Posted Date::10/13/2007
*Helikopta ya Barrick yapigwa jiwe angani
*Yatua kwa dharura, rubani ajeruhiwa
*FFU watumwa kumsaka aliyerusha jiwe
Na Mathias Marwa, Tarime
Mwananchi
HELIKOPTA ya mgodi wa North Mara imelazimika kutua kichakani katika Kijiji cha Kewanja, wilayani Tarime Mkoa wa Mara, baada ya kushambuliwa kwa mawe na watu wasiojulikana.
Helikopta hiyo mali ya mgodi huo unaomilikiwa na wawekezaji wa kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Barrick Tanzania, ilishambuliwa juzi kwa kupigwa mawe na kupasuliwa kioo cha upande wa na kumjeruhi rubani jicho.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, David Saibullu, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo lilitokea majira ya alasiri katika Kijiji cha Kewanja, Kata ya Kemambo, wilayani Tarime.
Helikopta hiyo ilikuwa ikiendeshwa na rubani Charles Wassira, mkazi wa Ukerewe Mkoa wa Mwanza.
Jiwe liliovunja kioo hicho na kumjeruhi rubani huyo, lilirushwa kwa kutumia kombeo na mtu ambaye hajafahamika, ikiwa umbali wa takriban mita 50 usawa wa bahari.
Baada ya rubani huyo kujeruhiwa jicho lake la kulia, alilazimika kutua na kupewa msaada wa kupata matibabu katika hospitali ya Nyamongo iliyopo katika Kijiji cha Nyangoto, wilayani humo.
Kufuatia huduma ya kwanza, rubani huyo akiwa na mwenzake mzungu waliyekuwa pamoja nwakati shambulio hilo likitokea, walifanya marekebisho ya kioo kilicho pasuliwa kisha kuondoka kurejea jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Mawasiliano wa Mgodi huo, Emmanuel Nyasigo, alisema tukio hilo lilitokea katika Uwanja wa Ndege wa Kijiji cha Kewanja Namongo wakati rubani akianza kurusha helikopta hiyo.
Nyasigo alisema kuwa helikopta hiyo ilishambuliwa wakati ikifanya doria katika eneo la mgodi huo na kudai kuwa aliyefanya kitendo ni miongoni mwa watu wanaodhaniwa kuwa wezi wa dhahabu na mafuta ambayo ni mali ya mgodi huo.
Alisema rubani huyo alitengeza kioo hicho kilichovunjwa kwa kutumia makaratasi meupe kuziba tundu na kurudi Dar es Salaam.
Kamanda Saibullu, alituma Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Tarime, kikiongozwa na mkuu wake, Costantine Bandola kumsaka mtu huyo au watu waliohusika na tukio hilo ili kuwakamata ili wafikishwe katika vyombo vya sheria.
Hadi tunakwenda mitamboni hakuna mtu aliyekuwa amekwisha kukamatwa.
Katika eneo la mgodi huo wa Northen Mara kumekuwepo mgogoro kati ya kampuni ya Barrick na wananchi wa eneo hilo ambao wanadia fidia kwa maelezo kwamba kiasi walicholipwa hakilingani na thamani ya maeneo yao.
Kufuatia kutolidhika na malipo hayo baadhi ya waliokuwa wakazi wa eneo hilo waligoma kuchukua malipo hayo wakidai mikataba yao kurekebishwa kulingana na thamani ya maeneo yao.
Katika harakati za kudai haki zao waziri mkuu Edward Lowassa alipotembelea eneo hilo mwezi uliopita walimlalamikia na alipowaambia atamtuma Waziri wa Nishati na Madini, Naziri Karamagi kushguliki suala hilo, lakini walipinga kwa madai kwamba hawamtaki.
[