Kidudu Mtu
Member
- Nov 7, 2009
- 64
- 0
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametaja nguzo kuu sita ambazo amesema kuwa zikitekelezwa ipasavyo zitaharakisha kasi ya maendeleo ya Bara la Afrika.
Miongoni mwa nguzo hizo ni Bara la Afrika kuhakikisha kuwa linabuni njia bora zaidi, endelevu zaidi na za uerevu zaidi wa jinsi ya kutumia raslimali zake muhimu kama vile madini na mafuta kwa ajili ya maendeleo ya watu wa Bara hilo.
Rais Kikwete ametaja nguzo hizo sita wakati aliposhiriki katika mdahalo kuhusu Fikra Mpya za Mkakati wa Maendeleo ya Afrika Rethinking Africas Development Strategy - kwenye siku ya kwanza ya Mkutano wa 40 wa Taasisi ya Uchumi Duniani ya World Ecocomic Forum unaofanyika mjini Davos, Uswisi.
Mkutano huo unaoshiriki viongozi kutoka zaidi ya nchi 30 duniani na baadhi ya viongozi maarufu na mashuhuri wa nyanja ya uwekezaji, biashara, uchumi na maendeleo duniani, umeanza leo, Jumatano, Januari 28, 2010, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Congress Centre.
Miongoni mwa washiriki wenzake katika mdahalo huo wa kwanza wa Mkutano huo wa WEF alikuwa ni Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Donald Kaberuka, Mwenyekiti na Rais wa Benki ya Exim ya China Li Ruogu na Maria Ramos, Mtendaji Mkuu wa Kundi la Benki ya Absa ya Afrika Kusini ambaye aliendesha mdahalo huo.
Akifafanua kuhusu nguzo hiyo ya kwanza ya Bara la Afrika kutumia vizuri, kwa njia endelevu na erevu raslimali zake, Rais Kikwete amesema kuwa uchimbaji wa madini na mafuta katika Afrika lazima uwasaidie Waafrika.
Ni jambo lisilokubalika kuwa madini ama mafuta yanachimbwa katika Bara la Afrika, lakini jamii zinazozunguka machimbo hayo havinufaiki na uchimbaji huo. Baadhi ya makampuni ya uwekezaji katika machimbo yanathubutu hata kuagiza maji ya kunywa, ama kuagiza chakula, ama hata kukodisha malori ya kusomba mchanga kutoka nje ya Bara hili, amesema Rais Kikwete.
Nguzo ya pili muhimu kwa maendeleo ya Afrika, kwa mujibu wa Rais Kikwete, ni umuhimu wa Bara la Afrika kuendeleza na kudumisha mageuzi ya kiuchumi ambayo yameuwezesha uchumi wa Bara hilo kukua kwa namna ya uendelevu kwa zaidi ya miaka 10 mfululizo kabla ya misukosuko ya karibuni ya uchumi duniani.
Rais Kikwete ameitaja misukosuko hiyo kuwa ni pamoja na kupanda ghafla na kwa kiwango kikubwa kwa bei za mafuta duniani, kupanda sana na ghafla kwa bei ya chakula duniani kabla ya kuanza kunyumba kwa kiasi kikubwa mno kwa uchumi wa jumla wa dunia.
Rais Kikwete ameitaja nguzo kuu ya tatu kuwa ni umuhimu wa Bara la Afrika kuendeleza uwekezaji wake katika sekta ya miundombinu, ili kuboresha kiwango cha uzalishaji wa wakulima na kuwawezesha kufikisha mazao yao haraka sokoni.
Rais Kikwete amesema kuwa nguzo kuu ya nne kwa uchumi wa Afrika kuweza kukua kwa haraka zaidi ni Bara la Afrika kuwekeza katika kilimo ambacho ni muhimili wa kati ya asilimia 70 na 80 ya Waafrika wote wanaoishi kwa kutegemea kilimo.
Kilimo kitatuwezesha kuwa na usalama na uhakika wa chakula. Tunaweza kuuza akiba nchi za nje ili kujipatia fedha zaidi za kilimo, amesema Rais Kikwete katika mdahalo huo.
Rais ameongeza kuwa nguzo kuu ya tano ya uchumi wa Bara la Afrika ni ulazima wa Bara hilo kuwekeza katika mtaji wa maendeleo ya binadamu yaani kuwekeza katika elimu na afya.
Tumewekeza sana katika elimu ya msingi. Tumefanya vizuri katika elimu hiyo, lakini elimu ya msingi ni elimu ya kufuta ujinga. Lazima sasa tuelekeze nguvu zetu katika elimu ya sekondari na elimu ya chuo kikuu. Na hasa katika elimu ya sayansi. Ni elimu ya namna hiyo itakayokabdilisha Bara letu, Rais Kikwete amewaambia watazamaji na wasikilizaji katika mdahalo huo.
Nguzo ya sita na ya mwisho, kwa mujibu wa Rais Kikwete, ni kukuza haraka ushirikiano wa kikanda (regional integration) kama kukusanya nguvu za pamoja za nchi mbali mbali kukabiliana na changamoto za maendeleo.
Akijibu swali kuhusu rushwa kama kikwazo cha maendeleo katika Afrika, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya watu nje ya Afrika wakiamini kuwa kila mtu katika Afrika, kila mtumishi wa umma katika Afrika, anakula rushwa.
Lazima tukumbe kuwa Bara la Afrika linalo mataifa 53 na mataifa haya yanatofautiana kwa namna nyingi. Ni kweli ipo rushwa katika Afrika, kama ilivyokuwapo rushwa katika sehemu nyingine duniani.
Lakini siyo kwamba kila Mwafrika ama mtumishi wa umma katika Afrika anakula rushwa. Ni vizuri tunachukua muda kujifunza mema yanayotoka katika Bara hili, amefafanua Rais Kikwete.
Chanzo: http://issamichuzi.blogspot.com/