Hatma ya Kenya mikononi mwa Annan, Mkapa, Graca

Kithuku

JF-Expert Member
Nov 19, 2006
1,395
208
Wakuu kuna matumaini gani hapa?

Hatma ya Kenya mikononi mwa Annan, Mkapa, Graca

*Viongozi wa dini wapinga mkutano wa ODM
*Wasema kipaumbele kwa sasa ni mazungumzo
*Wanajeshi wa Uganda wadaiwa kuingia Kenya

NAIROBI, Kenya

JUKUMU la kuhakikisha kuwa amani inarejea nchini Kenya sasa limeachwa mikononi mwa Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Kofi Annan, Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa na mke wa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Bibi Graca Machel.

Tayari Bw. Annan amewatahadharisha mahasimu wawili wa kisiasa nchini Kenya, Rais Mwai Kibaki na kiongozi wa ODM, Bw. Raila Odinga, kuachana na vikwazo vitakavyokwamisha mazungumzo hayo yatakayosimamiwa na Jopo la Watu Maarufu wa Afrika.

Bw. Annan ambaye ni mshindi wa Nishani ya Amani ya Nobel ya mwaka 2001, ametoa tahadhari hiyo huku Marekani kwa upande wake, ikitoa mwito kwa viongozi hao kufanya mazungumzo ya ana kwa ana ili kurejesha utulivu nchini mwao.

"Sisi tunadhani ni muhimu kwa Rais Kibaki na Bw. Odinga, kukutana ana kwa ana bila masharti na kuzungumza jinsi ya kumaliza mgogoro uliojitokeza baada ya uchaguzi kwa njia ambayo itajali maslahi ya watu wa Kenya," alisema Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Dkt. Jendayi Frazer.

Marekani pia ilitoa mwito wa kuheshimu utawala wa sheria na haki ya wananchi kukutana na pia kuwapo kwa uhuru wa vyombo vya habari.

"Hatukupendelea mtu wakati wa uchaguzi. Tuliunga mkono juhudi za kuwa na uchaguzi ulio wazi na wa haki. Kwa ujumla mchakato wa upigaji kura kwa amani na utulivu na hasa idadi kubwa ya wapiga kura waliojitokeza, vilionesha ushindi kwa watu wa Kenya, lakini udanganyifu katika matokeo ulitibua kila kitu," lilisema Taifa hilo kubwa.

Kauli hizo zimetoka huku ODM ikitoa notisi ya siku tatu ya kufanya mikutano yake nchini kote kesho kutwa, huku Serikali nayo ikiupigamarufuku, lakini pia ni wakati ambao Serikali iliendeleza msimamo wa kupiga marufuku matangazo ya moja kwa moja ya televisheni.

Dkt. Frazer alisisitiza kuwa upo ukweli, kwamba Wakenya wanaamini tatizo lililopo linaweza kutatuliwa kwa pande hizo mbili kugawana madaraka.

Aliongeza: "Pande zote mbili hazina budi kuelewa upungufu uliojitokeza katika kuhakiki kura, hali ambayo ilisababisha kukosekana uhakika wa matokeo ya mwisho na zinatakiwa pia kuchukua hatua za kumaliza ghasia na kurejesha heshima kwa utawala wa sheria, lakini pia na haki za binadamu."

Kauli hiyo ya Marekani ambayo safari hii ilionekana kuwa nzito kulinganisha na ya awali iliendelea: "Hii ni pamoja na kurejesha uhuru wa vyombo vya habari na wa kukutana kwa amani.

"Tunaamini kwamba watu wa Kenya wameshabaini wazi kuwa suluhisho linaweza kupatikana katika kugawana madaraka, kukomesha vurugu, upatanishi na makubaliano ya kuwa na ajenda mahususi kwa ajili ya mabadiliko ya Katiba na uchaguzi".

Bw. Annan, ambaye anatarajia kuanzia alikoishia Rais wa Ghana, Bw. John Kufuor ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, amewataka Serikali na Upinzani kufikiria maslahi ya Wakenya na kuonesha nia, uongozi na ukomavu.

Alisema wataunda sekretarieti itakayoliwezesha jopo hilo kufanya kazi yake vizuri katika kumaliza matatizo na kuirejesha Kenya katika hali ya kawaida.

Akizungumzia ziara ya Rais Kufuor nchini Kenya, Bw. Annan alisema ilikuwa muhimu sana kwani angalau imeonesha mabadiliko kwa kiasi fulani.

