Chief Mwanakijiji,
Hii inawezekana kuwa kutokana na hulka yetu watu tusio kwenye madaraka kuwaona kuwa viongozi ni malaika na hawawezi kukosea kwani si binadamu. Hii ni unrealistic expectation. Lakini, pia ni jukumu la viongozi hawa kuonesha kuwa wao ni binadamu na wana majukumu makubwa waliokabidhiwa na wananchi kwani tunaamini kuwa hawatakuwa na makosa ya kijinga au makosa mengi kama watu wa kawaida. Hii ni sifa ya kiongozi, kuwa mfano kwa wengine.
Tatizo nilionalo ni kuwa viongozi wengi tulionao wana ubinafsi na kujifanya miungu-mtu. Kwa upande wa ubinafsi, viongozi hawa hawataki kukubali lawama na kutaka kila kinachoandikwa au kusemwa kuhusu wao, kiwe ni heko, shangwe na wasifu mzuri. Kwa upande wa umungu-mtu, wanasahau (na kuchangia kuwapotosha wananchi) kwa kujifanya kuwa hawafanyi makosa; iwe ni utendaji au hata mambo binafsi kama vile ufuska.
Katika suala hili la Richmond (na hata EPA), viongozi wetu, nasikitika kuwaambia (kama hawana taarifa hii) wameshindwa kuwajibika. Kuwajibika, ni pamoja na kukubali kuwa "Wandugu, japo jambo A,B,C na D lilifanywa kwa nia njema ya kunufaisha taifa, tulipotoka, hatukufanya uhakiki unaotakiwa na tulichemsha. Tunaomba mtuwie radhi, tunahakikisha kuwa kilichoharibika kinatengenezwa, baada ya miezi mitatu, tutawapa mrudisho nyuma wa kinachoendelea". Hali hii ingekuwa rahisi, muda na pesa zisingepotezwa, na mimi kama binadamu ningeelewa na kama mwananchi ningekuwa satisfied. Ukweli ni kwamba, tatizo la Richmond halikufanywa kwa nia njema ya kusaidia taifa. Ubinafsi, uroho, uchu wa kujitakia utajiri kwa mgongo wa Taifa ndivyo vitu vilivyopelekea kwa sakata lote hili.
Zaidi ya hapo, viongozi wetu, wakiongozwa na Waziri Mkuu mjiuzulu Lowassa, wamedhihirisha kuwa si wawajibikaji. Yaani Lowassa hata baada ya kujiuzulu ametoa sababu ambazo zimefanya hata kujiuzulu kwake kulikoonekana kuwa na maana kuwa ni bure kabisa. Lowassa baada ya kujiuzulu, ameishia kutupia lawama mawaziri wake badala ya kujihoji na kusema kuwa mimi kama Waziri Mkuu nilikuwa mtawala mbovu (assuming he is innocent in the whole deal as he claims). Hii pia tulioona wakati Meghji alipomruka Ballali na kusema alidanganywa na gavana mtenguliwa. Je, ni lini viongozi wetu wataacha kutupia lawama watu wengine na kukubali uongozi ikiwa ni pamoja na uwajibikaji? Ni mabilioni mangapi Tanzania itapoteza kabla ya kiongozi mmoja kukubali makosa?
Kukubali makosa si jambo baya kwani wote tu wanadamu. Tatizo ni pale mtu haoni kuwa amekosa na anang'ang'ania kujihusisha na uongozi wa nchi. Nafikiri hata Mh. Rais Kikwete angeimarisha nafasi yake ya urais na hata historia ya nchi yetu pale ambapo angetamka hadharani kuwa alifanya makosa kumwamini sana rafiki yake Lowassa. Rais alishaanza hili pale aliposema kuwa aliamini sana wasaidizi waliomghilibu na kumshurutisha amfukuze kazi mtumishi mmoja wa nchi wakati mtumishi huyo hakuwa na makosa bali ni wasaidizi wake ndio walikuwa wanajaribu kujikosha.
Chief Mwanakijiji, shukrani kwa topic nzuri na nina imani wanaJF watajitoa katika kuichangia. We seriously need to revisit the concept of responsibility (individual na collective), na jinsi inavyounda/chukua nafasi katika serikali yetu.