Hata ikisainiwa kwa mbwembwe; sheria hii bado ni mbaya! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hata ikisainiwa kwa mbwembwe; sheria hii bado ni mbaya!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mzee Mwanakijiji, Mar 17, 2010.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Mar 17, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Rais Kikwete anatarajiwa kutia sahihi muswada wa sheria ya Gharama za Uchaguzi "kwa mbwembwe" kama alivyoahidi. Naomba nitofautiane kwa heshima na taadhima na wale wote wenye kuikubali sheria hii ilivyo sasa. Naendelea kusimama kuwa sheria hii ni sheria mbaya kwa demokrasia yetu changa, itadumaza demokrasia na itatishia mwelekeo wetu wa kisiasa.

  HATA IKISAINIWA KWA MBWEMBWE SHERIA HII BADO NI MBAYA
  Na. M. M. Mwanakijiji


  Kusema kweli haijalishi kama kusainiwa kwa sheria mpya ya Gharama za Uchaguzi ya 2009 kutafanywa huku kuna ngoma zinapigwa, matarumbeta yakipulizwa au watu wamejipanga mduara kushuhudia. Haijalishi kama kutanywa kwa mbwembwe au kwa mbinde, ukweli utabakia kuwa ni sheria mbaya ambayo inarudisha nyuma demokrasia yetu na tishio kubwa na dhahiri kwa haki za wananchi kuchagua na kuchaguliwa kama viongozi katika taifa letu.


  Sihoji nia au kusudio la Rais au wale wenye kutaka mabadiliko katika mfumo wa matumizi ya fedha wakati wa uchaguzi. Nakubaliana na haja ya kutengeneza mfumo mzuri utakaohakikisha kuwa fedha haiwi kizuizi kwa mtu kugombea na vile vile haiwi sababu ya mtu kugombea. Ninachodokeza ni kuwa japo nia na kusudio la kuleta sheria hii laweza kuwa nzuri kwa kadiri ukiiangalia kwa karibu sheria hii haitaondoa tatizo lililokusudiwa kuondolewa.


  Lengo la sheria hii kimsingi ni zuri kwani linajaribu kushughulikia mojawapo ya matatizo makubwa sana ya chaguzi zetu ambalo ni matumizi makubwa ya fedha yanaoathiri mchakato mzima wa uchaguzi. Lakini kwa kiasi kikubwa tukiisoma hiyo sheria tunaweza kuona kuwa ina lengo vile vile la kuweka vikwazo vingi vya kutumia fedha kwenye uchaguzi.


  Hofu yangu ni kuwa bado sheria hii haijatengeneza uwiano maalum kati ya haki ya mtu kuweza kutumia njia halali, safi na za wazi katika kutafuta nafasi ya kisiasa na haki ya jamii kulindwa kutoka kwa matumizi mabaya ya fedha wakati wa uteuzi, kampeni na uchaguzi.


  Tatizo kubwa zaidi ni kuwa sheria bado inaweka msisitizo mkubwa kwenye vyama vya kisiasa na haijalishi uwepo wa wagombe binafsi/ huru kama ilivyokwisha amriwa na mahakama. Kwa kutokuzingatia uamuzi wa mahakama ambao bado upo kama ulivyotolewa 2005 sheria hii inaendelea kulazimisha watu kujiunga na vyama vya siasa ilii waweze kushiriki katika uongozi wa nchi yao.


  Tatizo la kwanza: (Ibara ya 10)

  • Sheria kumpa Waziri uwezo mkubwa wa kuweka kikomo cha fedha zinazoweza kutumika katika kampeni na uchaguzi. Katika kuweka mipaka hiyo Waziri anatakiwa kuangalia ukubwa wa jimbo na aina ya wagombea .
  • Kuweka mipaka ya kiasi kinachoweza kutumika kwenye uchaguzi wa jimbo fulani ni kuzuia wagombea kutumia kwa uhalali fedha walizozipata. Ni sawa sawa na kuzuia haki ya kujieleza kwamba mgombea apewe mpaka wa kiasi cha kujieleza. Naamini sehemu hii kisheria ni kinyume na katiba.
  Tatizo la Pili: (Ibara ya 11)

