Naona tunapotezeana muda na Taifa letu haliwezi kujifunga katika nyuzi za kashfa miezi nenda miezi rudi. Haiwezekani watu wale wale waendelee kutuumiza vichwa kana kwamba katika Jamhuri mzima wenye akili timamu ni wao tu!
Binafsi siyo tu nimechoka na kuandika kuhusu kashfa lakini nimechoka na majina yale yale hadi inakuwa kama uchuro!
Mgonja
Chenge
Rostam
Lowassa
Wanatoka sayari gani hawa kiasi kwamba kuwaondoa hadi tuliite Bunge la Mbinguni? Wana maslahi gani kwenye ofisi za serikali kiasi kwamba wanaweza kuendelea kuendeshwa katika magari ya serikali kama vile malaika wa kheri?
Mhe. Rais, sijakuomba vitu vingi muda mrefu ila sasa naomba nilete ombi rasmi, vunja baraza unda jipya. Jipya siyo kwa sababu ya uundwaji wake bali jipya kwa watu watakaokuwemo, majukumu yatakayosimamiwa nayo, na uwazi na uwajibikaji wa wananchi hao.
Kwa miaka nenda rudi tumekuwa na wanaume kama mawaziri wakuu, inatosha majaribio hayo, naamini Taifa letu liko tayari kuwa na mama ambaye anaweza kusimama na kufanya kweli maana inawezekana kwa kuwaangalia kina baba zaidi tumefunga macho kuona vipaji vingine!
Tengeza Baraza ambalo siyo tu litakuwa ni msaada kwako, bali litakuwa na lengo moja kubwa nalo ni kupiga vita ufisadi katika kila nyanja na sekta. Kupiga vita upotevu (isomeke ukwapuaji) wa fedha za serikali na matumizi mabaya ya ofisi na madaraka.
Mhe. Rais unasimama katika wakati wa pekee wa historia yetu, Watanzania hata wasiokubaliana na wewe au wasiokipenda chama chako kilichogubikwa na kashfa hizi nyingi ndani ya serikali yake, bado wanakuangalia wewe kama kiongozi wa Taifa lao.
Wakati huu wa pekee na ambao bila ya shaka ni wa tunu, unakutaka wewe kusimama hata ikibidi peke yako kufanya maamuzi machungu kama vile Rambo alivyojishona kidonde chake baada ya kuanguka toka kwenye genge (Kwenye First Blood - I hope you saw the movie.. )na wewe ushone kidonda cha kujitakia na ambacho kinazidi kujeruhiwa kwa mlundikano wa kashfa!
Bado ninaamini kuwa ukitaka kusafisha serikali yetu unaweza. Hauhitaji kibali cha kiumbe mwingine yoyote yule duniani, na hauhitaji kusikiliza ushauri wa mizimu na mapepo!
Katika hili lazima ujisikie mpweke na peke. Ujisikie kama mtu aliyeachwa nyikani na rafiki zake, wakati huu ni lazima ubakiwe na machozi ya uchungu kwani uliyekula naye chakula, ndiye amekuinulia kisigino!!
Mhe. Rais ongoza Taifa katika vita vya ufisadi, vita ambavyo maadui wako ndani ya serikali yako! Ni wewe uliye Amiri wa majeshi yetu yote! Pigana mwana wa Tanzania, na ufanya kama alivyofanya Wallace kwenye "Braveheart"! Pambana usirudi nyuma.
Vinginevyo, nafasi hii ikipotea, siyo tu wataanguka wasaidizi wako, bali na wewe mwenyewe utaanguka kama gunia la lumbesa kwenye kona za Tandale! Utabwaga chini kama manyanga ya wazaramo!
Jifunge kibwewe Kikwete, uliomba kazi, ifanye!