Ingelikuwaje Nyerere angelikuwa Mzanzibari? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ingelikuwaje Nyerere angelikuwa Mzanzibari?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Kizibao, Sep 6, 2010.

 1. K

  Kizibao JF-Expert Member

  #1
  Sep 6, 2010
  Joined: Aug 24, 2010
  Messages: 738
  Likes Received: 344
  Trophy Points: 80
  Makala hii ilichapwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti huru la Dira Zanzibar, Na. 45, la Oktoba 10-16, 2003. Nimeamua kuileta tena hapa ukumbini baada ya kuiona hii video ilowekwa jana kuhusiana na mafuta ya Zanzibar.

  TANZANIA tuliyonayo sasa ni kati ya ishara ioneshayo kuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliishi juu ya ardhi hii ya Mungu Muumba.

  Hatuwezi kuizungumzia Tanzania, chimbuko, asili, mafanikio na matatizo yake, bila ya kumtaja na kumuhusisha yeye.

  Hatuna haja ya kujenga sanamu lake kumkumbuka na kumuenzi, madhali tu Tanzania ingalipo na inaendelea kubakia hai. Tanzania ni sanamu la Nyerere linalotosha kuyaakisi maisha, mawazo, khulka na uongozi wake. Kupasi kwa Tanzania ni kupasi kwake na kufeli kwa Tanzania ni kufeli kwake.

  Hivi sasa tunaingia katika kipindi cha maombolezo ya kifo chake. Namna tunavyoomboleza katika kipindi hiki, kunatokana na vile tulivyomchukulia katika maisha yetu. Kuna waliomchukulia kuwa ni kiumbe kitukufu chenye thamani kubwa mno kiasi ya kwamba wangelitamani aishi hadi baragumu la Kiama lipulizwe. Kwao, huyu alikuwa rafiki, mpenzi, mkombozi na mwalimu. Alikuwa malaika!

  Lakini pia kuna waliomchukulia kuwa ni kiumbe mkorofi na hivyo kufa kwake ndicho kitu chema pekee alichowafanyia. Kwao, Nyerere alikuwa hasidi, adui, mkaidi. Alikaribiana na Subiani!

  Na bado kwa wengine, kuwepo na kutokuwepo kwa Nyerere hakukumaanisha chochote katika maisha yao. Hawakujuwa khabari zake, wala naye hakujuwa zao. Hawakuhisi kuwepo kwake wala sasa hawahisi kuondoka kwake. Alikuwa kile Waingereza wanachokiita non entity!

  Ndiyo, hatuwezi kuwa sote na wazo au hisia moja juu ya kitu au mtu fulani. Wala tusiwalazimishe watu wote walione jambo kama tunavyoliona sisi, maana hivyo sivyo akili za wanaadamu zinavyofanya kazi. Nyerere hakuchukiwa na watu wote, lakini pia hakupendwa na kila mtu. Alikuwa maarufu lakini si kwamba alijuilikana na kila mtu!

  Kwa Wazanzibari, hata hivyo, Nyerere hakuwa non entity, bali mtu aliyeishi na aliyemaanisha kitu katika maisha yao. Alichokimaanisha chaweza kuwa chema au kibaya kulingana na ufahamu wa mtu. Na ni kwa sababu hiyo, kwamba Nyerere alikuwa na nafasi katika maisha ya Zanzibar, Wazanzibari na Uzanzibari, ndiyo maana ninaandika makala hii kuomboleza kifo chake kilichotokea miaka minne iliyopita.

  Najaribu kugeuka nyuma kuziangalia siku zilivyopita katika uhai wa Mwalimu Nyerere. Umri na uwezo wangu ni mdogo mno kuweza kuziona zote; lakini hizi chache nizionazo, zatosha kunipa picha.

  Kwamba zake hazikuwa siku za kawaida kama za Ghassani, bali za mtu aliyekuwa mtawala mwenye ushawishi mkubwa katika mwenendo wa siasa za nchi hii, Afrika na dunia nzima kwa jumla. Nyerere alikuwa na jina na satwa kubwa!

  Mimi ni Mzanzibari. Nyerere hakuwa Mzanzibari (na sijuwi hata kama alitamani kuwa angalau kwa siku moja tu kati ya siku hizo zote alizoishi), lakini kwa udadisi wa kitoto najiuliza: hivi ingelikuwaje kama naye angelikuwa Mzanzibari? Ingelikuwaje kama angelikuwa ndiye Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar? Je, angelifikia pahala pa kuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

  Kwanza hata huu Muungano wenyewe ungelikuwepo? Na kama ungelikuwepo, nafasi ya Zanzibar ingelikuwa ni ipi kwawo?

  Nasema pengine huu ni udadisi wa kitoto tu (na mutanisamehe kwa utoto wangu), lakini katika wakati huu wa kuomboleza kifo cha mtu aliyechangia kwa kiasi kikubwa kuifikisha Zanzibar hapa ilipofika, neno hili ‘ingelikuwa' ndiyo ruwaza pekee ya kujipumbaza. Na kujipumbaza ndiko kulikobakia!

  Jibu la mwazo ninalolipata kwa maswali hayo ni kwamba, kama Mwalimu Nyerere angelikuwa Mzanzibari, basi Muungano huu usingelikuwepo. Na kama ungelikuwepo, basi yeye ndiye ambaye angelikuwa Rais wake. Na baada ya hapo, hata siku moja nchi yangu ya Zanzibar isingelifikia pahala hapa ilipo sasa, pa manung'uniko ya mkubwa kummeza mdogo.

