Haya ni Mapambano ya Kifikra!

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,485
40,014
Siku ya kufa nyani miti yote huteleza. Sikuulewa kwa kina maana ya msemo huu wa wahenga kwa muda mrefu, kwani nilitatizwa na ukweli kuwa nyani ni mnyama aliyebobea katika sayansi na sanaa ya kuruka na kudandia miti! Hata hivyo, hivi sasa nimeulewa msemo huu kwa kina kuwa tatizo la siku hiyo ya nyani kufa siyo nyani kushindwa kurukia miti, tatizo ni kuwa miti ina utelezi! Haishikiki.Utambuzi huo mawazoni mwangu umekuwa kama msumari uliodondoka ardhini na mara mwanga wa radi ukaumulika na kuung’arisha. Nikakumbuka msemo mwingine wa wahenga kuwa “mfa maji, haachi kutapatapa.” CCM imekuwa nyani ambaye siku yake ya kufa imekaribia, na kutapatapa kwake kumekuwa kule kwa mfa maji.

Katika historia ya hivi karibuni haijawahi kutokea serikali ya CCM kujikanyaga kwa majibu ya hoja zilizo wazi kwa kutoa majibu nusu nusu. Siyo majibu nusu nusu tu bali pia kuongezea majibu ya ziada kwenye majibu nusu ya awali, yaliyofuatiwa na majibu yaliyoongezewa kwenye majibu nusunusu ya awali, ambayo na yenyewe yaliongezewa na majibu mengine ya ziada! Kama ni sinema za enzi ya “Drive In” basi wakati huu ni wakati wa kuagiza miogo ya kachumbari, na juisi ya miwa na kukaa mkao wa kula. Onesho linakaribia kuanza.

Mpendwa msomaji, unachokishuhudia sasa katika Tanzania ni kitu ambacho wachache wetu walitarajia kukishuhudia katika maisha yao. Unachoshuhudia ni zaidi ya malumbano, ni zaidi ya shutuma na shutuma za majibu, na ni zaidi ya hoja za upinzani na hoja za chama tawala. Mtanzania mwenzangu unachoshuhudia ni mapambano ya kifikra! Unachoshuhudia ni mstari ukichorwa ardhini kati ya watawala na watawaliwa, walio madarakani na walio nje ya madaraka, viongozi na wale wanaoongozwa. Unachoshuhudia ni kuyeyuka kwa ujiko wa CCM wa miaka karibu hamsini sasa ambako kunafanyika kwa haraka kama kuyeyuka kwa ice cream za Bakhresa kwenye jua kali la Dar! Ukiendelea kushangaa shangaa utakuta yote imedondoka ardhini na mikono yako imetota na kuwa chepe ikibakia kama ushahidi kuwa na wewe uliwahi kuwa na Ice cream mkononi!

Jumapili ya wiki hii itakuwa ni miaka nane tangu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere atutoke. Tunapoadhimisha siku hii muhimu katika historia ya taifa letu hatuna budi kuangalia ni kwa jinsi gani CCM ya Mwalimu na hii CCM ya kina Lowassa ni kama mtu na mkwewe. Hawatazamani. Matatizo mengi ambayo tunayaona leo katika nchi na hasa ndani ya CCM yanatokana na wao wenyewe siyo tu kuzipuuza bali kuzitupilia mbali dhana na fikra ambazo zilikijenga chama hiki na kukifanya kiwe ni chama cha wakulima na wafanyakazi wa nchi hii. Lakini kutokana na maamuzi ya ndani ya CCM leo hii mwelekeo wa CCM uko kama merikebu inayopigwa na mawimbi yanayotokana na uchafu uliorushwa toka ndani ya merikebu hiyo!

Mgongano huu wa kifikra ni wa lazima, hauepukiki na ulipaswa kutokea. Mwalimu Nyerere alipozungumza kwenye sherehe za Mei Mosi pale Mbeya mwaka 1995 kama mwonaji, aliweza kuona mgongano huu toka mbali. Na ni yeye aliyeuita “mgongano wa kifikra”. Mgongano huu asili yake kubwa ni tofauti ya mawazo, maono, mtazamo, na mwelekeo. Ni mgongano ambao chanzo chake ni wananchi kuchoka na kujihisi kuchoshwa.

