Historia ya Nkurunziza na Burundi yake

The Genius

JF-Expert Member
May 29, 2018
820
2,070
Historia ya Burundi ni ndefu sana, nimeielezea vizuri kwenye kitabu changu ambacho huenda mwezi ujao kikawa tayari (Inshallah). Jiandae kusoma uchambuzi yakinifu kuhusu siasa zetu za ndani na za nje hasa eneo la maziwa makuu. Leo nitaeleza machache lakini mengi utayapata kwenye kitabu. Jiandae.!

Baada ya kupata uhuru mwaka 1962 Burundi iliendelea kuwa chini ya utawala wa kifalme kwa miaka minne (1962-1966). Baada ya hapo ilitawaliwa na marais (Watutsi) kwa karibu miaka 30.

Licha ya kwamba wahutu ni wengi (majority population) lakini serikali ya kikoloni iliwanyima nafasi ya elimu na kuwapendelea zaidi watutsi. Hivyo watutsi ambao ni wachache walifaidi fursa nyingi za ajira na madaraka kwa sababu ya kuwa na elimu nzuri. Hali hii ilisababisha Wahutu kuamua kudai madaraka kwa nguvu ya mtutu.

Mwaka 1965 wahutu walifanya jaribio la mapinduzi lakini halikufanikiwa. Mwaka 1972 walifanya jaribio jingine likafeli na kusababisha mauaji ya zaidi ya watu 100,000. Mwaka 1988 walijaribu tena kutwaa madaraka lakini ikashindikana. Hata hivyo watu zaidi ya 20,000 waliuawa.

Kwa kuwa Wahutu walikuwa na msukumo wa muda mrefu wa kushika madaraka na kusababisha machafuko ya mara kwa mara ilibidi Rais Pierre Buyoya aitishe uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi nchini humo mwaka 1993 ili Warundi wamchague Rais wanayemtaka.

Katika uchaguzi huo Pierre Buyoya wa chama tawala cha UPRONA ambaye alikuwa anatetea kiti chake, aliangushwa na Melchior Ndadaye wa chama cha FRODEBU kwa kupata 32% dhidi ya 65% alizopata Ndadaye.

Melchior Ndadaye akawa Rais wa kwanza Mhutu na Rais wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasia nchini humo. Lakini October 21 mwaka 1993 akauawa katika mapinduzi yaliyoongozwa na wanajeshi wa battalion no.11 mjini Bujumbura iliyokuwa ikiongozwa na wanajeshi wengi watutsi. Mapinduzi hayo yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 100,000 wengi wao wakiwa Wahutu.

Baada ya Ndadaye kuuawa François Ngeze akateuliwa kuwa Rais wa mpito wa nchi hiyo. Akaongoza kwa siku sita tu na kukabidhi madaraka kwa mwanamama Sylvie Kinigi aliyekuwa Waziri Mkuu. Kinigi nae akaongoza kwa miezi minne hadi February 1994 akakimbia. Bunge la nchi hiyo likapiga kura na kumpitisha aliyekuwa Waziri wa kilimo Cyprien Ntaryamira kuwa Rais wa mpito.

Ntaryamira akaongoza kwa siku 60 tu kabla ya kuuawa baada ya ndege aliyokuwa amepanda na mwenzie Juvénal Habyarimana wa Rwanda kutunguliwa mjini Kigali April 06 mwaka 1994 wakitokea Tanzania kwenye usuluhishi.

Baada ya kuuawa kwa Ntaryamira, ilibidi Spika wa bunge la nchi hiyo Sylvestre Ntibantunganya aapishwe kuwa Rais aongoze hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika. Lakini nae alipinduliwa July 25 mwaka 1996 na Pierre Buyoya.

Marais wote wa kihutu waliuawa au walilazimishwa kuachia madaraka. Ndadaye (Mhutu) aliuawa. François Ngeze (Mhutu) alikimbia Ikulu baada ya siku 6 tu. Sylvie Kinigi (Mhutu) aliongoza miezi minne na kukuimbia nchi. Cyprien Ntaryamira (Mhutu) aliuawa. Sylvestre Ntibantunganya (Mhutu) alipinduliwa.

