Wanabodi,
1. Naona wengi mmeuona huu upungufu wa hotuba za JK kama nilivyowahi kuchangia huko nyuma na kumshauri atafute Mwandishi mwingine mahiri au yule aliyepo "ajifue zaidi" (ndiyo maneno niliyotumia).
BTW, ninavyokumbuka mimi, mwandishi wa hotuba wa BM alikuwa Balozi Tuvalo Manongi (alipelekwa UN na BM kabla hajaondoka madarakani-kama ni shukrani sijui! Kama pia alivyompa hadhi ya ubalozi Bw Kallaghe mwisho mwisho wa madaraka yake).
2. Huenda mifano ya hotuba za kwenye dhifa si mizuri sana kwani kwa kawaida, na inafahamika na hata kufundishwa hivyo kwenye diplomasia au uhusiano wa kimataifa, kuwa kwenye dhifa za kitaifa huwa ni "maneno maneno ya kusifiana, ili msiharibiane hamu ya kula na kunywa"; naweza kusema hapo blah blah inaruhusiwa. Hivyo huwa hakuna ujumbe mzito; hapo si mahala pake. Hata hivyo, pamoja na muktadha huo, binafsi ningependa kusikiliza hotuba yenye kuvutia na kuchangamsha; isiwe kavu, iwe na misemo miwili mitatu, na hakika ikiwezekana ikumbukwe siku zijazo, hata kama ilitolewa kwenye dhifa ya kitaifa.
3. Kama taifa, tuangalie uwezekano wa kuingiza kwenye mfumo wa elimu yetu namna ya kuwajengea uwezo watu wetu (wanapokuwa wanafunzi) namna ya kuongea kwenye hadhira mbalimbali (public speaking) kwa kujiamini. Tuliosoma zamani nakumbuka mambo ya "debate" mashuleni. Siku hizi ni shule chache tu wanafanya hivyo, sana sana hizo "academy" au "international schools" za Bongo. Kwa ujumla, binafsi naona tuna tatizo kubwa sana la "effective public speaking", kuanzia kwa wengi wa wahadhiri wetu mpaka hao wanasiasa. Kwa mtazamo wangu, hata mapadri na wachungaji wengi siku hizi hawana hotuba/mafundisho ya kuvutia kama ilivyokuwa zamani.
4. Binafsi, namuona BM kama "intellectual" (japo halikuwa lengo la mchokoza mada kujadili hili, lakini maadam limetokea ngoje tutoe hisia zetu!). Hii ni kutokana na hotuba zake hasa zile za kuandikwa rasmi. Bila shaka ndiyo maana alitunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Uandishi (Doctor of Letters) pale Open University of Tanzania. Nina mpango wa kukusanya hotuba zake ambazo zilichapishwa kama kitabu ili niwe nazipitia tena na hata "kuzifanyia shule".
Nimewahi kuwasikia baadhi ya maprofesa wa hapa Dar pia wakikiri kuwa BM ni "kichwa", msomi, na hazina kubwa ya taifa. Bila shaka ndiyo maana jamaa wa nje wanamtumia.
Nimewahi pia kuhudhuria hafla wakati BM akihutubia. Hakuwa mkavu sana; hakika alichekesha/kufurahisha hadhira kwa maneno yake. Na hapo alikuwa tofauti na hotuba alizokuwa anasoma za kila mwisho wa mwezi. Nyingi ya hizo zilikuwa kavu sana. Kwa ujumla pia nadhani BM alibadilika na akawa mahiri zaidi kadri alivyokaa madarakani. Huenda JK naye atakuja kuwa hivyo.
Pamoja na kumuona BM kama "intellectual" sina hakika kama alikuwa kiongozi mzuri. Sana sana alikuwa mtawala Mpaka sasa naamini kuwa mtu anaweza kuwa "intellectual" lakini asiwe kiongozi au mwanafalsafa. Wachache wanajaaliwa vyote, na hao ndio kina Nyerere na Ghandhi.
Mwisho, kama nilivyomshauri JK huko nyuma, aachane na ufunguzi wa mikutano na makongamano na warsha na semina "ndogo ndogo". Ahudhurie ambazo ni za muhimu kisera au kimkakati, ambazo kwazo, atatoa ujumbe mzito kwa taifa au jumuiya ya kimataifa. Vinginevyo ndiyo maana atakuwa anaishiwa maneno, anaonekana mwepesi.