  Nitafafanua. Kwanza, sina hakika ikiwa Mwalimu Nyerere (hapana shaka angelikuwa akiitwa Maalim Nyerere) angelimkubalia mwenzake wa Tanganyika (angelikuwa Mzee Abeid Amani Karume) kuziunganisha nchi zao. Anavyoonekana, kupitia fikra na maandishi yake, ni kwamba aliuthamini sana uhuru wa nchi yake na alikuwa anaishuku kila hatua ambayo aliidhani kuwa inatishia mamlaka na madaraka yake mwenyewe kama kiongozi mkuu.

  Kwa mfano, pamoja na sababu milioni zinazoweza kutolewa za kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, basi ile ya kuchelea nafasi na nguvu ya Tanzania katika eneo hili ni moja wapo.
  Kwa hivyo, hata kama Kijizanzibari chake kingelikuwa ni kiduchu hivi, lakini Maalim Nyerere alikuwa ni mtu aliyeujali na kuuhisi uhuru. Haielekei kwamba angeliipeleka Zanzibar sentimita moja mbele kuelekea kuupotza uhuru huo.

  Ni kweli kwamba alikuwa akizungumzia umoja wa Bara la Afrika na pia akizungumza dhidi ya ‘vidola vidogo vidogo', lakini palipohusika uhuru aujuwao yeye, alikuwa na pua kali ya kunusa harufu ya kutawaliwa. Ikijitokeza dalili tu, huigundua na mapema na akajiepusha nayo.

  Si tunakumbuka alivyounga mkono jitihada za jimbo la Biafra kujitenga na Nigeria mwaka 1967? Wakati huo ilikuwa ni miaka mitatu tu tokea Zanzibar iwe sehemu ya Tanzania, ilhali Biafra ilishakuwa sehemu ya Nigeria kwa miaka na kaka.

  Lakini kilichomfanya aunge mkono kujimegua kwake yalikuwa madai ya uhuru na haki ya kujitawala. Uhuru!
  Kwa hivyo, ni wazi kuwa kama angelikuwa ni yeye ndiye kiongozi wa kidola hiki kidogo cha Zanzibar, asingelikubaliana kamwe kuungana na jidola lile kubwa la Tanganyika. Angelikhofia uhuru wake, angelikhofia kutawaliwa tena kwa mlango wa nyuma.

  Kuna wakati aliwahi kuzungumzia The Second Scramble, kinyang'anyiro cha pili. Ilikuwa ni katika hadhara na wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, ambapo alielezea khofu yake kwa mwenendo wa siasa za kilimwengu. Kwamba namna unavyokwenda, basi Afrika ilikuwa imo katika hatari ya kunyang'anyiwa tena kwa mara ya pili na mataifa makubwa. Kinyang'anyiro cha kwanza kilichomalizika kwa Mkutano wa Berlin wa 1884-5, kiliyawezesha mataifa hayo kugawana Afrika kwa mafungu kama nyanya sokoni. Kukawa na fungu la Afrika ya Kiingereza, ya Kifaransa na ya Kijerumani.

  Basi kama Maalim Nyerere angelikuwa ndiye Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar wa wakati ule, kisha mwenzake wa Tanganyika akamjia na wazo la kuziunganisha nchi zao, angelitoa hotuba kali kwa wasomi wa Zanzibar na kisha akatunga kitabu chini ya jina la The Second Colonization, kuonesha wasiwasi na khofu zake juu ya kile ambacho kingelikikumba kijinchi chake kidogo mbele ya jinchi lile kubwa.

  Lakini hebu tuache hiyo. Natuseme kuwa kwa wakati ule Maalim Nyerere wa Zanzibar angelikuwa hana hiari illa kuingia katika Muungano na Tanganyika. Kwamba, kwa upande mmoja, siasa za ndani zilimlazimisha apate kipenu cha kujibanza ili kuyanusuru madaraka na ushawishi wake na, kwa upande mwengine, matakwa ya mataifa makubwa yalimtaka afanye hivyo.

  Bila ya shaka, pande zote mbili zingelimtanza Maalim Nyerere. Anajuilikana kwamba licha ya ujasiri wake, huyu alikuwa ni kiongozi aliyekhofu sana kupoteza madaraka na ushawishi wake. Alikuwa pia akiuhusudu sana uungwaji mkono kutoka mataifa makubwa. Kwa tabia zake hizo, kuna baadhi ya wakati alijikuta akifanya maamuzi yaliyomgharimu hata hishima na kauli yake, alimradi tu yambakishie vitu hivyo mikononi mwake.

  Mfano mmoja ni pale alipoiomba Uingereza iingilie kati kile kilichodhaniwa kuwa ni mapinduzi ya kijeshi dhidi yake, siku chache tu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 1964. Kwa tafsiri alizokuwa amezijenga ni kwamba Uingereza lilikuwa ni taifa la kikoloni na la kibeberu, kwa hivyo ilikuwa aibu kwa nchi huru kuomba msaada wa mkoloni na beberu hata miaka mitano bado tokea beberu huyo aondoshwe kwa fedheha ya kutokutakiwa nchiningwa!

  Lakini wakati huo alikuwa anatetea madaraka yake. Ubeberu na ukoloni wa Muingererza ni kitu kimoja na madaraka ya Maalim Nyerere ni kitu chengine. Panapohusika maslahi, haikuwa vibaya kwa beberu kumnusuru ‘mzalendo' huyu!