Vyombo vya habari nchini Ghana, viliripoti kuwa Bw. Annan atachukua muda mrefu kidogo nchini Kenya tofauti na alivyokaa Rais Kufuor ambaye alitumia siku mbili tu.

Katika siku hizo mbili, Rais Kufuor aliweza kuwashawishi viongozi hao wawili kukubali kufanya mazungumzo, ziara hiyo ilifanyika sambamba na ya viongozi wastaafu wa Afrika, Bw. Mkapa wa Tanzania, Dkt. Kenneth Kaunda wa Zambia na Bw. Ketumile Masire wa Botswana na Dkt. Frazer.

"Majadiliano ya kisiasa si tukio la mara moja, ni mchakato ambao unaweza kuchukua muda mrefu au mfupi, kutegemea na ushirikiano kutoka kwa viongozi," Bw. Annan alisema baada ya kukutana na Rais Kufuor.

"Huu nauona kama wajibu mkubwa kwangu na nitauchukulia kwa uzito mkubwa pia katika kurejesha utulivu na kumaliza haraka matatizo ya kibinadamu katika nchi hiyo," alisema.

"Hatuendi pale kupeleka suluhisho ila tutafanya kazi pamoja na pande zinazohusika na hatimaye tutafikia suluhisho muhimu na la muda mrefu," alisema.

Viongozi wa kidini nchini Kenya wamepaza sauti zao tena za kutaka mazungumzo ya amani yafanyike, wakiamini kuwa ndilo suluhisho pekee la matatizo hayo.

Kanisa Katoliki kwa upande wake, limepinga mkutano wa ODM na kutaka viongozi wakae mezani kujadili amani.

Kadinali John Njue, alisema juzi kuwa kutokana na vifo vya watu wengi na uharibifu wa mali uliofanywa, njia pekee ya kuondokana na hayo ni mazungumzo.

"Nchi imo katika hali mbaya hivi sasa, hivyo kuitisha mikutano kama hiyo ni sawa na kuongeza mafuta kwenye moto ambao tayari umewaka," alisema Kadinali Njue.

Jijini Nairobi, maaskofu 33 wa Kanisa la kianglikana la Kenya, waliwataka Rais Kibaki na Bw. Odinga kujitokeza kushiriki mazungumzo ya amani.

"Watu hawana budi kuingia katika mazungumzo. Machungu mengi yametokea. Mikutano itazidisha machungu haya, kwani itasababisha uporaji madukani tena. Itasababisha upotevu wa maisha ya watu," alionya Askofu Benjamin Nzimbi.

Viongozi wa kidini kutoka jamii ya Wakalenjin nao waliunga mkono kufanyika kwa mazungumzo na kuwaomba Wakenya waombee amani.

Nao viongozi walio chini ya mwavuli wa Chama cha Maendeleo ya Jumuiya ya Emo, walisema katika taarifa yao: "Tumetiwa moyo na juhudi mbalimbali za viongozi wa kimataifa na wa ndani ya nchi na maombi kutoka kwa watu wengi duniani kote wanaotaka kuwaona Wakenya wakiishi maisha ya amani na maendeleo kama ilivyokuwa awali."

Wanajeshi wa Uganda

Katika hatua nyingine, kuna madai ya kuonekana wanajeshi wa Uganda wakivuka mpaka kuingia Kenya.

Wakazi wa maeneo ya Busia walidai juzi kuwa baadhi ya wanajeshi wa Uganda walionekana mjini hapo na Port Victoria karibu na Mto Suo.

"Wamesambaa katika mpaka huku wengine wakishika doria katika Ziwa Victoria," alisema mwalimu wa sekondari wilayani Budalang'i.

Kwa mujibu wa Mbunge mteule wa Nambale, Bw. Chris Okemo, baadhi ya askari hao wameingia katika eneo huru la mpakani kuelekea Busia upande wa Kenya.

"Tumepokea taarifa, kwamba kuna wageni ambao malengo yao hayajulikani na wanaonekana katika makundi. Bado tunafanya uchunguzi wa madai hayo," alisema.

Naye Mbunge mteule wa Bondo, Dkt. Oburu Oginga, alidai kwamba watu waliovalia sare za kijeshi za Uganda walionekana katika kisiwa cha Mageta juzi jioni wakiwa makundi makundi.

"Kundi la kwanza lenye askari 12 wanaozungumza Kiswahili kibovu lilifika kisiwani Mageta saa 11 jioni Ijumaa na kuomba waelekezwe njia ya kwenda pwani mwa Usenge na Uhanya," alisema Bw. Oginga.

