SoC02 Hili la tozo litazamwe vizuri

Stories of Change - 2022 Competition

Nabii koko

Member
Aug 16, 2022
21
15
ILI NCHI IENDELEE, INAHITAJI MAPATO. Pato la taifa linachangiwa na vyanzo kama vile viwanda, kilimo, madini, uvuvi, usafirishaji, utalii, kodi, ushuru, na tozo mbalimbali. Kwa Sasa hebu yuzungumzie hizo tozo. Tangu kale Hapa Tanzania na nchi nyingine kumekuwa na Sheria ya ulipaji kodi, tozo na ushuru Kama sehemu ya kukuza pato la taifa ili kutimiza malengo mbalimbali ya kimaendeleo.

Hakika tunaunga mkono jitihada za serikali kuwa na nia ya dhati kutaka kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na nchi kwa ujumla kutoka tulipo hadi nafasi nyingine kwa vyanzo mbalimbali, ILA HILI LA TOZO.....

Hebu tupitie baadhi ya Kodi, Tozo na ushuru mbalimbali kwa mujibu wa Sheria.

(i) TOZO ZA MIAMALA YA FEDHA ZA SIMU. Mnamo mwezi Juni 2021, serikali kupitia bunge chini ya Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Mawasiliano (TCRA) Tanzania, ilipitisha Sheria mpya ya TOZO ZA MIAMALA YA FEDHA ZA SIMU kuanzia sh. 10 hadi 10,000 katika kutuma na kupokea pesa kwa simu.

(ii) Ikiwa hii haitoshi, kulikuwa na pendekezo la tozo za laini za simu kuanzia sh. 10 hadi 200 kwa siku kutegemea na uongezaji salio wa mtumiaji. Ongezeko hili lilikuja kufuatia kupitishwa kwa sheria hii katika bajeti ya 2021/2022 kwa madhimuni ya kutekeleza miradi mbalimbali ya UCHUMI nchini ikiwemo umeme, maji, barabara, elimu na afya.

View attachment 2345945
View attachment 2345947

Sambamba na tozo hizo, tangu mwaka 2021 hadi Sasa (2022) kumekuwa na utitiri wa TOZO nyingine kama ifuatavyo:

(iii) Ongezeko la Tozo ya sh. 100 kwa kila lita ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa lililoanza Kati ya mwezi June na Julai 2021. Tozo hii imeenda sambamba na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia iliyotokana na athari za UVIKO 19 pamoja na Vita ya Ukraine na hivyo kufanya mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa karibia zote. Kwa Sasa lita moja ya petroli imepanda na kufika Kati ya 3000/= na 3600/= kutegemea na eneo.

(iv) Ongezeko la Kodi ya majengo kutoka sh.10,000 hadi 12,000 kwa nyumba za kawaida na sh. 60,000 badala ya 50,000/ kwa ghorofa kwa mwaka.

(v) Tozo za umeme kupitia luku kwa sh. 1,000 kila nyumba kwa nyumba za kawaida na 5,000 kwa kila sakafu ya ghorofa kama kodi ya jengo kupitia mita za luku kila mwezi. Tozo hii imekuwa na athari ya moja kwa moja kwa kila mtumiaji wa luku bila kujali ni mmiliki au sio mmiliki wa nyumba. Maumivu haya ni makubwa zaidi kwa mpangaji kwani anfanya jukumu ambalo lilipaswa kuwa la mmiliki wa nyumba.

(vi) Tozo za miamala ya kielektroniki ya kibenki ambayo imenza kutekelezwa hivi karibuni (2022). Kiujumla tozo hii haikupaswa kuwepo ingali tayari kuna Makato ya miamala ya simu. Uwepo wake unapelekea mtu mmoja kukatwa Kodi zaidi ya mbili kutoka kwenye chanzo kimoja. Unakuta mfanyakazi anayelipwa mshahara kwa benki anakatwa 'PAYE' hata kabla hajatoa pesa benki. Baada ya hapo atakatwa ya kutolea ama ya kutumia iwapo atatuma kwenda katika miamala ya simu. Pesa ikifika kwa mpokeaji bado itakatwa ya kutolea, huku viwango vikiwa juu.

Isitoshe mtu huyu huyu analipa Kodi nyingine kama kawaida, mfano tozo za laini ya simu anaponunua vifurushi au anaponunua umeme. Miaka miwili tu iliyopita ilikuwa ukinunua kifurushi Cha intaneti cha sh. 1,000 unapata zaidi ya gb 1.5 ... Kwa Sasa ili upate mb 750 lazima uwe na kiasi cha pesa kuanzia Tsh. 1500+.

Kuna muda ukienda kununua umeme wa 2000 kwa mfano, inagoma Hadi pale utakapoweka cha juu.