Kwa muda mrefu sasa, Chama cha Mapinduzi kimekuwa na ujiko wa pekee ndani ya mioyo na mawazo ya watu wengi (mimi ni mmojawapo), na katika miaka ile ya katikati ya tisini baadhi ya wanachama walio “kidondokea” chama hicho walijulikana kama “wakereketwa”. Chama siyo tu kilipendwa na kuheshimwa bali pia kilikubalika na kuenziwa. Wengi wetu tulitarajia kuwa CCM itajiendesha kwa kufuata misingi iliyounda chama hicho na hasa msingi wake mkubwa ambao ni wakulima na wafanyakazi wa nchi hii.

Haikuwa hivyo. Mwalimu aliuliza kwenye hotuba ile “Ni lini nchi hii imeacha kuwa ya wakulima na wafanyakazi?”. Jibu ambalo naweza kutoa leo hii ni kuwa CCM iliacha kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi (jembe na nyundo) pale ambapo kilichangamkia mikataba ya nishati na madini na utalii na kukiweka kilimo nyuma. Kwa miaka kumi ya utawala wa Rais Mkapa, kilimo hakikipewa kipaumbele chochote kile. Hata leo hii vitu kama Azimio la Iringa na Siasa ni Kilimo havisikiki tena kwenye vyumba vya mikutano ya CCM. Watawala wetu wamechangamkia mambo ya madini utadhani wameambiwa siku ya mwisho ni wiki ijayo! Ukiangalia haraka tuliyoifanya miaka kumi iliyopita kutoa leseni za uchunguzi na uchimbaji wa madini kama njugu ni kana kwamba tumeambiwa kuwa tusipofanya hivyo madini hayo yataoza na ardhi hizo zitageuka kuwa jangwa! Tukafanya papara kujitahidi kuuza na kugawa sehemu kubwa kwa wachimbaji wakubwa hata kwa gharama ya kuwahamisha kwa nguvu wananchi wetu wenyewe! Tuliacha kuwa nchi ya wakulima na wafanyakazi! Wananchi wakaa kimya.

Tukajiingiza kwenye mikataba ya wehu kiasi kwamba tulipokaa baadaye kuingalia tukajikuta tunatikisa vichwa kwa masikitiko! Tukaharakisha kununua vitu tusivyohitaji huku watawala wetu wakitutambia kuwa “hata ikibidi kula majani tutakula” ilimradi tupate kandege ka Rais. Tukaruhusu watawala wetu waanza kuuza madodoki Ikulu kwa kisingizio cha ujasiriamali, na tulipotaka kuwauliza warithi wao wakatuambia tuwaache, kwani si heshima kuhoji viongozi wastaafu! Tuliacha kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi! Wananchi wakakubali hilo.

Wananchi wakakubali kuwa nchi inabadilika na ya kuwa shughuli za kiuchumi zimebadilika pia na wengi wakajiingiza katika kundi jipya ambalo linakua kwa kasi. Kundi hili sasa linaitwa wajasiriamali! Hilo si tatizo. Tatizo likabakia kwa wakulima na wafanyakazi. Machimbo makubwa ya madini yamebadilisha mazingira na kuleta huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi pasipo kubadilisha maisha ya wananchi hao. Bado wamebakia kuwa ni wakulima na wafanyakazi! Bado watu wanahangaika kuwa na nyumba bora, chakula cha uhakika na bora, fedha ya matumizi ya ziada, n.k Wakati wakulima na wafanyakazi bado wanahangaika na mishahara yao kiduchu na mapato duni ya kilimo cha kujikimu, wakubwa wanahangaika kuendelea kutoa vibali vya uchimbaji madini wakiweka vipengele ambavyo hata shetani akiviona anaweza kupatwa na mshtuko wa ubongo! CCM ikaacha kuwa nchi ya wakulima na wafanyakazi.