  • Sheria inaruhusu vyama vya siasa kuchangiwa na mtu yeyote au taasisi yoyote iliyoko Tanzania. Hii ina maana mashirika binafsi, makampuni ya umma na taasisi za kidini zinaweza kuchangia chama cha siasa bila kujali matokeo yake.
  • Sheria inaweka mpaka wa Shs 100,000 kwa mtu mmoja au 2,000,000 kuchangia chama cha siasa na kuwa mchango wowote unaozidi kiasi hicho utatakiwa uripotiwe kwa msajili wa vyama vya siasa ndani ya siku 30 tangu upokelewe. Kwa juu juu hili linaonekana ni zuri. Lakini itakuwaje kama mtu atachangia Shs 999,999 au taasisi ikichangia 1999,999? hawa watatakiwa kutoa ripoti kwa msajili? Jibu ni hapana! - Sheria ilitakiwa itake mchango wa kiasi chochote kile unaokusanywa toka mtu binafsi au taasisi binafsi lazima uandikiwe risiti, uorodheshwe. Vinginevyo, watu watatumia mwanya huo na mtashangaa msajili hapokei taarifa ya mtu hata mmoja aliyechangia kiasi kinachotajwa hivi sasa.
  • Lakini vile vile, sheria ingelazimisha wachangiaji wote wa vyama vya siasa kuwekwa hadharani na kiasi wanachochangia. Hili linawezekana kwa teknolojia ya hivi sasa. Haitoshi tu kusema watoe taarifa kwa msajili halafu waandishi wakitaka kujua nani amechangia chama hakuna utaratibu. Wote wanaochangia vyama vya siasa majina yao yawekwe kwenye tovuti za msajili na yatolewe kwa dhana ya uhuru wa habari. Sheria haiweki utaratibu wa watu kujua nani kachangia.
  • Ibara hii inazuia mtu kuchangia mgombea anayemtaka lakini inamlazimisha kukichangia chama cha mgombea wake. Huu ni udhaifu mkubwa sana. Sheria ilitakiwa iwape uwezo wagombea kuunda Kamati zao za Kampeni na Uchaguzi ambazo ndizo zingekusanya fedha kwa ajili ya wagombea. Wale wanaotaka kuchangia vyam vyao waruhusiwe na wale wanaotaka kuchangia wagombea moja kwa moja waruhusiwe! Kwa kulazimisha michango iende kwenye vyama vya siasa, serikali KIMSINGI inaendelea kupinga wazo la wagombe huru na binafsi maana itakuwa vigumu kwao kupata mchango wowote wakati hawako kwenye chama cha siasa!


  Tatizo la Tatu: (Ibara ya 12)


  Ibara hii kimsingi inawanyima Watanzania walioko nje ya nchi kushiriki katika mchakato wa kisiasa nyumbani kwao Tanzania. Wanakatazwa kutoa michango, kusaidia katika kutangaza kupigia kampeni au hata kumsaidia mgombea wanayemtaka kushinda. Kwa mara ya kwanza katika historia yetu Serikali ya Tanzania imeamua kuwatenga waziwazi raia wa Tanzania walio nje ya nchi ambao wangependa kutoa mchango au misaada kwa wagombea au vyama vyao.


  Binafsi naamini ibara hiyo ni kinyume na Katiba. Kwa sababu wakati inawakataza Watanzania walioko nje ya nchi kuchangia katika harakati za siasa wakati wowote, sheria haiwakatazi wageni walioko nchini kufanya hivyo. Kwa maneno mengine, inatengeneza mwanya kwa wageni walioko nchini kuchangia vyama vya siasa lakini Watanzania walioko nje ya nchi wakijikuta wanakatazwa. Katiba inatakaza Bunge kutunga sheria ya kibaguzi uwe wa moja kwa moja au unaotokana na taathira yake.