Alisema aliiarifu Polisi mjini Bondo baada ya askari zaidi kufika Mageta saa mbili baadaye.

"Tuna wasiwasi na wageni hawa wa kijeshi katika eneo hili. Wananchi wana hofu," alisema Bw. Oginga. Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa Nyanza, Bibi Grace Kaindi, alikanusha madai hayo.

"Huo ni upuuzi. Haiwezekani majeshi ya kigeni yaingie nchini wakati hatuna vita na mtu yeyote," alisema.

"Tuna sheria ambazo zinaweza kutusaidia kushughulikia tishio lolote la usalama jimboni. Wananchi hawana budi kupuuza uvumi kuhusu wanajeshi wa Uganda kupiga kambi mpakani mwa Kenya katika Ziwa victoria," alisema uchunguzi wa Polisi ulibaini kutokuwapo watu wa aina hiyo.

Wanajeshi kama hao walidaiwa pia kuwasili Bungoma, wakiwa katika mabasi sita.

Kumekuwapo na wasiwasi nchini Uganda dhidi ya Rais Yoweri Museveni kujihusisha na mgogoro wa uchaguzi uliotokea nchini Kenya.

Rais Museveni alikuwa Mkuu pekee wa nchi katika eneo la Afrika Mashariki kumpongeza Rais Mwai Kibaki kwa ushindi wake.

Viongozi nchini Uganda wamekanusha wanajeshi wake kuvuka mpaka na kuingia Kenya.

Mshauri wa Rais Museveni wa mambo ya habari, Bw. John Nagenda, jana alikanusha madai hayo sambamba na msemaji wa Jeshi la Uganda, Kapteni Paddy Ankunda, ambaye alisema wanajeshi pekee wa Uganda walioko Kenya ni wanaotoa mafunzo katika Chuo cha Kijeshi cha Karen jijini Nairobi.

Umoja wa Makanisa

Naye Rashid Mkwinda,anaripoti kutoka Mbeya kwamba Umoja wa Makanisa nchini umewataka viongozi wa kisiasa wa Kenya kumrejea Mungu iwapo watashindwa siasa kwa njia ya amani na utulivu na kukomesha mauaji yaliyosababishwa na mzozo wa kisiasa nchini humo.

Wakizungumza katika kongamano la maombi ya kuombea amani nchini katika uwanja wa Sokoine jijini hapa jana viongozi hao walisema kinachoendelea nchini Kenya kinaweza kuiathiri jamii ya watu wa Afrika kutokana na ukweli kwamba nchi hizi zina uhuhusiano wa karibu kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Akitoa tamko la maaskofu hao Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maombi hayo, Askofu John Mwela, kutoka Kanisa la Anglikana alisema Kanisa limepokea kwa masikitiko mgogoro unaoendelea nchini, ambao kwa vyo vyote vile uhusiano wa mgogoro huo unaweza kuenea katika jamii ya Afrika Mashariki.

Askofu Mwela alisema mara nyingi migogoro inayosababisha maafa na mauaji katika jamii huwaathiri akina mama na watoto ambao hawana hatia hivyo ni muhimu kwa viongozi wa kisiasa kumrejea Mungu, ili kuepusha maafa ya aina hiyo.

Kwa upande wake, Mwalimu na Nabii wa Kanisa la Anglikana kutoka Kenya, Bibi Margrethy Aduol ambaye alipokea msaada wa sh. 680,000 kutoka Umoja huo kwa ajili ya kusaidia walioathirika na mzozo wa kisiasa nchini mwake, alisema maombi ya amani kwa nchi za Afrika ni muhimu.

Waangalizi EAC

Naye Glory Mhiliwa anaripoti kutoka Arusha, kwamba waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika uchaguzi mkuu wa Kenya uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, wamependekeza kiitishwe kikao cha wakuu wa nchi za EAC kujadili masuala ya amani, usalama na utawala bora unavyoendelea sasa nchini humo.

Mapendekezo hao yamo katika taarifa ya waangalizi hao wa Jumuiya ya Afrika waliokuwa wanafuatillia uchaguzi mkuu wa Kenya iliyotolewa jana katika makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mjini hapa

Walieleza kuwa mkataba wa EAC unatoa mwongozo kwa marais wa nchi za Jumuiya kuchukua hatua kwa nchi mwanachama ambayo inakiuka utawala bora na masuala ya amani.

Walieleza kuwa marais wa EAC hawana budi kuchukua jukumu la kuhakikisha mchakato wa kuelekea katika upatikanaji na suluhisho la mgogoro nchini humo unaanza.

