Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,482
- 40,001
Rais Kikwete anatarajiwa kutia sahihi muswada wa sheria ya Gharama za Uchaguzi "kwa mbwembwe" kama alivyoahidi. Naomba nitofautiane kwa heshima na taadhima na wale wote wenye kuikubali sheria hii ilivyo sasa. Naendelea kusimama kuwa sheria hii ni sheria mbaya kwa demokrasia yetu changa, itadumaza demokrasia na itatishia mwelekeo wetu wa kisiasa.
HATA IKISAINIWA KWA MBWEMBWE SHERIA HII BADO NI MBAYA
Na. M. M. Mwanakijiji
Kusema kweli haijalishi kama kusainiwa kwa sheria mpya ya Gharama za Uchaguzi ya 2009 kutafanywa huku kuna ngoma zinapigwa, matarumbeta yakipulizwa au watu wamejipanga mduara kushuhudia. Haijalishi kama kutanywa kwa mbwembwe au kwa mbinde, ukweli utabakia kuwa ni sheria mbaya ambayo inarudisha nyuma demokrasia yetu na tishio kubwa na dhahiri kwa haki za wananchi kuchagua na kuchaguliwa kama viongozi katika taifa letu.
Sihoji nia au kusudio la Rais au wale wenye kutaka mabadiliko katika mfumo wa matumizi ya fedha wakati wa uchaguzi. Nakubaliana na haja ya kutengeneza mfumo mzuri utakaohakikisha kuwa fedha haiwi kizuizi kwa mtu kugombea na vile vile haiwi sababu ya mtu kugombea. Ninachodokeza ni kuwa japo nia na kusudio la kuleta sheria hii laweza kuwa nzuri kwa kadiri ukiiangalia kwa karibu sheria hii haitaondoa tatizo lililokusudiwa kuondolewa.
Lengo la sheria hii kimsingi ni zuri kwani linajaribu kushughulikia mojawapo ya matatizo makubwa sana ya chaguzi zetu ambalo ni matumizi makubwa ya fedha yanaoathiri mchakato mzima wa uchaguzi. Lakini kwa kiasi kikubwa tukiisoma hiyo sheria tunaweza kuona kuwa ina lengo vile vile la kuweka vikwazo vingi vya kutumia fedha kwenye uchaguzi.
Hofu yangu ni kuwa bado sheria hii haijatengeneza uwiano maalum kati ya haki ya mtu kuweza kutumia njia halali, safi na za wazi katika kutafuta nafasi ya kisiasa na haki ya jamii kulindwa kutoka kwa matumizi mabaya ya fedha wakati wa uteuzi, kampeni na uchaguzi.
Tatizo kubwa zaidi ni kuwa sheria bado inaweka msisitizo mkubwa kwenye vyama vya kisiasa na haijalishi uwepo wa wagombe binafsi/ huru kama ilivyokwisha amriwa na mahakama. Kwa kutokuzingatia uamuzi wa mahakama ambao bado upo kama ulivyotolewa 2005 sheria hii inaendelea kulazimisha watu kujiunga na vyama vya siasa ilii waweze kushiriki katika uongozi wa nchi yao.
Tatizo la kwanza: (Ibara ya 10)
Tatizo la Pili: (Ibara ya 11)
Tatizo la Tatu: (Ibara ya 12)
Ibara hii kimsingi inawanyima Watanzania walioko nje ya nchi kushiriki katika mchakato wa kisiasa nyumbani kwao Tanzania. Wanakatazwa kutoa michango, kusaidia katika kutangaza kupigia kampeni au hata kumsaidia mgombea wanayemtaka kushinda. Kwa mara ya kwanza katika historia yetu Serikali ya Tanzania imeamua kuwatenga waziwazi raia wa Tanzania walio nje ya nchi ambao wangependa kutoa mchango au misaada kwa wagombea au vyama vyao.
Binafsi naamini ibara hiyo ni kinyume na Katiba. Kwa sababu wakati inawakataza Watanzania walioko nje ya nchi kuchangia katika harakati za siasa wakati wowote, sheria haiwakatazi wageni walioko nchini kufanya hivyo. Kwa maneno mengine, inatengeneza mwanya kwa wageni walioko nchini kuchangia vyama vya siasa lakini Watanzania walioko nje ya nchi wakijikuta wanakatazwa. Katiba inatakaza Bunge kutunga sheria ya kibaguzi uwe wa moja kwa moja au unaotokana na taathira yake.