Kwahiyo utaona Marais watatu Watutsi waliongoza Burundi kwa miaka 30 (1962 - 1993) lakini ndani ya miaka miwili tu (1993 – 1995) Burundi iliongozwa na Marais watano Wahutu ambao either walipinduliwa au walilazimishwa kujiuzulu. Hii ilifanya Wahutu waamini kuwa wanahujumiwa na hivyo kuamua kuingia msituni kudai haki yao.

Vikundi vingi vya waasi vilianzishwa, kama vile FRODEBU, FNL-Palipehutu na CNDD kupigana na serikali. Mwaka 1994 kikundi cha CNDD kilianzishwa wa Leonard Nyangoma akishirikiana na Hussein Radjab kikaweka ngome yake huko Uvira mashariki mwa DRC. Kikundi hicho kilikuwa na askari zaidi ya 30,000 na kilikuwa na nguvu sana kulinganisha na vikundi vingine vya waasi.

Kutokana na hali ya kijiografia sehemu rahisi ya kupata chakula ilikuwa Burundi kuliko DRC. Kama wangetaka chakula DRC wangelazimika kusafiri kilomita 400 hadi Kasongo ambapo kulikuwa na mji mkubwa, lakini kwa Burundi ingewachukua kilomita 45 tu kufika Bujumbura. Kwahiyo askari wa CNDD waliovalia kiraia walikuwa wakienda Bujumbura kununua chakula na kusafirisha kwa meli hadi Uvira, DRC kupitia ziwa Tanganyika.

Siku moja askari wa CNDD wakamwambia Kamanda wao Hussein Radjab kwamba kuna kijana mmoja mjini Bujumbura amekua akiwasaidia sana wanapoenda kununua mahitaji. Na walipomchunguza wamegundua ni Mhutu mwenye msimamo wa wastani lakini anayekerwa na utawala wa nchi hiyo. Wakasema licha ya kwamba hawakujitambulisha kwake kama Askari lakini kijana huyo ni kama anatafuta nafasi ya kujiunga na kikundi cha waasi kupigana na serikali.

Hussein Radjab akaagiza waendelee kumpeleleza kwa muda wa miezi sita na wamuulize kama yupo tayari kujiunga na mapigano ya msituni. August mwaka 1995 baada ya kumsoma na kujiridhisha nae wakampeleka msituni. Kijana huyo ambaye kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 31 alikuwa Mhadhiri msaidizi (Assistant Lecturer) Chuo kikuu cha Bujumbura lakini alipoteza kazi kufuatia machafuko ya mwaka 1993 baada ya kuuawa kwa Rais Melchior Ndadaye.

Baba yake alikuwa Mbunge tangu mwaka 1965 hadi mwaka 1970. Mwaka 1971 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa (Gavornor) huko Gatara kaskazini mwa Burundi. Lakini aliuawa kwenye mapigano ya mwaka 1972 wakati wanajeshi wa kihutu walipojaribu kuipindua serikali ya Micombero na kusababisha machafuko.

Baada ya Hussein Radjab kumsaili alijiridhisha kuwa ni mtu sahihi na hivyo kumchukua kama kuruta kwenye kikosi cha mapigano cha CNDD. Kijana huyo aliitwa Pierre Nkurunzinza.

Kutokana na elimu yake nzuri na bidii jeshini alipanda vyeo haraka hadi kufikia Kanali ndani ya muda mfupi. Kufikia mwaka 2000 alikuwa miongoni mwa viongozi wakuu wa CNDD. Akiwa huko msituni alimuita mmoja wa wanafunzi wake aliowafundisha Chuo kikuu cha Bujumbura kujiunga na CNDD. Mwanafunzi huyo aliitwa Evariste Ndayishimiye (ambaye ndiye Rais mpya wa Burundi kwa sasa).

Mwaka 2000 ulitokea mpasuko ndani ya CNDD. Viongozi wa juu walipishana mitizamo. Leonard Nyangoma alitaka kikundi hicho kilinde maslahi ya wahutu tu, lakini Hussein Radjab alitaka maslahi ya watutsi pia yazingatiwe ili kikundi hicho kiungwe mkono na pande zote mbili (Wahutu na Watutsi).