  Basi hapa napo, pamoja na sababu nyengine, angelijikuta akikabiliana na hoja na haja ya kuendeleza madaraka na ushawishi wake ndani ya nchi na wakati huo huo nia ya kuvuna sifa za mataifa makubwa. Hivyo, tunaambiwa na mojawapo ya nadharia zilizopo, kwamba ndivyo vitu vilivyouumba Muungano huu. Marekani na Uingereza zilizitumia khofu za akina Karume na Nyerere juu ya kukuwa kwa ushawishi wa akina Abdirahman Babu ili wapate muradi wao wa kupambana na Ukomunisti.

  Kwa hivyo, licha ya ujanja na akili zake nyingi, Maalim Nyerere wa Zanzibar angelijikuta ameshasukumwa ukutani na hana uamuzi illa kutenda kwa mujibu wa mwenendo wa matukio. Angelijikuta yu mtumwa wa mazingira. Kuwa mtumwa wa mazingira na kuburuzwa na mtiririko wa matukio, bila ya shaka, lilingelikuwa tusi kubwa kwa mwanafunzi huyu wa Falsafa wa Edinburgh, shabiki mkubwa wa mawazo ya Socrates na Plato.
  Lakini angelijikaza kiume kumkata jongoo kwa meno na badala yake wala asingelionekana kujuta. Kwamba hiyo ndiyo iliyokuwa khulka yake, kutokujutia makosa yake.

  Siku zote, hata kama nafsini mwake alijuwa kabisa kuwa ameshateleza, hakutaka waliomzunguka waujuwe udhaifu huo. Badala yake, alijitahidi kuonesha kuwa yeye alikuwa sahihi na sisi wengine tuliomzunguka ndio tuliokosea kulitafsiri tendo au neno lake. Mfano mmoja wapo ni njozi yake iliyopotea katika Azimio la Arusha!
  Basi, katika hali kama hiyo, hata kama angelikuwa Mzanzibari, Maalim Nyerere angelijiingiza katika Muungano huu. Lakini mara tu baada ya kuingia, angelichukuwa hatua za haraka na za makusudi kujihakikishia kuwa hapotezi zaidi ya alivyokwishapoteza.

  Kitu cha mwanzo ambacho angelikipinga kwa nguvu zake zote ni kuyatoa sadaka madaraka yake yote mikononi mwa mwenzake wa Tanganyika. Na hapa hata hainipitikii kama angelikubaliana na wazo la muungano wenye muundo wa serikali mbili. Thubutu!

  Si unajuwa usomi wake? Angelisimama akaichambuwa mifumo yote ya miungano ulimwenguni na kisha akaonesha, kwa takwimu kabisa, kwamba hakuna muungano wa aina hiyo. Angelisema aidha muungano huwa wa serikali moja (unitary) au wa shirikisho (federal). Au ikibidi kuwapo na uhusiano mwengine ni kama ule wa Uingereza na Ireland ya Kaskazini, ambao, kwa hakika, ni uhusiano baina ya mkoloni (Uingereza) na koloni lake (Ireland). Hapo angelimtaka Karume achaguwe moja.

  Na hata baada ya kukubaliana kuwa uwe huo wa serikali mbili, naamini kuwa sasa angelipendekeza na kushinikiza kuwa yeye ndiye awe Rais wa Muungano huo. Si tunamjuwa alivyokuwa mwepesi wa kutafuta huruma, kujenga hoja na kulazimisha jawabu? Angelihutubia kwa masaa matatu, bila kumeza mate, akionesha kwa vipi ni muhimu na ni lazima kwa hiki kijidola chake kidogo kupewa madaraka ya kutosha katika muungano. Angelisema kuwa kufanya hivyo kungelikuwa ni kuonesha nia njema, kwamba hakuna dhamira yoyote ya kuimeza na kuifuta kabisa Zanzibar katika ramani ya ulimwengu.

  Angeliteta na kulitetea wazo la mkubwa kuonesha mapenzi na huruma kwa mdogo ili kumfanya mdogo aamini kuwa maisha yake hayako hatarini. Angelifanya hivi kwa nguvu na sauti zake zote hadi waliopo wote wakaingia maji, wakalainika. Wakampa akitakacho. Si tunakumbuka alivyokuwa na uwezo wa kulazimisha jawabu katika mikutano yake huku akizungumza kwa kila aina ya sauti: mara gonda, mara kisauti chembamba, mara ya kawaida, mara ya kunong'oneza; kulingana na hadhira imsikilizayo na, au, uzito wa ujumbe alioupeleka kwao?

  Baada ya kufanikiwa kupata akitakacho kutoka kwa mwenzake Karume, sasa Maalim Nyerere angelikwenda mbele zaidi kuitawalisha Zanzibar juu ya Tanganyika. Kwa mfano, ili kuonesha kuwapokuwapo na utukufutukufu wa Zanzibar ndani ya muungano huo, angeliita nchi hii Zantania: Zanzibar kwanza, Tanganyika baadaye.

  Kisha wizara zote ambazo zingelikubaliwa kuwa za Muungano na muhimu, kama Fedha, Ulinzi na Usalama, Mambo ya Ndani na ya Nje, zingelikuwa na makao yake makuu Zanzibar na angelihakikisha kuwa zinaongozwa na Wazanzibari tu (au kwa mbali wale ambao angeliwaita Zanzibari-oriented, yaani waliotayarishwa kuitumikia Zanzibar).

  Hata mabalozi wanaoiwakilisha Zantania, wangelikuwa ni Wazanzibari 20 kwa kila Mtanganyika 1.
  Vipi kuhusu bendera kama utambulisho wa Taifa moja huru na lililoungana? Nadhani bendera ambayo ingelitumika aidha ingelikuwa ile ya baada ya uhuru iliyokuwa na karafuu katikati au ya Afro Shirazi Party (ASP). Kama ingelikuwa ile ya baada ya uhuru, sasa ingeliongezwa na nazi, vipande vya dhahabu na madini ya Tanzanite (yangeliitwa Zantanite). Kwani kungelikuwa na ubaya gani, na hii ni bendera tu.

