOTELI ZA KITALII NDANI YA HIFADHI
Mheshimiwa Spika, takribani 80% ya watalii wanaoingia nchini hulala katika hoteli mbalimbali zikiwemo za ndani ya hifadhi. Licha ya hoteli za ndani ya hifadhi kuchangia kiasi kikubwa cha mapato ya Wizara hii, hoteli hizo zimekuwa na changamoto nyingi jambo linaloathiri ufanisi wake na mapato yatokanayo na hoteli hzio.
Mheshimiwa Spika, ndani ya hifadhi kuna hoteli za wawekezaji wazawa na zile za raia wa kigeni. Lakini hoteli za wazawa zimekuwa zikikumbwa na changamoto kubwa sana. Mathalani wakati wa msimu wenye wateja wachache (low season) hoteli za wawekezaji wa kigeni hutenga vyumba yaani hufanya “block booking” kwa wageni wao katika hoteli hizo za wazawa kwa kipindi cha muda mrefu na kwa gharama ndogo (low price), hivyo basi inapofika kipindi cha msimu wenye wateja wengi (high season) tayari unakuta hoteli hizi za wazawa zinakuwa haziwezi tena kuuza vyumba hivyo na hawawezi tena kufaidika na bei za high season kwa kuwa vyumba hivyo vinakuwa vimeshachukuliwa (blocked). Aidha; changamoto nyingine ni kwamba; fedha hii inayokuwa imelipwa kwa vyumba hivi vya hoteli za wazawa ni ndogo na inakatwa kodi kubwa , lakini Hoteli zile za wawekezaji wageni hupokea wageni wengi kwa kipindi hicho cha high season kwa bei kubwa na huwa haikatwi tena kodi.
Mheshimiwa Spika , pamoja na hayo, imekuwa ni vigumu sana makampuni madogo ya utalii kuweza kumudu soko la ushindani kwa kuwa vipaumbele vya kupata vyumba vya hoteli kwa ajili ya kulaza wageni kutolewa kwa makampuni makubwa pekee na zaidi yale ya kigeni. Hii inasababisha makampuni madogo ya ndani kushindwa kuhimili soko la ushindani na mengi hufilisika kabisa. Suala hili sio tu linaua hoteli za wazawa hapa nchini bali pia linaisababishia serikali hasara kubwa ya kupoteza mapato.
Mheshimiwa Spika, Nchi hii ina Tume ya Haki ya Ushindani (Fair Competition Commision) ambayo imebainisha wazi katika tovuti yake kwamba: “FCC has a mandate to regulate the competitive market. “FCC deals with all issues of anti- competitive conduct, abuse of dominance and has provision for curtailing merges and acquisitions if outcomes are likely to create dominance in the market or lead to uncompetitive behavior”
Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri rahisi kabisa ni kwamba tume hiyo ina mamlaka ya kuhakikisha kunakuwepo na kiwango cha uadilifu miongoni mwa washindani katika masoko. Hivyo basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuhakikisha jambo hili linatafutiwa ufumbuzi kwa kuwa ni wajibu wa serikali kunusuru makampuni haya ya wazawa ili kuweza kumudu soko la ushindani wa kibiashara. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutumbua pia majipu katika eneo hili ambapo wawekezaji katika hoteli za hifadhini wamekuwa wakiwanyonya wawekezaji wazawa na hivyo kudumaza juhudi za Serikali na wananchi za kukuza uwekezaji wa ndani katika sekta ya utalii.
LESENI YA KUENDESHA BIASHARA YA UTALII (TALA LICENCE)
Mheshimiwa Spika, Licha ya hotuba ya Rais John Pombe Magufuli wakati akilizindua Bunge la kumi na moja mwezi Novemba , 2015 kueleza nia ya kuwasaidia Watanzania wanaotaka kuwekeza hapa nchini; hakuna dalili za utekelezaji wa azma hiyo ya Serikali jambo linatoa taswira kuwa kauli ile ilikuwa ni ya kisiasa tu.
Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu kumekuwa na urasimu na tozo nyingi za kuendesha biashara hii ya Utalii jambo ambalo limekuwa ni kikwazo kikubwa kwa wawekezaji wa ndani na hivyo kushindwa kumudu ushindani katika sekta hiyo. Mzigo mkubwa umewaelemea wafanyabiashara wadogo na wengi wao wako katika hatari ya kufunga biashara hizo kwa kushindwa kupambana kwenye soko la ushindani. Kwa mfano katika malipo ya leseni , makampuni ya nje yanalipa dola elfu tano ($5000) na makampuni ya kitanzania ni dola elfu mbili ($2000).
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ina mtazamo kwamba hiki kiwango cha (flat rate) ya dola 200 kitazamwe upya kwa kuwa kwa kuwa kinawaumiza wawekezaji wadogo/wachanga katika sekta hiyo. Mathalani, unakuta kampuni yenye magari 5 inalipa tozo sawa na kampuni yenye magari 300. Huu ni uonevu wa hali juu kwa wafanya biashara hawa wadogo na ni kinyume na kauli ya Rais katika kuwasadia wafanyabiashara wadogo. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza tozo ya dola 1000 kwa wawekezaji wadogo . Aidha, tunapendekeza pia orodha ya tozo ipuguzwe ili kubaki na tozo chache ambazo ni nafuu ili wawekezaji wadogo waweze kumudu.
Mheshimwa Spika, Pamoja na tatizo hilo la tozo serikali inawataka wafanya biashara hawa wadogo katika sekta hii ya utalii kuwa na uwezo wa kumiliki idadi ya magari yasiyopungua matano (5) ili waweze kupata leseni. Hii inaonyesha dhahiri kuwa Serikali hii ya CCM inataka biashara ya utalii iendele kuhodhiwa na watu wachache wenye fedha nyingi jambo ambalo linaondoa dhana nzima ya uchumi shirikishi ambapo kila mtanzania anatakiwa kuwa na fursa sawa katika kujenga uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu gharama ya kumiliki gari kwa ajili ya safari za utalii mbugani ni shilingi za kitanzania milioni 120 mpaka 200. Bei ya chini kabisa ya gari ambalo limeshatumika ,kwa umbali wa kilomita 400,000 na kuendelea ni milioni 25 na kuendelea. Kwa hali hiyo, ni vigumu sana kwa mtanzania wa kawaida kuweza kumudu gharama hizo na kuweza kumiliki magari matano ili apatiwe leseni ya kufanya biasahara ya usafirishaji wa watalii.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kubadili utaratibu wa sasa wa utoaji wa lesni kwa wafanyabiashara wanaosafirisha watalii kwa kuondoa sharti la umiliki wa magari matano ndipo wapewe leseni ya kufanya biashara hiyo. Tunapendekeza kiwango cha umiliki wa magari kama kigezo cha kupata leseni kipunguzwe hadi kufikia magari mawili.