Sasa wananchi wakawa kama Punda wa kazi. Wakawa wanahenyeka kila siku kuinua maisha yao na kila wakishtuka bei nazo zinapanda! Kila wakishtuka huduma za afya ziko juu, kila wakishtuka kitu fulani kinafanya maisha yawe magumu zaidi. Mwaka huu kuna vifo viwili ambavyo vimenishangaza, mmoja ni mtu aliyejinyonga kwa kushinda kulipa ada, na mwingine alijiua baada ya kuhangaikia malipo yake Dar miaka nenda rudi.

Wana na mabinti wa taifa hili wanajitahidi, wanafanya kazi na kujituma tena wengi wanapoanza kazi za umma wanakuwa na hamu ya kutimizia maadili ya kazi hizo. Haichukui muda wanapogundua kuwa maadili hayalipi. Hawa wanaamua kuuza utu wao na hadhi zao na kuamua kuishi maisha ya kiujanja ujanja. Mtu akipandishwa cheo wanasema “ameula”! Na yule aliyepandishwa cheo kitu cha kwanza anachofikiria ni jinsi gani atanufaika katika nafasi yake hiyo mpya na jinsi gani ndugu zake na wale anaowajaliwa watanufaika! Baada ya siku chache anaanza kupata vitrip vya hapa na pale, na miezi michache visemina uchwara na vikongamano vilivyopitwa na wakati vinamualika. Haendi bila kuwa na uhakika wa pochi!

Kikao ambacho kinaweza kufanywa kwa nusu saa kinapangiwa siku mbili na kile ambacho kingefanyika siku moja kinachukua juma zima! Wanaamua kumegeana sasa kwa kuanzisha “ziara ya kufafanua bajeti na kujibu hoja za wapinzani”. Kwa mara ya kwanza wanatuma kundi la mawaziri na manaibu waziri kwenye mkutano mmoja kuzungumzia jambo moja ambalo lingeweza kabisa kufanywa na Mbunge au afisa aliyeko tayari mkoani humo!! Tukiwauliza wanasema “tunatekeleza ilani ya chama”.

Ndugu zangu, hii yote ni sehemu ya mapambano ya kifikra ambao msingi wake ni tofauti ya mtazamo wa wapi “tunatoka, wapi tulipo na wapi tunataka kwenda” kama Mwalimu alivyosema. Tulikotoka tunakujua siyo kuzuri sana lakini kulijaa matumaini, tulipo ni kuzuri sana japo kwa wachache, na tunakokwenda hatuna mwelekeo kwani imebakia kumwaga mabilioni ya fedha kila kona, na tukakupa jina la “maendeleo”. Wananchi bado ni wakulima na wafanyakazi, wanakataa!

Viongozi wanakokwenda wanazomewa wanashangaa! “Kulikoni”? Hawaelewi inakuwaje baada ya “mema” yote ambayo wameifanyia Tanzania pamoja na kumwaga mabilioni ya shilingi, iweje wananchi waoneshe kiburi namna hii! Wanasema “wananchi hawaelewi” kwa kiburi wanadai “ni sumu ya wapinzani”. Wako tayari kuilaumu dunia nzima isipokuwa wao wenyewe!

Walichosahau ni kuwa punda waweza kumtwisha mizigo mengi na akaenda kila utakako na huku ukimchapa vimijeredi. Wamezoea kumpelekesha punda huyo kwa miaka zaidi ya arobaini sasa, na wamezoea kuwa wakisimama tu punda naye anafuata! Leo hii wanasimama na kupiga kelele, huku tishio la mjeredi kuinuliwa, lakini punda hendi! Kumbe punda kafika kikomo! Na kikomo hicho ni pale kwa ujanja wao walipoamua kututwisha mzigo wa Buzwagi!

Mkataba wa Buzwagi umedhihirisha kiini na kina cha mapambano haya ya kifikra. Tunafahamu ni nani aliyesema uongo Bungeni na ni wazi si Zitto kama wanavyotaka tuamini. Kuna mtu alisema kuwa majadiliano ya kudurusu mikataba iliyopita yamemalizika. Kumbe leo hii tunaambiwa mkataba wa mgodi wa Geita bado unaendelea na uko katika hatua za mwisho! Kuna mtu aliyesema kuwa mkataba huu umeboreshwa zaidi kuliko mikataba mingine yote kwa kukata kampuni hiyo kulipa kodi kwa misingi inayoeleweka na kuweka vipengele vya kuruhusu serikali kuchukua ardhi ya wakulima na wafanyakazi kwa matumizi ya kampuni hiyo hata kama wameshindwa kufanya hivyo kwa njia ya kawaida!