  Wimbo wa taifa, je? Kuna kasida maarufu inayoitwa ‘Tala'al Badru ‘alayna' ambayo kihistoria inaaminika kuwa ilisomwa kwa mara ya mwanzo na wanawake na watoto wa Madina wakati walipokuwa wakimkaribisha Mtume Muhammad (SAW) katika mji wao baada ya kuwa amehama kwao Makka. Kutokana na historia yake hiyo kufungamana na ukweli kwamba zaidi ya asilimia tisiini na tisa ya Wazanzibari ni Waislam, basi Maalim Nyerere angelipendekeza kuwa huo ndio uwe wimbo wa taifa.

  Ambaye angelimuita mdini, shauri yake!
  Basi hapo akina Abeid Karume na Thabit Kombo, ambao wangelikuwa wametoka Mrima, wasingelikuwa na jinsi illa kukiwachia Kijizanzibari kiduchu kuwa na madaraka makubwa na Jitanganyika lao kubwa likawa limetiwa shemere. Wao wangelibakia kulalamikia ofisi ndogo tu, Lumumba: "Kambarage anajifanya mjanja!".
  Kuanzia hapo maagizo yote ya kuiendesha Tanganyika kiuchumi, kisiasa na kijamii yangelifanyika pale Kisiwandui. Wao wangelikwenda Chimwaga kuyapigia kofi na kuyapitisha tu. Kila siku wangelibakia kuazimia tu: "mara hii tukikutana, tutamueleza kuwa anavyofanya sivyo".

  Lakini siku hiyo kamwe isingelifikapo!
  Kutokana na uwezo wake mkubwa wa kiakili, nia yake ya kutokupoteza na ujasiri wake wa kuwavuna watu, Maalim Nyerere angelifahamishwa na watu wake hali ilivyo kwa wenzetu wa Mrima. Kwamba kuna watu ndani na nje ya serikali ambao hawapendezewi na jinsi alivyojikusanyia madaraka yote mikononi mwake. Watu hao walikuwa wamefikia pahala pa kuapa kuwa hawatostahmili tena kuiona nchi, iliyopigania uhuru wake kwa kucha na meno na hata ikafika kufanya mapinduzi, kwamba imetiwa shemere na nchi nyengine.

  Kwa kuwa angelilijuwa hilo, basi Maalim Nyerere angelifanya jitihada za kiakili na za kinguvu kuhakikisha kuwa ufalme za Zanzibar unaendelea kuwapo na kulindwa kwa gharama yoyote ile. Kwa mfano, ghafla moja angelilivunja Baraza la Mawaziri na wakati wa kuliunda tena, angeliwachukuwa wale wote ambao angeliwaona kuwa ni hatari kwa ufalme wa Zanzibar na kuwapa nafasi zitakazohakikisha kuwa hawakai tena Tanganyika milele.

  Wakati huo huo, kwa kuwa ulinzi na usalama ni miongoni mwa vipengele vya Muungano, basi angelitumia mwanya huo kupeleka vikosi vyetu ya jeshi katika ardhi yote ya Tanganyika. Angelihakikisha kuwa kila mkoa mmoja wa Tanganyika una kambi mbili za jeshi, ambazo zinaongozwa na kusimamiwa moja kwa moja kutoka Zanzibar. Lengo lingelikuwa ni kuwatisha wale Watanganyika waliobakia kuwa wasithubutu kuleta fyokonyoko zao dhidi ya Muungano.

  Hili kijuujuu lingeliitwa kuwa ni jeshi la watu wa Zantania (JWZ), lakini hasa lingelikuwa ni jeshi la watu wa Zanzibar, ambalo jukumu lake kubwa ni kuhakikisha kuwa ufalme wa Zanzibar unaendelea kutukuka na kutanuka. Lisingelikuwa na kamanda wala meja hata mmoja wa Kimrima.
  Tungelikuwamo akina yakhe watupu. Hapana shaka, kutokana na uchache wetu, basi ingelibidi sote tuwe majeshi, au hata kwa kupokezana baina ya wafanyakazi wa serikali na majeshi. Kwamba leo unakuwa kambini na kesho unarudi ofisini.

  Unajuwa kuna watu wengine wababe. Hata baada ya kukubaliana kuwa Zanzibar ndiyo yenye uamuzi wa mwisho kwa maswala yote ya nchi yakiwemo yale ya Mrima, kungeliweza kutokezea viongozi wengine wa Tanganyika ambao hawalikubali hilo. Kwa mfano, angelitokezea kiongozi wa Mrima kuiunga nchi yake na Jumuiya ya Misaada ya Vatican (VAT-AID?). Basi huyo angelikiona kilichomnyoa kanga manyoya.

  Maalim Nyerere wa Zanzibar angelimuambia akome kuiendesha nchi kama milki yake, kwamba asiuchezee Muungano. Kwamba Muungano ni mkubwa kuliko yeye. Na haraka angelitakiwa ajitowe katika jumuiya hiyo.
  Kamwe Maalim Nyerere asingelizingatia kuwa kujiunga huko kungelisaida kuikwamua nchi kutokana na matatizo ya kiuchumi, ambayo yeye (Maalim) ni sehemu ya matatizo hayo. Angelizingatia tu kuwa tendo hilo linahatarihsa Muungano na, hivyo, ufalme wake na utukufu wa Zanzibar. Itakuwaje bwana watu wakiuke katiba!

