Informer
JF-Expert Member
- Jul 29, 2006
- 1,582
- 6,627
- Thread starter
- #1
Historia ya jina la Kariakoo na soko la Kariakoo inaanzia tangu enzi za ukoloni wa Mjerumani wakati Tanzania Bara ikiitwa Tanganyika.
Mahala lilipo soko hilo palijengwa jengo la utawala wa Wajerumani ambalo lilikusudiwa litumike kama ukumbi wa kuadhimisha sherehe za kutawazwa kwa Mfalme Kaiser Wilheim wa Ujerumani kwa wakati huo.
Hata hivyo baada ya jengo kukamilika halikutumika kama ilivyokusudiwa kuwa na badala yake lilitumika kama kambi ya kikosi cha wapagazi waliobeba mizigo ya vita kuu ya kwanza ya dunia waliojulikana kama Carrier Corps.
Jina hilo la maaskari wabeba mizigo katika Kiswahili lilitamkwa karia- koo na liliendelea kutumika kama jina la eneo lote linalozunguka jengo hili la Soko la Kariakoo.
Baada ya vita kuu ya kwanza ya dunia kuisha rasmi mwaka 1919 na nchi Tanganyika kuanza kutawaliwa na Uingereza, jengo hilo lilianza kutumika kama soko na kuhudumia wakazi wa Dar es Salaam. Wakati huo wafanyabiashara walikuwa wakiuza bidhaa zao sakafuni kwa sababu hapakuwa na meza. Wafanyabiashara hao waliendelea kufanya biashara zao sakafuni hadi miaka ya 1960, meza za saruji zilipojengwa. Kwa kadiri jiji la Dar es Salaam lilivyokua na wakazi wake kuongezeka, ndivyo soko hilo lilielemewa kuhudumia wananchi.
Hali hiyo iliwafanya viongozi wa halmashauri ya jiji kuona haja ya kuwa na soko kubwa na la kisasa kulingana na maendeleo ya jiji, na hivyo wakaanza kujadili uwezekano wa kujenga soko jipya kubwa na la kisasa.
Ujenzi wa soko
Uamuzi wa kujenga Soko Kuu la Kariakoo ulifanywa na serikali mwaka 1970 ambapo Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam iliagizwa kujenga soko jipya la kisasa ambalo lingechukua nafasi ya soko la zamani.
Matarajio ya serikali ya kujenga soko hilo yalikuwa ni kuwapatia wakazi wa jiji soko kubwa la chakula ambalo lingetosheleza mahitaji yao kwa muda wa miaka 50 hadi 70 Mipango ilikamilika na ujenzi ulianza rasmi Machi 1971.
Ramani ya jengo la soko ilitayarishwa na mchoraji wa ramani za majengo Mtanzania Beda Amuli. Kwa mujibu ya machapisho yanayoelezea historia ya soko hilo, mkandarasi huyo alitakiwa kwenda kujifunza katika nchi za Accra – Ghana na Lusaka-Zambia, kuangalia masoko yaliyojengwa katika miji hiyo miwili, ndipo atengeneze ramani yake, ambalo ndiyo soko linaloonekana hivi sasa. Mkandarasi aliyechora jengo hili ameweka baadhi ya maumbo yanayofanana na majengo hayo aliyokwenda kuyatazama. Hii ndiyo sifa pekee inalolifanya soko hili la Kariakoo kuwa la tofauti na masoko mengine katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
Ujenzi wa soko ulikamilika Novemba 1975 kwa gharama ya shilingi milioni 22 na kufunguliwa rasmi Desemba mwaka huo huo ambapo Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa mgeni rasmi.
Zaidi:
1) Soko la Kariakoo lateketea kwa moto
2) TANZIA - Mzee Beda Amuli, mbunifu na mchoraji wa majengo, likiwemo Soko la Kariakoo afariki dunia