Lakini hawakukubaliana. Nyangoma alidai kuwa falsafa ya kikundi hicho ilikua kupigania wahutu na si watutsi. Kufuatia mvutano huo kikundi hicho kilivunjika na kuzaliwa vikundi viwili. Cha kwanza ni CNDD kilichoongozwa na Leonard Nyangoma mwenyewe. Kikimeguka na askari 8,000. Na cha pili ni CNDD-FDD kilichoongozwa na Hussein Radjab kikajitenga na askari 22,000.

Kutokana na mpasuko huo Pierre Nkurunzinza na kijana wake Evariste Ndayishimiye wakachagua kujiunga na CNDD-FDD cha Hussein Radjab.

CNDD-FDD kiliendelea kupata nguvu na uungwaji mkono kutoka makundi mbalimbali ya watu na wanasiasa wakubwa. Ndayishimiye alipanda cheo hadi kufikia Brigedia Jenerali katika kikundi hicho. Wakati wa mazungumzo ya amani mjini Arusha awali CNDD-FDD ilikataa kushiriki. Lakini mwaka 2004 ilikubali kushiriki kuunda serikali ya mpito iliyokuwa ikiongozwa na Domitien Ndayizeye.

Viongozi wa juu wa kikundi hicho ikabidi wakae na kukubaliana namna ya kugawana madaraka. Ndayishimye akapangwa kuwa Mnadhimu Mkuu wa jeshi katika serikali ya mseto, Adolphe Nshimirimana awe Mshauri wa Rais kuhusu ulinzi, Hussein Radjab awe mgombea Urais kwenye uchaguzi wa 2005 na Pierre Nkurunzinza awe Mwenyekiti wa chama.

Kwa kuwa CNDD-FDD ilikuwa ina-transform kutoka kwenye kikundi cha waasi kwenda chama cha siasa, Hussein alikataa kuwa mgombea Urais. Alitaka aendelee kuwa Mwenyekiti wa chama angalau kwa miaka mitano ndipo agombee Urais. Kwahiyo alimpa Pierre nafasi hiyo kwa makubaliano kuwa yeye akijenge kwanza chama na Pierre agombee urais, na baada ya miaka mitano Pierre arudi kujenga chama na Hussein agombee urais.

Mpango ukakamilika na wakatoka msituni. Askari wote 22,000 waliokuwepo msituni wakapewa nafasi katika jeshi la nchi hiyo. Pierre akagombea Urais na kushinda na Hussein akawa Mwenyekiti wa chama.

Sasa CNDD-FDD kikawa chama tawala na si kikundi cha waasi tena. Vikundi vingine vya waasi kama FRODEBU cha Léonce Ngendakumana na FNL-Palipehutu cha Agathon Rwasa vilikubali kuweka silaha chini na hivyo kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoisumbua nchi hiyo kwa zaidi ya maika 40.

Lakini baada ya Pierre kushika madaraka akanza mzozo na Hussein Radjab, Mwenyekiti wake wa chama. Mwaka 2007 akaagiza Hussein akamatwe kwa madai kuwa katika moja ya hotuba zake alimkashifu na kumuita chupa tupu (empty bottle). Hussein akakamatwa na kushtakiwa. Alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 13 jela.

Agathon Rwasa aliwahi kunukuliwa akisema huenda Pierre hakua tayari kuachia madaraka mwaka 2010 na kumpisha Hussein agombee (kama ilivyokuwa makubaliano yao), hivyo ilibidi amtafutie "zengwe" la kumzima kisiasa.

Mwaka 2010 Pierre aligombea na kushinda kwa awamu ya pili wakati Hussein akiwa jela. Lakini mwaka 2015 alipokuwa anakaribia kumaliza muhula wake wa pili Hussein alitoroka gerezani. Inadaiwa alitoroshwa na jeshi ya nchi hiyo japo jeshi lilikanusha madai hayo. Mpaka leo haijulikani alitorokaje katika gereza hilo lililokua na ulinzi mkali sana.