Kumbe walipomuadhibu Zitto walijikuta wanajihukumu wenyewe na sasa hivi wanalipa gharama ya hatua hiyo. CCM haina dira na inakoelekeaa haijui. Inafahamu ina pesa inapendwa lakini sasa hivi kiini cha mapenzi hayo kimefikia hatua za kikomo. Wasipojirudi na kubadilika na kuacha usanii na kugawa peremende kutuliza njaa ya muda, CCM wamejitundika wenyewe mtini na ni wao wenyewe wanajinyonyoa!

Ndugu zangu tatizo siyo wapinzani, tatizo si hoja za wapinzani, tatizo si upotoshaji unaofanywa na wapinzani. La hasha! Anayetaka wananchi wafikirie kuwa mgongano wa kifikra unaondelea sasa hivi ni matokeo ya “wivu” wa wapinzani na “uchungu” wa kushindwa uchaguzi ni mrahisishaji hoja! Kinachoendelea ni kuwa wananchi wameamua kuwaondolea uvivu CCM kwani wameburuzwa vya kutosha na wamepuuzwa vya kutosha. Sasa wanataka wachukue nafasi yao halali katika maamuzi yanayohusu maslahi ya nchi hii. Hawako tayari kusema “ndiyo mzee” na “sawa mzee”.

Hata hivyo CCM inaweza kutengeneza ilipoharibu. Najitolea ushauri wa bure, Kikao kijacho cha Bunge wajirudi na kumfungulia Mhe. Zitto ili arejee Bungeni (japo kwa vishindo kidogo). Wakubali kuwa adhabu waliyotoa ni kubwa zaidi na ya kuwa utaratibu wa kumfungia mwakilishi wa watu kutoka vikao vya chombo ambacho amechaguliwa kushiriki ni kinyume na dhana nzima ya utawala bora. Walikosea na wao ni binadamu, wananchi wataona hekima yao na japo litawaletea aibu kidogo na fedheha lakini kitawarudishia heshima kuwa wanawaskiliza wananchi!

Kingine wanachoweza kukitengeneza ni kusitisha mara moja utoaji wa leseni zote mpya za uchimbaji wa madini. Jambo hili linahitaji uamuzi makini, wa haraka na wa makusudi. Tulilalamika kuhusu mikataba kabla ya Rais Kikwete kuingia madarakani na yeye mwenyewe alitambua hilo na akaahidi kushughulikia. Ndani ya miaka miwili tumeona mikataba mikubwa miwili ya ajabu ule wa Richmond na huu wa Buzwagi. Kwa kifupi, tatizo bado tunalo. Wakati umefika kusitisha mikataba mipya yote hadi sheria ya Madini ya 1998 ifanyiwe mabadiliko makubwa. Tunao wataalam wa Kitanzania walioenea pote duniani na wako tayari wakiombwa na serikali yao japo kwa miezi michache waje washirikiane na wataalam wenzao kuja na sheria na taratibu mpya za sekta hiyo.

Wakishachukua uamuzi huo wanaweza kufanya jambo jingine la ziada ambalo kwa hakika litaonesha ni jinsi gani wako makini. Kusitisha mikataba yote iliyoingiwa hadi hivi sasa na makampuni makubwa na kuwataka kujadiliana upya mikataba hiyo. Haya mambo ya kupitia vipengele kwa vipengele ni kupotezeana muda. Makampuni ambayo yatakuwa tayari kukaa chini yatakaa chini, yasiyokubali yanaweza kufunga virago na nina uhakika kuna makampuni mengine ambayo yatakuwa tayari kukaa nasi chini na hata kulipia gharama ya kesi endapo kampuni za awali zitakimbilia mahakamani. Haiwezekani tuwabembeleze kuhusu madini yetu na haiwezekani wao watuamulie hata ni kiasi gani cha kodi wanataka kulipa! Hilo linaweza kufanyika kwa uwazi na kwa taratibu ambazo zina mantiki na ambazo hazilengi kurudisha utaifishaji au kwa namna yoyote kuwafukuza wawekezaji (isipokuwa wasioataka Tanzania nayo ifaidike kwa kiasi kikubwa tu).