UWEKEZAJI KATIKA IDARA YA UTANGAZAJI WA VIVUTIO VYA UTALII
Mheshimiwa Spika, Biashara ya Utalii ni matangazo. Pamoja na vivutio vingi vya utalii tulivyo navyo, kama vivutio hivyo havitatangazwa ipasavyo, tusitegemee kupata watalii wa kutosha na kwa sababu hiyo tusitegemee pia kukusanya mapato ya kutosha katika sekta hiyo. Ili tuweze kunufaika katika sekta hii kwa kiwango kinachokusudiwa ni lazima kuwe na mpango madhubuti na bajeti ya kutosha kufanya matangazo ya vivutio vyetu vya utalii nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili, imeandaa mpango gani wa utangazaji wa vivutio vya utalii na imetenga fedha kiasi gani kwa ajili ya kugharamia matangazo hayo kwa mwaka mpya wa fedha 2016/17. Lengo la kuitaka Serikali kufanya hivyo, ni kuisaidia kuwekeza katika utangazaji wenye tija, isije ikawa inatumia fedha nyingi kwenye utangazaji halafu faida inayopatikana ni ndogo kuliko fedha iliyotumika kufanya utangazaji. Hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani hapa ni kuwa na uwiano kati ya fedha tunazotumia kwenye utangazaji na tija inayopatikana (proportional result between input and output).

HASARA FEDHA ZA TOZO KATIKA HOTEL ZA KITALII NDANI YA HIFADHI ILIYOPATIKANA KUTOKANA NA SERIKALI KUKAIDI AMRI YA MAHAKAMA
Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na mvutano mkubwa kati ya wamiliki wa hoteli zilizopo mbugani na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kutokana na wamiliki hao kukwepa kulipa tozo zilizowekwa na Mamlaka hizo.
Mheshimiwa Spika, mvutano huo ulipelekea wamiliki wa hoteli hizo kufungua shauri mahakamani kupinga tozo hizo. Hata hivyo; katika shauri hilo, wamiliki wa hoteli hizo walishindwa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilimtaka Waziri wa Maliasili na Utalii kutangaza katika gazeti la Serikali tozo mpya zitakazotumika katika Mahoteli yaliyo ndani ya hifadhi za Taifa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ili zianze kutumika mara moja.
Mheshimiwa Spika, Mbali na uamuzi wa Mahakama, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira wakati ikishughulikia mgogoro huo wa wamiliki wa hoteli za mbungani na mamlaka hizo ilimshauri pia waziri wa Maliasili na Utalii kupitia azimio la Bunge kukazia hukumu ya Mahakama na kumpa muda wa hadikufikia mwishoni mwa Februari, 2015 awe ameshatoa tangazo hilo.
Mheshimiwa Spika, Serikali mpaka sasa imeshindwa kukazia hukumu hiyo jambo ambalo limeikosesha Serikali mapato ya Shilingi 3,076,728,545.57 hadi kufikia tarehe 15 Machi, 2015.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua kwamba Waziri wa sasa wa Maliasili na utalii hakuwa waziri wakati azimio la Bunge la kuitaka Serikali kukazia hukumu hiyo linapitishwa, lakini alikuwa Mbunge na analifahamu azimio hilo.
Mheshimiwa Spika, Waziri huyu wa sasa hana cha kujitetea kwa kuwa kazi yake ni kutekeleza maazimio ya Bunge hata kama hayakupitishwa wakati wake kwa kuwa Serikali ni hiyo hiyo. Kitendo cha kutokazia hukumu hiyo na kuisababishia Serikali hasara kubwa namna hii ni uzembe wa hali ya juu wa waziri binafsi na watendaji wake na tunaitaka Mamlaka yake ya uteuzi ijiridhe kama anafaa kuendelea kuongoza wizara hii ikiwa anashindwa kuokoa zaidi shilingi bilioni 3 za tozo katika mahoteli ya mbugani ambazo mahakama imeshaelekeza zikusanywe.
3. MIUNDOMBINU KATIKA SEKTA YA UTALII
3.1 MIUNDOMBINU NA HUDUMA KATIKA VIWANJA VYA NDEGE
Mheshimiwa Spika, Utalii wa nchi yetu unategemea sana huduma bora katika viwanja vya ndege. Hali ya viwanja vya ndege nchini bado hairidhishi. Hali hii inaathiri mapato yatokanayo na utalii kwa kuwa ubovu wa miundo mbinu na huduma katika viwanja hivi vinasababisha vishindwe kutumika kabisa au kutumiwa na wageni wachache kutokana na hadhi zake.
Mheshimiwa Spika, Mathalani uwanja wa Kilimanjaro International Airport (KIA) hakuna taa za kutosha za kutoa ishara nyakati za usiku na ni hatari sana kwa waongoza ndege na abiria, mashine za kupokea mizigo ziko chache sana na wageni husubiri muda mrefu sana ili kupokea mizigo na hakuna maeneo maalum lililojengwa kwa ajili ya kupokea wageni. Jambo hili linaleta usumbufu mkubwa kwa wageni na hata wale wanaowapokea wageni hao. Mfano mwingine ni kiwanja cha ndege cha Musoma kilichojengwa kwa kiwango cha changarawe na hivyo ndege nyingi haziwezi kutua. Uwanja wa Musoma ni muhimu hasa kwa wageni wanaotembelea Mkoa wa Mara kwa shughuli za utalii wa wanyama.Ni dhahiri uwanja huo ungeboreshwa ungechangamsha zaidi shughuli za kitalii kwa kuwa ni karibu na nchi jirani ya Kenya,na pia ungehamasisha wageni kutembelea kaburi la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mheshimiwa Spika, Changamoto za miundo mbinu na huduma ziko takribani kwenye viwanja vyote nchini ikiwa ni pamoja na Songwe,JKNA, Dodoma, Kigoma n.k . Athari za Changamoto hizi zilijionyesha dhahiri wakati wa mgogoro kati ya Tanzania na Kenya ambapo Idadi kubwa ya wageni waliokuwa wanakuja Tanzania walionyesha kuwa hushukia uwanja wa Jomo Kenyatta.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuboresha viwanja hivi vya ndege ili kuvutia wageni wengi zaidi na hata wawekezaji wanaotamani kuleta ndege zao hapa nchini waweze kuwa na uhakika wa usalama wa ndege zao na abiria pia. Vilevile, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuhakikisha watendaji wote ndani ya viwanja hivi wanapata elimu ya namna ya kuwahudumia wateja kwa ukarimu zaidi (customer care and hospitality).