  Na wababe wengine kutoka Zanzibar yake mwenyewe wanaojidai kutaka serikali tatu, wangelimjuwa kuwa yeye ni nani. Hata kama angelikuwa amekwishang'atuka, basi angelifunga safari kutoka nyumbani kwake, Michamvi Kaye, na kuja moja kwa moja hadi Kikwajuni, pale Baraza la Wawakilishi. Angeliwashikisha adabu viongozi hao na kuwaambia kama hawakubaliani na Muungano huu, basi bora wahame chama na waunde chama chao. Maana sera ya chama kilichopo madarakani, na ambacho wao ni wanachama wake ni serikali mbili.

  Angeliwashambulia kwamba wao ni mahasidi wa Muungano, kwamba wanapandikiza chembe chembe za ubaguzi na kwamba kilichowasukuma ni uchoyo wao kwa wenzao wa Mrima. Kwa hakika, Maalim Nyerere angelikaribia kutokwa na machozi, kama si kulia kabisa.

  Mwisho angelimalizia kwa kuwalaani kwamba kama wangelivunja Muungano huu au kama wangeliunda serikali yao ya Zanzibar, basi yeye akifa asije akazikwa katika ardhi ya Zantania. Akitoka hapo, angelikwenda kuandika kitabu chake Uongozi wetu na Khatima ya Zantania, ambapo angelianza kwa beti za kuililia Zantania ambayo aliipenda na kuichukulia kama mwanawe mzazi.

  Angeliomboleza kuwa sasa mwanawe huyu, watu walikuwa wanataka kumtoa roho!
  Na, je, vipi kuhusu mafuta ya Zanzibar? Ama haya nina hakika kabisa kuwa yasingepata kamwe kuwa jambo la Muungano. Tungelikuwa tunachuma karafuu zetu wenyewe na tunachimba mafuta yetu wenyewe. Na kama kuna mtu kutoka Mrima ambaye angelibisha hilo na kujidai ati "mbona almasi na dhahabu ni za Muungano, kwa nini mafuta yasiwe?", basi Maalim Nyerere wa Zanzibar angelimtosha kwa jawabu.

  Angeliitisha mkutano wa waandishi wa habari kule kwenye nyumba yake ya mapumziko, Mazizini, na kuwaambia maneno mazito: "Nawatumeni mukawaambie hao wanaohoji kuchimba mafuta yetu. Kwamba Mungu aliyoiumba ni Zanzibar akawapa Wazanzibari. Akaumba na Tangayika akawapa Watanganyika. Ni sisi, mimi na mwenzangu Abeid, ndio ambao kwa matashi, haja na mahitaji yetu na watu hawa nchi hizi, tukaiumba hii Zantania na kuwapa. Kuanza hapo ndio watu hawa wakawa ni Wazantania.

  Kabla ya hapo hapakuwa na Zantania. Mafuta yetu yalikuwepo na kugunduliwa kabla ya Zantania kuwepo, lazima walijuwe hilo. Yalikuwa yetu na yataendelea kuwa yetu leo na hata milele. Ikiwa wameshachoka na yale makubaliano yaliyoiumba Zantania, wanaweza kusema, maana hili si zao la fikra za Kiungu, kwamba hazitenguki. Ni zao la fikra za kibinaadamu tu, zangu mimi na Abeid. Sasa waamue moja, ama warudi kwa kile alichowapa Mungu au waendelee na hiki tulichowaumbia sisi. Lakini sio kuingia katika eneo letu la udhibiti, umiliki na urithi".

  Salamu zingelifika na hao waliodai wangeliubana kimya. Si hasha kesho yake, ndio hao hao ambao wangeliandamana kulisifu jibu hilo la Al Hakir, Maalim Julius Kambarage Nyerere!
  Mwisho
   
 2. Sokomoko

  Sokomoko JF-Expert Member

  #2
  Sep 6, 2010
  Joined: Mar 29, 2008
  Messages: 1,918
  Likes Received: 22
  Trophy Points: 135
  Nakumbuka makala hii iliandikwa na Mohammed Ghassan jamaa anaandika kwa mtirirko mzuri ukisoma mpaka unapata raha Wallahi sijui nae amepotelea wapi!
   
 3. Companero

  Companero Platinum Member

  #3
  Sep 6, 2010
  Joined: Jul 12, 2008
  Messages: 5,474
  Likes Received: 168
  Trophy Points: 160
 4. BinMgen

  BinMgen JF-Expert Member

  #4
  Sep 6, 2010
  Joined: Jun 18, 2008
  Messages: 1,816
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 145
  Dah! huyu jamaa mwisho, Huyu alimfahamu sana Mwalimu,

  na huu ndio mtazamo wa WaZenj Nyerere.

  Na ndio mtazamo sahihi.
   
 5. U

  Ubungoubungo JF-Expert Member

  #5
  Sep 6, 2010
  Joined: Jul 28, 2008
  Messages: 2,508
  Likes Received: 24
  Trophy Points: 135
  TAMA mate chini. nyerere asingekuwa mzenji hata siku moja.
   
 6. M

  Mkandara Verified User

  #6
  Sep 6, 2010
  Joined: Mar 3, 2006
  Messages: 15,443
  Likes Received: 132
  Trophy Points: 160
  Mkuu wangu hii hoja ni Upuuzi mtupu, vioja vya hadithi za Buricheka... Utanisamehe.
  Ni sawa na kuandika kitabu ukasema - Ingekuwaje Nyerere angekuwa samaki?.. - basi bila shaka angekula binadamu wote wanaoogelea kwa sababu tu tayari umekwisha mpa mji. Hii akili kweli mkuu hizi hadithi za kufikirika wala hazina nafasi isipokuwa Disneyland!