Ndugu zangu, ni lazima turejee kwenye mafundisho ya Mwalimu ambayo msingi wake mkubwa ni kuelewa kuwa “binadamu wote ni sawa” na ya kuwa “maendeleo ni maendeleo ya watu”. Turudi kwenye fikra “sahihi” za Mwalimu ambazo bado ni msingi ambao unaweza kulisimamisha tena taifa letu, kutuunganisha na kutupa mwanga wa tunakotaka kwenda.

Tunapoadhimisha miaka nane tangu Baba wa Taifa atutoke, Watanzania wakumbuke kuwa kuna kizazi ambacho kipo na ambacho pole pole kimeanza kujifunza kwa kina mawazo ya muasisi wa Taifa letu na kiko tayari kuyaelezea upya mawazo yake kwa mwanga mpya wa maendeleo mapya duniani (a new synthesis of Nyerere's ideas is now underway). Ni wazi kuwa mawazo ya kizazi hiki yanagongana kabisa na mawazo ya wale ambao kwa namna fulani wanafurahia kutokuwepo Mwalimu kwani sasa wanaweza kula bila kujificha na kumeza bila kutafuna! Sasa hivi hakuna kiongozi ambaye anaweza kuwakemea hadharani kama alivyofanya Mwalimu.

Bahati nzuri (au mbaya kwao), mahali fulani kuna Mtanzania, na kundi la Watanzania ambao wanaanza kuchukua nafasi yao katika kuongoza mapambano haya ya kifikra hadi kuhakikisha kuwa Tanzania yenye neema, yenye mafanikio, na yenye nafasi za mafanikio inawezekana, hata ikibidi kuiweka CCM nje ya ulingo wa siasa. CCM wasipoanza kujirudi ndani ya siku chache zijazo, wataanza kuadhibiwa kwenye huu uchaguzi mdogo wa madiwani. Wananchi watawakataa madiwani hao si kwa sababu binafsi bali kama ishara ya kuikataa CCM na kuipa adhabu inayostahili. Katika hili CCM wamepata washindani. Wajiulize ni wapi wamekosea, wabadilike, vinginevyo watabadilishwa na waamue kuongoza sasa, vinginevyo watajikuta wanafuata!! Wameonywa.

Niandikie: mjengahoja(at)jamboforums.com
Niachie ujumbe: + 1 248 686 2010
 
Naomba kujibu kupitia kichwa cha habari maina shairi hili refu sana, unajua at least wabongo siku hizi tuko busy hatuwezi kusoma ngonjera na mashairi!!! hahahaha...

My take:
Mabadiliko ya fikra jambo jema kama ni kwa uzuri, lakini kama ni kwa ushabiki ule tunaoujua wa MKJJ bora tu,,, tusibadilike tusubiri viongozi wengine wazuri!!!
 
Duh! Jamani ningetaka kuweka pointi ndogondogo ningeweka kwenye mahala husika. Kichwa cha eneo hili kinasemaje?
 
Ndugu Mwanakijiji waswahili wasema UKIPENDA CHONGO UTASEMA NI KENGEZA. Watu wanaweza kukwambi Khamis mke wako mbona ana chongo basi nani najibu, jamani hana chongo bali ana makengeza tu.
Huyo Nyani mara nyingi HAIONI NGOKWE YAKE!

Ahsante!
 
Dr. Khamis nashukuru kwa ile sheria ya Canada.. yaani nilipoisoma kwa kweli nilijikuta nasema "kweli aliyenacho ataongezewa na yule asiyenacho hata kile kidogo anachodhania anacho kitachukuliwa".. Nimeibadili na kuiweka kwenye pdf...
 