3.2 NJIA YA MALIPO KATIKA VIWANJA VYA NDEGE NA HUDUMA MBALIMBALI ZA HOTELI KWA WATALII (MODE OF SERVICE PAYMENT)
Mheshimiwa Spika, katika viwanja vyetu vya ndege na hata mahoteli ya kitalii nchini bado malipo mbalimbali yanafanyika kwa pesa taslimu (cash payment). Takribani 9.3% ya wageni wanaoingia nchini hulipa kwa kutumia credit card na 89.8% wanafanya malipo kwa njia ya fedha taslimu kwa mujibu wa ripoti ya International Visitor’s Exit Survey Report ya mwaka 2013/2014.
Mheshimiwa Spika, nchi nyingi duniani zinatumia mfumo wa kieletroniki wa kufanya malipo mbalimbali kwa njia ya kadi yaani (credit card) . Nchi nyingi zilizoendelea hutumia mfumo huu ili kupunguza hatari za kubeba fedha nyingi ikiwa ni pamoja na kuibiwa, kupoteza n.k
Mheshimiwa Spika, wageni wanapokuja nchini hukutana na changamoto za kulazimika kufanya malipo kwa njia ya fedha taslimu ilhali wengi wao hawasafiri na fedha.Wageni hawa wanakumbana na usumbufu mkubwa wa kuchukua fedha katika mashine (ATM) ili waweze kufanya malipo. Hali hii imewafanya wageni wengi wanaoingia nchini kupata usumbufu mkubwa na kuona nchi yetu ni nchi iliyojaa urasimu.
Mheshimiwa Spika, Serikali kuendelea kuruhusu tabia ya kutumia mfumo wa kizamani wa kupokea fedha taslimu ilhali njia ya kadi ni salama zaidi kwa wageni wetu na hupunguza mianya ya wizi, ubadhirifu na hata rushwa basi huko ni kuendelea kuturudisha nyuma kusikoendana na matumizi sahihi ya mabadiliko ya kiteknolojia. Mfumo huu ukitumiwa vizuri utarasihisha kuongeza zaidi manunuzi (purchasing power) ya bidhaa zetu za kitanzania zinazouzwa katika mahoteli na maeneo mengine ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuanza kuwaelimisha wadau wa sekta ya utalii kujua manufaa ya matumizi ya kadi (credit card),pia kuwahamasisha kuanza kutumia mfumo huu ili kuendana na soko la utalii la kimataifa,na kuendelea na mabadiliko ya kiteknolojia duniani.
Vilevile Kambi Rasmi inaitaka serikali kuhakikisha kuwa pale mgeni anapolipia fedha za visa anapewa risiti ya kielectroniki kama ilivyo katika mfumo wa serikali unaowataka wafanya biashara wote nchini kuzitumia.
3. 3. KUATHIRIKA KWA SHUGHULI ZA UTALII NCHINI
Mheshimiwa Spika, Suala la ulinzi na usalama kwa watalii wanaoingia nchini ni la muhimu sana kwa kuwa sekta ya utalii inachangia takribani 5.1 % ya uchumi wetu sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 2,975.6 kwa mujibu wa World travel and tourism Council of Tanzania 2015.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na kwamba suala la utalii SIO suala la Muungano kama ilivyoanishwa kwenye orodha ya mambo ya Muungano katika nyongeza ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini kwa kuwa linahusisha moja kwa moja masuala ya fedha na uchumi ambao kimsingi ni suala la Muungano basi haina budi kulizungumzia kwa maslahi mapana ya uchumi wa taifa letu. Ikiwa ni pamoja na namna pato la utalii linaweza kuathiriwa endapo tutakosa siasa safi na uongozi bora.
Mheshimiwa Spika, Zanzibar kama kitovu kikuu cha utalii wa fukwe na Tanzania Bara kama kivutio kikuu cha utalii wa wanyama pori,milima na malikale hutegemeana sana ,kwa kuwa watalii wengi wanaoingia Tanzania Bara huelekea Zanzibar kwa ajili ya utalii wa fukwe. Halikadhalika kwa wageni wengi wanaoingia Zanzibar hutembelea vivutio vya utalii Tanzania Bara. Lakini utalii huu huathirika moja kwa moja pale panapotokea misuguano ya kiasiasa baina ya vyama hasa nyakati za chaguzi kama ilivyotokea Zanzibar wakati wa uchaguzi mkuu mwaka huu kutokana na ukiukwaji wa demokrasia na utawala bora.
Mheshimiwa Spika,Ni lazima sasa serikali itazame kwa kina athai za matukio ya kisiasa katika uchumi wetu hususani katika sekta hii nyeti ya utalii . Utulivu wa nchi, usalama, demokrasia na utawala bora ni kivutio cha kwanza katika Utalii. Na katika serikali zilizostaarabika siku zote uchumi ndio hubeba siasa (economy run politics). Kwa bahati mbaya sana hapa kwetu siasa ndizo zinazoongoza uchumi. Hii inaonyesha kwamba bado tuna dola yenye matatizo (Problemativ State) .
Mheshimiwa Spika, Katika gazeti la New York Times, nchi kama Srilanka iliwahi kupata hadhi ya kujulikana kama nchi ya kwanza duniani kwa kivutio cha watalii. Lakini kukandamizwa kwa demokrasia na misukosuko ya kisiasa nchini Srilanka kama inavyotokea Tanzania leo ilipelekea utalii wa nchi hiyo kushuka kwa kasi ya asilimia 43 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na hivyo kuanguka kabisa kwa uchumi wa nchi hiyo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuliambia Bunge lako tukufu hasara iliyopatikana kutokana na matukio yaliyotokea nyakati za uchaguzi na kama yameathiri idadi ya Watalii walioingia nchini baada ya uchaguzi na hata mpaka sasa.
UTARATIBU WA KUTOA ZABUNI KATIKA KUUZA UTALII NCHINI NJE YA NCHI
Mheshimiwa Spika, Mara nyingi kumekuwa na changamoto kubwa katika utaratibu wa utoaji zabuni katika shughuli mbalimbali za serikali. Hii inapelekea kazi nyingi kushindwa kufanyika ipasavyo, kutumia fedha nyingi kuliko kusudio, au kushindwa kufikia malengo tuliyojiwekea.
Mheshimiwa Spika Kambi Rasmi ya Upinzani inazo taarifa kwamba katika Mwaka wa fedha 2013/2014 Bodi ya Utalii nchini ilitoa zabuni ya kufanya matangazo ya utalii kwa timu ya Sunderland Association Football Club na Seatle Sounders F.C Mwaka 2014
Mheshimiwa Spika Zabuni zilizotolewa ni namba PA/036/2013-14/NC/05 ya Sunderland yenye thamani ya shilingi za Kitanzania 1, 252,500,000 na zabuni namba PA/036/2013-14/NC/06 ya Seattle Sounders yenye thamani ya Shilingi 1,593,000,000.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutoa majibu mbele ya Bunge lako kwa maswali yafuatayo:
Je, serikali ilitumia utaratibu gani katika kutoa zabuni hiyo?
