Jenista Muhagama: Hotuba ya Hali ya Dawa za Kulevya Tanzania 2022

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,813
11,991
MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI
TAARIFA YA MHE. JENISTA J. MHAGAMA (MB.) WAZIRI WA
NCHI - OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU)
KUHUSU KUWASILISHWA BUNGENI KWA TAARIFA YA HALI DAWA ZA KULEVYA YA MWAKA 2022
IMG-20230530-WA0028.jpg

Ndugu Wanahabari,

Leo tarehe 30 Mei, 2023, kama ilivyo ada nimewasilisha mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya Nchini ya mwaka 2022 nikitekeleza matakwa ya Kifungu cha 60 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015, kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 15 ya mwaka 2017. Kifungu hicho kinaielekeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kuandaa na kuiwasilisha Bungeni kila mwaka Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya Nchini.

Ndugu Wanahabari,

Lengo la Taarifa hii ya Hali ya Dawa za Kulevya ni kuwafahamisha wananchi hali ya tatizo la dawa za kulevya kitaifa na kimataifa pamoja na jitihada zilizotekelezwa na Serikali katika kukabiliana na tatizo hili ikiwemo ushirikiano uliopo kati ya Nchi yetu na Nchi nyingine katika kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.
IMG-20230530-WA0027.jpg

Ndugu Wanahabari,

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Jemedari wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kupambana na tatizo la dawa za kulevya nchini kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya namba 5 ya mwaka 2015 pamoja na kufuata miongozo ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC).

Ndugu Wanahabari,

Bangi imeendelea kuwa ni dawa inayotumika zaidi nchini pamoja na juhudi za Serikali za kutaka kutokomeza matumizi ya dawa hii ya kulevya. Mwaka 2022, Serikali ilifanikiwa kuteketeza hekari 179 za mashamba ya bangi na tani 20.58 za dawa hiyo ambazo zilikamatwa katika mwaka huo. Aidha, hivi karibuni, kumeibuka tabia ya kuchanganya bangi yenye kiasi kikubwa cha kilevi kwenye vyakula kama vile biskuti, asali, juisi, majani ya chai na keki. Tukiangalia Taarifa ya Dunia ya Dawa za Kulevya ya mwaka 2022 utaona kuwa asilimia 40 ya nchi zenye matumizi makubwa ya bangi, zilikumbwa na idadi kubwa ya magonjwa ya afya ya akili, uhalifu na uvunjifu wa amani yaliyosababishwa na matumizi ya dawa hizo.

Ndugu Wanahabari,

Operesheni za ukamataji wa dawa za kulevya nchini kwa mwaka 2022, zilifanikisha kukamata tani 15.2 za mirungi, kilo 254.7 za heroin na kilo 1.7 ya cocaine. Kumekuwepo na mwendelezo wa ukamataji wa dawa ya kulevya aina ya methamphetamine ambapo kwa mara ya kwanza mwaka 2021 zilikamatwa kilo 430.8 na kufuatiwa na gramu 968.7 ambazo zilikamatwa mwaka 2022. Vilevile, mwaka 2022 tumeshuhudia ukamataji wa dawa nyingine ngeni nchini inayojulikana kama mescaline ambapo gramu 56 zilikamatwa.

Ndugu Wanahabari,
Serikali imefanikiwa kuandaa Mwongozo wa Utoaji Elimu Juu ya Tatizo la Dawa za Kulevya Nchini lengo ni kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi juu ya tatizo hili. Tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya iliendelea kutolewa ambapo kwa mwaka 2022 jumla ya waraibu 871,010 walinufaika na tiba hiyo nchini.
Aidha, Serikali imeendelea kufadhili mafunzo ya stadi za kazi kwa waraibu wanaopata nafuu ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea. Katika kipindi cha mwaka 2022, Waraibu 245 waliopata nafuu waliunganishwa katika vyuo vya VETA na Don Bosco kwaajili ya kupapata ujuzi wa kujiajiri ili wasirejee kwenye matumizi ya Dawa za Kulevya. Mafanikio haya ni matunda ya ushirikiano mkubwa baina ya wadau wa ndani na nje ya nchi pamoja na jamii kwa ujumla. Nawapongeza kwa jitihada hizi.
IMG-20230530-WA0022.jpg

Ndugu Wanahabari,

Nihitimishe kwa kutoa rai kwa Wananchi wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ikiwemo kilimo cha bangi na mirungi kuacha mara moja. Serikali itahakikisha kwamba, wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo viovu watatafutwa popote walipo na kukamatwa kisha kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake. Napenda kuwahimiza kila mtu kwa nafasi yake atimize wajibu katika kuhakikisha anatoa taarifa ya wanaojihusisha na kilimo au biashara ya dawa za kulevya na kuwasaidia wale waliopata uraibu kupata tiba.


Aidha, nawaasa vijana wa kizazi kipya na watumiaji wote wa madawa ya kulevya hususan bangi kuacha kwa kuzingatia madhara yatokanayo na matumizi ya madawa hayo, kwani vijana ndiyo nguvukazi ya Taifa.

Jenista J. Mhagama (Mb.)
WAZIRI WA NCHI - OFISI YA WAZIRI MKUU
(SERA, BUNGE NA URATIBU)
 
Mizaha mizaha hii tena ikifanywa na taasisi za serikali itasababisha wananchi wazizarau na mwishowe siku tukio halisi likitokea patakuwa na maafa makubwa.
Inanikumbusha hadithi ya kijana mmoja akichunga ng'ombe akifanya mzaha wa kuomba msaada kwa kumuona simba. Kwa siku mbili watu walikuwa wakienda kumsaidia ila wanakuta kumbe akifanya mzaha. Siku ya tatu simba kweli katokea na kijana alivoanza kuomba msaada wanakijiji wakasema huo ni mzaha wake tu.
Ilipofika jioni wanakijiji wakaona ng'ombe wakirejea wenyewe bila yule kijana, wakafuatilia na kukuta mabaki yake tu.
 
Back
Top Bottom