  Tatizo la Nne: (Ibara ya 14)
  Ibara hii inazuia wagombea na watu wanaotaka kugombea kugharimia juhudi zao hizo na badala yake gharama hizo zinatakiwa kuingiwa na vyama vya siasa. Lengo hili ni kuzuia wagombea binafsi au wagombea huru. Sheria ilitakiwa itoe mwanya na kutengeneza mazingira ambapo mtu binafsi anaweza kuunda timu yake ya kampeni ambayo ingesimamia uchangiaji wa fedha na hata gharama za kampeni yake bila kulazimisha chama cha siasa kufanya hivyo. Hilo linarudiwa tena kwenye ibara ya 15 ya sheria hiyo.


  Lakini pia ni ukweli kuwa wagombea wangepewa uwezo wa kuunda timu zao za kampeni ambazo zingesimamia uchangishaji wa fedha, matumizi na maandalizi yote ya mgombea. Kwa kuweka jukumu hili kwenye chama sheria inarudisha nchi katika mfumo wa kikomunisti na siyo wa kidemokrasia.


  Tatizo la Tano: (Ibara ya 21)
  Ukiisoma ibara hiyo unaweza kuona kuwa wagombea hawaruhusiwi kutoa ahadi yoyote ile ambayo itawafanya wananchi wawapigie kura! Sheria inakataza hata kutoa ahadi ambazo zitamfanya mtu apigiwe kura kwani hiyo inawezekana kuonekana ni rushwa vile vile. Inaonekana hata kujaribu kuingia makubaliano kuwa "mkinichagua nitafanya hivi au vile" yaweza kuwa kosa kama sheria hii itakubaliwa ilivyo.


  Ibara hiyo haizuii kutumika kwa kampeni za uongo zenye kushambulia watu au kuchafia majina ya watu kama ilivyofanywa wakati wa kampeni ya 2005. Huu ni udhaifu mkubwa. Tayari kuna kila dalili za mchezo mchafu kuanza katika baadhi ya majimbo.


  Tatizo la Sita (Ibara ya 25, 26)
  Sheria hii inatoa adhabu ndogo mno kwa vyama vya siasa na watu wanaohusika na matumizi mabaya ya fedha au kuvunja sheria yenyewe. Adhabu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ni rahisi mtu kuamini kuwa ni nyepesi na chama kinaweza kumudu. Adhabu zote zilizowekwa hazihusishi kifungo, zote ni faini tu! Kama kweli serikali iko makini faini ilitakiwa iwe kubwa ambayo imeambatanishwa na adhabu ya kifungo kwa maofisa wa vyama na wagombea wanaokiuka sheria hii. Vinginevyo, yale "meno" ambayo tunafikiria yapo kwenye sheria hii hayapo kwani ni meno ya utotoni tu.


  Hivyo, japo sheria yaweza kuwa ina lengo zuri lakini kwa kadiri ya kwamba wanaoivunja hawatishwi na kifungo, basi vyama vya siasa vitathubutu kuikaidi huku wakijua adhabu kubwa zaidi ni malipo ya fedha tu.


  Tatizo la Saba (Ibara ya 27)
  Sheria inatoa upendeleo kwa wagombea wa kiti cha urais kutumia vyombo vya habari vya umma. Hata hivyo, haiweki utaratibu wa wazi wa kuhakikisha kuwa Rais aliyeko madarakani hatumii nafasi yake hiyo vibaya na hivyo kuwanyima fursa watu wengine. Sheria haiweki utaratibu wa kuwepo kwa mdahalo wa nafasi ya Urais.


  Kwa mfano Rais wa nchi bado ataweza kutumia utaratibu wa kuhutubia mwisho wa mwezi lakini wagombea wenzake hawatapewa nafasi hiyo. Kwa msingi huo sheria inampa aliyeko madarakani (incumbent) upendeleo wa pekee.


  Tatizo la Nane (Ibara ya 29)
  Sheria inawawekea kinga maofisa wa serikali kuwa wanaweza kufanya maamuzi kwa nia njema (good faith) bila kuweka wigo wa kuelewa hiyo nia njema inapimwaje. Kwa maneno mengine maafisa wa tume, serikali n.k wanaoshughulikia mambo ya uchaguzi wanaweza kufanya maamuzi ambayo ni ya upendeleo lakini wakidai kuwa walifanya kwa "nia njema". Ni lazima kuwekwa utaratibu wa kisheria kuhakikisha kuwa watumishi hao hawatumii nafasi zao vibaya na pale wanapozitumia wajue wanaweza wao wenyewe na ofisi zao kuwajibishwa.