(vii) Kodi ya Ongezeko la thamani (VAT). Japokuwa Kodi hii ipo kwa muda mrefu sasa, bado kuna wakati inapanda sana na Hivyo kuongeza machungu kwa mnunuaji ama mtumiaji wa bidhaa kwa sababu ya mfumuko wa bei za bidhaa. Angalia bei ya mafuta ya kupikia; yamepanda kutoka Tshs. 3000 hadi 7000+. Mche wa sabuni kutoka elfu 2000 hadi 4000+; Sukari je? Vipi juu ya vitu vingine?

SASA: Hivi karibuni ilitangazwa kuwa watoto pia watapaswa kulipiwa kodi na mzazi. Sijui hili nalo litakuwaje?

HIVI, huwa zinafanyika tafiti za kutosha kabla ya kuanzisha Kodi hizi? SINA HAKIKA JUU YA HILO kwa sababu Kama zingefanyika tafiti, wangebaini kuwa huu utitiri wa tozo unamwelemea Mtanzania wa hali ya chini. Haimwathiri yule anayetembelea gari la serikali, anayejaziwa mafuta na serikali bure. Halafu bado analipwa posho kubwa zaidi hata ya mshahara wa sisi tiamaji tiamaji. Mshahara Yao Ndio usiseme. Ndio maana wengi wao ndio hawa wanaoshabikia KODI KILA KUNAPOKUCHA. Kwani maumivu yake wanayajua?

Watafiti wananifanya niwe na wasiwasi juu ya matokeo ya tafiti zinazotangazwa juu ya Kodi. Yawezekana zile kauli za eti "ONGEZEKO LA TOZO NI PENDEKEZO LA WANANCHI" ama "WANANCHI WAMEKUBALI KULIPA TOZO" sio zetu!
Kuna watu (vigogo) waliotusemea ambao ndio waliofanyiwa tafiti. Haiwezekani mtu wa chini aliyeelemewa na hilo furushi la kodi akapendekeza kuongezewa Kodi nyingine wakati hata kodi alizobebeshwa zinamtesa na kumpa ugumu wa maisha.
(Soma nukuu ya Waziri wa fedha. Chanzo: intaneti)
View attachment 2348726

(Tazama maoni halisi ya baadhi ya WANANCHI wa hali ya chini kutoka facebook)
View attachment 2348731

ATHARI ZA TOZO
i. Gharama za maisha kwenda juu wakati huyu mlipa Kodi bado kipato chake kiko palepale.
ii. Kudorola kwa biashara ya miamala kutokana na wateja kutumia njia nyingine kwa kukwepa tozo.
iii. Mfumuko wa Bei za bidhaa.
iv. Kupungua kwa mzunguko wa fedha.

NINI KIFANYIKE?

i) Serikali ipunguze utitiri wa kodi/tozo kwa wananchi wa kawaida na wenye kipato cha chini na kuzielekeza kwa Tabaka la juu la vigogo. Miamala ya simu ilikuwa msaada mkubwa kwa wanyonge wasio na huduma ya benki. Tozo za luku zihusike kwa wamiliki wa nyumba na si wapangaji. Makato ya benki yaondolewe kwani zinafanya mteja mmoja kulipa Kodi nyingi.

ii) Serikali iwekeza kwenye vyanzo vingine Kama vile kilimo, uvuvi, usafirishaji. Mfano, katika kilimo, pembejeo, viwatilifu na zana vipunguzwe Bei kiasi ambacho kila mkulima aweze kumudu kununua ili azalishe kwa wingi.

iii) Yawekwe mazingira rafiki kwa wawekezaji hususani wa viwanda vya kuchakata bidhaa za shambani na kuzitengeneza.

iv) Kuwekeza katika sekta ya usafirishaji kwa kununua treni, au ndege zitakazosafirisha baadhi ya mazao ghafi Kama vile matunda kwenda nje.

v) Kuboresha sekta ya za uvuvi kwa kuwawezesha wavuvi kwa zana Bora na Bei rafiki.

vi) Sekta ya nishati na madini iboreshwe. Utajiri wa madini tulionao bado hautunufaishi wananchi.

vii) Sekta ya utalii iwekewe mazingira mazuri zaidi ingawa kwa Sasa inafanya vizuri kutokana na Kuitangaza kupitia michezo na Sanaa Kama ya uigizaji wa ROYAL TOUR. Sekta nyingine ziige mfano huu.

viii) Wataalamu wa UCHUMI wafanye kazi Yao vizuri katika kuwashauri viongozi kwenye masuala ya kiuchumi na ushauri wao ufanyiwe kazi.

AHSANTE!
 
Back
Top Bottom