Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,809
- 15,443
Huwa tunaamini kwamba hakuna binadamu aliyekamilika. Hii ina maana kwamba kila binadamu ana udhaifu wake lakini udhaifu huo unatofautiana kati ya mtu na mtu.
Kuna tabia moja mbaya huwa haizungumzwi sana, labda ni kutoakana na kuonekana kama jambo la kawaida au kutotiliwa maanani na watu lakini hii ni tabia ambayo ikiachwa inaweza kuwa ni ugonjwa ambao unaweza kuhama kutoka kwa mhusika na kutembea katika familia na kuathiri hata kizazi cha mhusika.
Hapa nazungumzia udokozi wa vitu vidogo vidogo mahali pa kazi, majumbani kwa watu au kwenye mahoteli au mighahawa ambapo kwa mtu mwingine anaweza kuona ni jambo la kawaida. Huu ni udokozi mbaya sana ambao unaweza hata kumdhalilisha mtu. Kumbuka kwamba udokozi wa aina hii haujali kiwango cha kipato alicho nacho mtu.
Rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia kwamba anashangazwa na tabia ya mkewe kila anaposafiki kikazi pamoja na nafasi yake kikazi na kipato lakini lazima atarudi amefungasha vifaa vya hoteli aliyofikia. Si kwamba amepewa na wahusika, la hasha, ameiba. Nyumbani kwao kuna kila kitu na hawana shida ya hivyo vitu alivyobeba bali ni tabia ya mkewe ambayo aliigundua tangu wakiwa wachumba wakati huo wakiwa na mitoko kwenye mighahawa mbalimbali hapa jijini.
Aliniambia kwamba walikuwa kila wakitoka kwenda kula kwenye mghahawa ilikuwa aidha mpenzi wake aibe kitambaa cha kujifutia wakati wa kula (Napkins) au uma na visu, vijiko au hata vichupa vya kuwekea chumvi na pilipili manga (Salt and pepper shakers). lakini pia alikiri kwamba hata nyumbani kwao kuna vitu vingi vidogo vidogo vya ofisini kwa mkewe ambavyo alividokoa na kuvileta hapo nyumbani na vingine haina hata maana.
Si kwamba kwao wana shida hiyo, au si kwamba ametoka familia duni. Hapana ni binti ambaye amezaliwa katika familia yenye kipato cha kati na wazazi wake wana uwezo wa mahitaji yote muhimu na ya ziada ya familia kiasi kwamba wote kwao yaani watoto sita pamoja na ndugu zao wengine waliolelewa na baba yao wamesomeshwa katika shule bora hapa nchini.
Awali hakuitilia maanani tabia hii lakini hivi sasa imekuwa ni kero kwake na anahisi kama tabia hiyo imehamia kwa watoto baada ya siku moja wakiwa wametoka kula katika Hoteli moja maarufu hapa jijini Dar kumuona binti yake wa miaka mitano kabeba mwanasesere (toy) ambaye si wake na alipomdadisi akasema ameliokota pale hotelini. Yeye ili kuonyesha kwamba amekerwa na ile tabia aligeuza gari na kurudi Hotelini kurudisha yule mwanasesere na kwa Bahati nzuri alimpata mwenye mwanasesere wake. Mkewe alijitahidi kumtetea bintiye kwa kudai kwamba pale hotelini huwa kuna vitu vinatupwa baada ya wenye navyo kuondoka na kuviacha hivyo mtoto hana makossa, lakini alipinga kauli ya mkewe na kukemea tabia ile kwa kuonyesha msisistizo.
Alipofika nyumbani alimwadhibu bintiye na kumuonya kuacha tabia hiyo mbaya la sivyo atampeleka polisi kwa wizi. Alitumia vitisho ili kukemea tabia ile mbaya ambayo aliona dhahiri inahama kutoka kwa mama kwenda kwa watoto.
Naam, huenda humu wapo wenye tabia hii au wanaoishi na tabia hii. Wengi wetu tumeshuhudia watu wenye tabia za aina hii tangu mashuleni. Ni tabia ambayo isipokemewa inaweza kubakia na kuwa sugu, Huenda shuleni ikaonekana kama ni utoto, lakini kama wazazi tuna jukumu kubwa la kukagua vitu wanavyobeba watoto wetu mara warudipo kutoka shuleni au wanaporudi kutoka kucheza na watoto wenzao na kuwahoji iwapo wamebeba vitu ambavyo hatuvijui.
Kwa kukemea itasaidia kujenga tabia njema kwa watoto wetu. Tukumbuke kwamba mazoea hujenga tabia, kwa kuacha tabia ya udokozi kumea kwa watoto wetu huku tukiwasifu kwa ujanja, ni sawa na kupanda mbegu mbaya kwenye akili ya kina kwa watoto wetu ambapo watakapokua watu wazima tabia hiyo itawaathiri katika maisha yao na hata mahali pao pa kazi.
Hakuna tabia mbaya kama udokozi, kwani inafedhehesha na hata kuvunja uhusiano na wenzi wetu. Hakuna mtu mwenye tabia zake nzuri anayependa kuambatana na mwenzi mdokozi, kwani nia aibu na fedheha kwa jamii.