IGUNGA, TABORA: Waganga wa kienyeji wawili wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kupiga ramli chonganishi

Kunguru Mjanja

JF-Expert Member
Aug 22, 2012
2,036
3,929
Waganga wawili wa tiba mbadala na watu wengine watano wanashikiliwa na polisi wilayani Igunga mkoa wa Tabora, kwa tuhuma za kupiga ramli chonganishi na kuchoma moto nyumba tatu

Kutokana na kitendo hicho, familia za nyumba zilizochomwa zimekosa makazi na kuhifadhiwa na wasamalia wema.

Kwa upande wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Willibrod Mutafungwa, aliwataja wanaoshikiliwa ni waganga hao Chemani Ndishiwa (79) na Nzali Mayunga (40). Wengine ni Masanja Seni (65), Kasura Msomi (31), Michael James (19), Dotto Lukelesha (41) na Samuel Jonas (18), wote wakazi wa Kijiji cha Mwakwangu Kata ya Igurubi.

Mutafungwa alisema tukio hilo lilitokea Jumanne majira ya usiku katika kijiji cha Mwakwangu na kuwa baadhi ya wananchi walikwenda kwa waganga hao wawili kupiga ramli na kuambiwa kwamba katika kijiji hicho, kuna baadhi ya familia ni wachawi.

Kwa mujibu wa Mutafungwa, baada ya kuelezwa hivyo, ndipo waliamua kukodi vijana kwa kuwalipa fedha ambazo hata hivyo, kiasi chake hakukitaja na ndipo vijana hao walikwenda hadi kwenye nyumba ya Luli Lukeresha na kuchoma makazi yake.

Alisema baada ya kufanya unyama huo, walikwenda tena kwenye sehemu zingine ambazo hakuzitaja, ambako nako walichoma nyumba moto na kutoweka kusikojulikana, hivyo kutoa taarifa kituo cha polisi Igunga.

Kamanda Mutafungwa alisema baada ya kupata taarifa hizo, alimwagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Igunga kwenda katika kata hiyo na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilaya ya Igunga, Meshack Sumuni, aliongozana na askari kumi kwenda eneo la tukio na kuendesha msako mkali.

Kamanda huyo, alisema katika msako huo walifanikiwa kuwakamata waganga hao wawili na vijana waliokuwa wakituhumiwa kukodiwa kwa kupewa fedha kuchoma nyumba na kufanya mauaji.

Alisema waganga hao walikamatwa na vitu mbalimbali vya kupigia ramli chonganishi vikiwamo vibuyu, mikia ya wanyama na fedha za nchi mbalimbali.

Aidha, Kamanda Mutafungwa alisema jeshi lake linawatafuta watuhumiwa wengine na kuwataka wananchi kuwapuuza waganga wanaoendelea kupiga ramli chonganishi sambamba na kutoa onyo kali kwa vijana wanaotumiwa na baadhi ya watu kuacha tabia ya kuchoma nyumba, akisema kwa kuwa Jeshi la Polisi litakabiliana nao.

Mutafungwa alisema kwamba familia zilizokosa makazi zimehifadhiwa na majirani na kwamba watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani leo

Chanzo; Nipashe
 
Back
Top Bottom