  Yapo vile vile matatizo mengine ambayo ni makubwa zaidi. Naamini waathirika wa kwanza wa sheria hii watakuwa ni wagombea wa CCM zaidi kuliko wagombea wa vyama vingine. Hii ni kwa sababu tayari CCM imeweka utaratibu mwingine ndani ya chama wa kuhakikisha kuwa kura za maoni zinakuwa za haki na kutoa nafasi sawa kwa wagombea. Ukiongoza sheria hii kwenye mabadiliko hayo utaona kuwa matatizo mapya kabisa yataibuka ndani ya CCM. Miongoni mwao:  • Tuhuma za mgombea mmoja kubebwa na viongozi wa juu wa chama.
  • Kushindwa kwa wagombea kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa sababu ratiba na vitendea kazi vitatolewa na chama.
  • Kudorora kwa kampeni za uchaguzi kwani chama kitakuwa kinaingilia kati taratibu za wagombea kujitangaza na wagombea hawatotaka kuwatibua wakuu wa chama.
  • Badala ya kuondoa rushwa kwa wanachama, rushwa sasa itaingizwa katika kushawishi chama chenyewe zaidi na hasa vikao vikuu vya chama. Katika mazingira ya kisiasa ya sasa ambapo kuna mpasuko ndani ya CCM ni wazi kuwa yule mwenye ushawishi zaidi ndiye atakuwa na nafasi kubwa ya kupendelewa.


  Naweza kuendelea kuchambua madhaifu mbalimbali lakini madhaifu yote hayo yatatokana na kile kinachojulikana kama "Sheria ya matokeo yasiyotarajiwa" (The Law of Unintended Consequences). Sheria hii inasema kimsingi "katika utendaji wa jambo lolote lililokusudiwa, matokeo yasiyotarajiwa huambatana na jambo hilo". Kwa maneno mengine sheria inapoandikwa kushughulikia jambo fulani ni lazima ifikirie vile vile yale ambayo hayakutarajiwa na hivyo kuondoa uwezekano wa sheria hiyo kutumika vibaya.


  Kupigiwa makofi kuambiwa kuwa ndiyo sheria bora tuliyokuwa tunaisubiri hakuna msingi wowote ule. Ni sheria mbaya ambayo inahatarisha demokrasia yetu changa na kuikumbatia ni sawa na kukumbatia gunia la misumari. Naamini kabla haijaanza kutumika serikali itachukua muda kufanyia marekebisho yanayohitajika vinginevyo miaka michache kutoka hapa watakaa na kutaka kufanya mabadiliko ya mambo machache ambayo nimeyadokeza. Baada ya wao kushinda mwaka huu!


  Niandikie: mwanakijiji@mwanakijiji.com
   
 2. Selous

  Selous JF-Expert Member

  #2
  Mar 17, 2010
  Joined: Jan 13, 2008
  Messages: 1,322
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  Itanibidi nikaisomee kwenye kichuguu changu hii makala, asante sana MKJJ and hope will be useful.

  Hivi unajua hii ni week ya mambo mepesi? Jana kulikuwa na jezi ya Ronaldo and Picha alipelekewa!!!!
   