Tatizo la Nne: (Ibara ya 14)
Ibara hii inazuia wagombea na watu wanaotaka kugombea kugharimia juhudi zao hizo na badala yake gharama hizo zinatakiwa kuingiwa na vyama vya siasa. Lengo hili ni kuzuia wagombea binafsi au wagombea huru. Sheria ilitakiwa itoe mwanya na kutengeneza mazingira ambapo mtu binafsi anaweza kuunda timu yake ya kampeni ambayo ingesimamia uchangiaji wa fedha na hata gharama za kampeni yake bila kulazimisha chama cha siasa kufanya hivyo. Hilo linarudiwa tena kwenye ibara ya 15 ya sheria hiyo.
Lakini pia ni ukweli kuwa wagombea wangepewa uwezo wa kuunda timu zao za kampeni ambazo zingesimamia uchangishaji wa fedha, matumizi na maandalizi yote ya mgombea. Kwa kuweka jukumu hili kwenye chama sheria inarudisha nchi katika mfumo wa kikomunisti na siyo wa kidemokrasia.
Tatizo la Tano: (Ibara ya 21)
Ukiisoma ibara hiyo unaweza kuona kuwa wagombea hawaruhusiwi kutoa ahadi yoyote ile ambayo itawafanya wananchi wawapigie kura! Sheria inakataza hata kutoa ahadi ambazo zitamfanya mtu apigiwe kura kwani hiyo inawezekana kuonekana ni rushwa vile vile. Inaonekana hata kujaribu kuingia makubaliano kuwa "mkinichagua nitafanya hivi au vile" yaweza kuwa kosa kama sheria hii itakubaliwa ilivyo.
Ibara hiyo haizuii kutumika kwa kampeni za uongo zenye kushambulia watu au kuchafia majina ya watu kama ilivyofanywa wakati wa kampeni ya 2005. Huu ni udhaifu mkubwa. Tayari kuna kila dalili za mchezo mchafu kuanza katika baadhi ya majimbo.
Tatizo la Sita (Ibara ya 25, 26)
Sheria hii inatoa adhabu ndogo mno kwa vyama vya siasa na watu wanaohusika na matumizi mabaya ya fedha au kuvunja sheria yenyewe. Adhabu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ni rahisi mtu kuamini kuwa ni nyepesi na chama kinaweza kumudu. Adhabu zote zilizowekwa hazihusishi kifungo, zote ni faini tu! Kama kweli serikali iko makini faini ilitakiwa iwe kubwa ambayo imeambatanishwa na adhabu ya kifungo kwa maofisa wa vyama na wagombea wanaokiuka sheria hii. Vinginevyo, yale "meno" ambayo tunafikiria yapo kwenye sheria hii hayapo kwani ni meno ya utotoni tu.
Hivyo, japo sheria yaweza kuwa ina lengo zuri lakini kwa kadiri ya kwamba wanaoivunja hawatishwi na kifungo, basi vyama vya siasa vitathubutu kuikaidi huku wakijua adhabu kubwa zaidi ni malipo ya fedha tu.
Tatizo la Saba (Ibara ya 27)
Sheria inatoa upendeleo kwa wagombea wa kiti cha urais kutumia vyombo vya habari vya umma. Hata hivyo, haiweki utaratibu wa wazi wa kuhakikisha kuwa Rais aliyeko madarakani hatumii nafasi yake hiyo vibaya na hivyo kuwanyima fursa watu wengine. Sheria haiweki utaratibu wa kuwepo kwa mdahalo wa nafasi ya Urais.
Kwa mfano Rais wa nchi bado ataweza kutumia utaratibu wa kuhutubia mwisho wa mwezi lakini wagombea wenzake hawatapewa nafasi hiyo. Kwa msingi huo sheria inampa aliyeko madarakani (incumbent) upendeleo wa pekee.