  Listen, sii ndio nyie mnaodai Nyerere anaongozwa na kanisa? sasa kama angekuwa Mzanzibar sii angekuwa Hizbu akiongozwa pengine na Sultan maanake yaonyesha alikuwa mtu wa tamaa ya madaraka..Na iweje huyu Nyerere awe Mzanzibar bado awe na roho mbaya hali nilidhania Ubara wake ndio unampa roho mbaya..

  Nyerere angekuwa Muislaam na sijui wa asili ya Comoro au Mmachinga roho mbaya ingetoka wapi tena!. Muungano kwani usingewezekana hali yeye angekuwa Hizbu pengine hata asingeweza kuwa rais kabisa na mambo yakawa bora zaidi kwa Tanganyika na Zanzibar..

  Na Hakika Nyerere kama angekuwa Mzanzibar na pengine sii kutoka Hizbu, Basi Zanzibar ingekuwa ni nchi ya Kikomunist hadi leo maanake wangekutana wote wakomunist (wajamaa) kina Abrahman Babu, Khamis Abdallah Amir, Ali Sultan Issa, Ali Mahfoudh, Salim Rashid, Badawi Kulatein, Abdallah Kassim Hanga, Abdulazizi Ali Twala, Hassan Nassor Moyo na wengine wengi kiasi kwamba Zanzibar ingebakia kuwa North Korea au Cuba ya Afrika.

  Na hakika kutokana na kuwepo gas Songo Songo na sehemu za Mafia sii ajabu hadi leo tuna vita na bara Nyerere akidai hiyo ilikuwa sehemu ya Zanzibar, vita na Kenya akidai Mombasa ni sehemu ya zanzibar maanake yaonyesha Nyerere alikuwa mtu mwenye tamaa sana kwa sanbabu ni mbara au angekuwa mtu mzuri sana kwa sababu ni Mzanzibar.. sasa sielewi huyo Nyerere angekuwa Nyerere yupi kama angekuwa Mzanzibar!
   
 7. K

  Kizibao JF-Expert Member

  #7
  Sep 6, 2010
  Joined: Aug 24, 2010
  Messages: 738
  Likes Received: 344
  Trophy Points: 80
  Lame analysis
  Mr Mkandara hahahaaaa yaani wewe hujafahamu kabisa Muandishi ameandika nini na amekusudia nini.hizo rhetoric ulizoandika hapo zimekufanya uonekane MR.Wacha nikusaidie kidogo kwa nini muandishi ameandika Zantania baada ya Tanzania?Fikiria kwa makini ukishidwa kafanye IQ test matokeo yanaweza kukushangaza...
  Ile report inayosema watanzania wana score poor kwenye analytical reading kumbe ni kweli....
   
 8. Junius

  Junius JF-Expert Member

  #8
  Sep 6, 2010
  Joined: Mar 11, 2009
  Messages: 3,183
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 133
  Yupo Ujerumani katika idhaa ya kiswahili ya DW kwa masomo ya vitendo ya habari...ni mmoja kati ya waandishi wa kizanzibar wenye uwezo mkubwa kiuandishi.
   
 9. Junius

  Junius JF-Expert Member

  #9
  Sep 6, 2010
  Joined: Mar 11, 2009
  Messages: 3,183
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 133
  Mkuu masahihisho kidogo, mtunzi wa hicho kitabu siyo Mohammed Khelef Ghassany, ambaye ndiye aliyeandika hiyo makala ya Dira, bali kitabu hicho unachokitaja,kimeandikwa na Dr. Harith Ghassany ambaye pia ni Mzanzibari, sina hakika kama wawili hawa wana uhusiano wa damu japo hilo linawezakana.
   
 10. M

  Mkandara Verified User

  #10
  Sep 7, 2010
  Joined: Mar 3, 2006
  Messages: 15,443
  Likes Received: 132
  Trophy Points: 160
  Mkuu wangu IQ haipimwi kwa kufikiria mtu fulani kama angekuwa hivi angekuwaje?.. Labda wewe mwenye IQ nambie ungekuwa mwanamke ungekuwaje?..
   
 11. Kichuguu

  Kichuguu Platinum Member

  #11
  Sep 7, 2010
  Joined: Oct 11, 2006
  Messages: 7,202
  Likes Received: 863
  Trophy Points: 280
  Nimemsamehe mwandishi kwa vile alikiri kuwa alikuwa na mawazo ya kitoto. Msingi mkubwa wa hoja yake ni kuhusu madaraka, kudhani kuwa muungano ule ulifanyika kusudi Nyerere awe na madaraka juu ya Zanzibar, lakini anasahau kuwa Nyerere hakuwa anapenda madaraka namna hiyo anavyodhani. Nyerere ndiye rais wa kwanza Afrika kiuachia madaraka kwa hiari tena kwa amani, kwenye ile rasimu ya kwanza ya kuunda shirikisho la afrika ya mashariki, Nyerere alikuwa anataka Mzee Kenyatta ndiye awe rais wa shirikisho, na Nyerere mwenyewe awe mwakilishi nchi za nje. Mojawapo ya sababu ambazo Nyerere alikuwa akipgia debe kubwa sana kuacha muungano katika hali yake ya leo ambapom Zanzibar wana serikali yao ndnai ya Muungano ni kuwapa huru wa kujiamulia. Kwa nini aliua serikali ya Tanganyika? kwa sababu ilikuwa ni gharama isiyokuwa ya lazima; Tanganyika haikuwa na wasiwasi wowote wa kuonekana imemezwa kama ambavyo Zanzibar inavyojiona leo.
   