Je, kulikuwa na ushindani katika utangazwaji wa zabuni hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Manununuzi ya Umma(Public Procurement Act)
Je, kufanyika kwa matangazo ya Utalii kwa kutumia timu hizo ilikuwa kwenye Mpango wa Bodi ya Utalii (TTB)?. Na kama kutolewa kwa zabuni hiyo haikuwa kwenye mpango wa bodi. Je, bajeti hiyo ya kugharamia zabuni hiyo ilitoka wapi?
NANI MNUFAIKA WA RASILIMALI NA VIVUTIO VYA TANZANIA? JE, NI WATANZANIA AU MAJIRANI WA TANZANIA?
Mheshimiwa Spika, sambamba na utangazaji wa vivutio vya utalii bado kuna shida kubwa katika kulinda, kuthamini na kutangaza fahari zetu. Hivi karibuni katika mitandao mbalimbali ya kijamii ilisambaa video moja ikionyesha binti wa Kenya akitangaza kuwa Mali Kale ya Olduvai Gorge(Oldupai) iko nchini Kenya. Pamoja na hayo kuna ujumbe wa aina mbalimbali ukionyesha kuwa Mlima Kilimanjaro unaonekana vizuri ukiwa Nchini Kenya kuliko Tanzania. Hata baadhi ya ndege za Shirika la Kenya zinatangaza mlima Kilimanjaro kuwa uko nchini Kenya. Mfano, baadhi ya ndege za Shirika la Kenya (Kenya Airways maarufu kama KQ, zimeandikwa katika mbawa zake “The home of Mount Kilimanjaro” huku zikitumia alama ya Mlima Kilimanjaro”.Jambo hili limesababisha watalii wengi kupita nchini Kenya ili waweze kuuona mlima huo na hivyo kwa namna moja au nyingine inapunguza idadi ya watalii kuja kutembelea mbuga zetu, mali kale au hata Milima tuliyonayo. Hata kama uhalisia ni kuwa Mlima huo hauko nchini Kenya lakini ni mali halali ya Watanzania basi ni lazima kuhakikisha mtu yoyote anayetumia alama ya Mlima huu kujitangaza kibiashara ahakikishe anaruhusiwa na serikali ya Tanzania kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, Inashangaza serikali imebaki kutoa makanusho badala ya mkakati madhubuti wa kutangaza zaidi vivutio vyetu hivi na kuhakikisha umiliki wake unatunufaisha ipasavyo.katika hali kama hiyo unakuta tayari taifa linakuwa limeshapata hasara.
Mheshimiwa Spika, Kukosekana kwa mkakati madhubuti (Strategic plan) wa kutangaza rasilimali na vivutio vyetu kunasababisha nchi nyingine kunufaika zaidi. Kuwepo kwa ubinafsi, uzembe uliokithiri unaofanywa na watu wachache na kutowatumia Watanzania wenzetu walio nje ya nchi vizuri katika kutangaza na kuuza fahari ya nchi yetu kunasababisha vivutio vyetu kutotangazwa ipasavyo. Hivyo ni lazima sasa serikali kutoa fursa kwa taasisi au watu wenye uwezo ili waweze kutangaza vivutio na rasilimali zetu kimkakati zaidi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi inaitaka serikali hususani Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka nyingine chini ya Wizara hii kuhakikisha zinaitekeleza kazi zake kwa ufanisi ikiwa ni kutangaza kwa nguvu zaidi vivutio na rasilimali zetu. Ni vyema sasa Mheshimiwa Rais afanye ziara yenye tija ya kuwahamasisha Watanzania walio nje ya nchi kuweza kuwekeza hapa nchini hii ni kwa uzito wa nafasi yake na kuonyesha kuwathamini na kuwajali kaka na dada zetu walio nje ya nchi. Mwaka 2014 Rais Kenyatta wa Kenya alifanya ziara ya namna hii katika nchi za Ulaya ambapo alitoa hamasa kubwa kwa Wakenya kuwekeza nyumbani.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na hayo Kambi Rasmi inataka kujua ni hatua gani zitakazochukuliwa na serikali endapo Taifa lolote litabainika kuwa ‘linapoka’ umaarufu wetu au kutumia rasilimali zetu pasipo makubaliano ?
6. VIUMBE HAI NA WANYAMA PORI
6.1 VYURA WA KIHANSI
Mheshimiwa Spika, Tanzania ni moja ya nchi iliyo na vivutio vya kipekee zaidi duniani. Vyura wa kihansi wajulikanao kitaalamu kama (Nectophrynoides apserginis) ni vyura pekee duniani wanaozaa na pia huwa wananyonyesha vitoto vyao tofauti na amphibia wengine. Vyura hawa wanaopatikana katika maporomoko ya milima ya Udizungwa, wanaishi katika maji yanayotiririka kwa kasi na yenye mvuke mwingi unaosababishwa na nguvu ya maji.
Mheshimiwa Spika, Vyura hawa wanatoweka kwa kasi kubwa sana kunakosababishwa na uharibifu mkubwa wa mazingira na kufanya miradi mbalimbali ya kibinadamu bila kuchukua tahadhari za utunzaji wa mazingira. Vyura hawa wangeliweza kuliingizia taifa pato kubwa sana kwa upekee wao, na vilevile kutengeneza ajira kwa vijana endapo wangehifadhiwa vizuri kama kivutio cha kipekee kwenye utalii.
Mheshimiwa Spika, Mnamo mwaka 2009, tafiti zilionyesha vyura hao wanatoweka na hivyo serikali iliamua kuwasafirisha na kuwapeleka Chuo Kikuu cha Colorado nchini Marekani ili kutengenezewa mazingira bandia ya kuwazalisha. Kwa taarifa zisizo rasmi serikali ilikwisha warudisha baadhi ya vyura hawa kwa awamu ya kwanza ila bado inafanya utaratibu wa kuwarejesha wengine hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Ni wazi kuwa kwa kupeleka vyura hao nje ya nchi tumepoteza mamilioni ya fedha ambazo zingetumika kutoa elimu kwa jamii, kuboresha mazingira na hata kutengeneza mazingira mbadala kwa vyura hawa kuzaliana hapa hapa nchini. Serikali imekuwa dhaifu katika kuwatumia wataalamu wetu na hivyo kulisababishia taifa hasara kubwa ya kulazimika kuwapeleka viumbe hawa nje ya nchi bila kujali ni kwa namna gani upekee wa viumbe hawa utaathiriwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ituambie inafanya mkakati gani wa kuwanusuru vyura hawa wa kipekee kabisa duniani ambao wako mbioni kutoweka? Vilevile, ituambie kwamba vyura ambao walisalia nchini Marekani wote wamerudishwa?Je, imefanya tathimini kwa vyura hao kuhakikisha kuwa huko kubadilishiwa mazingira hakujawaletea vyura hao athari zozote ?
