Siyo hiyo mkuu, ya mwaka 1985 anawaaga Watanzania anang'atuka anamuachia nchi Mwinyi.
Hatari ya kufarakana baada ya Nyerere
Misingi ya umoja iliwekwa na wazee
Waliepuka chuki za kidini, kikabila
Walikuwa wakarimu, wastaarabu
"NAWAELEZENI haya wazee kwa sababu huko tulikotoka, tulikotoka pamoja na wazee, wazee wa nchi tulishikamana sana".
Hiyo ni sehemu ya hotuba ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyoitoa jioni ya Jumamosi Novemba 2, 1985 katika ukumbi wa Diamond Jubilee wakati akiwaaga wazee wa Dar es Salaam baada ya kung'atuka wadhifa wa Urais.
Tangu kufariki dunia Mwalimu Julius Nyerere baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiirudia mara kwa mara hotuba hiyo kama wasia wa mwasisi huyo kwa Watanzania.
Kwa upande mwingine watu kadhaa waliopata fursa ya kusikiliza hotuba hiyo wamekuwa wakitoa maelezo yanayolenga kuonesha hekima na busara aliyokunayo Hayati Mwalimu Nyerere.
"Mwalimu alikuwa na hekima kubwa ndiyo maana aliweza kuishi na watu wa aina zote", amedai Afisa mmoja Mwandamizi wa chombo kikongwe cha habari nchini.
Aidha, Mwanadiplomasia mmoja alidai kuwa hotuba hiyo ni mojawapo ya hotuba nzito alizowahi kutoa Mwalimu Nyerere.
Uchunguzi wa gazeti hili umeonesha wananchi wengi wamekuwa na hisia tofauti kinyume na vile ambavyo mkondo wa historia unavyotaka kuelekezwa.
Uchunguzi huo pia umegundua wasiwasi walionao wananchi juu ya unakoelekezwa mkondo wa historia hasa mara baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere.
Makundi ya watu yamekuwa yakiujadili ukarimu na bashasha za wazee wa Dar es Salaam kumpokea kijana mdogo wanayetofautiana naye kidini ambao historia hiyo inajaribu kuufunika.
"Nani angestahili kupongezwa zaidi hivi sasa yule mkaribishaji au aliyekaribishwa?" Amehoji Mzee Rashid Mohammed mkazi wa Ubungo katika maongezi ya moja ya vikao vya mitaani vinavyojaribu kutafakari hali ya baadaye ya Tanzania.
Aidha, Bwana Sadiki wa Mwanyamala amehadharisha kuwa vyombo husika kujaribu kupotosha ukweli huku vikiimiza amani na mshikamano wa kitaifa ni kuitumbukiza nchi kusikofaa.
AN-NUUR pia ilibahatika kuongea na baadhi ya wananchi katika soko la Kariakoo ambao nao kama wananchi wengine walikuwa na maoni yao ambapo wengi wameshauri kujengwa kwa mahusiano ya kijamii kwa njia ya haki, ukweli na uadilifu badala ya propaganda na vitisho.
Muafaka huo umeelezwa kuwa ndio utakaodumisha amani na utulivu nchini.
"Watu wa dini zote watazamwe kwa muono sawia, malalamiko yapokelewe kwa uzito unaostahiki na yashughulikiwe", amesisitiza Amiri wa Maimamu Sheikh Juma Mbukuzi wakati akiongea na Waislamu Msikiti wa Kibo jijini Dar es Salaam.
Naye Katibu wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu Sheikh Issa Ponda aliliambia AN-NUUR kwa njia ya simu kuwa Hayati Mwalimu Nyerere aenziwe sambamba na wale alioshirikiana nao katika harakati za kudai uhuru.
"Alichokisema Mwalimu katika hotuba yake ni kile ambacho Waislamu wamekuwa wakikikumbushia mara zote wanapolalamikia kunyongeshwa kwao kulinganisha na mchango mkubwa walioutoa katika kudai uhuru wa nchi yetu". amesema Sheikh Ponda.
Mwalimu Julius Nyerere ambaye kesho anazikwa kijijini kwake Butiama alizaliwa miaka 77 iliyopita ambapo baada ya masomo yake ndani na nje ya nchi alijiunga na harakati za kudai uhuru wa Tanganyika mnamo mwaka 1952.
Chama kilichokuwepo wakati huo ni Tanganyika African Association (TAA) kilichokuwa kikiongozwa na marehemu Abdulwahid Sykes.
Pamoja naye walikuwepo wazee kadhaa wa maeneo ya Gerezani, Kariakoo na Kisutu.
Miongoni mwa wazee hao ni pamoja na Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Suleiman Takadir, Sheikh Haidar Mwinyimvua na Mzee Jumbe Mohammed Tambaza.
Wengine ni Mzee Mshume Kiyate, Mwinyijuma Mwinyikambi, Mzee Idd Faiz Mafongo, Idd Tosir, Sheikh Mohamed Ramia na wengineo.
Hayati Nyerere alichaguliwa kuwa Rais wa TAA mnamo mwaka 1953.
Mnamo mwaka 1954 TAA iligeuzwa kuwa TANU chama ambacho kilikuja kunyakuwa uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.
Kwa mujibu hotuba ya Mwalimu kwa wazee wa Dar es Salaam mwaka 1985, jina la TANU lilipendekezwa na marehemu Abdulwahid Sykes.