Jenista Mhagama, awasilisha Bungeni taarifa ya hali ya dawa za kulevya nchini Tanzania kwa mwaka 2023

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,984
12,307
IMG-20240517-WA0007.jpg

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (Kushoto) akipokea Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya Nchini kwa mwaka 2023 kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo (Kulia) katika Ukumbi wa Habari Bungeni tarehe 16 Mei 2024 Jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi - Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Jenista J. Mhagama leo tarehe 16 Mei, 2024 amewasilisha Bungeni taarifa ya hali ya dawa za kulevya nchini kwa mwaka 2023 inayoelezea mafanikio yaliyopatikana katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

Akizungumza mbele ya waandishi wa Habari Waziri Jenista amesema, mwaka 2023, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ilifanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 1,965,340.52 za dawa za kulevya aina ya heroin, cocaine, methamphetamine, bangi, mirungi, skanka na dawa tiba zenye asili ya kulevya na kuwakamata watuhumiwa 10,522.

“Takwimu za mwaka 2023
zinaonyesha mafanikio makubwa, kwani kiasi cha dawa za kulevya kilichokamatwa ni kiasi kikubwa kuliko kiasi kilichowahi kukamatwa wakati mwingine wowote nchini. Kiasi hiki ni karibu mara tatu ya kile kilichokamatwa kuanzia mwaka 2012 hadi 2022, ikiwa ni ishara ya dhamira ya dhati na utashi wa kisiasa wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupambana na janga hili” amesema Mhe. Jenista.

Aidha, amesema Serikali imepanua huduma za tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya ambapo hadi kufikia mwezi Disemba 2023, vituo vya tiba saidizi na unasihi kwa waraibu wa dawa za kulevya (MAT Clinics) vilivyohudumia waraibu 15,912 vilifikia 16, na nyumba za upataji nafuu (sober houses) 56 zilizohudumia waraibu 3,488. Pia, jumla ya waraibu 903,062 wa dawa za kulevya na vilevi vingine walipata huduma katika hospitali za wilaya, mikoa na rufaa nchini.

Waziri Jenista amesema, Serikali imeanza ujenzi wa kituo cha Taifa cha Utengamao kwa ajili ya kuwahudumia waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu.

‘Kituo hiki kitajengwa katika eneo la Itega Jijini Dodoma na kitasaidia kuwajengea uwezo waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu ili waweze kujikimu kimaisha na kuepuka kurejea kwenye matumizi ya dawa za kulevya” ameongeza Waziri Jenista.

Vilevile ameeleza kuwa, serikali imeweka jitihada kubwa katika kuzuia matumizi ya dawa za kulevya nchini kwa kuimarisha elimu na mikakati ya kukabiliana na tatizo hili kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, semina, makongamano, mikutano, vilabu vya kupinga rushwa na dawa za kulevya shuleni na vyuoni.

Ameendelea kueleza kwamba, mwaka 2023, Serikali ilianzisha kituo maalumu cha Habari na Mawasiliano (Call Centre) kilichopo makao makuu ya ofisi za DCEA ambapo wananchi wanaweza kupiga simu namba 119 bila malipo na kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya au kupata elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya.

Katika kupanua wigo wa udhibiti dawa za kulevya nchini, Serikali imefungua ofisi mpya tano za Mamlaka katika ngazi ya kanda ambazo ni nyanda za juu kusini ambayo ofisi zake ziko Mkoa wa Mbeya inahudumia mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi, Rukwa Njombe na Iringa; Kaskazini ambayo ofisi zake ziko Mkoa wa Arusha inahudumia mikoa ya Arusha, Manyara Kilimanjaro na Tanga; Pwani Yenye ofisi katika Mkoa wa Mtwara, inahudumia Mikoa ya Pwani, Mtwara, Lindi, Ruvuma na Morogoro; Kanda ya ziwa ambayo ofisi zake ziko Mkoani Mwanza inahudumia Mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Simiyu na Shinyanga, pamoja na Kanda ya kati yenye ofisi Mkoani Dodoma inahudumia Mikoa ya Dodoma, Kigoma Singida na Tabora.

Pamoja na mafanikio hayo bado serikali imeendelea kuwekeza katika udhibiti wa dawa za kulevya ambapo mwaka 2023 imenunua boti yenye kasi (Speed Boat) itakayotumika kufanya doria baharini kukabiliana na uingizaji wa dawa za kulevya kama vile heroin na methamphetamine. Uwekezaji huu unaonyesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kupambana na dawa za kulevya nchini.

Aidha, Serikali imetunga Sera ya Taifa ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Mwaka 2024 ili kuhakikisha ushiriki wa wadau wote katika mapambano haya.

“Sera hii itaimarisha udhibiti wa dawa za kulevya zinazozalishwa nchini kama vile bangi na mirungi. Pia itatoa maelekezo ya kufanya utafiti wa mazao mbadala katika maeneo yanayolima mazao haya ili wananchi wapate kilimo cha mazao halali. Zaidi ya hayo, sera hii inaelekeza kuwajengea uwezo wadau mbalimbali katika udhibiti wa dawa za kulevya na kongeza ufanisi katika mapambano haya” amesisitiza Mhe. Jenista.

Mhe. Jenista ametoa wito kwa jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya na kusisitiza kuwa elimu ya kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya inapaswa kuanzia ngazi ya familia. Wazazi na walezi waashiriki katika vita hii kwa kuwajengea misingi bora watoto wao ili wasijiingize kwenye vitendo viovu na makundi hatarishi yanayoweza kuwaingiza kwenye matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
 

Attachments

  • TAARIFA 2023 final (2)_240517_145113.pdf
    7.3 MB · Views: 3
Back
Top Bottom