Tatizo la Nane (Ibara ya 29)
Sheria inawawekea kinga maofisa wa serikali kuwa wanaweza kufanya maamuzi kwa nia njema (good faith) bila kuweka wigo wa kuelewa hiyo nia njema inapimwaje. Kwa maneno mengine maafisa wa tume, serikali n.k wanaoshughulikia mambo ya uchaguzi wanaweza kufanya maamuzi ambayo ni ya upendeleo lakini wakidai kuwa walifanya kwa "nia njema". Ni lazima kuwekwa utaratibu wa kisheria kuhakikisha kuwa watumishi hao hawatumii nafasi zao vibaya na pale wanapozitumia wajue wanaweza wao wenyewe na ofisi zao kuwajibishwa.
Yapo vile vile matatizo mengine ambayo ni makubwa zaidi. Naamini waathirika wa kwanza wa sheria hii watakuwa ni wagombea wa CCM zaidi kuliko wagombea wa vyama vingine. Hii ni kwa sababu tayari CCM imeweka utaratibu mwingine ndani ya chama wa kuhakikisha kuwa kura za maoni zinakuwa za haki na kutoa nafasi sawa kwa wagombea. Ukiongoza sheria hii kwenye mabadiliko hayo utaona kuwa matatizo mapya kabisa yataibuka ndani ya CCM. Miongoni mwao:
Naweza kuendelea kuchambua madhaifu mbalimbali lakini madhaifu yote hayo yatatokana na kile kinachojulikana kama "Sheria ya matokeo yasiyotarajiwa" (The Law of Unintended Consequences). Sheria hii inasema kimsingi "katika utendaji wa jambo lolote lililokusudiwa, matokeo yasiyotarajiwa huambatana na jambo hilo". Kwa maneno mengine sheria inapoandikwa kushughulikia jambo fulani ni lazima ifikirie vile vile yale ambayo hayakutarajiwa na hivyo kuondoa uwezekano wa sheria hiyo kutumika vibaya.
Kupigiwa makofi kuambiwa kuwa ndiyo sheria bora tuliyokuwa tunaisubiri hakuna msingi wowote ule. Ni sheria mbaya ambayo inahatarisha demokrasia yetu changa na kuikumbatia ni sawa na kukumbatia gunia la misumari. Naamini kabla haijaanza kutumika serikali itachukua muda kufanyia marekebisho yanayohitajika vinginevyo miaka michache kutoka hapa watakaa na kutaka kufanya mabadiliko ya mambo machache ambayo nimeyadokeza. Baada ya wao kushinda mwaka huu!
Niandikie: mwanakijiji@mwanakijiji.com

- Sheria kumpa Waziri uwezo mkubwa wa kuweka kikomo cha fedha zinazoweza kutumika katika kampeni na uchaguzi. Katika kuweka mipaka hiyo Waziri anatakiwa kuangalia ukubwa wa jimbo na aina ya wagombea .
- Kuweka mipaka ya kiasi kinachoweza kutumika kwenye uchaguzi wa jimbo fulani ni kuzuia wagombea kutumia kwa uhalali fedha walizozipata. Ni sawa sawa na kuzuia haki ya kujieleza kwamba mgombea apewe mpaka wa kiasi cha kujieleza. Naamini sehemu hii kisheria ni kinyume na katiba.
Tatizo la Pili: (Ibara ya 11)
- Sheria inaruhusu vyama vya siasa kuchangiwa na mtu yeyote au taasisi yoyote iliyoko Tanzania. Hii ina maana mashirika binafsi, makampuni ya umma na taasisi za kidini zinaweza kuchangia chama cha siasa bila kujali matokeo yake.
- Sheria inaweka mpaka wa Shs 100,000 kwa mtu mmoja au 2,000,000 kuchangia chama cha siasa na kuwa mchango wowote unaozidi kiasi hicho utatakiwa uripotiwe kwa msajili wa vyama vya siasa ndani ya siku 30 tangu upokelewe. Kwa juu juu hili linaonekana ni zuri. Lakini itakuwaje kama mtu atachangia Shs 999,999 au taasisi ikichangia 1999,999? hawa watatakiwa kutoa ripoti kwa msajili? Jibu ni hapana! - Sheria ilitakiwa itake mchango wa kiasi chochote kile unaokusanywa toka mtu binafsi au taasisi binafsi lazima uandikiwe risiti, uorodheshwe. Vinginevyo, watu watatumia mwanya huo na mtashangaa msajili hapokei taarifa ya mtu hata mmoja aliyechangia kiasi kinachotajwa hivi sasa.