6.2. BIASHARA YA NYARA (TROPHY DEALERS LICENCE-TDL)
Mheshimiwa Spika, biashara ya viumbe hai hapa nchini biashara inayoongozwa na sheria Namba 5 ya Wanyamapori ya mwaka 2009, Sehemu ya Kumi, kifungu cha 80(1). Leseni ambayo inatolewa kwa mujibu wa kifungu hiki inatolewa kila mwanzo wa mwaka na leseni. Biashara hii ya usafirishaji wa viumbe hai kwa sehemu kubwa inahusisha; ngedere, nyani, vyura, mijusi, konokono, ndege, kenge, nyoka na wadudu wengine watambaao. Biashara hii imegawanyika katika madaraja 21 kwa kulingana na aina ya kiumbe husika.
Mheshimiwa Spika, baada ya kupatiwa leseni mhusika hutakiwa kulipia ada kwa ajili ya viumbe husika serikalini na hulazimika kuingia mikataba ya kibiashara ndani na nje ya nchi na wengine inawalazimu kwenda katika taasisi za fedha kukopa fedha za kufanyia kazi hiyo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imeanza kwa kutoa utangulizi huo ili kueleweka vyema na kwamba pale inapotokea kwamba Serikali imekamata viumbe au wanyama waliopo katika orodha ya leseni sio kwamba kuna kuwa na rushwa bali ni Serikali kutafuta nani hasa wa kumrushia mzigo pale mambo yanapoonekana kutokwenda vyema.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilisitisha biashara hii tarehe 17 March, 2016 ikiwa ni miezi miwili na nusu baada ya msimu wa biashara hiyo kuanza rasmi tarehe 1 Jan.2016 bila ya kuwashirikisha wadau wa sekta hii na bila sababu za maana. Hii inaweza kuitwa kuwa ni hujuma kwani tayari wafanyabiashara walikamata viumbe hao kwa ajili ya kuvisafirisha nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa leseni zao, maduhuli ya serikali ni asilimia 10 ya thamani halisi ya mauzo ya viumbe hai nje ya nchi. Takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka wa fedha 2008-2010 maduhuli yatokanayo na biashara ya hii ya Nyara ilikuwa ni shilingi 408,724,551/-, takwimu za maduhuli kwa sasa zitakuwa zimepanda kutokana na wadau kuongezeka katika biashara hii, kumbukumbu za Wizara zinaonesha kuwa kuna makampuni 214 nchi nzima yanayojihusisha na biashara ya nyara.
Mheshimiwa Spika, tukumbuke kuwa biashara hii inaongozwa na Mgawo (QUOTA) unaopangwa na wataalam mbalimbali wa Idara ya wanyamapori kwa kuzingatia matumizi endelevu (sustainable utilization) kwa kila kiumbe husika.
Mheshimiwa Spika, mbali ya mapato ambayo serikali inapata bado pia ajira zinazotolewa na wafanyabiashara kwa wananchi wanapopatikana viumbe hao. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mhe Waziri kuruhusu wafanyabiasharaambao tayari wanamikataba ya kusafirisha na tayari wana mzigo wa kusafirisha nje waruhusiwe, kwa kusitisha barua ya tarehe 19/05/2016 yenye kumb. Na. HD.28/563/01/83 iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori.
Mheshimiwa Spika, kusitisha kwa biashara ambayo tayari wahusika wamekatia leseni na biashara ni ya kipindi kifupi ni hasara kubwa sana kwa wahusika kwani tayari mitaji yao iko rehani na tukumbuke kwamba katika biashara kupata soko ni kazi ya miaka kadhaa na kupoteza soko hilo ni kitu cha dakika kadhaa. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwa chombo wezeshi kwa wafanyabiashara badala ya kuwa chombo filisi kwa wafanyabiashara.
7. UJANGILI NCHINI MFUPA MGUMU KWA SERIKALI YA CHAMA CHA MAPINDUZI
Mheshimiwa Spika, bado suala la ujangili nchini limekuwa ni tishio kwa wanyama na hata binadamu wanaofanya shughuli halali ndani ya hifadhi. Ujangili nchini umeiletea Taifa sifa mbaya Kimataifa. Vipo vyombo mbalimbali vya habari duniani vimekuwa vikitangaza uwindwaji haramu, utoroshwaji wa wanyama pori wakiwa hai, na mauaji ya wanyama pori hasa tembo yanayoendelea kutokea nchini.Vilevile, makampuni binafsi ya utalii, watu binafsi na hata mashirika walishirika katika harakati za kupaza sauti kuhakikisha kuwa tembo wetu wanalindwa.
Mheshimiwa Spika, Katika ripoti ya utafiti kuhusu ujangili wa meno ya tembo uliofanywa na Benki ya dunia (WB), Shirika la Umoja wa Mataifa Kupambana na Madawa ya Kulevya na Ujangili (UNODC) na Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) ulibaini asilimia themanini na tano (85%) ya meno ya tembo yaliyokamatwa maeneo mbalimbali duniani yalitokea Tanzania. Mnamo mwezi Julai 2006 kilo 2,500 za meno ya tembo yenye vinasaba kutoka Tanzania yalikamatwa nchini Taiwan katika mji wa Kaohsiung, mwezi machi mwaka 2009 nchini Filipino katika mji wa Manila zilikamatwa kilo 3,300,na kilo nyingi zaidi takribani 6043 zilikamatwa mwezi Desemba 2012 katika mji wa Port Klang,Malaysia.
Mheshimiwa Spika, Katika Bunge la Kumi(10) aliyekuwa Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Wizara ya Mali Asili na Utalii katika hotuba yake ya mapato na matumizi ya wizara hiyo 2013/2014, alizungumzia suala la Ujangili kwa kina na hata kutaja jina la wakala wa meli iliyokamatwa ikielekea Hong Kong ikiwa imebeba shehena ya meno ya tembo kutoka Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Katika kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii wakati huo alikiri kuwepo kwa tatizo hili kubwa la ujangili, na usafirishaji wa meno ya tembo kwenye meli iliyoitwa Delmas Nakadha chini ya mmiliki Bus Herman Ledley. Waziri huyo wa Maliasili na Utalii alikiri kukamatwa kwa watuhumiwa na kufunguliwa mashtaka. Japokuwa mpaka leo hatukuwahi kusikia mrejesho wowote katika Bunge hili tukufu au kupata taarifa yoyote endelevu juu ya kesi ile au kujua endapo watuhumiwa walishinda kesi, waliachiwa kinyemela au bado kesi inaendelea kwa kuwa kesi hizi za ujangili zimechukua na tabia ya kuchukua muda mrefu sana.