Walipendekeza pia wote ambao wamekuwa chanzo cha machafuko ya kisiasa Kenya yaliyosababisha mamia ya watu kufa na wengine kukimbia makazi yao wafikishwe kwenye vyombo vya sheria na kushitakiwa

"Uchunguzi kuhusiana na uhesabuji wa kura ufanyike na endapo itabainika kwamba ofisa yeyote wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya(ECK) alihusika basi awajibike," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Waangalizi hao pia wamewataka viongozi wa vyama vya siasa nchini humo kuwasihi wafuasi wao kusitisha vurugu na badala yake uitishwe mdahalo wa pamoja wa kutafuta ufumbuzi wa mgogoro uliojitokeza nchini na kutaka pia vyombo vya Dola kuacha matumizi ya nguvu za kupita kiasi kwa waandamanaji.

Kwa upande wa uchaguzi, waangalizi hao walibaini kwamba kuhesabu na kutangazwa kwa matokeo ya kura za urais kulicheleweshwa na hivyo kuwa chanzo cha mtafaruku mkubwa uliosababisha machafuko.

Waangalizi hao walieleza kwamba kucheleweshwa kwa matokeo hasa kutoka eneo moja ambalo mgombea mmoja wa urais ana nguvu zaidi kulizua tetesi kwamba matokeo yao eneo hilo yalipangwa.

Katika taarifa yao hiyo pia walieleza kuwa Mwenyekiti wa ECK Bw. Samuel Kivuitu, alishindwa kudhibiti mchakato wa kuhesabu kura na baadaye kutangazwa kwa matokeo.

Kutoka na dosari mbalimbali zilizofanywa na Mwenyekiti wa Tume hiyo waangalizi hao walieleza kuzua utata wa uwezo na umakini wake katika Tume.

EAC ilituma waangalizi 13 ambao ni wabunge wa Jumuiya hiyo kutoka Uganda na Tanzania na maofisa waandamizi wa Sekretariati ya Jumuiya hiyo wakiongozwa na Bw. Mike Sebalu ambaye ni mbunge wa Afrika Mashariki kutoka Uganda. (The Standard/Waandishi Wetu)

Source: Gazeti la Majira, 14 Jan 2008.
 
Matumaini ni madogo ukizingatia kasi yenyewe inayotumiwa kutatua mzozo unapotokea uhsusani katika Afrika. Kibaki katangaza baraza la mawaziri na sasa bunge linakaribia kuanza kazi, hiki ni kiashirio kwamba maisha yanaendelea na wanaoitwa wasuluhishi hawana lolote jipya katika kusimamia demokrasia.Dunia na Afrika haijui ni waafrika wangapi wakiuliwa afrika, Dunia inapaswa kuchukua hatua sahihi.

Ni wakenya wenyewe ndio wanaoweza kuamua mustakabali wa nchi yao wakizingatia yaliyotekea Rwanda, Siera leon au Zanzibar.

Wasuluhishi pia ndio tatizo, wanaenda kusuluhisha lakini hawawezi kuchukua hatua yeyote. Kupeleka wastaafu haitoshi kwani hawana madaraka na hawawezi kufanya chochote. Wasuluhishi wanapaswa kuwa marais ambao wako madarakani na wenyeuwezo na utashi wa kuchukua hatua.

Nina wasiwasi sana kama mheshimiwa Mkapa ni msuluhishi kweli au ameenda kubadilishana uzoefu na Kibaki, nikiangalia na hatua zinazochukuliwa ni ushahidi tosha kwamba kunawasuluhishi na wanaopeleka uzoefu.
 
Mkapa atasaidia nini wakati ya kwake huku Zanzibar yalimshinda. Sanasana atamfundisha Kibaki namna ya kuwa jeuri zaidi. Huyo ndio ataharibu kabisa na akina ODM wanatakuwa wamkatae haraka sana huyu, yaani hafai!
 
Mambo mengine naona viongozi wa Afrika hawafikirii hata haiba yao. Mfano unaondoka nyumbani kwako(nchini) kwenda kutatua mgogoro ambao unauhakika hauna mawazo mbadala,sasa huo si ujinga. Tumeshuhudia akina dESMOND tUTU, mARAIS wastaafu, akina John Kofour, na sasa anatafutwa Anani, kwangu mimi sijaona lolote la maana walilofikia kama si kuuhadaa ulimwengu na kuwa fool wakenya tu! .. . Maoni yangu wakenya wachuhue hatua muafaka, hata kama ni kwa gharama ya damu zaidi
 
Jamani mtoeni Mkapa kwenye hiyo list, mbona mnazidi kuharibu?