- Lakini vile vile, sheria ingelazimisha wachangiaji wote wa vyama vya siasa kuwekwa hadharani na kiasi wanachochangia. Hili linawezekana kwa teknolojia ya hivi sasa. Haitoshi tu kusema watoe taarifa kwa msajili halafu waandishi wakitaka kujua nani amechangia chama hakuna utaratibu. Wote wanaochangia vyama vya siasa majina yao yawekwe kwenye tovuti za msajili na yatolewe kwa dhana ya uhuru wa habari. Sheria haiweki utaratibu wa watu kujua nani kachangia.
- Ibara hii inazuia mtu kuchangia mgombea anayemtaka lakini inamlazimisha kukichangia chama cha mgombea wake. Huu ni udhaifu mkubwa sana. Sheria ilitakiwa iwape uwezo wagombea kuunda Kamati zao za Kampeni na Uchaguzi ambazo ndizo zingekusanya fedha kwa ajili ya wagombea. Wale wanaotaka kuchangia vyam vyao waruhusiwe na wale wanaotaka kuchangia wagombea moja kwa moja waruhusiwe! Kwa kulazimisha michango iende kwenye vyama vya siasa, serikali KIMSINGI inaendelea kupinga wazo la wagombe huru na binafsi maana itakuwa vigumu kwao kupata mchango wowote wakati hawako kwenye chama cha siasa!
Tatizo la Tatu: (Ibara ya 12)
Ibara hii kimsingi inawanyima Watanzania walioko nje ya nchi kushiriki katika mchakato wa kisiasa nyumbani kwao Tanzania. Wanakatazwa kutoa michango, kusaidia katika kutangaza kupigia kampeni au hata kumsaidia mgombea wanayemtaka kushinda. Kwa mara ya kwanza katika historia yetu Serikali ya Tanzania imeamua kuwatenga waziwazi raia wa Tanzania walio nje ya nchi ambao wangependa kutoa mchango au misaada kwa wagombea au vyama vyao.
Binafsi naamini ibara hiyo ni kinyume na Katiba. Kwa sababu wakati inawakataza Watanzania walioko nje ya nchi kuchangia katika harakati za siasa wakati wowote, sheria haiwakatazi wageni walioko nchini kufanya hivyo. Kwa maneno mengine, inatengeneza mwanya kwa wageni walioko nchini kuchangia vyama vya siasa lakini Watanzania walioko nje ya nchi wakijikuta wanakatazwa. Katiba inatakaza Bunge kutunga sheria ya kibaguzi uwe wa moja kwa moja au unaotokana na taathira yake.
Tatizo la Nne: (Ibara ya 14)
Ibara hii inazuia wagombea na watu wanaotaka kugombea kugharimia juhudi zao hizo na badala yake gharama hizo zinatakiwa kuingiwa na vyama vya siasa. Lengo hili ni kuzuia wagombea binafsi au wagombea huru. Sheria ilitakiwa itoe mwanya na kutengeneza mazingira ambapo mtu binafsi anaweza kuunda timu yake ya kampeni ambayo ingesimamia uchangiaji wa fedha na hata gharama za kampeni yake bila kulazimisha chama cha siasa kufanya hivyo. Hilo linarudiwa tena kwenye ibara ya 15 ya sheria hiyo.
Lakini pia ni ukweli kuwa wagombea wangepewa uwezo wa kuunda timu zao za kampeni ambazo zingesimamia uchangishaji wa fedha, matumizi na maandalizi yote ya mgombea. Kwa kuweka jukumu hili kwenye chama sheria inarudisha nchi katika mfumo wa kikomunisti na siyo wa kidemokrasia.
Tatizo la Tano: (Ibara ya 21)
Ukiisoma ibara hiyo unaweza kuona kuwa wagombea hawaruhusiwi kutoa ahadi yoyote ile ambayo itawafanya wananchi wawapigie kura! Sheria inakataza hata kutoa ahadi ambazo zitamfanya mtu apigiwe kura kwani hiyo inawezekana kuonekana ni rushwa vile vile. Inaonekana hata kujaribu kuingia makubaliano kuwa "mkinichagua nitafanya hivi au vile" yaweza kuwa kosa kama sheria hii itakubaliwa ilivyo.