Mheshimiwa Spika, Serikali hii yenye falsafa ya kutumbua majipu ni lazima sasa ijielekeze katika kuwatumbua wale wote wanaohusika katika kukwamisha kesi hizi ili zisimalizike kwa wakati .Vilevile Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali ituambie mbele ya Bunge lako ni nini kinaendelea katika kesi hizi na kwa nini kesi za ujangili zimekuwa zikichukua muda mrefu kumalizika?
8. UNYANYASAJI UNAOFANYWA NA SERIKALI KWA WANANCHI WANAOISHI JIRANI NA HIFADHI
Mheshimiwa Spika, bado kumekuwepo na tatizo sugu la migogoro kati ya misitu ya hifadhi na wananchi wanaoishi vijiji jirani na hifadhi. Wananchi hao wamekuwa wakipatwa na madhila ikiwa ni pamoja na kufyekewa mazao yao, kupigwa na askari wa hifadhi,kufukuzwa katika nyumba zao, kubakwa na kutozwa faini zisizo za kimsingi na baadhi ya askari wa hifadhi wasio waaminifu. Mfano, wananchi wa kijiji cha Nyamikoma kata ya Kyanyari Butiama na wale wa hifadhi ya Kyanyari ambao wanashindwa kufanya shughuli zozote za kimaendeleo kutokana na hifadhi za misitu kuweka mipaka ndani ya makazi ya wanakijiji hao. Aidha katika kitongoji cha Kangamburi kuna kisima cha maji salama ya kunywa kunadaiwa kuwa kipo ndani ya hifadhi hiyo ya msitu.
Mheshimiwa Spika, taarifa zilizopo ni kwamba Serikali imetoa tangazo kuwa wananchi hao wanatakiwa kuwa wamehama eneo hilo mpaka tarehe 9/6/2016 ambapo mazao yao bado yako mashambani na hayajakuwa tayari kwa ajili ya kuvunwa . Jambo baya zaidi ni kuwa serikali haijatoa eneo mbadala kwa ajili ya wanakijiji hao ili waweze kuanza makazi mapya.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, Vipo vijiji vingi nchini ambavyo vimepimwa na vina hati lakini bado wanavijiji wanaoishi maeneo hayo wananyanyaswa sana na watendaji wa hifadhi. Iweje, serikali itengeneze miundo mbinu katika vijiji hivyo zikiwemo shule, miundombinu ya maji, barabara, umeme lakini iwafukuze kwa hoja kuwa vijiji hivyo vipo ndani ya hifadhi?
Mheshimiwa Spika, Pamoja na jitihada za Wabunge wengi kuzungumzia migogoro hii bado serikali inasua sua katika kutafutia ufumbuzi migogoro hii. Haijaonesha nia ya dhati katika kutafuta suluhu ya kudumu
Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mhe Waziri aingilie kati suala la mgogoro wa kijiji cha Nyamikoma, na na kile cha hifadhi ya Kyanyari kwa kuwa wananchi hao wameishi hapo miaka mingi sana. Serikali ihakikishe inatafuta suluhu ya kudumu kwenye migogoro kati ya wananchi wanaoishi vijiji jirani na hifadhi . Pia serikali iwachukulie hatua za kinidhamu askari wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma kwa kudhalilisha utu wa wananchi wetu.
8.1 OPERATION TOKOMEZA
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Serikali, vitendo vya ujangili vinavyofanyika nchini vimegawanyika katika makundi mawili yafuatayo:-
i. Ujangili wa Kujikimu (subsistence poaching)
Aina hii ya ujangili inahusisha watu wenye kipato kidogo na hulenga zaidi katika kujipatia kitoweo na fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji mengine. Ujangili wa aina hii huathiri zaidi wanyama wanaoliwa na si Tembo.
ii. Ujangili wa Biashara (commercial poaching)
Aina hii ya ujangili inahusisha zaidi watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha na hulenga kupata nyara zenye thamani kubwa. Wanyama wanaoathiriwa zaidi na aina hii ya ujangili ni pamoja na Tembo, Faru, Simba na Chui.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kulitambua hilo tarehe 04 Oktoba 2013 ilizindua Operation Maalum ya kupambana na ujangili huo ili kuzuia vitendo hivyo ndani nan je ya hifadhi za Taifa, katika Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu. Pia kuwatambua mapema majangili na kujua nyendo zao ndani na nje ya maeneo ya hifadhi kwa kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wahusika wakuu wa nyara hizo za Taifa.

Mheshimiwa Spika, badala ya Operation hiyo kufanyakazi kwa mujibu wa hadidu rejea tajwa, ni dhahiri hadi sasa wahusika wakubwa wa ujangili wa Biashara bado wapo na wanaendelea na biashara hizo. Waathirika wakubwa ambao kwa mujibu wa kamati maalum ya Uchunguzi ya Bunge hili hadi sasa bado hawajalipwa fidia kama ilivyoelekezwa. Je fidia kwa waathirika zitalipwa lini?

Mheshimiwa Spika, Rais wa awamu ya nne aliunda Tume maalum iliyoongozwa na Mhe Jaji Msumi ya kushughulikia suala hilo, lakini kwa bahati mbaya taarifa ya Tume hiyo hadi sasa imeishia kwenye makabati ya Ikulu na Watanzania hawakupata nafsi ya kuelewa nini Jaji Msumi aliona na kushauri, aidha hakuna hatua zozote za fidia zimechukuliwa kwa waathirika wa Operation hiyo ambao wengi walipoteza mifugo yao,walichomewa nyumba zao,walibakwa,walidhalilishwa na wengine walipoteza ndugu na jamaa zao na wengine wamekuwa walemavu.

Mheshimiwa Spika,ni muda mwafaka sasa Kambi Rasmi kutaka kuelewa ni majangili wangapi baada ya Operation hiyo kumalizika mali zao zimekamatwa na tayari kesi zao ziko mahakamani au tayari wamefungwa?

