Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 23,242
- 33,851
MOHAMED MANGIRINGIRI KAMA ALIVYO NDANI YA KITABU CHA ABDULWAHID SYKES
Ofisi ya wilaya ya TANU, Tabora, sasa chini ya uwenyekiti wa Mohamed Mangiringiri, fundi cherahani aliyeajiriwa na mfanyabiashara wa Kiasia, G. B. Somji, iliwashirikisha wanachama wote na vyama vilivyokuwa na udugu na TANU kwa kuwaomba wachange kwa ukarimu fedha ili kufanikisha mkutano ule na vilevile wachangie chochote watakachoweza kutoa kwa ajili ya kuwakirimu wageni waliokuja kuhudhuria Mkutano Mkuu wa TANU wa mwaka wa 1958 utakaojadili Kura Tatu.
Wanachama walitoa nyumba zao kwa ajili ya malazi ya wajumbe, wengine walitoa vyakula, mablanketi, shuka, magodoro na samani. Wale matajiri walijitolea fedha taslimu.
Usalama wa wajumbe ulikabidhiwa kikundi cha TANU Bantu Group.
Ramadhani Abdallah Singo, wakati huo akiwa na umri wa miaka ishirini na nane na aliyekuwa na sifa ya ubabe na Abdallah Saidi Kassongo, akiwa na umri wa miaka 24 wote wawili wanachama wa Bantu Group walikabidhiwa kazi ya kumlinda rais wa TANU, Nyerere mara tu atakapokanyaga ardhi ya Tabora.
Issa Kibira, mwanachama muasisi wa tawi la African Association mjini Tabora na sasa mwanasiasa mkongwe na mwenye kuheshimiwa alijitolea kumkaribisha Nyerere nyumbani kwake.
Makamu wa rais wa TANU John Rupia na Michael Lugazia walilala katika nyumba nyingine ya Kibira. Kijana mmoja kwa jina Jaffari Idd alichaguliwa maalum kumpikia chakula Nyerere.
Mwaminifu kama alivyokuwa, Jaffari alilazimika kula yamini - kiapo cha Kiislamu, kuwa hatashawishika kwa namna yoyote ile na katika hali yoyote kumruhusu adui amshawishi kumtilia Nyerere sumu katika chakula.
Jaffari alikumbushwa na wale waliomlisha yamini kuwafikiria Waafrika milioni tisa nchini Tanganyika waliokuwa wanamtegemea Nyerere kama mkombozi wao.
Tabora iliwakilishwa na Mzee Fundi Mhindi, Mohamed Mangiringiri na Dharura bint Abdulrahman.
Baada ya kutia saini kwa Azimio la Tabora Mzee Fundi Mhindi, Nyerere, Dossa, Mwalimu Kihere na Mohamed Mangiringiri waliondoka pale Parish Hall na kwenda mjini kutafuta simu ili kumpigia Katibu Mkuu wa TANU Zuberi Mtemvu Makao Makuu, New Street, Dar es Salaam kumuagiza awatangazie wananchi kuwa TANU imepiga kura kuingia katika Uchaguzi wa Kura Tatu.
Mangiringiri alimchukua Nyerere hadi kwa mwajiri wake G. B. Somji kupiga simu kwa Zuberi Mtemvu.
Siku iliyofuata wakati mkutano bado ukiendelea Mtemvu alituma simu ya maandishi kwa rais wa TANU, Julius Nyerere kupitia ofisi ya TANU Tabora, akitangaza kujitoa kutoka TANU na kuanzishwa kwa chama chake cha upinzani - African National Congress (ANC).