 3. Shadow

  Shadow JF-Expert Member

  #3
  Mar 17, 2010
  Joined: May 19, 2008
  Messages: 2,908
  Likes Received: 71
  Trophy Points: 145
  Naomba kuchangia Ibara ya 27 kuhusu vyombo vya umma. Mimi nafikiri sheria ya utangazaji inatakiwa ifanyiwe marekebisho na kuweka kipengele kinachosema kwamba kila mgombea wa kiti cha urais apewe wasaa sawa na bila upendeleo. Kuwepo na adhabu kali kwa watendaji wa vyombo hivi kama wakikiuka hii sheria. Baada ya kusema haya basi Ibara ya 27 ifanyiwe hayo marekebisho na wakati huohuo hayo mabadiliko yajumuishwe pia kwenye sheria ya utangazaji
   
 4. taffu69

  taffu69 JF-Expert Member

  #4
  Mar 17, 2010
  Joined: Feb 26, 2007
  Messages: 2,089
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 135
  Mkuu Mwanakijiji, tatizo kubwa tulilonalo Watanzania na hususani viongozi walioko madarakani ni kupenda kwao ama kutokana na uelewa mdogo, mara nyingi kukimbilia kutafuta ufumbuzi wa viashiria vya tatizo badala ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo lenyewe kwa ujumla. Tanzania kuna sheria nyingi sana lakini aidha hazitekelezwi ama zimetungwa kulinda kundi fulani hivyo matatizo yaliyokusudiwa yanabaki kama yalivyo na yanaendelea kukua siku hadi siku. Ni sheria ngapi zimesainiwa na Rais wa sasa na hata wale waliomtangulia lakini hazina manufaa yoyote kwa Mtanzania wa kawaida ama zimeishia kupigwa vumbi kwenye makabati? Ni ujumbe gani Rais anawapa wananchi kwa kutangazia umma kuwa atasaini sheria ya gharama za uchaguzi kwa mbwewe wakati imebaki miezi takribani saba tu kufanya uchaguzi mkuu? Ni kitu gani amaegundua mpaka aamue kusaini sheria hiyo sasa na sio miaka minne nyuma tangu aingie madarakani? Je kwa kusaini sheria hiyo sasa atakuwa amejisafisha na uchafu/njama mbaya alizotumia/zilizotumika kumwingiza madarakani mwaka 2005?. Nafikiri Rais alitakiwa kufikiria kwa kina kabla ya kutangazia umma kwamba atasaini sheria hiyo kwa mbwembwe.
   
 5. M

  Mtanzania JF-Expert Member

  #5
  Mar 17, 2010
  Joined: May 4, 2006
  Messages: 4,818
  Likes Received: 49
  Trophy Points: 145
  Mzee Mwanakijiji,

  Mimi nitatofautiana na wewe juu ya hili; ni kweli sheria hii ina mapungufu mengi lakini pia kama ikitekelezwa ipasavyo inaweza kusaidia sana kupunguza tatizo la rushwa hasa kwenye chaguzi za vyama ( kwa mfano kura za maoni ndani ya CCM).

  Ilipofikia sasa ni kwamba hata kama mgombea hataki kutoa posho (takrima) wananchi wanadai bila hata aibu na mtu yeyote ambaye hawezi kutoa hiyo posho anakuwa ameshindwa kabla hata mpira haujawekwa uwanjani.

  Hii sheria inatoa nafasi kwa vijana ambao hawana pesa ili waweze kutumia maneno na ushawishi mwingine kuwavutia wananchi wawape nafasi ya uongozi.

  Pia inaondoa tatizo la wenye pesa kutumia mamilioni kuwasafirisha wapambe kwenda kwenye mikutano yao ili ionekane wanaungwa mkono kumbe ni watu hao hao ambao kila siku wanasafirishwa toka pande moja kwenda nyingine.

  Hii sheria ikitumika vizuri itasaidia wagombea wapya hasa kwenye vyama maana watakuwa na platform sawa na walioko madarakani au wenye pesa ya kuweza kuuza sera zao. Ndio maana hata wakati wa kuipitisha, wabunge wengi walioko madarakani waliipinga kwasababu walijua ikitumika vizuri inaweza kupunguza kasi zao za kununua uongozi.

  Kama zilivyo sheria zingine ina mapungufu mengi tu kama ulivyoandika na labda huko mbele kuna haja ya kuifanyia marekebisho ili iwe na faida zaidi. Tatizo kubwa ni hilo la wagombea wapya kutokuwa na nafasi au muda wa kutosha kujiuza huku walioko madarakani wakiendelea kutumjia majukwaa mbalimbali kujiuza kwa wananchi kwa kisingizio cha mikutano ya kuhimiza maendeleo.