Mheshimiwa Spika, katika kuweka kumbukumbu sawa naomba kunukuu sehemu ya taarifa ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na mazingira ya mwaka 2015/16;
“Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo imewapa masuala makubwa wananchi kwa kuwa Ripoti ya Kamati ya Bunge iliyochunguza sakata hilo haikuwatia hatiani mawaziri hao bali waliwajibika kwa makosa yaliyofanywa na maafisa waliokuwa wanawasimamia. Watanzania wanajiuliza, Ripoti inasema nini kuhusu wananchi waliouliwa, wananchi walioteswa, walioporwa mifugo yao na ambao mifugo yao ilipigwa risasi? Ni busara kwa Serikali kuweka hadharani Ripoti hiyo ya Tume ya Kimahakama ili watanzania waweze uamini kama haki imetendeka kwa wote.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa suala la kuchelewa kutoa hukumu na wakati mwingine ushahidi wa kesi za ujangili kuharibiwa ni changamoto kubwa katika mapori ya akiba na Hifadhi za Taifa, Kamati inatoa rai kwa vyombo vya Serikali kama vile Jeshi la Polisi na Mahakama kushirikiana na Idara ya wanyamapori kuhakikisha watuhumiwa wa kesi za ujangili wanashtakiwa kwa kupewa adhabu kali kwa mujibu wa Sheria. Kamati haipendi kuamini kuwa kesi hizi zinahujumiwa kutokana na askari polisi na mahakimu wachache kujihusisha na vitendo vya rushwa”.

Mheshimiwa Spika, Serikali iliahidi kuwa wananchi hao watalipwa fidia lakini mpaka leo imekaa kimya. Kitendo cha kukaa kimya maana yake ni kwamba haijajali madhila wananchi wake waliyoyapata. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili kuwa ina mpango gani wa kuwalipa wananchi hawa fidia?

9. KAMPUNI YA GREEN MILES SAFARIS LIMITED
Mheshimiwa Spika, Katika hotuba ya Maliasili na Utalii iliyowasilishwa Bungeni na aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani mnamo Mwezi May 2014, alilieleza Bunge hili kuhusu uwindaji haramu usiozingatia Sheria na taratibu uliokuwa ukifanywa na kampuni ya uwindaji ya Green Miles Safaris Limited.
Mheshimiwa Spika, katika ripoti hiyo ya Kambi Rasmi ya Upinzani ilielezea kwa kina namna kampuni hii ya Green Miles Safaris Limited ilivyokuwa imekiuka Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya Mwaka 2009, kifungu cha 19(1), 24(2), (42),(47) (a),b(1),(56), 64(2), 65(1)a (i),(iv) na (v) ,na Sera ya Manyama Pori ya Mwaka 2007. Na, hivyo kupelekea Mhe Waziri aliyekuwepo wakati huo kuwanyang’anya Leseni ya kufanya biashara ya uwindaji hapa nchini. Ushahidi wa uharifu huo wa uvunjifu wa sheria ulitolewa na wahusika walikubaliana nao.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inashangaa, ni kwanini Mheshimiwa Waziri wa sasa kwa barua yake ya tarehe 9 may,2016 yenye Kumb. Na.SEC.315/563/01C/7 inaonekana kuwa inaipatia tena Kampuni hiyo kitalu cha uwindaji wakati tayari ilikwisha pokonywa leseni kwa kuwa ilivunja sheria.
Mheshimiwa Spika, kwa barua hiyo hiyo inaonesha kuwa Waziri anaizuia kufanya uwindaji kampuni ya Wengert Windrose Safaris Ltd kuacha shughuli zake za uwindaji katika kitalu cha Lake Natron Game Controlled Area (East) Hunting. Hoja hapa ni je Kampuni hii iliingiaje na kufanya shughuli zake katika kitalu hicho? Na je, Kampuni ya Green Miles ilikuwa inafanyia wapi shughuli zake hadi kampuni nyingine ikawa inafanyia shughuli za uwindaji katika kitalu hicho?
10. MALI KALE
10.1 DINOSARI KUTOKA TANZANIA (DINOSAUR FROM TANZANIA)
Mheshimiwa Spika, Kabla ya vita kuu ya kwanza ya dunia mabaki ya mjusi mkubwa ajulikanae kama dinosari yalipatikana eneo la Tendaguru mkoani Lindi mwenye urefu wa mita za mraba takribani 22. Mabaki ya mjusi huyo yalichukuliwa na serikali ya Ujerumani kwenda mjini Berlin mwaka 1918 hadi 1919 kutoka kijiji cha Mipingo mkoa wa Lindi.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti ya DW ya Januari 2016 inaonyesha kuwa watalii takribani 542,000 kwa mwaka 2015 walitembelea makumbusho ya mabaki ya mifupa ya mjusi huyu mkubwa zaidi duniani ukilinganisha na idadi ya 463,000 ya watalii waliotembea makumbusho hiyo mwaka 2014. Hii inaonyesha idadi ya watalii hao inaongezeka mwaka hadi mwaka kulingana na umuhimu wa kihistoria wa mijusi wa aina hii.
Mheshimiwa Spika, tukirejea katika kumbumbuku za mabunge yaliyopita suala la mjusi huyu lilijadiliwa na aliyekuwa Waziri wa Mali asili na Utalii Mheshimiwa Shamsa Mwangunga .Alieleza mbele ya Bunge hili kuwa serikali inafanya tathimini kujua faida na hasara za kumleta mjusi huyo nchini ikiwemo gharama za kumsafirisha na kujenga jengo la ghorofa tatu kwa ajili ya kumuhifadhi au namna ya kuzungumza na serikali ya Ujerumani ili wabaki na mjusi huyo na kisha nchi hizi zigawane mapato. Mh.Bernard Membe akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa waliahidi kulifuatilia suala hili na kuhakikisha kuwa mjusi huyu atarudishwa nchini kwa msaada wa serikali ya Ethiopia yenye wataalamu na uzoefu uliofanikisha kurudisha nguzo za kihistoria nchini humo. Mpaka leo bado mjusi huyu hajarudishwa nchini kama Waziri huyu alivyoahidi na serikali ya Ujerumani inaendelea kufaidi. Kambi rasmi ya upinzani inataka kujua ni kwanini serikali ya CCM inachukulia mzaha chanzo hichi kikuu cha mapato ambacho kingeweza kusaidia bajeti za wizara zaidi ya moja.Ambapo mpaka sasa kila mtalii mmoja anayekwenda kumuona Mjusi huyo analipia kiasi cha Euro 20 mpaka Euro 25.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na hayo hakuna mtaala wowote kuanzia shule za msingi mpaka sekondari ambao unatoa fursa kwa watoto wetu kuweza kujifunza historia ya mjusi huyu mkubwa zaidi duniani.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kutoa majibu ya kina ni kwa nini mpaka leo mjusi huyu hajarudishwa nchini na ni nini mpango wa serikali kuhakikisha kuwa mjusi huyu anarejeshwa nchini ?