Usishangae ukisikia serikali ya Kibaki inamtaka Mkapa ndiyo awe msuluhishi wa mgogoro huo, maana tayari wameishamkataa Annan! Mkapa watamkubali kwa kuwa ni mwizi mwenzao na ana jeuri kama wao!
 
ODM wasimkubali Mkapa kama Annan hatakiwi na Kibaki basi labda wamwite Mungu aja awasaidie kutatua wizi huu wa kura uliofanywa na Kibaki. Afrika haina mtu ambaye kwa sasa hivi anaheshimika duniani kama Koffi Annan (labda mwingine ni Mandela lakini umri haumruhusu kusafiri safiri) Pamoja na Marekani kutaka kumharibia reputation yake baada ya kulaumu uvamizi wa Iraq walishindwa kufanya hivyo na njama zao zikajulikana.
 
Jamani mimi nilisema kumwambia mkapa asuluhishe ni sawa na kumwambia Moi asuluhishe.Tangu lini Mwizi akatoa uamuzi kwenye kesi ya wizi jama?
 
Hivi Mkapa si alisema amestaafu mambo ya siasa alipokataa kujibu maswali juu ya biashara zake Ikulu?
Sasa haya ya Kenya ninini?sio siasa? Kama karejea kwenye siasa akirudi toka Nairobi atujibu yale maswali aliyokataa awali kuyajibu.
 
Mkapa atashauri nini wakati alichofanya kibaki ni sawa na alichofanya yeye zanzibar? Acha unafiki mkapa rudi ujibu maswali ulioulizwa kuhusu biashara ikulu.
 
Mkapa atasaidia nini wakati ya kwake huku Zanzibar yalimshinda. Sanasana atamfundisha Kibaki namna ya kuwa jeuri zaidi. Huyo ndio ataharibu kabisa na akina ODM wanatakuwa wamkatae haraka sana huyu, yaani hafai!

KITILA NA TIMU YAKO DHIDI YA MKAPA NINAOMBA KUTOA MAONI YANGU JUU YA HILO LINALOTOKEA KENYA KWA MSINGI WA NINYI KUMHUKUMU BEN ETI KWA SABABU YA ZENJ, NADHANI HATUKO FAIR KWA KUMUANGALIA MKAPA KUWA NDIYO CHANZO CHA YALE YA ZANZIBAR,TUWAULIZE WALIOWANYIMA CUF USHINDI 1995,MATOKEO YALE NA KUAPISHWA KWA DKT.SALMIN KULIFANYIKA WAKATI BEN NI MGOMBEA TU CCM,MUULIZENI MWALIMU KWANINI ALIWANYIMA CUF ZENJ,MUULIZENI MWINYI KWANINI ALIWANYIMA CUF NCHI LAKINI MUWAULIZE WAZEE HAWA WALIMPA KIAPO GANI BEN DHIDI YA CUF ZENJ LAKINI PIA TUWAULIZE JK NA EL ILIKUWAJE WAKAMPA ZENJ KARUME!!

KTK HALI ILE 2001 HATA KAMA RAIS ANGELIKUWA BABA MZAZI WA WEWE KITILA RISASI NA BAADAE MUAFAKA ANGEVIFANYA.

YUPO PALE KWA REFERRENCE HIYO 2001 KWANI TUNAJUA WALIVYOWATANGAZA WAPEMBA WETU KUWA NI WAKIMBIZI KWA NGUVU ZAO ZOTE 2001, SASA WATAFUNE MANENO YAO KWA VINYWA VYAO WANAPOKUTANISHWA NA JASUSI, MSULUHISHI NA MUHANGA WA HALI HIYO HAPA KWETU.

BEN IS NOT PROUD OF WHAT HAPPENED INA ZANZIBAR BUT NANI ALIPASWA KUCHUKUA MAAMUZI YALE KWA LEVEL YA NCHI? NI YEYE NA NDIO MAANA ALIPOKUWA ANAAGA WTZ ALISEMA " NIMEFANYA MAMBO MENGI KAMA KIONGOZI WA NCHI ,YAPO MAZURI MYACHUKUE NA YAPO MABAYA MNISAMEHE NA KUYAACHA LAKINI DAIMA SINTASAHAU JANUARY 2001 ZANZIBAR,NAWASIHI WATZ WENZANGU TUSIFIKIE HALI HIYO TENA"
 
Back
Top Bottom