  Kama mgombea mmoja wapo, naamini hii sheria ina faida nyingi kuliko hasara. Ila tu yote yatategemea kama vyombo vya dola vitaitekeleza ipasavyo.

  Nimesikia rais ataweka sahihi yake leo, wacha tusubiri utekelezaji wake utakuwaje.
   
 6. Kabuche1977

  Kabuche1977 JF-Expert Member

  #6
  Mar 17, 2010
  Joined: Feb 10, 2009
  Messages: 462
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 35
  sasa kama mgombea haruhusiwi kutoa ahadi sasa anagombea kwenda kufanya nini, mimi sijawahi kuona mgombea wa uongozi fulani haruhusiwi kutoa ahadi, sasa atakuwa anaanisha sera zake za maendeleo vipi, sasa mgombea si atakuwa bubu, yaani sawa sawa na umeambiwa uchinje ng'ombe halafu huna kisu, then hao watu anaoomba wamchague watamchagua vipi kama haonyeshi nia na madhumuni ya yeye kugombea? Mwanakijiji naona hapa hii sheria haijakaa sawa, halafu hao wabunge wa upinzani mbona hili hawakuliona?? mimi sijawahi ona sehemu ya ushindani mtu huruhusiwi kutoa kutoa sera, make sera ndo ahadi hizo, sasa kama ahadi haziruhusiwi then hakuna uchaguzi na maana yenyewe ni kuwa hakuna demokrasia ya kweli.

  Au failure ya maisha bora kwa kila mtanzania ndio imesasabisha yote haya??? make hiyo sera hata marekani haipo, watu wanahitaji basic needs like safe and clean water, ordinary shelters, and good education system, system ambayo hata mtoto wa mkulima can afford either through contributions or self reliant. For this huhitaji kuja na kauli mbiu zenye kuhadaa Watanzania, it is a small thing and if you have got willing people, ordinary Tanzanians can acquire all those basic needs.
   
 7. Kubwajinga

  Kubwajinga JF-Expert Member

  #7
  Mar 17, 2010
  Joined: Jan 23, 2008
  Messages: 2,190
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 135
  Mwanakijiji,
  Obvious utakuwa unayo kopi ya huo waraka wa sheria. Je unaweza kutusaidia kuu-attach kwenye hii post ili tuukague kama tutakuwa na muda? Thanks in advance.
   
 8. W

  WildCard JF-Expert Member

  #8
  Mar 17, 2010
  Joined: Apr 22, 2008
  Messages: 7,477
  Likes Received: 70
  Trophy Points: 145
  Marmo anaongea sasa kabla Rais hajaweka sahihi.
   
 9. W

  WildCard JF-Expert Member

  #9
  Mar 17, 2010
  Joined: Apr 22, 2008
  Messages: 7,477
  Likes Received: 70
  Trophy Points: 145
  Kwa maoni yangu sheria hii itamsaidia sana JK kwa kuwadhibiti maadui wake wa sasa akina Mramba, Yona, EL, RA, Karamagi, Chenge..... ambao wanazopesa, wanahisi wamesalitiwa na JK, wameonewa sana, wamedhalilishwa sana, na JK waliomsaidia kufika hapo alipo amewatosa!
   
 10. S

  Sir Leem JF-Expert Member

  #10
  Mar 17, 2010
  Joined: Mar 14, 2008
  Messages: 564
  Likes Received: 25
  Trophy Points: 45
  TBC wanaleta Live nawaona Jaji mkuu,msaijili wa vyama mabalozi nk,Msajili wa vyama anaifagilia sheria hii anadai kabla ya kuwasilishwa bungeni walichukua maoni kutoka taasisi mbali mbali viongozi wa siasa,vyama vya siasa ,viongozi wa dini na taasisi mbali mbali
   
 11. S

  Sir Leem JF-Expert Member

  #11
  Mar 17, 2010
  Joined: Mar 14, 2008
  Messages: 564
  Likes Received: 25
  Trophy Points: 45
  Msajili wa vyama anadai sheria imejitosheleza!!
   