11. IDARA YA MISITU NA NYUKI
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa fedha 2016/2017 idara hii na tasisi zake imetengewa jumla ya shilingi 70, 760, 767,000/- katika utekelezji wa shughuli zote ndani ya Idara hii. Katika kiwango hicho cha fedha kilichotengwa kwenye mchanganuo hakuna fedha iliyoidhinishwa kwa ajili ya kujenga vituo vya kudhibiti moto jirani na hifadhi ya misitu ili kukabiliana na mioto inayojitokeza mara kwa mara kwa sababu ya shughuli za kurina asali au ajali za moto zinazoweza kujitokeza katika hifadhi za misitu.
Mheshimiwa Spika, serikali chini ya Wizara hii haina budi kulichukua jambo hili kwa umuhimu wake kutokana na kuwepo kwa matukio ya mioto katika misitu mingi ya hifadhi nchini. Tunaharibu mazingira na kupoteza mamilioni ya hekari kwa kuwa tu vituo vya zima moto viko maeneo ya mbali na mara nyingi maeneo ya mijini.
12. MAKADIRIO YA BAJETI
Mheshimiwa Spika, Katika bajet ya Mwaka 2015/2016 Wizara ilitenga Bajeti ya Matumizi ya Miradi ya Maendeleo jumla ya shilingi 7,709,150,000 .Kati ya fedha hizo shilingi 5,709,150,000 ni fedha za nje na Shilingi 2,000,000,000 ni fedha za ndani. Katika ripoti ya Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya 2015/2016 Wizara ilipokea shilingi 1,000,000,000 mpaka Mwezi Machi 2016, zikiwa ni fedha za nje.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji Wizara ilipokea fedha za ndani kiasi gani na ilitumia kiasi gani? Je, kwa nini katika ripoti hii haikutajwa? Hali hii ya kukwepa kwepa kuonyesha matumizi sahihi ya fedha zote ambazo Wizara imekuwa ikipokea ndio haswa chanzo cha ufisadi katika wizara mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni initaka serikali kuja na majibu ya kutosheleza ni kwa nini fedha hizi za ndani hazikuonyeshwa zimetolewa kiasi gani na zimetumika kiasi gani? Serikali ituambie ni kwa nini imeendelea kukusanya fedha kidogo tofauti kabisa na mapato ambayo sekta hii ingeweza kuchangia pato la taifa kutokana na wingi wa rasilimali zilizo chini ya wizara hii?
12.1. UJENZI WA JENGO LA UTALII PHASE 11
Mheshimiwa Spika, Katika Mpango wa Bajeti wa Mwaka 2015/2016 serikali iliidhinishiwa jumla ya shilingi 1,000,000,000/- kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo hili.Serikali ya Marekani imekamilisha ujenzi wa Upande mmoja na Serikali ya Tanzania ilitakiwa kumalizia upande wa pili.
Mheshimiwa Spika, mpaka ninapoongea sasa hivi fedha hizi hazijatolewa. Hivi serikali inawezaje kunufaika na jengo hilo endapo bado ujenzi huo unasuasua. Hii ni fedheha kubwa kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi ambayo inasaidiwa lakini imeshindwa hata kumuonyesha yule anayesaidia kuwa inasaidika.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuliambia Bunge hili ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa jengo hili linajengwa na kukamilika kwa wakati ili kuondoa tabia ya serikali kuacha viporo ambavyo kimsingi vinaisababishia serikali hasara kubwa.
13. HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema hapo awali, ili taifa linufaike na utalii pamoja na maliasili za nchi yetu ni lazima Serikali iwekeze vya kutosha katika sekta hizo. Nilidokeza hapo awali kwamba ni aibu kwa taifa hili ambalo linasifiwa duniani kuwa na maliasili zenye thamani kubwa pamoja na vivutio vya utalii vilivyotia fora duniani kuendelea kuzama katika lindi la umasikini.
Mheshimiwa Spika, unapoona kuna kitendawili (paradox) kati ya utajiri tulionao na kuongezeka kwa umasikini, ujue lipo tatizo la msingi linalohitaji kutatuliwa. Na tatizo hilo si jingine bali ni ukosefu wa mfumo wa uongozi ambao umeshindwa kutumia fursa za kiuchumi tulizonazo kuondoa umasikini ili kuifikia ndoto ya taifa – ndoto ya kuondokana na umasikini.
Mheshimiwa Spika, ni aibu kwa Serikali hii inayojigamba “hapa kazi tu” wakati nchi haina usafiri wa ndege wa uhakika (No reliable air transport). Katika hali kama hiyo, ni vigumu sana kunufaika na sekta ya utalii kutokana na ukosefu wa usafiri wa ndege wa uhakika.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapata tabu kuelewa kama kweli Serikali hii ina nia ya dhati ya kupata mapato katika sekta ya utalii. Nasema hivi kwa sababu, Serikali haiko mstari wa mbele katika kutangaza utalii wa nchi yetu. Kutokana na ombwe hilo, nchi jirani kama Kenya inatumia vivutio vya Tanzania kutangaza utalii wake. Hii ina maana kwamba kama Tanzania ingekuwa imeshatangaza vivutio vyake kwa utoshelevu na dunia ikajua kwamba Mlima Kilimanjaro mathalani uko Tanzania, Kenya isingeweza tena kuutumia mlima huo kutangaza utalii wake.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuacha kufanya mzaha na maliasili ya nchi yetu. Miaka 55 ya umasikini chini ya utawala wa CCM inatosha. Kizazi cha taifa hili kinataka kunufaika na rasilimali za nchi hii na kuondokana na umasikini. Kwa sababu hiyo, tunaitaka Serikali kulieleza bunge hili, ina mpango mkakati gani wa uwekezaji katika maliasili na utalii wa nchi yetu utakaoliwezesha taifa kupata mapato endelevu na hivyo kulivusha taifa kuelekea uchumi wa kati kama Mpango wa Maendeleo wa Taifa unavyoelekeza.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.

Esther Nicholas Matiko (Mb)
WAZIRI KIVULI NA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
24 Mei, 2016
 
.....

......Soko la Ajira Makampuni ya Utalii kutawaliwa na wageni kila section kama wanyampara !!!
 
Mie kaniudhi kujumlisha miaka 55 ya Uhuru. Kamjumuisha na Baba wa Taifa (JKN) aliye hakikisha urithi wa mali asili zetu unakuja kutunafaisha kizazi hiki. Angewa taja hawa wa sasa hivi (1984 - 2016)na sio mzanaki wetu. Tofauti na hapo ipo vizuri saaanaaa.
 
Back
Top Bottom