Bado naamini kuwa ili kupata Katiba bora itakayoweza kutuunganisha ni lazima iwe ya maridhiano, si kwa wingi au uchache wa waungaji mkono. Bado pia naamini kuwa si mfumo wa Serikali mbili au tatu utakaotatua kinachoitwa kero za muungano na hasa kama tutauchukua bila maridhiano ya pande zote. Bahati mbaya sana maridhiano haya yanaongozwa na wanasiasa, kwani matakwa ya kisiasa (political will) ndiyo kuu katika suala hili.
Kuyapata maridhiano ni la kutokane na kuaminiana kwa Wajumbe na mchakato ulio sahihi unaokubalika na pande zote. Nikiangalia jinsi mambo yanavyokwenda, hivi vyote havipo. Sijaona Wajumbe wakijadili hoja bali misimamo. Mchakato wenyewe unaonekana kupingwa na pande zote ikiwemo hasa ule wa msingi wa tunda wanalojadili huko Dodoma! Kama hawaamini mchakato wa tume ya Katiba (na Wajumbe wake kwa pamoja na binafsi) na tunda lake sijui watafikiaje maridhiano na hasa sijui wanachokifanya Dodoma. Tunaona mashindano ya kupata mshindi na mshindwa ndani na nje ya bunge. Hii ni bahati mbaya kweli kweli!
Misimamo ya makundi na hasa ya kivyama imevuruga sana mchakato huu. Imefanya Wajumbe na watu nje ya bunge kuhairisha kufikiri na kusimamia misimamo hii. Imani zimekuwa kwenye misimamo hii. Mjumbe anasimama na kuanza kwa kutamka yeye ni 'muumini wa dini' gani - mbili au tatu! Ukisikiliza hoja anazotoa unabaki kinywa wazi kama anaelewa maana ya mfumo anaouchagua.
Sijasikia mjumbe ambaye ameongelea kwa kina ni masuala gani ya muungano, ama ndani ya Serikali tatu au mbili yatauimarisha muungano wetu. Muungano umefikisha miaka 50 badala ya kuuimarisha kwa kuongoza mambo tunayoshughulikia na kusimamia kwa pamoja eti tunayapunguza na kujitapa kuwa tunaimarisha muungano!
Mungu atubariki, tupite salama.