Kufuatia tukio hilo Pierre alibadilisha Katiba ili agombee kwa awamu ya tatu. Pamoja na kupata upinzani mkubwa ndani na nje ya nchi yake lakini aligombea. Taarifa zinaeleza kuwa alihofia Hussein anaweza kuwa Rais wa nchi hiyo na kulipiza kisasi. Hivyo ili kujiweka salama ilimlazimu kugombea tena na kuendelea kubaki madarakani.

Mwaka 2015 lilifanyika jaribio la mapinduzi Pierre akiwa ziarani nchini Tanzania. Inadaiwa jaribio hilo lilikua na mkono wa Hussein na liliongozwa na Mnadhimu mkuu wa Jeshi la nchi hiyo Meja Jenerali Godefroid Niyombare ambaye amewahi pia kuwa Mkurugenzi wa shirika la Ujasusi nchini humo (SNR).

Hata hivyo jaribio hilo lilizimwa na Niyombare alikamatwa na kuwekwa kizuizini. Baadhi ya askari walioshiriki jaribio hilo waliuawa. Hata hivyo Hussein Radjab alikanusha kuhusika na tukio hilo alipohojiwa na gazeti la Liberation la nchini Ufaransa.

Mwaka 2016 Hussein alihojiwa na BBC na kusema anaendesha vuguvugu la kudai mabadiliko akiwa nje ya nchi hiyo. Hata hivyo inadaiwa Pierre alijiapiza kuwa hataondoka madarakani hadi amtie mbaroni Hussein kwa hofu kuwa Hussein anaweza kuchaguliwa Rais wa nchi hiyo akamsumbua.

Mtandao wa "Burundi Bwacu" mwaka jana mwezi June uliandika kwamba Hussein alipotea katika moja ya nchi jirani na Burundi na haijulikani kama yu hai au ameuawa.

Utawala wa Pierre umeshutumiwa kwa matumizi ya nguvu na kuongoza nchi hiyo kwa mkono wa chuma. December mwaka 2015 shirika la Human Right Watch liliripoti mauaji ya kinyama ya wakosoaji wa serikali. Taarifa hiyo ilisema baadhi ya wakosoaji wamekuwa wakikatwa shoka kichwani, au kuchomwa moto wakiwa hai na kisha kuzikwa katika makaburi ya pamoja.

Mwezi March mwaka 2016 makaburi kadhaa ya halaiki yaligundulika nchini Burundi lakini serikali ilikanusha tuhuma za kutesa watu, kuwaua na kuwazika humo. Shirika la kutetea haki za binadamu la IPHR la nchini Ubelgiji linadai kuwa watu zaidi ya 600,000 wamegeuka wakimbizi kipindi cha utawala wa Pierre, vifo zaidi ya 20,000 vimetokea na familia zaidi ya 1,000 zimepoteza ndugu zao ambao hadi leo hawajulikani walipo.

Mwaka huu Pierre alikubali kung'atuka madarakani baada ya kutawala kwa miaka 15. Hata hivyo alipitisha sheria ya kuzuia kushtakiwa. Pia bunge la nchi hiyo lilitunga sheria ya kumfanya kuwa Kiongozi Mkuu wa taifa hilo (Supreme Leader) nafasi ambayo inampa madaraka makubwa zaidi ya Rais aliyepo madarakani.

Pia shera hiyo ilimtaka kupewa kiinua mgongo cha Franc 1.2Bil sawa na TZS 1Bil. Alitaka pia kujengewa kasri kubwa la kisasa kijijini kwake lenye mfanano sawa na Ikulu ya Bujumbura na kulipwa mshahara sawa na Rais aliyepo madarakani kwa kipindi chote cha maisha yake. Lakini amefariki kabla ya yote hayo kufanyika.

PICHA: Mwenyekiti wa CNDD-FDD Hussein Radjab (kulia) akitoa maelekezo kwa Kanali Pierre Nkurunzinza (mwenye sare za jeshi) huko msituni mwaka 2002.
..............
Malisa GJ
 
Aisee..

Now I Know Better.

Tuwaombee. Imani yao ipo mashakani.
 
Huyu hapa Hussein Radjab akiwa na raisi wa nchi ya jirani
EDZmZ-BWwAAHTQD.jpg
 
R.I.P Nkurunzinza.PK hajawaishindwa misheni.kila anavyozeeka ndo akili yake inapanuka zaidi.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom