MakinikiA
JF-Expert Member
- Jun 7, 2017
- 5,831
- 8,184
Mchungaji amtambulisha mke wa pili kanisani, akidai Biblia inaruhusu wake wawili
Chanzo cha picha, LifeWorks Church
Mchungaji mmoja katika jimbo la Ohio, Marekani, amezua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii na miongoni mwa waumini baada ya kumtambulisha mke wake wa pili kwa waumini wa kanisa lake, huku mke wake wa kwanza akiunga mkono hatua hiyo.
Israel T. Ford, mwanzilishi na mchungaji mkuu wa kanisa la LifeWorks Church lililoko Wickliffe, karibu na mji wa Cleveland, alimtambulisha mke wake wa pili, Shakayla Ford, wakati wa ibada ya Jumapili hivi karibuni.
Katika video iliyorekodiwa wakati wa tukio hilo na kusambaa sana mtandaoni, mke wake wa kwanza ambaye pia ni mchungaji mwenza, Lydia Ford, alisimama madhabahuni kumkaribisha Shakayla, akimtaja kama “dada yangu katika ndoa.”
Baadaye, Shakayla alilihutubia kanisa na kufichua kuwa yeye na Mchungaji Ford walikuwa wameoana kwa siri kwa karibu miaka mitatu.
Utetezi wa kibiblia na ukosoaji
Baada ya tangazo hilo, Mchungaji Ford alitumia mitandao ya kijamii kutetea ndoa hiyo, akidai kuwa msimamo wa mwanamume kuwa na mke mmoja pekee ni mtazamo uliobuniwa na binadamu, wala si sharti la Biblia.
Akinukuu vifungu vya Agano la Kale, ikiwemo Kutoka 21:10, alisema kuwa mwanamume kuwa na wake wengi kunaruhusiwa kwa mujibu wa maandiko.
“Tumezoeshwa kama jamii kuamini kuwa mwanamume anaweza kuwa na mke mmoja tu. Hilo halipatani na mafundisho ya Biblia,” alisema Ford katika video aliyochapisha mtandaoni akijibu utata ulioibuka. Naelewa kuwa ukweli huu hauwapendezi watu wengi na kwamba viongozi wengi huepuka kuuzungumzia. Lakini jukumu langu si kuwapendeza watu, bali kufuata yale ambayo yamefunuliwa.”
Ford alikiri kuwa msimamo wake unaweza kuwafanya baadhi ya waumini kuondoka kanisani, akisema yuko tayari kupoteza waumini kutokana na uamuzi huo.
Mwitikio wa umma na masuala ya kisheria
Tangazo hilo limeibua hisia tofauti kwenye mitandao ya kijamii. Wasomi wa Kikristo na wakosoaji wamepinga tafsiri ya Ford ya maandiko, wakirejelea mafundisho ya Agano Jipya, hususan 1 Timotheo 3:2, ambayo inasema kuwa kiongozi wa kanisa anapaswa kuwa “mume wa mke mmoja.”
Pia, maswali yameibuka kuhusu uhalali wa mpango huo kisheria. Sheria za jimbo la Ohio zinakataza mtu kufunga ndoa na mtu mwingine wakati bado yuko kwenye ndoa halali na mtu mwingine.
Hata hivyo, haijabainika iwapo ndoa ya pili ya Ford ilisajiliwa rasmi kwa kupata leseni ya ndoa kutoka kwa mamlaka za serikali au ni makubaliano ya kidini pekee ndani ya kanisa lake.
Kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya watu walionyesha mshangao kuhusu tukio hilo, hasa kutokana na namna mke wa kwanza alivyomkaribisha mke wa pili madhabahuni. Wengine walimshutumu Ford kwa kutafsiri maandiko ya Biblia kwa namna inayolingana na maisha yake binafsi.