RUCCI
JF-Expert Member
- Oct 6, 2011
- 1,702
- 1,716
Halima Mdee
Huyu ni mbunge kijana ambaye baada ya kuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwa kipindi cha miaka mitano, aliamua kupambana kwenye uchaguzi mkuu wa 2010 na kufanikiwa kukinyakua kiti cha jimbo la Kawe.
Ni miongoni mwa wanawake wachache katika taifa letu aliyepata ubunge wa kuchaguliwa. Wengine wanasema Mwana Mama huyu Jembe, wengine wanamwita Kamanda, wengine wamembatiza jina mpambanaji, mwanasiasa mzalendo, kiongozi na mwakilishi wa kweli wa watu wake.
Sifa za Halima Mdee, zilivuma wakati akiwa Mbunge wa Viti Maalumu. Ingawa ni mwanachama wa CHADEMA, lakini muda wote walisimamia hoja za kitaifa na kuzitetea.
Muda wote alionyesha uzalendo, huyu si miongoni mwa wale wanaopayuka na kutukuza ushabiki wa vyama siasa, bali anaangalia maslahi ya taifa.
Sote tumeshuhudia alivyosimama kidete kutetea suala zima la ardhi. Jimbo lake la Kawe, lina migogoro mingi ya ardhi na Halima amekuwa mstari wa mbele kuwatetea watu wanaodhulumiwa ardhi yao.
Bila kuweka chumvi au ushabiki, Mwana Mama huyu anaweza kusimama kugombea jimbo lolote Tanzania.
Kazi anayoifanya bungeni inaonekana, si miongoni mwa wale wanaokwenda kusinzia na wakiziduka usingizini wanashangilia na kupitisha kila hoja bila ya mchango wowote wa mawazo.
Huyu si miongoni mwa wabunge wanaotega vikao vya Bunge; tumeshuhudia sote anavyofuatilia masuala yote yanayokuwa yakijadiliwa bungeni.
Ingawa wakati mwingine naye ana vijembe vya hapa na pale, lakini si vijembe vya kijinga kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia waheshimiwa wakiporomosha matusi makubwa kama wendawazimu vile na badala ya kuwapuuza wanapandishwa vyeo, na wengine sasa hivi ni mawaziri.
Halima, ana vijembe vya siasa na lugha za vijana. Katika hali ya kawaida vijembe kama hivi, ambavyo si matusi vinakubalika. Lakini vingine vya kuwatukana kuwadhalilisha watu ni mwiko kwenye jamii iliyostaarabika.
Bunge letu lina watu wanaoongea sana na wengine ni wataalamu wa kuongea na kuchekesha kama Jangala vile, lakini kuna wabunge wachache wanaoongea kwa umakini, kwa kuhesabu maneno na kuhakikisha mbali na mantiki kila neno lina maana nzito kulingana na hoja inayojadiliwa, Halima Mdee ni miongoni mwa wabunge hawa wachache.
Kuna wabunge ambao unaona wanajiandaa kabla ya kuongea na wanakuwa wamepitia kwa undani hoja zinazokuwa mezani.
Unaona kwamba kazi hiyo ya kuwawakilisha wananchi wanaifanya kwa moyo wao wote; si kwa lengo la kufurahisha washabiki wa vyama vyao vya siasa, bali kwa lengo la kuijenga nchi yetu. Halima Mdee, ni miongoni mwa wabunge hawa wachache.
Na kusema ukweli, wabunge vijana kwa vyama vyote, wanajitahidi kuwa makini kwa kazi yao ya ubunge. Hata chama tawala kuna vijana makini sana, bahati mbaya ni kwamba baadhi yao wanalewa uchama na kusahau kwamba kitu muhimu ni Tanzania na wala si vyama vya siasa.
Na wengine wanalewa si kwa vile wana mapenzi makubwa na chama chao, bali wanatamani na kutaka kukikutumia chama chao kupata madaraka au kama njia ya kujitajirisha.
Si lengo la makala hii kumpamba Mwana Mama huyu, maana hata bila kumpamba sifa zake zinajitosheleza.
Huyu ni msomi mwanasheria ambaye hadi leo hii bado anaendelea kusoma na kuchimba vitabu hadi atakapofikia Uzamivu.
Hoja inayojengwa hapa ni kwamba ukweli ni lazima usemwe: Halima Mdee, ni Mbunge asiyekuwa na makeke, hana uchu wa madaraka, ni msomi ambaye ameamua kuwawakilisha watu wake.
Anafanya kazi ya uwakilishi na wala si kutumia ubunge kujitajirisha. Mwana Mama huyu, anajisimamia, hayumbishwi na anaishi maisha yake anavyoamini yeye bila kuiga au kufuata mkumbo bila kutafakari kwa kina mwelekeo wa maisha.
Na kwa vyovyote vile huyu ni Mwana Mama wa kuaminika, labda apigwe juju, lakini si ndumakuwili au mnafiki. Tunamfahamu wengi kwamba kwake ndiyo ni ndiyo na hapana ni hapana! Na mara chache kuwapata watu wa namna hii!
Sote tunamfahamu kwa jina la Halima, lakini mwana mama huyu alibatizwa jina la Theodosia, hata hivyo anatumia zaidi jina alilorithi kutoka kwa bibi yake mzaa baba, Halima.
Mdee alizaliwa katika familia ya Wakristo na alibatizwa na kuitwa Theodosia. Ukoo wake ni waumini wa dini ya Kiislamu isipokuwa baba yake na kaka yake ambao walibatizwa na familia yao ikaridhia wawe Wakatoliki.
Halima James Mdee alizaliwa Machi 18 mwaka 1978 katika kijiji cha Makanya, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro akiwa ni mtoto wa mwisho katika familia ya Profesa James Mdee ambaye alikuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alianza kusoma elimu ya msingi katika shule ya msingi Mlimani, Dar es Salaam na kuhitimu mwaka 1991. Alichaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya wasichana Zanaki mwaka 1992 na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1995.
Mwaka 1996 hadi 1998 alisoma kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari ya wasichana Kilakala mkoani Morogoro na 1999 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisomea sheria na kuhitimu mwaka 2003.
Alipata ajira katika Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Vijana mwaka 2004 akiwa Ofisa Maendeleo kama Mwanasheria mpaka 2005, alipoamua kuacha kazi na kuingia katika kinyanganyiro cha uchaguzi mkuu ambako alishiriki kuwapigia kampeni wagombea mbalimbali wa CHADEMA kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa Viti Maalumu.
Uchaguzi mkuu wa 2010, alijitosa kugombea ubunge kiti cha jimbo la Kawe na kushinda kwa kishindo.
Ingawa Halima, amezaliwa mkoa wa Kilimanjaro, lakini ameishi maisha yake yote Dar es Salaam, ndo maana aliamua kugombea Ubunge Dar es Salaam na si Kilimanjaro, maana mbunge makini ni lazima ajue kwa undani maisha ya watu anaowawakilisha.
Na kusema kweli hata watu wa jimbo la Kawe, wanafahamu pasi na shaka kwamba mbunge wao, anayafahamu matatizo yao.
Tunaona fahari kubwa kuwaletea Mwana Mama huyu katika safu yetu hii. Tuna imani tumemtendea haki na tumewatendea haki wasomaji wetu.
Source:Tanzania Daima