Jinsi ya kupona mapema baada ya mwanamke anapojifungua kwa upasuaji

JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Feb 7, 2022
2,308
5,460
Upasuaji.jpg
Kujifungua kwa njia ya kawaida kuna tofauti na kujifungua kwa upasuaji. Pamoja na furaha yote, lakini kumbuka kwamba kujifungua kunakuja na mzigo mwingine hasa wa mabadiliko ya mwili wako.

Shepu itabadilika sana na utahitaji kuzoea tabia mpya. Kama umejifungua kwa upasuaj, utahitaji muda nwingi zaidi wa kupumzika.

Andiko la Dkt. Geofrey Charles 'Dkt Chale' ambaye ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akina Mama na Watoto wa Dar es Salaam linafafanua hatua mbalimbali za namna ya kukusaidia kupona mapema baada ya kujifungua kwa upasuaji:

PATA MUDA ZAIDI WA KUPUMZIKA
Kama ilivyo kwa upasuaji mwingine, upasuaji wa kujifungua unataka upumzike zaidi ili kupona mapema. Baada ya kujifungua unaweza kukaa hospitali kwa siku 3 mpaka 5 na baada ya hapo itachukua mpaka wiki 6 kupona kabisa.

Hakikisha unalala kila wakati mtoto anapopata usingizi, maana akiamka atahitaji uwepo wako.

Pata usaidizi kutoka kwa ndugu au uwe na mfanyakazi (dada wa kazi) kwa ajili ya kumbeba mtoto na kubadilisha nguo, itakusaidia kupumzika zaidi.

USIFANYE KAZI NGUMU
Unapojifungua kwa upasuaji mwili unalegea na unahitaji matunzo kama ya mtoto mdogo. Usipandishe ngazi wala kuinua vitu vizito sana. Hakikisha kila kitu unachohitaji kwa haraka kama vile nepi, pempasi na chakula kinakuwa karibu yako.

Usibebe kitu chochote Kizito zaidi ya mtoto wako. Waambie ndugu wa karibu wakusaidie kubeba maji kupeleka bafuni na vitu vingine vizito. Unapotaka kukohoa au kupiga chafya basi hakikisha unashikilia tumbo lako ili kuulinda mshono.

Ongea na daktari akujulishe ni baada ya muda gani utaruusIwa kuanza kazi zako na pia mazoezi ili kutengeneza tena shepu yako.

USIANZE MAZOEZI MAGUMU HARAKA
Fanya mazoezi mepesi, kama kutembea kila siku kadiri utakavoweza. Pia usianze kufanya tendo la ndoa mapema, subiri mpaka pale daktari atakapokuruhusu.

Usisahau pia kuwa makini na afya ya akili kama vile unavotunza mwili wako, tunza na hisia zako pia. Kuwa na mtoto mchanga itakupa hisia mbalimbali ikiwemo hasira za hapa na pale, uchovu na nyinginezo.

Zungumza na rafiki yako wa karibu namna unavojisikia au mshauri wa afya ya akili.

TUMIA DAWA ZA MAUMIVU INAPOBIDI
Ongea na daktari kabla ya kumeza dawa pale maumivu yanapokuwa makali sana. Kumeza dawa kiholela kwa kipindi hiki unaponyonyesha ni hatari.

PATA LISHE YA KUTOSHA
Mlo kamili ni muhimu sana kwa kipindi hiki unaponyonyesha na unapouguza kidonda chako. Kumbuka kwamba mtoto wako anategemea sana chakula unachokula wewe.

Hakikisha unakula aina nyingi za vyakula katika siku husika. Tafiti zinasema kwamba kutumia mboga za majani kwa wingi wakati wa kunyonyesha zinafanya ladha ya maziwa kwa mtoto kuwa nzuri na mtoto hufurahia zaidi anaponyonya.

Pia muhimu kunywa maji ya kutosha ili usipate choo kigumu au kukosa choo.

LINI MTU ANATAKIWA KUMWONA DAKTARI?
Wakati unajiuguza unaweza kupata hali ya kidonda kupata malengelenge na damu kutoa kidogo hiyo ni kawaida. Lakini ukiona dalili hizi hapa chini hakikisha unakwenda hospitalini haraka.

Dalili mbaya ni pamoja na kidonda kuwa chekundu, kuvimba na kutoa usaha, maumivu makali sana eneo la kidonda, homa kali ya zaidi ya nyuzi joto 38, kutokwa na uchafu wenye harufu kali ukeni, kutokwa na damu nyingi ukeni, miguu kuvimba, kushindwa kupumua vizuri, maumivu ya kifua na maumivu kwenye eneo la matiti.

Kama kuna ndugu au rafiki yako aliwahi kujifungua kwa upasuaji usijilinganishe naye katika kupona kwako. Kila mwanamke ana mwili wa tofauti, wekeza nguvu na hisia zako katika afya yako itakusaidia kupona mapema.
 
Back
Top Bottom