 12. Mpita Njia

  Mpita Njia JF-Expert Member

  #12
  Mar 17, 2010
  Joined: Mar 3, 2008
  Messages: 7,012
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  Ipo kwenye website ya Bunge pia
   
 13. W

  WildCard JF-Expert Member

  #13
  Mar 17, 2010
  Joined: Apr 22, 2008
  Messages: 7,477
  Likes Received: 70
  Trophy Points: 145
  Wazee wa Upinzani nao wapo. Mwanakijiji, mapungufu haya unayoyaeleza humu wengi hatuyaoni!
   
 14. S

  Sir Leem JF-Expert Member

  #14
  Mar 17, 2010
  Joined: Mar 14, 2008
  Messages: 564
  Likes Received: 25
  Trophy Points: 45
  Rais ameshatia sahihi !!
   
 15. S

  Sir Leem JF-Expert Member

  #15
  Mar 17, 2010
  Joined: Mar 14, 2008
  Messages: 564
  Likes Received: 25
  Trophy Points: 45
  wawakilishi wa vyama vya siasa wote walikuwepo kushuhudia utiaji wa sahihi wa sheria hii!shughului zimeisha!
   
 16. Mtazamaji

  Mtazamaji JF-Expert Member

  #16
  Mar 17, 2010
  Joined: Feb 29, 2008
  Messages: 5,972
  Likes Received: 33
  Trophy Points: 0
  tujipongeze
  ila Itabidi wajiandae kuunda na mahakama ya uchaguzi kama ilivyo mahakama ya kazi, mahakama ya ardhi na mahamakama ya biashara.
   
 17. Elusive

  Elusive JF-Expert Member

  #17
  Mar 17, 2010
  Joined: Nov 26, 2008
  Messages: 223
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Naomba nifahamisheni sheria hii itatumika upande wa Zanzibar katika uchaguzi wa Rais wa Zanzibar na wajumbe wa Baraza La Wawakilishi?
   
 18. Kasheshe

  Kasheshe JF-Expert Member

  #18
  Mar 17, 2010
  Joined: Jun 29, 2007
  Messages: 4,690
  Likes Received: 91
  Trophy Points: 145
  Kama kuna mtu hapa ambaye anaweza kunipa sheria moja(1) ambayo imekubaliwa na waTanzania by 100%. Nitavua uanachama wangu wa JF. Kwa maana ya sheria inayozungumzia wizi, waTanzania wezi hawaipendi.

  Maoni yangu ni jambo la kihistoria kwa nchi iliyoku huku kweusi ku-enact sheria ya namna hiyo.

  Nalipongeza Bunge letu, vyama vya siasa na Mh. Rais kwa kuridhia sheria hii, Ambayo inabadilisha kwa kiasi kikubwa mfumo wetu wa uchanguzi kwa mema zaidi.

  Ukweli ni kwamba makundi yote yanaikubali hiyo sheria angalau kwa zaidi ya 75%... Na hiyo ni % inayoyotosha sana kwa mstakabali wa nchi.
   
 19. K

  Kinnega Member

  #19
  Mar 17, 2010
  Joined: Apr 8, 2009
  Messages: 52
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Duu, ndugu mwandishi umetuchambulia na kututafsiria sheria na katiba kwa staili ya meza kama ilivyo, bila kutupa nukuu ya kipengele hata kimoja.

  Sheria inakosea, sheria inasema, sheria inakataza... Sheria inasemaje?
   
 20. B

  Boramaisha JF-Expert Member

  #20
  Mar 17, 2010
  Joined: Apr 29, 2009
  Messages: 820
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  Hamna cha historia yoyote hapo, tunasubiri utekelezaji wake.

  Asilimia 80 ya wananchi ni wale wanaohangaikia maisha yao na wala hawajui na hawana habari yoyote kwamba kuna sheria inapitishwa na inahusika vipi na maisha yao ya ubangaizaji wa kila siku.

  Kwa kifupi, sheria hii imepitishwa kwa manufaa ya wachache tu.
   
Loading...