 12. Mtu wa Pwani

  Mtu wa Pwani JF-Expert Member

  #12
  Sep 7, 2010
  Joined: Dec 26, 2006
  Messages: 4,095
  Likes Received: 27
  Trophy Points: 135

  Dr usitudanganye Nyerere alikuwa ni sungura mjanja nauma na kupuliza.

  ni muhuni tu japo kwa wengine ni malaika
   
 13. Zungu la Unga

  Zungu la Unga Member

  #13
  Sep 7, 2010
  Joined: Nov 26, 2008
  Messages: 40
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Ni uongo kudai kuwa Nyerere alikuwa Rais wa kwanza Afrika kuachia madaraka. Kulikuwa na Kaunda aliyekubali vyama vingi na kukubali matokeo ya uchaguzi na kuachia madaraka baada ya kushindwa. Si huyu aliyekuwa ana-control serikali mpaka kifo chake.
   
 14. K

  Kizibao JF-Expert Member

  #14
  Sep 7, 2010
  Joined: Aug 24, 2010
  Messages: 738
  Likes Received: 344
  Trophy Points: 80
  Woo naona bado hatujafahamiana
  Hiyo angekuwa hivi au vile yeye muandishi ameshasema kuwa ni mada ya kitoto kwani haiwezekani kabisa kama nyenye kuwa mzanzibar lakini ameajaribu kuonyesha jee kama nyere angekuwa mzenj basi huu muundo wa muungano ungekuwa tofauti na ulivo sasa na ndiyo maana muandishi akalileta jina la Zantania badala ya tanzania.Sasa tunataliwa kutumia logical thinking kwani amezungumza hivyo huku huku akiwa amekiri haiwezekani.so i it up to us to use aor ability to visualize, articulate and making sence wahat does he really mean based on available information.lakini wewe leo unaja na maelezo kama wazanzibar wanaomba nyerere angekuwa mzazibar.sifikirii kamawazanzibar wana mawazo hayo hata ukienda kumuuliza mtoto wa darasa la kwanza kama akiambie vyerere amepewe uzanzibar basi ahatokubali.
  Kama ulivyo suggest hapo mimi kzmz ingekuwa mwanzmke vitu vingi sana vigebadilika kutokana na mila za kwetu ningekuwa nimeshapea mke mara baada ya **** liza kidacho cha nne na nafasi ya kuchukua PhD ingekuwa ndoto tu.
  Sasa katika maelezo yako wewe umetumia low probability explanations.
  Kwa hivyo fikiria upya jinsi namna ganu muungano wetu ulivyoundwa na katika conditio gani na matatitizo tuliona nayo leo....na siyo unakuwa too superficial
   
 15. M

  Mkandara Verified User

  #15
  Sep 7, 2010
  Joined: Mar 3, 2006
  Messages: 15,443
  Likes Received: 132
  Trophy Points: 160
  Kizibao,
  Mkuu wangu siku zote ni wewe p[eke yako ndiye unaweza kusema kama ungekuwa hivi au vile huwezi kufikiria mtu mwingine angekuwa vile angekuwa vipi kwa sababu huwezi ku visualize vitu ambavyo tayari vimekwisha tokea ili kubadilisha past result kwa jinsi unavyofikiria wewe ila logic hutumika kutazama what might happened if certain policies or strategies zingetumika. Kwa mfano Kama Nyerere asingekuwa Mjamaa lakini kumwondoa mtu mahala pamoja na kumweka pengine unaondoa logic kwani kule alikoondoka inatakiwa awepo pia ili dhana yako ikamilike.

  Chkulia mfano wa huyu mwandishi unaosema kama Nyerere angekuwa Mzanzibar.. Mkuuu wangu huoni kama hapo ameondoa na ku alter tayari historia ya Uhuru wa bara alipomwondoa Nyerere ambaye amekuwa Mzanzibar. Sasa utazungumzia vipi Muungano ikiwa Nyerere wa bara hayupo tena ila huyo wa Zanzibar na pengine bara sii huru au rais wake sijui ni AbdulWahid Sykes ambaye anakuja kufa mwaka 1968. Hivi kweli unaweza andika Historia ya nchi kwa fikra kama hizi kweli ati una visualize.... Aaammmmhhhhhhhh!

  Mkuu wangu habari nzima ya Nyerere kuwa Mzanzibar ni ufinyu wa kufikiri hakuna cha logic wala upuuzi wowote. Sasa jisome wewe mwenyewe ulipo suggest kama wewe ungekuwa mwanamke.. Umesema vitu ambavyo vingebadilisha maisha yako wewe (ingawa sikukusoma vizuri) na sii maisha na mazingira ya watu wengine. Na wakati huo huo unaacha room ya kukutokea vitu vingenevyo (umetumia tu mila) kama vile kutopata kuolewa kwa sababu huna sifa za Mke..Yaani una tabia mbaya, changudoa au sura kaa pacha wa Dr. Remi na kadhalika...haaa! haa! haa! baada ya kuchangnyikiwa na maisha matokeo yake ukaamua kujiua na hii leo tulipo hapa usingekuwepo dunaiani.

  I mean mkuu huoni kaa huu ni ujinga kufikiria vitu ambavyo havijengi isipokuwa ndoto za mchana mchana tena ktk kijiwe kama hiki.

  Aaaah pengine ndivyo Wanzanzibar mnavyofikiria na kupima hizo IQ, lakini kusema kweli mimi sijui Labda nisema Nyerere angekuwa Mzanzibar bila shaka angekuwa shoga kulingana na mila zetu.. au bado nimekosea nako!.. nayo sii inakubalika au only alichoandika huyo msomi ndio chenye logic ya kuwa na Nyerere wawili sehemu mbili ili kukidhi kile alichtaka kukijjenga kwa faida ya sehemu moja.