Ibara hiyo haizuii kutumika kwa kampeni za uongo zenye kushambulia watu au kuchafia majina ya watu kama ilivyofanywa wakati wa kampeni ya 2005. Huu ni udhaifu mkubwa. Tayari kuna kila dalili za mchezo mchafu kuanza katika baadhi ya majimbo.
Tatizo la Sita (Ibara ya 25, 26)
Sheria hii inatoa adhabu ndogo mno kwa vyama vya siasa na watu wanaohusika na matumizi mabaya ya fedha au kuvunja sheria yenyewe. Adhabu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ni rahisi mtu kuamini kuwa ni nyepesi na chama kinaweza kumudu. Adhabu zote zilizowekwa hazihusishi kifungo, zote ni faini tu! Kama kweli serikali iko makini faini ilitakiwa iwe kubwa ambayo imeambatanishwa na adhabu ya kifungo kwa maofisa wa vyama na wagombea wanaokiuka sheria hii. Vinginevyo, yale "meno" ambayo tunafikiria yapo kwenye sheria hii hayapo kwani ni meno ya utotoni tu.
Hivyo, japo sheria yaweza kuwa ina lengo zuri lakini kwa kadiri ya kwamba wanaoivunja hawatishwi na kifungo, basi vyama vya siasa vitathubutu kuikaidi huku wakijua adhabu kubwa zaidi ni malipo ya fedha tu.
Tatizo la Saba (Ibara ya 27)
Sheria inatoa upendeleo kwa wagombea wa kiti cha urais kutumia vyombo vya habari vya umma. Hata hivyo, haiweki utaratibu wa wazi wa kuhakikisha kuwa Rais aliyeko madarakani hatumii nafasi yake hiyo vibaya na hivyo kuwanyima fursa watu wengine. Sheria haiweki utaratibu wa kuwepo kwa mdahalo wa nafasi ya Urais.
Kwa mfano Rais wa nchi bado ataweza kutumia utaratibu wa kuhutubia mwisho wa mwezi lakini wagombea wenzake hawatapewa nafasi hiyo. Kwa msingi huo sheria inampa aliyeko madarakani (incumbent) upendeleo wa pekee.
Tatizo la Nane (Ibara ya 29)
Sheria inawawekea kinga maofisa wa serikali kuwa wanaweza kufanya maamuzi kwa nia njema (good faith) bila kuweka wigo wa kuelewa hiyo nia njema inapimwaje. Kwa maneno mengine maafisa wa tume, serikali n.k wanaoshughulikia mambo ya uchaguzi wanaweza kufanya maamuzi ambayo ni ya upendeleo lakini wakidai kuwa walifanya kwa "nia njema". Ni lazima kuwekwa utaratibu wa kisheria kuhakikisha kuwa watumishi hao hawatumii nafasi zao vibaya na pale wanapozitumia wajue wanaweza wao wenyewe na ofisi zao kuwajibishwa.
Yapo vile vile matatizo mengine ambayo ni makubwa zaidi. Naamini waathirika wa kwanza wa sheria hii watakuwa ni wagombea wa CCM zaidi kuliko wagombea wa vyama vingine. Hii ni kwa sababu tayari CCM imeweka utaratibu mwingine ndani ya chama wa kuhakikisha kuwa kura za maoni zinakuwa za haki na kutoa nafasi sawa kwa wagombea. Ukiongoza sheria hii kwenye mabadiliko hayo utaona kuwa matatizo mapya kabisa yataibuka ndani ya CCM. Miongoni mwao:
- Tuhuma za mgombea mmoja kubebwa na viongozi wa juu wa chama.
- Kushindwa kwa wagombea kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa sababu ratiba na vitendea kazi vitatolewa na chama.
- Kudorora kwa kampeni za uchaguzi kwani chama kitakuwa kinaingilia kati taratibu za wagombea kujitangaza na wagombea hawatotaka kuwatibua wakuu wa chama.
- Badala ya kuondoa rushwa kwa wanachama, rushwa sasa itaingizwa katika kushawishi chama chenyewe zaidi na hasa vikao vikuu vya chama. Katika mazingira ya kisiasa ya sasa ambapo kuna mpasuko ndani ya CCM ni wazi kuwa yule mwenye ushawishi zaidi ndiye atakuwa na nafasi kubwa ya kupendelewa.