Attachments

  • canadamininglaw.pdf
    113.9 KB · Views: 13
Mwanakijiji uko sawa kabisa. watanzania wachache wameanza kugundua taratibu kuwa wao wanatumiwa kama njia tu ya baadhi ya watu kuingia kwenye siasa na kujinifaisha kwa mgongo wao. Zamani tulikuwa hatuna neno la watawala tulikuwa tunatumia neno la viongozi, na viongozi hao leongo lao ilikuwa ni kutuelekeza wananchi namna ya kufikia malengo yaliyokuwa yamepangwa na Chama cha mapinduzi(ambacho kulikuwa ni cha wakulima na wafanyakazi).
Lakini sasa hivi ni kweli tuna watawala ambao lengo9 lao hasa sio kutuongoza, ila ni kututawala kwa maana ile ile aliyokuwa nayo mkoloni, ndio maana sasa hivi unaona watu wameanza kubadilika baada ya kugundua ukweli huo. Fikra ya kuwa wao ni viongozi wetu sasa imefutika kabisa, kwa sababu haionekenai tunaongozwa kwenda wapi, na wao pia wanatumia neno hilohilo "viongozi" lakini uongozi wao kweli hatuuoni isipokuwa tunaona utawala wao. Tunachokiona zaidi ni kuwa si viongozi kwa sababu hata wao hawajui tunaelekea wapi, lakini wao wanajua kabisa wanaelekea wapi. Kuna baadhai ya watanzania sasa wameanza kufikiri kuwa ukitaka kukata vizuri keki ya manufaa ya kiuchumi Tanzania ni lazima uingie kwenye siasa na walau upate ujume wa NEC uwe mbunge na zaidi uwe waziri. Ndio maana utaona maprofesa wengi waliacha kazi zao muhimbili, mlimani wakijiingiza kwenye kitu kinachoitwa mchezo mchafu, lengo lao halisi ni kukata hiyo keki, na wanaikata kwelikweli.
Sasa hivi ukitaka kujua ukweli wa hili angalia malipo anayopata mbunge baada ya kumaliza kipindi cha ubunge cha miaka mitano, na uangalie malipo anyopata mwalimu baada ya kutumikia ualimu kwa miaka 40, hapa ndio utajua kuwa siasi imekuwa sio uongozi tena kama ilivyokuwa zamani, sasa kimekuwa ni kisu kikali cha kukata keki nono.
Na wewe ukitaka kukata keki hiyo hata kama umesoma kiasi gani "inakulazimu" kuwa mmoja wao. Hii inasikitisha. Taaluma nyingine kwa kiasi kikubwa zinadharauliwa, tofauti na kwa wenzetu
 
Wanajamivini tumepiga kelel we sasa muda uliobaki ni mchache sana. Ninawasihi watanzania wafanye maamuzi magumu ya kuweka serikali mpya madarakani.Wakenya wameweza sisi kwa nini tushindwe. Na kwa taarifa yenu ni kwamba viongozi akina kibaki wana heshima kwa wananchi si wakati wa uchaguzi tu hata pia wakati wanaindesha serikali kwa kuwa wanaamini tukifanya mchezo hapa wananchi wanatuondoa madarakani kwa sababu ya "under-perfromance"Akina kibaki wamekuwa serious sasa.
Jamani watanzania kuiweka ccm pembeni mwaka huu ni fundisho kuwa hii nchi ni yetu wote na si ya kikundi fulani tu cha matajiri na wafanyabiashara na mwaka huu nashukuru mungu watanzania wamezinduka na kugundua kikwete analeta UBRAZAMENI kwenye kiti cha uraisi nafikiri yeye shida yake ilikuwa ni lazima awe na cheo cha uraisi katika nchi hii na si kuwakwamua watanzania na shida walizonazo na ndio maana jimbo lake la chalinze alichemsha.
Huu ni muda wa kuipumzisha CCM ambao wao wanaamini kwamba hawawezi kuwekwa pembeni kwa kuwa hii nchi waliitafutia uhuru tuwafunze adabu jumapili hapo.
Mungu ibariki Tanzania na wananchi wake
 
Back
Top Bottom