  Na Ramadhan hii ni sawa na mimi kufikiria kama Mtume Muhammad angekuwa Mtanzania basi nianze kuijenga fikra za Tanzania hiyo ya Macca na Madina ndani ya Tanzania....Ama kweli tumekosa kazi.
   
 16. Kichuguu

  Kichuguu Platinum Member

  #16
  Sep 7, 2010
  Joined: Oct 11, 2006
  Messages: 7,202
  Likes Received: 863
  Trophy Points: 280
  Sisemi kuwa Nyerere alikuwa Malaika, bali ni lazima tukubulai kuwa alikuwa ni binadamau aliengalia maslahi ya nchi kuliko yale ya kwakwe mwenyewe. Kuna makosa ya Nyerere kadhaa ambayo hadi tunayo leo, lakini makosa hayo hayaondoiukweli kuwa hakuwa na tamaa ya madaraka namna hiyo. Kama alikuwa anatawala Tanganyika ilikuwa kubwa vile hakuna sababu ya kutamani Zanibar ambayo ni karibu sawa na visiwa cha Ukerewe na Ukara kwa pamoja.


  Hapana, Kaunda aliruhusu vyama vingi wakati Nyerere akiwa keshastaafu siku nyingi sana, na vile vile Kaunda alishindwa uchaguzi. Ungekuwa unajua historia ya siasa za afrika nadhani ungefahamu kuwa nchi zote zilizoruhusu mfumo wa vyama vingi hazikufanya hivyo kwa hiari bali ni kwa sababu ya kulazimishwa kutokana na kuanguka kwa utawala wa kikomunist wa Urusi uliokuwa ni kinara wa kuwa na walichoita Vanguard Party. Nyerere aliondoka madarakani wakati Urusi bado ina nguvu.
   
 17. K

  Kizibao JF-Expert Member

  #17
  Sep 7, 2010
  Joined: Aug 24, 2010
  Messages: 738
  Likes Received: 344
  Trophy Points: 80
  Si mchezo kumbuka hiyo maada ya mwanamke umeileta wewe na nashangazwa sasa na hizo chuki zako kwa wazinzibar na mpaka ukaniwe mimi ni miongoni mwa hao wanzanzibar. hatati kweli kweli...Muandishi amesema kama nyerere angekuea mzanzibar kinadharia tu.. na ilikiuweza kufikisha ujumbe wake kwa lile alilolikusudia..kwa sababu hivi sasa wazanzibar wengi wanaona muungano unaipendelea T.bara.so kiongozi wa tanzania Tanganyika wakati na tanzania mara baada tu ya kupata uhuru.na katiba ya tanganyika ndiyo iliyotumika kuwa kama akatiba ya mpito ya muungano.sasa utaona hapo ya kuwa nyerere alikuwa anavutia ule upande ambao uko kwake na matokeo yake ndiyo kama tunavyoyaona. pengine alifanya hivyo kutokana na kuwa ushawishi mkuu sana wa kisiasa.sasa wakati ule kama nyerere angekuwa mzenj basi naona T. bara ingekuwa inalalamika sasa hivi baada ya zanzibar.Mwisho nasema muandishi alikuwa anamaanisha Hizi nchi mbili zilipounganishwa Nyerere alivutia sana kwake au alijipendelea na ndio matatizo yote yalipoanzia.
  Na mwisho kijana mkandara siyo mwalimu tu Hata wewe leo ukienda Zanzibar magari yataanza kukupigia honi na nakupa wiki moja tone ya sauti yako itaanza kubadilika na Mrs somebody
   
 18. K

  Kizibao JF-Expert Member

  #18
  Sep 7, 2010
  Joined: Aug 24, 2010
  Messages: 738
  Likes Received: 344
  Trophy Points: 80

  Samahani lakini naona kijana huna Idea ya kile unachokizungumza.nenda kasome maada iko hapa JF inaitwa Questioning Mwalimu is of benefit to our understanding.baadae njo kwenye hii mada tutajadili
   
 19. J

  JokaKuu Platinum Member

  #19
  Sep 7, 2010
  Joined: Jul 31, 2006
  Messages: 12,730
  Likes Received: 4,949
  Trophy Points: 280
  ..mimi nadhani hizi zote ni mbinu tu za wa-Zenj kutengeneza adui wa nje ili waweze kuungana.

  ..matatizo ya Zenj yalikuwepo tangu Mwalimu hajaingia ktk ulingo wa siasa. tatizo kubwa hapo ni historia ya UTUMWA,UBAGUZI,na USULTANI, ambayo Mwalimu hahusiki nayo kabisaaa.

  ..kama wa-Zenj hawataki Muungano basi wanaweza kupiga kura ya maoni kama walivyofanya ktk suala la kuanzisha serikali ya mseto.

  ..pia kama kuna suala ktk muungano wanaona linawaumiza wanaweza kuliondoa kama walivyo ondoa suala la Mafuta.

  ..these ppl have too much time for politics. husikii hata siku moja wakijadili masuala mengine ya maendeleo kwa mfano, kilimo, uvuvi,miundmbinu. WHY? wa-Tanganyika tukiwaiga hawa kwa kweli itakula kwetu.
   
 20. M

  Mkandara Verified User

  #20
  Sep 7, 2010
  Joined: Mar 3, 2006
  Messages: 15,443
  Likes Received: 132
  Trophy Points: 160
  Kwa hiyo wewe ni mrs Somebody? - ndio maana sikukuelewa toka mwanzo.
   
Loading...